KIVUMISHI ARIFU na NOMINO ARIFU

By , in Shahada on .

Kivumishi Arifu

Kivumishi arifu hutambuliwa kuwa ni kijalizo kimojawapo. Kivumishi arifu ni neno linalotoa habari zaidi kuhusu kiima cha sentensi ila tu hakikai upande wa kiima bali hukaa upande wa kiarifu na huja mara tu baada ya kitenzi husishi. Kwa mfano:

(a) Mama ni mpole.

(b) Dada si mweupe.

(c) Baba yu mcheshi.

 

Utaona kwamba katika sentensi (a) neno mpole hutoa taarifa zaidi kuhusu nomino ya kiima mama, katika sentensi (b) neno mweupe hutoa taarifa zaidi ya nomino ya kiima dada na katika sentensi (c) neno mcheshi hutoa taarifa zaidi ya nomino ya kiima baba. Neno lolote ambalo hutoa taarifa zaidi kuhusu nomino huitwa kivumishi, na mara nyingi huja mara baada ya nomino k.m. Mama mrefu, dada mweupe au baba mcheshi. Lakini wakati mwingine kivumishi hicho chaweza kuja baada ya kitenzi husishi ndani ya kiarifu na kukamilisha taarifa za kitenzi husishi pia. Kwa hiyo hutambuliwa kama kijalizo.

 

Nomino Arifu

Nomino arifu hutambuliwa kuwa ni kijalizo pia. Nomino arifu ni neno linalofanya kazi ya kutaja kiima au kukibainisha. Hutokea sehemu ya kiarifu na huja mara tu baada ya kitenzi husishi kwa mfano:

(a) Mlima mrefu Barani Afrika ni Kilimanjaro.

(b) Yule kijana ni Askari.

 

Utaona kwamba katika sentensi 9 (a) neno Kilimanjaro hufanya kazi ya kubainisha kiima kinachoelezwa kwenye sentensi na sentensi 9 (b) neno askari hutaja au hubainisha kiima ni nani. Kwa kuwa maneno haya ni viambajengo vya sentensi na yako ndani ya kiarifu na hukamilisha taarifa za vitenzi husishi basi hutambuliwa kuwa ni vijalizo.

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!