KF 120: UHAKIKI WA KIHISTORIA WA DHAMIRA ZA FASIHI

By , in Shahada on . Tagged width:

UHAKIKI WA KIHISTORIA WA DHAMIRA ZA FASIHI

KF 120

MANENO YANAYOJENGA MSINGI WA KOZI HII NA UFAFANUZI WAKE;

 •  FASIHI
 • DHAMIRA
 • UHAKIKI

                                             DHANA YA NENO FASIHI

Mulokozi (2017) Anaeleza dhana ya neno fasihi. Anasema “ Huko Ulaya Dhana ya neno fasihi imekuwa ikihusishwa na neno la Kilatini Littera ambalo maana yake ya asili ni Herufi au Uandikaji. Neno la kiingereza Literature limechipukia hapo.

KATIKA KULIZUNGUMZIA NENO LITTERA/LITERATURE/UANDIKAJI,WANAZUONI  WANATOFAUTIANA KIMAWAZO. TOFAUTI HIZI TUNAZIITA MITAZAMO.

Mitazamo inayotawala dhana hii ipo mitano (5) na dosari zake;

 1. Ni ule unaodai kuwa “Literature” ni jumla ya maandishi yote katika lugha fulani.

                                                             dosari zake 

       (a) Mtazamo huu unapanua sana dhana ya neno fasihi na kuingiza vitu ambavyo sio vya kifasihi.

       (b) Mtazamo huu unaibagua fasihi simulizi.

 1. Mtazamo huu unadai kuwa “Literature” ni maandiko bora. (Wasanii si watu wakawaida)

                                                                 Dosari

 

(a) Mtazamo huu unaupa uzito usanii na uwezo wa kubuni, lakini pia unaifinya fasihi kwa kuihusisha na maandiko yaliyo bora tu.

 1. Huu unadai kuwa “Literature” ni sanaa ya lugha yenye ubunifu bila kujali kama imeandikwa au la. (Mtazamo huu unahalalisha kuwa masimulizi ya kisanaa na nyimbo ni fasihi).

Mtazamo huu wa tatu ndio unatawala hivi sasa katika taaluma ya fasihi ya Kiswahili. Inadaiwa kuwa neno “fasihi” limetokana na neno “Fasuh” katika lugha ya Kiarabu lenye maana ya “Ufasaha wa Lugha”

 1. Mtazamo wa nne (4), ambao ulizuka hapa Afrika Mashariki na kuenea sana miaka ya 1970 ni ule usemao kuwa “Fasihi ni hisi….ambao zinajifafanua kwa njia ya lugha” (Ramadhani, J.A Mulika 2:6). Mtazamo huu unachanganya mambo matatu (3) ambayo ni (i) fasihi yenyewe (ii) mambo yaelezwayo na fasihi (iii) mtindo wa kifasihi.

                                                                     Dosari 

Wenye mtazamo huu wamesahau kuwa, mtindo wa kifasihi mara nyingi ni wa kifasihi, bali fasihi yenyewe si hisi. Vivyo hivyo, fasihi huweza kueleza mapenzi, lakini fasihi yenyewe si mapenzi.

 1. Mtazamo wa tano (5), ambao hususan ni wa karne ya ishirini (20), ni ule ulioanzishwa na wafuasi wa nadharia ya uumbuji (formalism). Mtazamo huu, ambao ulianzishwa na wanaisimu wa Kirusi mwanzoni mwa karne ya 20. unadai kuwa fasihi ni tokeo la matumizi ya lugha kwa njia isiyo ya kawaida ili kuleta athari maalumu. (wanamaanisha… fasihi hukiuka taratibu za kawaida za matumizi ya lugha katika sarufi, maana na sauti ili kumvutia na kumuathiri msikilizaji au msomaji).

                                                                 Dosari 

(a) Mtazamo huu umekosolewa kuwa unaelemea mno upande wa fani na kupuuza maudhui, maana na muktadha wa kazi ya fasihi.

(b) Mtazamo huu unasadifu zaidi ushairi kuliko kumbo zingine za fasihi kama tamthiliya na riwaya ambazo si lazima zitumie lugha kwa namna ya pekee.

MAANA YA FASIHI KWA MITAZAMO YA UJUMLA……

Williady, (2015) Fasihi ni tawi moja wapo la sanaa linalotumia lugha katika kuwasilisha ujumbe wa mdomo au wa maandishi.

Wamitila (2004) Fasihi ni sanaa inayotumia luha na ambayo hujishughulisha na binadamu pamoja na maisha yake na huathri, hugusa au huacha athari fulanina hupatikana katika umbo ambalo linatambuliwa na jamii Fulani.

Kwakuwa fasihi ni aina ya sanaa, ni vyema mwanafunzi akajua pia maana ya sanaa.

   MAANA YA SANAA

(Williady: 2015) Sanaa ni ujuzi au ufundi wenye kuleta manufaa kwa umma.

       AINA/ KUMBO/ TANZU ZA FASIHI

Katika tasnia ya fasihi na taaluma zake kuna aina kuu mbili za fasihi, ambazo ni;

 • Fasihi Simulizi
 • Fasihi Andishi

UMBO LA SANAA

Tunaposema umbo la sanaa tunamaanisha matawi yanayojenga sanaa. Matawi hayo nipamoja na;

Fasihi, maonyesho, ususi, uhunzi, ufumaji, utarizi, uchongaji, ufinyanzi, uchoraji na muziki.

CHIMBUKO LA FASIHI

Kuna nadharia kuu nne (4) za chimbuko la fasihi na dosari zake;

 1. Nadharia ya kidhanifu.Nadharia hii inadai kuwa chimbuko la fasihi ni Mungu. Nadharia hii ni kongwe sana, ilikuwa kabla ya Kristo. Nadharia hii ilianzia huko kwa Wayunani ambao wanafahamika pia kama Wagiriki wa kale huko Ulaya. Hawa walikuwa na Miungu wa ushairi na muziki waliowaitaMuse, ambao yasemekana ndio waliowapa watunzi muhu au kariha (msukumo wa kiroho, kinafsi na kijaziba (inspiration) ) wa kutunga. Pia, wanadai kuwa Mungu ndiye msanii mkuu. Kaumba ulimwengu kwa usanii wa ajabu. Mwanadamu pia ni zao la sanaa ya Mungu. Hivyo uwezo wa mwanadamu wa kubuni kampa Mungu, ambaye ndiye msanii mkuu.

                             DOSARI

 •  Dosari kuu ya nadharia hii ni kwamba inachanganya imani na taaluma (Ni nadharia isiyo na uthibitisho au ushahidi kisayansi, hivyo ni ngumu kuijadili kitaaluma).
 •  Pia, nadharia hii inatafuta chimbuko la vitu vya kitamaduni nje ya maisha ya mwanadamu na nje ya dunia hii.
 1. 2.Chimbuko la fasihi niSihiri”. “Sihiri” hapa inamaanisha uwezo au nguvu ya kimiujiza inayotumiwa na watu kusababisha matokeo fulani. Katika lugha ya kiingereza Sihiri huitwa Magic. Hawa wanadai kuwa katika hatua ya awali katika maendeleo ya mwanadamu sayansi na teknolojia vilikuwa katika hatua ya mwanzo kabisa. Hivyo Sihiri na miujiza vilitumia nafasi ya sayansi, teknolojia na ugunduzi. Fasihi na sanaa viliibuka kama chombo cha kuendeshea sihiri. Mfano wawindaji kabla ya kwenda kuwinda waliichora picha kisha wakaichoma picha hiyo kwa mshale, tendo hili lilimaanisha mavuno ya kutosha porini. Nyimbo walizoimba na maneno waliyonuiza wakati wa kufanya sihiri hiyo ndiyo ushairi wa mwanzo.

                 DOSARI

 •  Dosari ya nadharia hii ni kwamba inachanganya dhima na chimbuko. Kutumika kwa sihiri katika fasihi hakuthibitishi kuwa sihiri ndiyo chimbuko lake.
 1. Fasihi imetokana na mwigo(uigaji).Katika nadharia hii ambayo kwa lugha ya kiingereza inaitwaimitation, na katika Kiyunani inaitwa mimesis, inaelezwa kuwa mwanadamu alianza kuwa mbunifu kwa kuiga maumbile yaliyomzunguka, hivyo sanaa za mwanzo mara nyingi zilijaribu kumathilisha vitu vilivyomo katika mazingira, kwa mfano wanyama, ndege, miti, watu, na kadhalika.

                      DOSARI

 • Nadharia hii inasisitiza sana uigaji na kusahau suala la ubunifu katika sanaa na fasihi. Pia, wamesahau kuwa ndani ya uigaji kunavionjo vinavyotokana na ubunifu wa msanii.
 1. Chimbuko la fasihi ni ile hali ya kiyakinifu. Nadharia hii ambayo imejikita kwenye fikra za Marx na Engels (rej. On Literature and Art, 1976) na nadharia ya ubadiliko (evolution) ya Charles Darwin, hudai kuwa mwanadamu ni zao la maumbile asiliaya ulimwengu, kuwa ubadilikaji wa taratibu wa mwanadamu kutoka katika hali ya unyama kuingia katika hali ya utu umechukua mamilioni ya miaka, halikuwa tukio la siku au wiki moja tu. Utamaduni, ikiwapo lugha na fasihi, ni zao la mabadiliko hayo.

.

                       DOSARI

Baadhi ya maelezo yahusuyo mabadiliko ya mwanadamu kutoka katika usokwe kuingia katika utu,na hatua zake za mwanzo za kujenga utamaduni  na lugha, bado ni mambo ya kidhahania ambayo hayajathibitishwa kwa ukamilifu.

 Hata hivyo, nadharia ya kiyakinifu inaelekea kukubalika zaidi kitaaluma kuliko nadharia zingine.

                          DHIMA ZA FASIHI

Fasihi hufanya kazi mbalimbali katika maisha:

Kuelimisha jamii-Fasihi hutumika kama nyenzo ya kuelimisha jamii, kupitia fasihi wanajamii wanaweza kuelimishwa juu ya mambo mabalimbali, kama vile juu ya umuhimu wa kuishi kwa amani, umuhimu wa kijikomboa kifikra, umuhimu wa kujikomboa kiuchumi, ubaya wa ufisadi na kadhalika.

Kukuza utamaduni-Kupitia fasihi simulizi, tamaduni na mila za jamii husika huhifadhiwa. Kwa mfano kupitia methali, misemo, nahau na vitendawili unaweza kujua mila na tamaduni za jamii husika.

Kukuza lugha-Fasihi hutumia lugha kufikisha ujumbe wake katika jamii, lugha ya fasihi huwa ni ya kisanaa zaidi na hivyo kuifanya iwe yenye mvuto kwa wasikilizaji au wasomaji. Mtu anaposoma au kusikiliza kazi ya fasihi anapata ujuzi wa lugha. Lakini pia fasihi yenyewe inaweza kutumika kama chombo cha kukuza lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na utajiri mkubwa wa lugha.

Kuburudisha jamii-Pamoja na mambo mengine fasihi inalenga kuburudisha jamii. Kupitia takribani vipera vyake vyote, fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira, kwa mfano kupitia nyimbo, hadithi, mashairi na kadhalika.

Kukomboa jamii.

Kuonya jamii-Fasihi ina jukumu la kuhakikisha wanajamii wanakaa katika mstari wa maadili ya jamii husika. Kupitia fasihi wanajamii wanapewa mwongozo wa jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.

Kukuza uwezo wa kufikiri-Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. Kwa mfano, vitendawili, ngano za mtanziko na kadhalika.

                   FASIHI YA KISWAHILI

Dhana ya “Fasihi ya Kiswahili” imekuwa inawachanganya wanataaluma wengi. Hii kwa sababu inachanganya kwa pamoja dhana kadhaa, ambazo ni:

 • Fasihi ya Kiswahili
 • Fasihi kwa Kiswahili
 • Fasihi ya Waswahili

Ili kuzielewa vema dhana hizo za fasihi ya Kiswahili , kwanza tunatakiwa kumjua Mswahili.

Mswahili ni nani?

Ponera (2010:69), Mswahili ni mtu mwenye kiwango kikubwa cha umilisi wa lugha ya Kiswahili. Vilevile, ni mtu ambaye amefungamana sana na mila na desturi za jamii ya watumiao lugha ya Kiswahili kiasi hata cha kumuathiri kifikra, kimtazamo na kiitikadi.

FASIHI YA MSWAHILI

Hii ni ile ambayo  hutungwa  au kuandikwa  kwa lugha ya Kiswahili na Mswahili wa asili na fasihi hii hufuata mila na utamaduni wa waswahili unaopatikana katika mazingira yake na hivyo humtambulisha mswahili.

SIFA BAINIFU ZA FASIHI YA WASWAHILI

 •  Hutungwa au kuandikwa na Mswahili wa asili.
 •  Hutumia lugha ya Kiswahili.
 •  Huakisi mila na desturi za Waswahili.
 •  Nikitambulisho cha Mswahili.
 •  Huwakilisha mtazamo na falsafa ya Mswahili kuhusu maisha na ulimwengu.

FASIHI YA KISWAHILI NI IPI?

Syambo na Mazrui (1992:ix) wanafafanua maana ya Fasihi ya Kiswahili kuwa: …..hatuna budi kuichukulia Fasihi ya Kiswahili kuwa ni ile iliyoandikwa kwa Kiswahili tu, iwapo inazungumzia utamaduni wa kiswahili au utamaduni mwingineo. Maadamu fasihi hiyo imetumia lugha ya Kiswahili na imefuata mbinu za ufasaha wa lugha hiyo, basi, kwa tafsiri yetu ni Fasihi ya Kiswahili.

SIFA BAINIFU ZA FASIHI YA KISWAHILI

 •  Hutungwa au kuandikwa kwa Kiswahili.
 •  Hutumia lugha ya Kiswahili.
 •  Huakisi mila, utamdunina tajiriba ya mwananchi wa Afrika ya Mashariki na Kati.

FASIHI KWA KISWAHILI

Mulokozi (2017), anasema, “Kuenea kwa Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki, na hata nje ya bara la Afrika, na maingiliano kati ya wazungumzaji wa Kiswahili na mataifa mengine, kumezua fungu la fasihi ya kigeni katika lugha ya Kiswahili; kwa mfano tafsiri mbalimbali. Mifano mizuri ni Biblia, Shakespeare Juliasi Kaizari, Kitereza (1980), hadithi za Alfu Lela – Ulela, na kadhalika. Fasihi ya aina hiyo ndiyo tunayoiita “Fasihi kwa Kiswahili” Hivyo “Fasihi kwa Kiswahili” ni tafsiri ya fasihi ya mataifa mengine kwa lugha ya Kiswahili.

SIFA BAINIFU ZA FASIHI KWA KISWAHILI

 •  Ni fasihi iliyoandikwa kwa lugha nyingine isiyokuwa Kiswahili na kisha kufasiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
 •  Huakisi mila, utamaduni na tajiriba ya kule ilikotoka, hivyo haimtambulishi Mswahili.
 •  Kwa kawaida huwakilisha mtazamo na falsafa ya jamii ya lugha chanzi.

AINA KUU ZA FASIHI YA KISWAHILI

Kuna aina kuu mbili (2) za fasihi ya kiswahili ambazo ni:

           Fasihi Simulizi

 1.           Fasihi Andishi

FASIHI SIMULIZI

Mulokozi (2017), anafafanua istilahi ya neno “Simulizi” na mapungufu yake . Anasema “Fasihi simulizi ni istilahi inayotumiwa kuelezea dhana ya fasihi itolewayo kwa mdomo bila kuandikwa. Istilahi  hii, ambayo imezuka miaka ya 1970, ina dosari, kwani neno “Simulizi” halina maana ya “Kitu kinachonenwa” (Kwa Kiingereza: Oral) bali lina maana ya “Kitu kinachosimuliwa” (Kwa Kiingereza : narrative). Hivyo tafsiri sahihi ya “Fasihi simulizi” katika kiingereza ni “narrative Literature” siyo “Oral Literature”. Hata hivyo kwa kuwa istilahi hiyo imekwishaenea na kukubalika, ni vigumu kuibadili.

MAANA YA FASIHI SIMULIZI KWA UJUMLA……

Williady (2015) Fasihi simulizi ni aina ya fasihi inayotumia mdomo na utendaji wa viungo vya mwili katika kuwasilisha maudhui ya fanani kwa hadhira iliyokusudiwa.

 TANZU ZA FASIHI SIMULIZI

Uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi bado unautata, wataalamu wengi wa taaluma za fasihi wanakinzana katika kutoa idadi ya tanzu za fasihi na vipera vyake.

Balisidya (1987), anaainisha “Mafungu” (kumbo/tanzu) tatu (3) za fasihi simulizi ambazo ni:

 1. Nathari
 2. Ushairi
 3. Semi

Balisidya, hakuishia kwenye uainishaji wa tanzu tu, pia anaainisha na vipera vyake;

 1. Nathari
 1. a)Ngano
 2. b)Tarihi
 3. c)Visasili
 4.    Ushari
 5. a)Nyimbo
 6. b)Maghani
 7.    Semi
 8. a)Misemo
 9. b)Misimu
 10. c)Mafumbo

Nao TET (1976, 1988:120), wanaainisha tanzu za fasihi simulizi na vipera vyake, kuwa ni:

 1. Hadithi

       (a) Ngano

       (b) Tarihi

       (c) Visasili

       (d) Vigano

       (e) Soga

 1. 2.Nudhumu/ushairi

      (a) Ngonjera

                    (b) Maghani

      (c) Nyimbo

                     (d) Ushairi

 1.     Semi

                     (a) Methali

                     (b) Misemo

                     (c)  Nahau

                     (d) Vitendawil

                      (e) Mizungu

       M.M. Mulokozi (1996)

 1. Semi

       (a) Methali

       (b) Vitendawili

       (c) Mafumbo

       (d) lakabu

       (e) Vitanzi – Ndimi

       (f) Kauli – taulia

 1. MAZUNGUMZO

       (a) Hotuba

     (b) Malumbano ya watani

     (c) Ulumbi

     (d) Mizaha

     (e) Sala

 1. MASIMULIZI/HADITHI

     (a) Ngano

     (b) Istiara

     (c) Mbazi

     (d) Michapo

     (e) Hekaya

     (f) Visasuli

     (g) Visakale

     (h) Mapisi

     (i) Tarihi

     (j) Nasabu

     (k) Kumbukumbu

     (l) Visasili vya ibada

     (m) Visasili vya usuli

     (n) Visasili vya miungu/ibada

 1. MAIGIZO

       (a) Maigizo ya watoto

     (b) Maigizo ya sherehe

     (c) Maigizo ya misiba

     (d) Maigizo ya kidini

 1. USHAIRI/NYIMBO

     (a) Tumbuizo

     (b) Tukuzo

     (c) Chapuzi

     (d) Tendi

 1. USHAIRI / MAGHANI

     (a) Ghani Nafsi

     (b) Ghani Tumbuizi

     (c) Ghani Sifo

     (d) Ghani Masimulizi

 1. NGOMEZI

     (a) Ngomezi za Taarifa

     (b) Ngomezi za Tahadhari

     (c) Ngomezi za uhusiano (mf. Wa kimapenzi)

 1. FASIHI ANDISHI

 Hii ni aina ya Fasihi ambayo uwasilishaji wake huwa kwa njiaya maandishi. Wataalamu wengi wa fasihi wanakubaliana kuwa fasihi andishi imegawanyika katika tanzu kuu tatu (3) ambazo ni:

 (i) Ushairi

(ii) Riwaya

(iii) Tamthiliya

Katika ngazi ya juu ya stadi za fasihi andishi tanzu nyingine huongezeka, ambayo ni hadithi fupi.

MAANA YA USHAIRI

(WANA – MAPOKEO)

Shaaban Robert katika kitabu chake cha “Kielezo cha Fasili” (1968:61) ana sema “Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari. Mwauliza, shairi na tenzi ni nini? Wimbo ni shairi dogo, ushairi ni wimbo mkubwa na tenzi ni upeo wa ushairi. Mwauliza tena kina na ufasaha huweza kuwa nini? Kina ni mlingano wa sauti za herufi. Kwa maneno mengine huitwa mizani ya sauti, na ufasaha ni uzuri wa lugha. Mawazo maono na fikra za ndani zinapoelezwa kwa muhtasari wa shairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu”.

Udhaifu wa fasili hii 

 • Udhaifu uliopo katika fasili hii ni kwamba, ingawa ushairi wa aina yoyote unaweza kuimbwa, lakini siyo kila kiimbwacho kitaitwa ushairi. Kwa mfano uimbaji wa hesabu kama vile wafanyavyo baadhi ya walimu kuwakaririsha wanafunzi orodha ya kwanza mpaka kumi na mbili kwa  hesabu za mara, huo si ushairi.
 • Sheikh Amri Abed Kaluta katika kitabu chake cha “Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri” (1954:1) anafafanua maana ya ushairi, anasema: ”Shairi au Utenzi ni wimbo, hivyo kama shairi haliimbiki halina maana yoyote”

Udhaifu wa fasili hii 

 • Udhaifu uliopo katika fasili hii ni kwamba, Sheikh Amri Abed Kaluta amehusisha tanzu chache sana za ushairi katika fasili yake yaani mashairi na tenzi na kusahau maghani, nyimbo na ngonjera.

Pia si lazima kila shairi liimbike, yapo badhi ya mashairi ambayo hutolewa kwa kusemwa kama vile Maghani, ambayo hughanwa.

(WANA-USASA)

 1. Mulokozi na K. Kahigi katika “Kunga za Ushairi na Lugha” (1982:25) wanasema “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalum wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha au sitiari au ishara, katika usemi, maandishi , au mahadhi ya wimbo, ili kueleza wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi Fulani, kuhusu maisha au mazingira ya binadamu, kwa njia inayogusa moyo”.

Masamba D.P. B (1983:59) anaeleza kuwa “Ushairi ni utungo uliokusudia kueleza hisia za ndani alizonazo msemaji au mshairi kwa kutumia lugha ya mkato au fupi, yenye mvuto kwa namna maneno yanavyopangwa kwa kisanifu kwa uangalifu na ulinganifu, lugha yenye mvuto kwa utamu wa maneno yake yenye mguso wa moyo kwa ajili ya mpangilio wa maneno yake”.

VIPENGELE VYA USHAIRI WA KISWAHILI

Ushairi wa Kiswahili unavipengele vikuu viwili (2) Fani na Maudhui.

VIPENGELE VYA FANI

Hivi ni vipengele vya kiufundi avitumiavyo msanii katika kuwasilisha ujumbe wa kazi yake kwa hadhira. Fani huundwa na vipengele (vipera) vifuatavyo:

 1. WAHUSIKA
 2. MANDHARI
 1. MUUNDO/UMBO (Vipande, Mshororo, Ubeti, Vina na

       Mizani)

 1. MATUMIZI YA LUGHA
 1. RIWAYA

Nadharia ya Riwaya

Kumekuwa na misuguano kadhaa kutoka kwa wanazuoni waliothubutu kutoa fasili ya riwaya. Imeonekana wazi kuwa kunakukubaliana kwa baadhi ya masuala na kutofautiana pia katika kutoa fasili hii. Miongoni mwa masuala yaliyopelekea misuguano katika utoaji wa fasili hii ni pamoja na:

Dhima / maudhui ya riwaya

Mipaka ya riwaya pindi inapohusishwa na hadithi fupi au novela

Ukubwa / urefu wa riwaya

Aina za riwaya

Kuna wengine huchanganya utanzu wa riwaya na vijitanzu vingine vya kinathari (yaani, vile vitumiavyo lugha ya mjazo) kama vile Hadithi fupi, Novela, Tawasifu na Wasifu.

Hadithi fupi

Tofauti yake na riwaya hujikita katika upeo na uchangamani. Hii inamaana kuwa hadithi fupi huwa sahili sana ilihali riwaya huwa imetanza zaidi.

Novela

Hii huwa ni changamani zaidi kuliko hadithi fupi. Huweza kuwa na visa vingi kiasi kulinganisha na hadithi fupi.

Tawasifu

Ni utungo utumiao lugha ya mjazo ukisimulia habari za mtunzi mwenyewe.

Wasifu

Ni utungo utumiao lugha ya mjazo ambapo mtunzi husimulia habari za mtu mwingine.

Ukichunguza kwa makini vijitanzu hivyo utaona kuwa vinatofautiana na riwaya katika vigezo vya: urefu, uchangamani, idadi ya wahusika, lugha, vitushi, U―Kina, dhamira n.k.

Sifa bainifu za riwaya

Ilinganishwapo na tanzu nyingine, riwaya huwa nasifa bainifu zifuatazo:

 • Kutokufungwa na sheria nyingi (kinyume na makumbo mengine ya tamthiliya na ushairi).
 • Matumizi ya lugha ya kinathari.
 • Kuwa na mawanda mapana katika urefu na kina.
 • Ni zao halisi la kibepari.
 • Kuwa na uhalisi kwa kiasi kikubwa.
 • Mahitaji ya kusoma na kuandika.
 • Kuwepo kwa maisha na makazi yenye utulivu.
 • Kuwa na uwezo wa kugusia hadi vitu vionekanavyo kama vidogo (kwa maelezo zaidi, tazama. Madumulla, 2009).

TANZU ZA RIWAYA

Kwa kuzingatia vigezo vya maudhui, dhima na mtindo, tanzu za riwaya ziko nyingi sana, ambazo ni:

      (i)            Istiara (Umbo la nje la riwaya hii ni kiwakilishi cha jambo jingine)

    (ii)             Riwaya – barua

   (iii)             Riwaya – chuku

  (iv)             Riwaya – sira (Husimulia habari za maisha ya mhusika tangu kuzaliwa)

    (v)             Riwaya – tendi (Matendo ya ushujaa)

  (vi)             Riwaya – teti (Ni riwaya inayosimulia vituko na masaibu ya watu wapuuzi, walaghai, wajanja (maayari) )

 (vii)             Riwaya – Jusura (Mikasa ya kussiimua damu)

(viii)             Riwaya ya Kifalsafa

  (ix)            (ix) Riwaya ya Kifanyakazi

    (x)            (x)  Riwaya ya Kihistoria

  (xi)            (xi) Riwaya ya Kijamii

 (xii)            (xii) Riwaya ya Kingano

(xiii)            (xiii) Riwaya ya Kisaikolojia

(xiv)            (xiv) Riwaya ya Kimahaba

(xv)            (xv) Riwaya ya Kimajaribio

(xvi)            (xvi)  Riwaya ya Ufungwa

(xvii)            (xvii) Riwaya ya Uhalifu/Ujambazi

(xviii)            (xviii) Riwaya ya Ujasusi

(xix)            (xix) Riwaya ya Upelelezi

(xx)            (xx)  Riwaya ya Utumwa/Simuluzi za Watumwa

(xxi)            (xxi)  Riwaya ya Vita

(xxii)            (xxii) Riwaya ya Vitisho

(xxiii)            (xxiii) Riwaya ya Watoto

(xxiv)            (xxiv) Riwaya ya Kisayansi

TAMTHILIA

Istilahi ya “Tamthilia” inatokana na neno “Mithali” ambalo lina maana ya “mfano” au ishara ya kitu fulani. Hivyo katika tamthilia kitu kimoja humathilishwa {ufananishwa} au huwakilishwa na kitu kingine.

MAANA YA TAMTHILIA

Tamthilia au drama ni igizo la kifasihi lililokusudiwa kutendwa jukwaani kwa ajili ya hadhira fulani. Hivyo, kwa lugha ya kawaida, tamthilia huitwa mchezo wa kuigiza. Kwa kawaida tamthilia huwa na masimulizi ambayo huigizwa na wahusika wa pande mbili au zaidi zinazogongana. Mgongano huo hujenga mgogoro ambao unaposuluhishwa au kutatuliwa mchezo huwa umemalizika.

TAMTHILIA NI SANAA ZA MAONYESHO

Mlama (1983:203) anasema, sanaa za maonyesho ni sanaa ambazo huwasilishwa, ana kwa ana, tukio fulani kwa hadhira kwa kutumia usahii wa kiutendaji. Kwa mfano badala ya kuwasilisha wazo kwa hadhira kwa kutumia maneno kama katika ushairi, sanaa za maonyesho huliweka wazo lile katika hali ya tukio linaloweza kutendeka kwa kutumia usanii wa utendaji kama vile vitendo, uchezaji ngoma n.k.

SIFA ZA TAMTHILIA / SANAA ZA MAONYESHO

Muhando (Mlama) na Balisidya (1976:4) wanatoa sifa (4) za sanaa za maonyesho;

 1. Dhana inayotendeka
 2. Mtendaji
 3. Uwanja wa kutendeka
 4. Watazamaji

Mulokozi (2017) anatoa sifa (7);

 1. Dhana inayotendeka
 2. Uwanja wa kutendea
 3. Watendaji
 4. Hadhira
 5. Kusudio la kisanaa
 6. Muktadha wa kisanaa

Ubunifu (Umathilishaji)

                                                    UHAKIKI

Uhakiki ni kitendo cha kusoma kazi ya fasihi simulizi au andishi na kuchambua vipengele vya fani na maudhui kwa kuangalia ubora na udhaifu wa kazi hiyo.

MHAKIKI NI NANI?

Mhakiki ni yule mtu anayechambua kazi ya fasihi, yaweza kuwa fasihi andishi au fasihi simulizi na kuchunguza vipengele vya fani na maudhui.

DHIMA ZA MHAKIKI

 • Kuchambua vipengele vya fani na maudhui.
 • Kueleza ubora na upungufu wa kazi hiyo.
 • Kueleza umuhimu wa kazi hiyo.
 • Kufafanua matumizi ya lugha ya picha, taswira na mafumbo yaliyojitokeza katika kazi hiyo.
 • Kumshauri mwandishi juu ya maboresho ya kazi yake.

VIPENGELE VINAVYOFANYIWA UHAKIKI


Fani

 • Wahusika
 • Mtindo
 • Muundo
 • Mandhari
 • Matumizi ya lugha

 Maudhui

 • Dhamira
 • Falsafa
 • Mtazamo/msimamo
 • Ujumbe
 • Migogoro

DHAMIRA

Tumeona kuwa dhamira ni kipengele cha maudhui, hivyo ili kufaamu vizuri maana ya dhamira tunatakiwa kujadili kwanza dhana ya maudhui.

Maudhui ni nini?

 • Maudhui ni maana ya kazi ya fasihi au ni mawazo yanayozungumzwa ndani ya kazi ya kifasihi.
 • Kwa kawaida; mwandishi hufafanua maana au mawazo  hayo kwa kupitia vipengele vyake ambavyo ni dhamira, falsafa, mtazamo au msimamo, ujumbe na migogoro.
 •  Wazo kuu huitwa dhamira.

DHAMIRA

Dhamira ndio wazo kuu la mtunzi katika kazi yake, linapotangamana na mtazamo wake hutupatia ujumbe auletao kwa hadhira yake.

UHAKIKI WA KIHISTORIA WA DHAMIRA ZA FASIHI YA KISWAHILI

Wataalamu katika taaluma za fasihi ya kiswahili wanajadili historia na maendeleo ya fasihi ya kiswahili kwa kugawa vipindi kadhaa tangu kuwako kwa kazi za kifasihi ulimwenguni. Katika fasihi ya kiswahili wataalamu wanajadili vipindi vikuu tatu (3) ambavyo ni:

 1. Kipindi kabla ya ukoloni
 2. Kipindi cha ukoloni
 3. Kipindi baada ya uhuru

KIPINDI KABLA YA UKOLONI

Miongoni mwa tanzu kuu tatu (3) za fasihi ya Kiswahili, ushairi ndio tanzu ya kwanza kuwako kihistoria, ikifuatiwa na riwaya na baadae tamthilia.

Tunapofuatilia historia ya ushairi wa Kiswahili hatuna budi kuzingatia mambo mawili ya msingi:

Kwanza, ushairi simulizi ulianza pale mwanadamu alipoanza kutumia lugha.

Pili, historia ya ushairi andishi wa Kiswahili inahusishwa na ujio wa wageni katika Pwani ya Afrika Mashariki. Hususani Waarabu ambao walileta hati ya Kiarabu na baadaye watu wa Ulaya ambao walileta hati za Kirumi.

MAENDELEO YA FASIHI YA KISWAHILI KIPINDI KABLA YA UKOLONI (Miaka ya 1000 hadi 1500 BK)

Kipindi kabla ya ukoloni ni kipindi ambacho miji mingi ya Waafrika ilikuwa ikistawi polepole sana. Kipindi hicho ushairi na kazi zingine za kifasihi zilipewa jukumu zito sana katika jamii.

JUKUMU LA USHAIRI KIPINDI HIKI

Ushairi ulikuwa na jukumu la kuelimisha, kuonya, kuelekeza, kulea, kuburudisha n.k. Majukumu haya ya ushairi yalikuwa ni kwa wanajamii wote kuanzia watoto wachanga hadi wazee, kuanzia uzima, makuzi hadi kifo ushairi ulihusika. Mtoto alipozaliwa alipokelewa kwa nyimbo, alipewa jina kwa nyimbo, akilia alibembelezwa kwa nyimbo, alijifunza vitu mbalimbali vinavyozunguka mazingira yake kwa nyimbo, jando na unyago kwa nyimbo, aliolewa au kuoa kwa nyimbo hadi kusindikizwa kaburini kwa nyimbo.

 Nyimbo za wakati huo hazikuandikwa mahali popote, na ushairi ulikuwa katika hali ya usimulizi. Maudhui yake yalihimiza kazi na mambo fulanifulani katika jamii. Zipo tungo chache zilizohifadhiwa, mfano Tungo za Fumo Liyongo. Fumo Liyongo alitunga tungo mbalimbali kama vile Sifa za Mwana Munga, inasemekana utungo huu ulitungwa mwaka 1517. Utungo huu  ulihifadhiwa kichwani, kwa sasa upo kama muswada. Wimbo huu ulimsifu mke wake, sifa za kuanzia kichwani hadi nyayoni.

Utungo wa Hamziya ni miongoni mwa tungo za kishairi za kale. Huu ni utungo wa kikasida unaomsifu Mtume Mohammed, inasadikika kuwa ulitungwa mwaka 1652 au kabla ya hapo. Utungo huu ni tafsiri ya utungo wa kiarabu Umma ul Qura (yaani mama wa mji) wa mshairi wa ki – sufi kutoka Misri. Tungo zingine za zamani ni Utenzi wa Tambuka (pia Chuo cha Herekali), Utenzi wa Vita vya BadriUtendi wa AyubuUtendi wa Mikidadi na MayasaSiri li – AsrariAyi WangiwangiUtendi wa QiyamaKasida ya BurdaiAl – InkishafiShamiuniDuaDura MandhumaUkawafi wa MirajiUtendi wa HaudajiTakhmisa ya LiyongoUtenzi wa Shufaka n.k.

Kipindi hiki kilikwisha baada ya uvamizi wa Waarabu katika miji ya Pwani ya Afrika ya Mashariki. Kumbuka kabla ya Wareno tayari Waarabu walikuwa wana mahusiano mazuri na wenyeji wa miji ya Pwani na miji mingine ya Pwani ilikuwa imestawi sana kwa sababu za kibiashara. Ijapokuwa maandishi ya Kiarabu yalikuwepo lakini washairi wengi waliendelea kutunga kwa ghibu kwa kuwa hayakukusudiwa kuhifadhiwa katika maandishi.

WAKATI WA WARENO (Miaka ya 1500 hadi 1750)

Ikimbukwe kuwa katika miaka hii ya 1500 hadi 1750 (Kipindi cha utawala wa wareno) kazi za kifasihi zilizotungwa na kuandikwa bado zilikuwa ni zile za ushairi na tendi.

Historia inaeleza kuwa Wareno waliingia Pwani ya Afrika ya Mashariki mwaka 1498. Kuingia kwao kulipigwa vikali sana na wenyeji kwa kuwa walitaka kutumia mabavu kuhodhi biashara iliyokuwa imeshamiri kati ya wenyeji na watu wa Bara la Asia. Kwa kuwa Wareno walikuwa ni wafanyabiashara walitaka kumiliki bandari zote za miji ya Pwani ya Afrika ya Mashariki.

Mwaka 1698 Ngome ya Wareno iliangushwa rasmi na miaka ya 1728/30 Wareno walikuwa tayari wameondolewa Pwani ya Afrika Mashariki. Kutokana na mapigano hayo miji mingi ya Afrika Mashariki iliyokuwa imestawi kwa kiwango chake mfano Lamu na Pate iliporomoka kabisa. Utenzi wa Al –Inkishafi unaelezea vizuri anguko la miji hii. Hivyo kipindi cha Wareno hakikuwa na tungo nyingi, labda kwa sababu tungi nyingi zilikuwa bado tungo simulizi. Hata hivyo zipo tungo chache zilizotungwa kwa ajili ya kumpinga Mreno, ushairi wa mtunzi mwanamke ulioitwa Mzungu Migeli, wake Mwana Mwinyi Mvita.

Katika moja ya mabeti yake anasema:

                                        Mzungu Migeli umwongo,

                                        Mato yako yana tongo,

                                        Kwani kuata mpango,

                                        Kwenda kibanga uani (Hichens 1979:88).

Utungo mwingine ni Portugezi Afala, Mmoja wa washairi alitongoa hivi:

                                         Portugezi afala, faliki afala velo,

                                         Baziiada sponyila watarafai biselo,

                                         Si nyama ya kuanila, defehati defehalo,

                                         Vinyo inakusumbula, vinyu na butizialo (Abdulazizi, 1979:90).

Kipindi hiki cha utawala wa Wareno kazi za kifasihi zilizotawala katika ulingo wa fasihi ya kiswahili zilikuwa ni ushairi tu na kwa kuwa hakukuwa na mabadiliko makubwa katika  ushairi, hivyo hakukuwa na athari zozote za kiarudhi zilizojitokeza.

WAKATI WA WAARABU (1750 – 1900)

Bado ushairi iliendelea kutamba katika kipindi hiki.

Baada ya kufukuzwa Wareno, Waomani nao hawakutaka kuondoka Pwani ya Afrika ya Mashariki, waliamua kukaa na kutawala. Utawala wa Waarabu wa Omani ulipata nguvu zaidi kuanzia mwaka 1832. Sultan Seyyid Said alipohamishia makao yake makuu katika kisiwa cha Zanzibar. Waarabu kuanzia hapo wakafanya Pwani ya Afrka Mashariki kuwa koloni lao. Hapo mapambano yakahamia kati ya Waswahili na Waarabu.

Kipindi hiki kilitawaliwa na maisha ya Kimwinyi, Kibwanyenye na anasa nyingi. Ujio wa Waarabu ulileta athari kubwa katika maendeleo ya ushairi (ikimbukwe kuw ushairi wa kiswahili kipindi hiki ndio ilikuwa tanzu pekee katika fasihi  ya Kiswahili). Waarabu walileta dini ya Kiislamu na taaluma ya kuandika kwa hati ya Kiarabu. Hivyo waswahili walishiriki katika utamaduni huo wa Waarabu kwa kila namna, halikadhalika taaluma mbalimbali kwa kutumia lugha ya Kiarabu. Wapo wenyeji walioslimu dini na wakajifunza kusoma na kuandika kiarabu kupitia madrasa. Hivyo kusoma na kuandika kulienea sana miongoni mwa wale walioslimu.

Ukweli ni kwamba washairi wengi wa ushairi wa Kiswahili wa mwanzo walikuwa ni Waislamu kwa sababu hiyo, ijapokuwa hata ambao hawakuwa Waislamu wapo japo kwa idadi ndogo, waandishi wengi walikuwa Mashekhe na walimu wa dini, hawa walijua hasa lugha ya kiarabu na Korani tukufu.

Katika kipindi hiki kila Mswahili aliyeishi maeneo haya alipenda chohote chenye uarabu, na uarabu ukawa ndio kipimo cha ustaarabu.

Athari zilizotokana na utawala wa Waarabu katika kazi za kifasihi (Ushairi) wa Kiswahili

 • Athari za Kimsamiati na  Kiistilahi 

Lugha ya Kiarabu ina maneno mengi katika ushairi hata katika lugha ya Kiswahili. Mfano maneno kama alasiri, magharibi, darasa, kitabu n.k. Pia kuna istilahi inazohusiana na ushairi tu, mfano shairi, tathmina, tathnia, tathlitha, tarbia n.k.

 • Athari za Kimaudhui 

Ushairi uliotungwa kipindi cha Waarabu ulikuwa na maudhui yaliyogusa nyanja mbalimbali kama za kisiasa, kidini, kibiashara na mahusiano ya kitabaka yaliyokuwepo.

Mfano kuwepo kwa upinzani kutoka kwa Waswahili dhidi ya utawala kandamizi wa Waarabu kulichochea uandishi wa mashairi mengi ya kisiasa, moja wapo ni Diwani ya Muyaka.

Muyaka alikuwa ni mwanasiasa aliyetumia ushairi wake kupinga utawala wa Waarabu na alihimiza watu kuungana ili kumng’oa Mwarabu. Utenzi wa Akida pia ulizungumzia harakati za ukombozi dhidi ya Waarabu wa Omani.

 • Athari za Kiarudhi 

Ushairi wa Kiswahili uliathiriwa sana na taratibu za kiutunzi za Kiarabu. Mfano ushairi wa Kiarabu ulisisitiza sana suala la utoshelevu wa kimaana katika mshororo na ubeti. Hali hii pia tunaiona katika ushairi wa Kiswahili kwa wanamapokeo.

Ushairi wa kiarabu uligawa mshororo vipande vikuu viwili, kwa kiarabu mgawanyo huu wa vipande uliitwa misraa. Hata hivyo ushairi wa Kiswahili unavipande viwili na wakati mwingine vitatu.

WAKATI WA UKOLONI WA WADACHI NA WAJERUMANI (Miaka ya 1885 hadi 1910)

Kihistoria kipindi hiki kilikuwa na upinzani mkali kati ya wenyeji na Wajerumani, hivyo kulikuwa na vita. Mfano Mkwawa waliongoza majeshi yake kupigana na Wajerumani mwaka 1891 hadi 1898, Abushiri na Bwana Heri 1888 hadi 1889, Isike wa Unyanyembe 1893, Mangi Meli wa Moshi 1900 na Vita vya Majimaji 1905 hadi 1907.

Mbali na upinzani uliokuwepo, wajerumani walisisitiza matumizi ya Kiswahili kwa watumishi wa serikalini na Mashuleni na katika dini, mfano Biblia ilitafsiriwa katika lugha ya Kiswahili.

Magazeti mbalimbali yalianzishwa katika kipindi hiki, kama vile Kiongozi (1905), habari za MweziPwani na BaraBaraza n.k. hivyo mashairi mengi na hadithi fupi zilitungwa na kuchapishwa magazetini. Mashairi na hadithi hizo ziliwapinga wakoloni, kazi hizo ziliandikwa kisitiari ili kukwepa udhibiti. Mfano wa mashairi yaliyopinga ukoloni waziwazi enzi hizo ni pamoja na Utenzi wa Vita vya Wadachi na Utenzi wa Vita vya Majimaji. Pia mashairi na hadithi za kikasuku hazikukosekana. Wapo baadhi ya waandishi waliotunga kwaajili ya kuwatukuza wakoloni na ukoloni. Hali kadhalika kazi zingine za kifasihi zilizungumzia dhamira mbalimbali kama vile mapenzi, kazi n.k.

Katika kipindi hiki ndipo sasa riwaya ya kiswahili iliibuka. 

KUIBUKA KWA RIWAYA YA KISWAHILI

Kuibuka kwa riwaya ya kiswahili kwa kiasi kikubwa kumechangiwa na wageni (wakaloni na wamishenari).  Katika kuibuka na makuzi yake riwaya ya kiswahili imepitia hatua nne (4) muhimu. Hatua hizi nne zimeibuka ndani ya utawala wa kijerumani pamoja na ule wa kiingereza ndani ya Afrika mashariki.

Kwanza, wageni (wakoloni na wamishenari) walikusanya nathari za wenjeji.

Pili, ikafuata hatua ya kutafsiri ngano za wenyeji katika lugha za kigeni. Kwa mfano, mwaka 1870 Edward Steere alianza kutafsiri hadithi kutoka Zanzibar katika lugha ya Kiingereza. Mwaka 1889 alichapisha kitabu kiitwacho Swahili Tales as Told by the Native of Zanzibar. Hiki ni kitabu cha muhimu kwa sababu kinatoa dira kuhusu historia ya mwanzo ya riwaya za Kiswahili. Mwaka 1907 Carl Vetten alichapisha kitabu kiitwacho Prosa and Poesie de Suaheli kwa lugha ya kijerumani.

Tatu, ilikuwa ni kutafsiri fasihi za kigeni kuwa ya Kiswahili. Kwa mfano, mwaka 1928 Edwin Brenn alitafsiri kitabu kiitwacho Alaza. Mifano mingine ni: Alfu Lela UlelaMashimo ya Mfalme SuleimaniHadithi za EsopoHadithi za Mjoma Remas na Hekaya za Abunuasi. Kazi hiyo ya kutafsiri ilipamba moto tangu mwaka 1930 wakati halmashauri ya Kiswahili ya Afrika mashariki ilipoanzishwa.

Nne, waafrika kuanza kutunga riwaya. Walitunga kutokana na kuhamasishwa na halmashauri hiyo ya Kiswahili. Mfano, mwaka 1934 James Mbotela alitunga riwaya ya Uhuru wa Watumwa. Riwaya hii ilisanifiwa na Halmashauri ya Kiswahili kwa sababu iliwaponda Waarabu na kuwakweza Waingereza ambao walikuwa katika Halmashauri ya Kiswahili.

Riwaya ya Uhuru wa Watumwa ni kielelezo kimojawapo cha riwaya za mwanzo za Kiswahili. Watunzi wengine wa kiafrika ni pamoja na Shaaban Robert na Abdallah S. Farsy (aliyetunga riwaya ya Kurwa na Doto: 1961).

Baadhi ya waandishi wa kiafrika baada ya uhuru walipanua wigo na kuandika juu ya mambo mengi zaidi. Mfano, zikatungwa riwaya za upelelezi. Faraji katalambula alitunga riwaya ya Simu ya Kifo. mohammed Said Abdallah alitunga riwaya nyingi za upelelezi mhusika wake mkuu aliitwa MSA. Mifano ya kazi zake ni:

o   Duniani Kuna watu

o   Kisima cha Giningi

o   Mzimu wa watu wa kale

o   Mwana wa yungi Hulewa

o   Siri ya sifuri

o   Kosa la Bwana MSA

Kisha, watunzi wakageukia kutunga juu ya siasa wakiongea juu ya masuala mbalimbali kama vile viongozi wanafiki, mikutano ya siasa. Mifano ya kazi hizi ni: Njozi iliyopotea na Gamba la Nyoka. Kwa ujumla, wanariwaya walikuwa wanaandika juu ya masuala ya jamii wakiwa na nia ya kukosoa, kuelimisha na kadhalika. Waandishi wamekuwa wakikomaa katika kuandika kwa kuzingatia maudhui na fani inayorandana na miktadha. Kabla ya uhuru waliandika kikasuku pasipo kuchambua. Kwa mfano, Mbotela alipowasifia waingereza katika Uhuru wa Watumwa. Pia uchoraji wa wahusika umekuwa ukikomaa kutoka kipindi kimoja hadi kingine.

WAKATI WA UKOLONI WA WAINGEREZA (Miaka ya 1919)

Kama ilivyokuwa wakati wa Wajerumani, Waingereza nao walikikuza Kiswahili na kazi za kifasihi kupitia elimu, dini, mashirika ya uchapishaji vitabu, kuendelezwa kwa hati ya Kirumi n.k. vitabu vingi vilitungwa katika kipindi hiki vikiwemo vya somo la Kiswahili sanifu na fasihi. Vitabu vingine vilitungwa ili kutoa maarifa mbalimbali kama vile jinsi ya kutunga mashairi.

Baadala ya kutumia hati za Kiarabu wakati huu zilitumika hati za Kiruni katika kuandika kazi za kifasihi, wakati huo sanaa ilikuwa ni ya watu wa Pwani tu, lakini kipindi hiki ilienea hadi ndani katika miji ya bara. Mfano Dodoma akina Mathias Mnyampala. Wakati huo ushairi na kazi zingine za kifasihi zilikuwa zikitungwa na watu mbalimbali tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo watunzi walikuwa ni Waislamu tu

.

Kwa upande wa ushairi…… Kipindi hiki mashairi yalikuwa yakihoji, yakipinga na kujiuliza kuhusu utawala wa wazungu. Pia yalikuwepo yale yaliyomsifu Malkia Elizabeth. Mashairi ya Saadan Kandoro ni mfano mzuri wa harakati za kudai uhuru; kama yale ya Ondoka Nchini MwetuWaafrika NjooniSiafu Wamekazana, Kwetu ni Kwao Kwanini? Mashairi haya yalikuwa ni ya kisiasa, pia yalikuwepo mengine yaliyotaka uhuru wa kiutamaduni na uhuru wa kiuchumi. Mfano mashairi ya S. Robert, Koja la Lugha na Pambo la Lugha.

Kanuni na taratibu za utunzi hazikuathiriwa sana wakati wa Waingereza, ingawa wapo baadhi ya wanazuoni wanaodai kuwa mashairi huru yalianza kipindi hiki cha utawala wa Waingereza.

Upande wa riwaya…. Wakati wa mwingereza utanzu wa riwaya ulishaanza kukomaana, kazi nyingi za kinathari zilishaandikwa.  Kipindi hiki ndicho kilikuwa kipindi cha kutamba kwa kazi za shaaban Robert. Riwaya ya Utubora Mkulima ilitungwa miaka hii (yasemekana ilitungwa mwaka 1946).

 Ikafuatiwa na riwaya ya Kufikirika 1947, Kusadikika 1951, Adili na Nduguze 1952 na Siku ya Watenzi Wote 1968. Karibu riwaya zote za Shaaban Robert ziliathiriwa sana na ngano na hekaya, hasa katika muundo wake na uchorajiwa wahusika (karibu wahusika wote wakuu ni bapa).

KUIBUKA KWA TAMTHILIA

Tamthilia za Kiswahili zilizoandikwa kwanza kabla ya kuigizwa jukwaani zimeanza kutokea miaka ya 1950. tamthilia za mwanzo zilikuwa ni za kidini. Kwa mfano, mwaka 1951 ilichapishwa tamthilia ya C. Frank iliyoitwa Imekwisha. Tamthilia nyingiza kidini ziliandikwa na kuigizwa tu shuleni na makanisani, lakini hazikuchapishwa vitabuni.

Tamthilia za mwanzo zisizokuwa za kidini zilianza kutungwa kati ya 1952 na 1956. shughuli za tamthilia wakati huo wa “Hali ya Hatari” nchini Kenya zilisimamiwa na Graham Hyslop, mwingereza aliyekuwa katika utumishi wa serikali ya kikoloni ya Kenya. Hyslop alianzisha kikundi cha maigizo kwa ajili ya askari mwaka 1944, na miaka ya 1950 alianza kutunga michezo ambayo iliigizwa na kikundi chake. Michezo yake ya mwanzo katika lugha ya Kiswahili ni Afadhali Mchawi (EALB 1957) na Mgeni Karibu (EALB 1957). michezo hiyo iliigizwa kati ya 1954 – 1956. Baadaye Hyslop alianza kuzunguka katika shule na vyuo mbalimbali nchini Kenya akifundisha muziki na uigizaji.

Miongoni mwa wanafunzi wa Hyslop waliokuwa wakisoma Alliance High School, Nairobi, ni Henry Kuria, Kimani Nyoike, Gerishon Ngugi na B.M. Kurutu. Tamthilia ya Kuria, Nampenda Lakini… (EALB 1957) iliigizwa kwa mara ya kwanza 1954. tamthilia ya Nyoike, Maisha ni Nini iliigizwa mwaka 1955. tamthilia ya Gerishon Ngugi, Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi (EALB 1961) iliigizwa mwaka 1956, na ya Kurutu, Atakiwa Polisi, mwaka 1957.

kwa jumla, hadi tunapata Uhuru, tamthilia zote za Kiswahili zilizochapishwa zilikuwa zimeandikwa na Wakenya. Watanzania hawakujitokeza katika uwanja huu hadi baada ya Uhuru.

Kipindi hiki pia kilikuwa ni kipindi cha kudai uhuru. Dhamira za kupigania uhuru ziliandikwa kupitia vitabu na magazeti ingawa kwa lugha ya kificho sana ili kukwepa udhibiti wa wakoloni. Ni kipindi hiki ambapo harakati za kudai uhuru ziliendelea kupamba moto, wananchi walizidi kupata mwamko wa kisiasa, kiutamaduni, mwamko wa Uafrika, kuanzishwa vita vya MAUMAU, kuanzishwa kwa chama cha TANU, waandishi waliakisi mawazo kutoka katika fukuto la kimapinduzi lililokuwepo katika jamii. Fasihi ilipata nguvu kwa kuwa kulikuwa na vitu vingi vya kutolea hisia, mfano redio, magazeti, vitabu n.k.

BAADA YA UHURU (Miaka ya 1961 hadi 1970)

Baada ya kupata uhuru toka kwa Waingereza watunzi wengi wa kazi za fasihi ya Kiswahili walisheherekea na kushangilia hilo katika redio, magazeti na katika vitabu.

Kwenye ushairi. Dhamira kuu ilikuwa ni masuala ya siasa. Mfano Saadan Kandoro katika Diwani ya Saadani katika shairi la Nyerere Pokea Hicho (Yaani Kiti cha Uwaziri Mkuu wa Tanganyika) uk. 145 na Tumshukuru Manani uk. 146 ni mfano wa mashairi yaliyotungwa kipindi hiki ya kiwa na uwelekeo wa kisiasa. Pia zipo baadhi ya Tenzi zilizotungwa kipindi hiki, mfano Utenzi wa Uhuru wa Tanganyika (1967) uliotungwa na Mwinyi Khatibu Muhamed Amiri, Utenzi wa Uhuru wa Kenya (1972) uliotungwa na Salum Kibao, Utenzi wa Jamhuri ya Tanzania (1968) uliotungwa na Ramadhani Mwaruka n.k.

Kwenye Tamthilia.  Baada ya Uhuru utunzi wa tamthilia ulipamba moto zaidi, hasa upande wa Tanzania. Mashindano ya utunzi yaliendeshwa na Youth Drama Association (Chama cha Drama cha Vijana) nchini Tanzania yaliwawezesha watunzi chipukizi kujitokeza, mmoja wao akiwa ni Ebrahim Hussein ambaye tamthilia yake ya kwanza, Wakati Ukuta (EAPH 1967) ilishinda tunzo katika mashindano hayo. Wakati huo pia ndipo walipoanza kutokea watunzi waliohitimu fani ya sanaa za maonesho katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baadhi yao ni E. Hussein mwenyewe, Penina Muhando (Mlama), N. Ngahyoma, G. Uhinga na E. Mbogo. Watunzi hao, hasa Hussein, Muhando na Mbogo, wametoka mchango wa pekee katika maendeleo ya tamthilia ya Kiswahili

Kimaudhui, tunaweza kuzigawa tamthilia za Kiswahili za 1960 – 2015 katika mikondo ifuatayo:

Migongano ya kitamaduni 

Dhamira hii inajitokeza katika umbo la mgongano wa utamaduni wa jadi wa Kiafrika na utamaduni wa Kizungu, au katika mgongano kati ya mjini na shamba (tamthilia za vichekesho). Suala hili limejadiliwa kwa kina zaidi katika baadhi ya tamthilia za Hussein (Wakati Ukuta na Kwenye Ukingo wa Thim), Muhando Hatia na Ngugi Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi… 

Matatizo ya Kijamii na Kinafsi (k.m. mapenzi, ndoa, ufukara, urithi n.k)

karibu tamthilia zote za mwanzo zilihusu kipengele hiki. Kwa mfano Nakupenda Lakini… na Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi, zilizungumzia matatizo ya mapenzi yanayokumbana na vikwazo vya kiuchumi au vinginevyo; na tamthilia za Hyslop zilihusu matatizo ya urithi, rushwa, fitina na tamaa. Tatizo la mimba limejitokeza katika Hatia. Katika Mke Mwenza tunakutana na tatizo la wivu katika muktadha wa tatizo pana zaidi la ndoa za mitara, ambalo ni la kijinsia. Tamthilia ya Semzaba ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe inalitazama suala la mapenzi katika muktadha wa utumishi wa umma, na kuonesha kuwa mapenzi huweza kuathri uwajibikaji kikazi. Katika Pambo (P. Muhando) suala la elimu ya kishule na dhima yake katika maendeleo ya jamii linamulikwa. Pambo mhusika mkuu, ni msomi wa chuo kikikuu ambaye anaoneshwa kuwa ana ‘Kichaa’ cha kusaka pesa na raha badala ya kujinyima ili kuitumikia jamii. Inabidi jamii nzima iingilie kati Kumrejesha katika njia inayofaa.

Dini.

Tamthilia zihusuzo dini zipo katika makundi mawili.

Kwanza, ni kundi la tamthilia za kanisani zenye kufundisha dini au kuadhimisha matukio ya kidini. Tamthilia hizi, ambazo ziliigwa moja kwa moja kutoka Ulaya, hatutazizungumzia hapa kwa vile hazihusishwi katika mijadala ya kifasihi.

Kundi la pili, ambalo ndilo linatuhusu hapa, ni tamthilia zinazochambua na kuhakiki asasi na mafundisho ya dini kifasihi.

Dini, kama asasi ya kijamii, imejitokeza katika tamthilia kadha, hususan Topan Aliyeonja Pepo, Muba Maalim, Mulokozi Mukwava wa Uhehe na Semzaba Tendehogo. Kwa mfano katika Tendehogo, dini (Uislamu) inaoneshwa kama nyenzo ya kutengua utu wa mtu wa mtumwa (Mwafrika) na kumdhibiti ili kumtawala.

Kwa upande wa dini ya asili haijadiliwi sana katika tamthilia, na inapojadiliwa ama hubezwa, ama huoneshwa kuwa ina nguvu na uwezo wa kuwaunganisha na kuwakomboa watu (mfano katika Kinjekitile na Kija). Mara chache sana dini hiyo huoneshwa kuwa ni bora kuliko dini za kigeni (kwa mfano katika H. Muhanika Njia Panda)

Matatizo ya kijinsia

Matatizo ya kijinsia, aghalabu kwa mtazamo wa kifeministi, yanasawiriwa katika baadhi ya tamthilia. Watunzi wanajaribu kuonesha hali duni ya mwanamke katika jamii ya sasa, kutafuta sababu za hali hiyo, na kupendekeza ufumbuzi. Baadhi ya tamthilia zinazogusia suala hili ni Muhando Nguzo Mama, Mulokozi Mukwava wa Uhehe, Mazrui Kilio cha Haki, Hussein Kwenye Ukingo wa Thim na Mbogo Tone la Mwisho.

Ukombozi wa taifa

Hili ni suala lililojitokeza katika tamthilia nyingi. Baadhi ya watunzi wanaliangalia suala la ukombozi katika muktadha wa ukoloni; wanasawiri harakati za upinzani dhidi ya ukoloni, au ukombozi wa taifa. Mifano ni Nkera Mkwawa Mahinya na Johari Ndogo, Hussein Kinjeketile, Mulokozi Mukwava wa Uhehe, na Mbogo Tone la Mwisho.

Kwa ujumla, tamthilia hizi zinauona ukombozi kama jambo la hakika ambalo haliepukiki, na haziishii katika ukombozi wa kisiasa tu, bali zinaangalia pia ukombozi wa kiuchumi na kitamaduni. Kuna uwezekano pia kuwa tamthilia ya kimafumbo ya Tambueni Haki Zetu (P. Muhando) inasawiri dhana ya ukombozi wa taifa na utetezi wa haki (ukiongozwa na Mundewa) dhidi ya kani za kitabaka na kijadi zinazoukinza ukombozi huo.

Ujenzi wa jamii mpya

Hatua inayofuata baada ya ukombozi wa kitaifa ni ujenzi wa jamii mpya. Hili ni suala ambalo linawashughulisha watunzi wengi. Baadhi, kama N. Ngahyoma Kijiji Chetu na M, Rutashobya Nuru Mpya, wanalitazama kimageuzi na kupendekeza marekebisho katika mfumo uliopo, baadhi wanaonesha tu kuwa mambo siyo sawa, kwamba ukombozi haujakamilika kwa vile mkoloni kabakia katika sura tofauti (mfano Mbogo Giza Limeingia) na Hussein Mashetani, na baadhi wanalitazama suala hili kitabaka na kuhimiza mapambano ya wafanyakazi dhidi ya mabepari na ubepari (Kahigi na Ngemera Mwanzo wa Tufani na Mazrui Kilio cha Haki.

Tamthilia za mwelekeo wa Thieta ya Umma ambazo nyingi hazijachapishwa zinalitazama suala hili kwa mkabala wa umma, kwa kuzingatia matatizo yao na mahitaji yao, siyo ya kitaifa tu, bali hata ya pale walipo. Udikteta na ukandamizaji uliokithiri miaka ya ‘Uhuru’ katika nchi nyingi za Afrika unashambuliwa kisanaa katika tamthilia kadha. Mfano mzuri ni tamthilia ya Kaptura la Marx (E. Kezilahabi) inayoshutumu ukiritimba na matumizi mabaya ya madarak katika mfumo wa Ujamaa aliouanzisha Raisi J.K. Nyerere nchini Tanzania. Mageuzi ya soko huria (utandawazi wa kibepari) yaliyowageuza wanasiasa kuwa wafanyabiashara na baadhi kuwa mafisadi yamesawiriwa katika tamthilia kadha pamoja na filamu za Kiswahili. Mfano ni tamthilia ya F.P. Nyoni Mabepari wa Bongo.

Falsafa ya Maisha. Tamthilia zenye kuzungumzia maisha kifalsafa, kama tunavyoona katika Utenzi wa Inkishafi au katika riwaya za Kezilahabi bado hazijajitokza. Hata hivyo, falsafa hugusiwa hapa na pale katika baadhi ya tamthilia, hasa zile za Ebrahim Hussein. Kwa mfano, Kinjeketile haizungumzii suala la vita vya ukombozi tu, bali pia inatupa tatizo la kifalsafa kuhusu nabii au mkombozi anayeleta jambo ambalo linakua na kumzidi uwezo, na hivyo kumwangamiza yeye na wafuasi wake. Kiistiara hapa tunaona usawiri wa nabii mkombozi (pengine J.K. Nyerere au Kwame Nkrumah) anayeshindwa kufikia malengo yake. Kwenye Ukingo wa Thim, pamoja na mambo mengine, inazungumzia falsafa ihusuyo dhana za majaaliwa, bahati na malipo katika mazingira ya utamaduni wa Kiluo. Kija ni tamthilia tata inayoibua falsafa ya Uafrika katika muktadha wa utandawazi.

Uchawi, Uganga na Itikadi za Jadi

Masuala haya yanajitokeza katika tamthilia kadha, mathalan Muhanika Njia Panda, Mbogo Ngoma ya Ngw’anamalundi, Hussein Kinjeketile, Kitsao Mafarakano na Kitogo Kija. Kwa jumla uganga na itikadi za jadi katika tamthilia hizi zinasawiriwa kama amali muhimu za jamii zifaazo kutumiwa kutanzulia baadhi ya matatizo ya kimaisha. Katika baadhi ya tamthilia za Thieta ya Umma uchawi na itikadi za ushirikina zinaonyeshwa kama tatizo sugu lenye kukwamisha maendeleo.

KUIBUKA KWA TAMTHILIA ZA KIMAJARIBIO

Watunzi wengi wa tamthilia ya Kiswahili wanaiga mbinu na kanuni za tamthilia ya Ulaya, hasa ya Ki – Aristotle. Hivyo kisanaa tamthilia zao hazitofautiani na tamthilia za Kiingereza, hasa za Kihalisia. Tofauti yao na watunzi wa Ulaya iko katika maudhui na lugha iliyotumika tu. Watunzi wachache, kuanzia miaka ya 1970, hawakuridhika na ukopaji huu; walihisi kuwa palihitajika tamthilia ya Kiafrika yenye kuchota mbinu zake kutokana na sanaa za jadi za Kiafrika. Hiyo watunzi hao walianzisha maigizo ya majaribio.

Miongoni mwa wana – majaribio hao wa mwanzo ni Ebrahim Hussein. Mtunzi huyu alijaribu kutumia mbinu za utambaji wa ngano katika maigizo yake ya Ngao ya Jadi na Jogoo Kijijini. Mpaka sasa wataalamu hawajakubalia kama tungo hizo mbili ziitwe tamthilia au tendi. Penina Muhando pia, katika tamthilia zake za Lia Ubani na Nguzo Mama, vilevile alijaribu kutumia mbinu ya utambaji wa ngano.

Majaribio ya kuifanya tamthilia ioane na utamaduni na mazingira ya Kiafrika bado yanaendelea, na ni vigumu kwa wakati huu kubashiri hatima yake itakuwaje. Yumkini kutokana na majaribio kama haya tutapata aina ya tamthilia tunayoweza kuuita ya Kiafrika au ya Kiswahili hasa.

KUIBUKA KWA THIETA YA UMMA (POPULAR THEATRE)

Williady 2013, anaeleza maana ya thieta ya umma. Anasema “Thieta ya Umma ni aina ya sanaa za maonyesho au maigizo yaliyofanywa moja kwa moja jukwaani na wanajamii wa eneo fulani wakishirikiana na wataalamu wa sanaa kwa lengo la kuyaibua, kuyaeleza na kuyatolea suluhisho matatizo ya watu wa eneo husika.”

Muhando 1991,katika kitabu chake kiitwacho Culture and development: The Popular Theatre Approach in Africa, anaielezea vizuri dhana ya “Thieta ya Umma” au sanaa kwa maendeleo ya jamii. Mhando anaitaja miaka ya 1970 kama nyakati za mwanzo katika vuguvugu la Thieta ya Umma kwa nchi nyingi za Afrika. Majaribio kadhaa yalifanyika yaliyokuwa na lengo la kuitambulisha dhana hii ya Thieta ya Umma kwa wanajamii. Kwa mfano nchini Kenya dhana ya Thieta ya Umma ilijulikama sana kwa jina la “Thieta ya Ukombozi”. Maigizo mengi ya namna hii yalizungumzia sana harakati za ukombozi wa kifikra, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa kwa mwafrika dhidi ya utawala wa kikoloni.

Funzo kubwa tunalolipata kutokana na vuguvugu la “Thieta ya Umma” ni kwamba watu wenyewe katika utamaduni wao wanao uwezo na mbinu za kubuni drama zao wenyewe zenye kulingana na mahitaji na matakwa ya kiujumi na kimaisha. Hivyo si lazima watunzi wetu wafuate kanuni za Ki –Ulaya au Ki – Aristotle za utunzi wa tamthilia.

KUIBUKA KWA FILAMU YA KISWAHILI

Mchepuo wa filamu katika drama ya Kiswahili ulianza tangu miaka ya 1930 au kabla, wakati wakoloni walipoanza kutengeneza na kuonesha filamu za Kiswahili, aghalabu zenye mafunzo kuhusu masuala ya maendeleo kwa mfano afya, elimu, historia, sayansi kimu, na kadhalika. Utaratibu huo uliendelea hadi miaka ya 1950 huku ukiratibiwa na Idara za Ustawi wa Jamii. Nchini Tanzania Rashid Mfaume Kawawa, ambaye baadaye alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, alikuwa mwigizaji katika filamu hizo, hususani filamu mashuhuri za mwanzoni mwa miaka ya 1950 za Muhogo MchunguMeli Inakwenda na Chalo Amerudi. Wakati wa Ujamaa Kampuni ya Filamu Tanzania (TFC) ilitengeneza filamu kadha, baadhi zikashadidia sera  ya nchi ya Ujamaa.

Tasnia ya filamu za Kiswahili imekua zaidi miaka ya karibuni baada ya kuenea kwa televisheni, DVD na Video; maigizo mengi ya tangu mwaka 1990 yanatumia vifaa hivyo. Katika miaka ya leo filamu zimechukua nafasi ya tamthilia na kuwa ndiyo sanaa ya Umma ya maigizo kwa Kiswahili.

Tasnia ya filamu ya “Bongo Movies” inasemekana kuwa ya pili kwa ukubwa katika Afrika ikitanguliwa na filamu za Kinaijeria.

RIWAYA BAADA YA UHURU

 

Baada ya uhuru riwaya ya Kiswahili imepiga hatua kubwa sana. Umekuwepo mwondoko mpya katika maeneo kama vile ya:

 •  Idadi ya kazi za riwaya
 •  ubora wa riwaya zenyewe
 •  Matumizi ya Lugha
 •  mwelekeo wa maudhui
 •  mabadilio ya motifu n.k.

Maendeleo haya ya ubunilizi wa riwaya, pamoja na sababu nyingine, yamechochewa sana na ongezeko la hali ya usomi na wasomaji katika jamii ya waswahili. Mchango wa ongezeko hilo la hali ya usomi na wasomi katika jamii ya waswahili linaweza kutazamwa kupitia maeneo kama vile; Utungaji, Usomi na utafiti kuhusu masuala ya riwaya.

AINA ZA RIWAYA  KWA KUZINGATIA MAUDHUI

Baada ya uhuru kulikuwa na ongezeko kubwa sana la kazi za riwaya, hivyo pia tunaweza kuziweka riwaya kwenye makundi kwa kutumia kigezo cha kimaudhui.

Riwaya za kihistoria

Riwaya za mwegamo huu huakisi matukio ya kihistoria. Wahusika wake husawiri kwa makini ili kutia kumbukizi ya wakati uliopita. Riwaya hizi si kitabu cha kihistoria, bali ni huakisi tu matukio ya kihistoria. Huwa na urazini wa historia ya jamii. Mifano ya riwaya za mtazamo huu ni: Miradi bubu ya Wazalendo (G. Ruhumbika), Kifo cha Ugenini (Olaf Msewe), Kasri ya Mwinyi Fuadi (Shaffi Adam Shaffi), Zawadi ya UshindiKwa heri Islamagazi (Mapalala) na Moto wa Ngoma ya Mianzi (Mulokozi).

Riwaya za Kimaadili (Riwaya za kidini)

Maranyingi hudokeza mapito ya mhusika mkuu toka utoto wake. Hujaribu kueneza maadili kwa jamii. Wahusika huwekwa ili wawe chachu ya maadili kwa jamii na kupinga uovu. Kwa mfano, Adili na nduguze na Kusadikika vya Shaaban Robert. Aghalabu, hujikita katika masuala ya dini. Misingi yake hukitwa katika vitu au mambo matatu ambayo ni:

Pathema (yaani makosa au kosa),

Mathema (yaani mafunzo au funzo) na

Catharsis (yaani utakaso).

Riwaya za Kiamapinduzi

Huwazindua wasomaji ili wapambane na udhalimu na kubomoa mifumo ya ukandamizaji iliyopo katika jamii. Hudodosa dhana za mapambano, mikinzano na matabaka, riwaya hizi maranyingi ni za kihalisia. Mifano ya kazi za kundi hili ni: Kabwela (Abdulhaman Jumbe Safari), Ubeberu Utashindwa (Kiimbika), Kuli na Haini (Shafi Adam Shafi), Kusadikika (Shaaban Robert), Utengano (S.A. Mohamed na Dunia Mti Mkavu (S.A. Mohamed).

Riwaya za Kisosholojia

Riwaya zake huchunguza na kuibua maswali ya kijamii na kupiga darubini kali katika jamii. Hukazia vipengele vihusuvyo maisha ya kila siku katika jamii (desturi, mila na mabadiliko ya jamii). Huwa na uhalisi katika vipengele vyake. Maranyingi huwa na maudhui yenye kuhuwisha. Hugusia migongano ya kijamii kama vile ukale na usasa, umji na uvijiji, familia na ndoa kwa ujumla. Kwa mfano: Kurwa na Doto (M. Farsi), Dunia Uwanja wa FujoMzimu wa Babu ana Radhi (F. Nkwera), Bwana Mnyombekera na Bibi Bugonoka na Harusi (A.J. Safari).

Riwaya za Kisaikolojia

Hujaribu kufichua hali ya kisaikolojia katika jamii kwa kuwatumia baadhi ya wahusika. Maudhui yake huhusu vita vya mazoea dhidi ya uhalisi. Hujadili mikinzano aipatayo mtu ki―nafsi, ki―jamii na ki―uana. Hukitwa katika kuwako kwa (Kosa/udhaifu/jambo hasi/ utata na misawajiko kwa mhusika kuu). Mfano: Tata  za Asumini (S. Ahmed) Kichwamaji (Kezlahabi).

Riwaya za Kifalsafa

Hujadili mambo yenye urazini fiche. Mtunzi hudadisi mambo mbalimbali kwa jicho la kifalsafa (udodosi wa kina). Aghalabu, hutumia lugha tata na ngumu. Miongoni mwa mambo hayo yanayododoswa ni kuishi, ukweli, maisha, utu, kifo, kuwa na kutokuwapo kwa viumbe, kuwepo kwa Mungu n.k. baadhi ya maswali ya kifalsafa yaulizwayo ni kama vile:

 • Maisha ni nini?
 • Kuwapo na kutokuwapo kwa dunia ni kwatokeaje?
 • Kuishi ni nini?
 • Utu ni nini?
 • Kwa nini watu au vitu vipo hivyo vilivyo?
 • Kwa nini mambo yapo hivyo yalivyo?
 • Mifano ya riwaya za kifalsafa ni riwaya kadhaa za Kezilahabi. Nazo ni: MzingileNagonaRosa MistikaKichwamaji. Riwaya za kifalsafa zilizoandikwa na waandishi wengine ni pamoja na: Babu AlipofufukaUmleavyoWalenisiMafuta na Bin―Adamu.

Riwaya Pendwa

Husisimua na huwa na mvuto wa pekee kwa wasomaji. Aghalabu, fani hujichomoza zaidi kuliko maudhui. Pia humfikirisha sana msomaji. Rejea sifa mbalimbali zilizojadiliwa katika tapo la riwaya pendwa pamoja na mifano yake.

Riwaya za kitawasifu (riwaya sira)

Hizi ni tofauti na tawasifu. Riwaya zenye mwegamo wa kitawasifu zimetungwa kama vile tawasifu. Tawasifu hueleza maisha ya mtunzi. Riwaya ya kitawasifu hueleza maisha ya mhusika aliyeteuliwa na mtunzi. Huweza kuegemea u―chanya tu na kuacha kudokeza mambo hasi. Hulenga kutoa kumbukizi ili kuwahimiza wengine kuwa kama mhusika wa tawasifu. Katika riwaya ya kitawasifu, sauti ya mtunzi husikika kupitia maisha ya mhusika. Mfano mzuri wa tawasifu ni: Maisha yangu na baada ya Miaka Hamsini na Tippu Tip.

Riwaya za kiwasifu

Hizi hutungwa kama wasifu. Mtunzi hueleza maisha ya wahusika fulani. Katika wasifu mwandishi hueleza juu ya mtu aliyewahi kuishi au anayeishi. Wakati katika riwaya ya kiwasifu mtunzu hueleza maisha ya kubuni ya mtu ambaye labda hajawahi kuishi. Mifano ya riwaya ya kiwasifu ni: Shida (Ndyanoa Balisdya), Wasifu wa Siti Binti Saad (S. Robert), Salum Addallah (J. Mkabarab), Maisha ya Seti BenjaminiMtemi Mirambo na Mkwawa na Kabila Lake.

KIPINDI CHA AZIMIO LA ARUSHA

Azimio la Arusha lilileta sura na dhamira mpya katika fasihi ya Kiswahili, watunzi wengi waliathiriwa na itikadi hiyo ya siasa ya ujamaa na kujitegemea. Baadhi ya watunzi walitumiwa katika kueneza na kufundisha siasa ya ujamaa na kujitegemea akiwemo Mathias Mnyampala katika Ngonjera za Ukuta namba 1 na 2. Mashairi ya Azimio la Arusha (1971) ambacho kilihaririwa na G. Kamenju na F. Topan. Baada ya kutangazwa azimio hilo kazi za fasihi zilijitokeza katika sura tatu:

 • Fasihi ya Kindoto au Kinjozi
 • Fasihi ya kikasuku na

Fasihi ya kitabiri

Fasihi ya Kinjozi

Kazi za fasihi za Kinjozi ni zile zilizosawiri matamanio ya Wananchi baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha kwamba wangekuwa na jamii mpya ambayo inajali haki na usawa wa binadamu. Jamii inayoleta usawa na uhuru katika elimu, jamii inayopinga unyonyaji, jamii inayopiga vita uzururaji na vijana kukimbilia mjini, jamii iliyoamini kwamba vijiji vya ujamaa ndio suluhisho la matatizo yote ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Kazi kama riwaya ya Shida N.Balisidya, Ndoto ya Ndalia J. Ngoma, Njozi za Usiku W. Seme na J. Mhina. Hii ni pamoja na Tamthilia za Hatia, Dunia IliyofarakanaMwanzo wa Tufani, Kijiji Chetu na Bwana Mkubwa.

 

Fasihi ya Kikasuku

Kazi za fasihi za Kikasuku ni zile zilizoandikwa kwa kurudia yale yaliyosemwa na wanasiasa. Mwandishi anakuwa kama kipaza sauti cha mwanasiasa, mwandishi hukosa muda wa kutulia na kuchambua kwa kina kile kilichosemwa na wanasiasa. Kwa mfano katika Ngonjera za Ukuta namba 1 na 2. Mathias Mnyampala anakariri yote yaliyokuwa yakisemwa katika kulitangaza Azimio la Arusha.

Fasihi ya Kitabiri

Kazi za fasihi za Kitabiri huwa katika namna ya kutabiri mambo mazuri ya wakati ujao, lakini hushindwa kuelezea jitihada zipi zifanyike ili kufikia mafanikio hayo.

KIPINDI CHA MWAKA 1970 HADI 1980

Hiki ni kipindi kinacho husisha miaka kumi baada ya Azimio la Arusha, kipindi hiki nacho kilikumbwa na mambo mengi; kulikuwa na kuvamiwa na Dikteta Idd Amini. Kwa mfano Utenzi wa Vita vya Kagera na Anguko la Idd Amini Dada (1981) uliotungwa na Henry Mhanika. Katika kipindi hichi pia kulikuwa na ukosoaji wa mambo yanayojitokeza katika utawala. Fasihi ilikuwa kwa namna ya kiuhakiki, mambo yalichunguzwa kwa undani zaidi, hali ya kusifia sifia ilikoma. Kwa mfano riwaya ya Rosa Mistika (E. Kezilahabi) iliihakiki jamii na kuwakosoa viongozi, Njozi iliyopotea (C. Mng’ong’o), Njota ya Huzuni (Liwenga), Gamba la Nyoka (E. Kezilahabi), kazi hizi zilionyesha matamanio na matarajio ya wananchi kushindikana.

Baadaye ilijitokeza riwaya ya kimapinduzi ambayo iliwahimiza wananchi kufanya mapinduzi ili kuondokana na hali mbaya zilizopo. Ijapokuwa riwaya ya kimapinduzi ilisisitiza kupindua, ilikuwa na ukasuku ndani yake. Kwa mfano Ubeberu Utashindwa, Uzalendo, Kuli na Dunia Mti Mkavu. Palikuwepo na kitabu cha ushairi kilichoitwa Miaka 10 baada ya Azimio la Arusha (1977) kilitolewa na Ukuta na Mhariri alikuwa Abdullatif Abdalla.

Baada ya miaka kumi ya Azimio la Arusha tamthilia nayo ilianza kugeuza mwelekeo wake.  Badala ya kuusifu ujamaa kama ni ukombozi na ujenzi wa jamii mpya tamthilia ikaanza kukosoa wanasiasa. Kati ya tamthilia za aina hii ni Arusi, Nuru Mpya, Lina Ubani, Ayubu, Harakati za Ukombozi na Mkokoteni.  Nyingi kati ya tamthilia hizi pia zilijitahidi kuondoka kwenye muundo wa uandikaji wa tamthiliya kama ulivyopokelewa toka kwa wakoloni.

Tukumbuke kipindi hiki hali ya uchumi haikuwa nzuri, kulikuwa na mambo ya ulanguzi, hivyo magazeti, vitabu hata wanafasihi waliyaandika hayo. Hata hivyo waandishi makasuku waliosifia viongozi waliendelea kuwapo. Wafuatao ni waandishi walioandika kazi zao katika mkondo wa kiuhakiki:

Kwa upande wa ushairi kulikuwa na; Euphrase Kezilahabi katika Kichoni na Karibu ndani (1988), M. Mulokozi na K. Kahigi katika Malenga wa Bara (1976), Mohamed Seif Khatibu katika Fungate ya Uhuru (1988) na Z. Mochiwa katika Mvumilivu Hula Mbovu (1988). Washairi hawa wanawahimiza wananchi juu ya mambo fulani fulani ya kufanya na wametoa mapendekezo yao. Wanataka ujenzi wa jamii mpya, yaani pawepo na mabadiliko ya kiuchumi, kiutamaduni, kuwepo na haki, viongozi kujirekebisha, uwepo wa usawa na utu na kuwepo na umoja. Kwa mfano katika Karibu Ndani Kezilahabi katika shairi la Mkesha anaeleza uovu wa viongozi, anawatanabaisha wananchi kuwa wanakesha wakati wengine wanakula.

Pia katika shairi la Sisi kwa Sisi na la Hatumwoni kwamba kiongozi yupo tu kama kivuli hakuna anachokifanya. Katika Fungate ya uhuru kuna Mashairi kama vile Haki, Tumesalitiwa, Unganeni na Ningekuwa na Sauti.

Watunzi walionekana kana kwamba wanadai uhuru tena kwa mara nyingine, hapa tunaweza kusema ni sawa na kunywea chai ileile katika kikombe kipya. Dhamira ya siasa inaonekana kupewa nafasi kubwa katika kujenga dhamira za watunzi.

Katika miaka ya 1980 ulijirudia kwa nguvu mkondo wa riwaya pendwa, ambao ulijitokeza miaka ya 1960. Sababu za riwaya pendwa kuibuka kwa nguvu katika kipindi hiki ni pamoja na Masuala ya vita, matatizo ya kiuchumi na uhuru katika uchapishaji wa vitabu. Riwaya za M.S. Abdulla  ni Mzimu ya Watu wa Kale (1960), Kisima cha Giningi(1968), Duniani kuna Watu(1973),  Siri ya Sifuri (1974), Mke mmoja, Waume watatu (1975), Mwana wa Yungi hulewa (1976) na Kosa la Bwana Msa (1984).

Naye F. H. H Katalambulla ameandika Simu ya Kifo. (1965), Pendo pevu (1976) Pilipili (1977) na Unono (1978).

Musiba Aristablus Elvis akaandika Kufa na Kupona (1974), Kikosi cha Kisasi (1979), (1980), Njama (1981) na Hofu (1991).

Dhamira zilizoushughulisha mkondo huu ni pamoja na mapenzi, upelelezi, ujambazi na ujasusi.

FASIHI KIPINDI CHA MFUMO WA VYAMA VINGI

Mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania ulianza rasmi Julai mosi 1992. Uanzishwaji wa mfumo huo ulitokana na mabadiliko ya kiulimwengu ya kisiasa, kufuatia kuanguka kwa dola la Kisosholisti lililoongozwa na Urusi ambao ndio walikuwa na siasa za Usosholisti (Ujamaa).

Kuanguka kwa dola hizi kulifanya jumuiya za Ulaya mashariki kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Mabadiliko haya ya Ulaya yaliungwa mkono na nguvu za Soko Huria ambapo wananchi walikuwa na uwezo wa kuuza na kununua badala ya uchumi kuwa hodhi na serikali.

Mfumo huu unampa uhuru mtu yeyote yule kujiunga na chama chochote cha kisiasa, hali kadhalika kwa kuzingatia kanuni na sheria, mtu yeyote au kikundi cha watu wana haki ya kuanzisha chama cha siasa.

Madhumuni ya uanzishwaji wa mfumo huo ni kuimarisha demokrasia na kuwafanya watu waishi maisha bora.

MAFANIKIO YANAYOTOKANA NA MFUMO WA VYAMA VINGI 

 • Uhuru wa kutoa kero na kukosoa serikali.
 • Kufanya bunge kuwa chombo cha kuielekeza serikali badala ya bunge kuelekezwa na chama.
 •  Serikali kukubali kukosolewa na kufanya marekebisho ili kukidhi matakwa ya wananchi.
 • Chama tawala kuwa tayari kukosolewa na kujikosoa ili kiweze kuendelea kubaki madarakani.

MATATIZO YATOKANAYO NA MFUMO HUU

 • Migogoro ndani ya vyama. Migogoro hii husababishwa na harakati za kugombea uongozi na ruzuku.
 •  Migogoro ya chama na chama. Hii husababishwa na kutoridhika na utekelezaji wa sera fulani au kupinga matokeo na kukosekana kwa uaminifu.

Kutokana na mfumo huo, watunzi nao waliakisi hali hiyo katika kazi zao ingawa si kwa kiasi kikubwa. Mfano T. mvungi katika “Mashairi ya Chekacheka”, shairi la “Taifa wamelizika” uk. 2 beti 3 za mwisho. Anasisitiza umuhimu wa vyama vingi.

UHURU WA KUJIELEZA NA KUKUA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kukua kwa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza kumesaidia kuzuka na kuenea kwa kazi nyingi za kifasihi ambazo zimekuwa na mchanganyiko wa dhamira kutokana na mfumo huu. Kazi hizi za kifasihi mbali na kuburudisha, vilevile hubeba dhamira nzito zenye lengo la kubadili mwenendo wa jamii husika. Mfano kipindi cha “Twende na wakati” kilichokuwa kinarusha mubashara redio RTD (Redio Tanzania Dar es Salaam), “Orijino Komedy” kilichokuwa kinarushwa TBC 1 na “Futuhi” kinachorushwa Star TV.

Kukuwa kwa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza pia hujitokeza kama dhamira mojawapo katika kipindi cha vyama vingi. Suala hili kwa kiasi kikubwa linajitokeza katika Riwaya ya “Makuadi wa Soko Huria” ya Chachage. Kupitia riwaya hii tunabaini kwamba, pamoja na kuanzishwa kwa vyombo vingi vya habari lakini uhuru wa kujieleza wa waandishi wa habari na wanafasihi kwa ujumla bado ni mdogo.

FASIHI YA KISWAHILI KIPINDI CHA UTANDAWAZI

Utandawazi ni mchakato wa kuunganisha uchumi, siasa na uhusiano wa kitamaduni wa mataifa mbalimbali duniani

.

Utandawazi unaifanya dunia kuwa kama kijiji kimoja kisichokuwa na mipaka. Mahusiano hayo ya jamii hupaliliwa na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia hasa kupitia sekta ya mawasiliano.

Utandawazi unasisitiza uondoaji wa vikwazo vya biashara na kuifanya dunia kuwa soko moja. Kwa hiyo unahimiza Soko Huria, Demokrasia, Utawala Bora, Usawa wa Kijinsia, Haki za Binadamu na Utunzaji wa Mazingira miongoni mwa jamii husika.

ATHARI ZAKE KWA NCHI MASKINI (ZINAZOENDELEA)

 

Athari zake nipamoja na kuongezeka kwa hali ya umaskini, uchache wa vitegauchumi kwa wawekezaji,

kuendelea kukabiliwa na madeni, hakuna ufanisi katika kilimo ambacho ndicho uti wa mgongo kwa kila nchi, uhaba wa chakula na kuagiza kutoka nje, pamoja na maendeleo yote ya sayansi na teknolojia rasilimali za nchi zinazidi kupungua thamani kutokana na tabia ya unyonyaji inayofanywa na nchi tajiri kwa nchi masikini, kuibuka kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yasababishwayo na uroho wa madaraka na tamaa ya kupata mali za haraka haraka na kiwango kikubwa cha ujinga wa kutojua kusoma na kuandika.

KAZI ZA FASIHI ANDISHI KIPINDI HIKI

Kipindi tunachoishi sasa ni kipindi cha utandawazi wenye kushabihiana na kiwango kikubwa cha matumizi ya Sayansi na Teknolojia.

Kipindi hiki kama ilivyo ada, kazi za kifasihi hazipo nyuma katika kujadili masuala mbalimbali. Kazi nyingi za kifasihi zinagawanyika katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni lile linaloungamkono utandawazi na teknolojia.

Kundi la pili ni lile linalopinga utandawazi na teknolojia ya hali ya juu kwa kuhofia kuporomoka kwa maadili yetu ya Kiafrika.

Vilevile kazi nyingi za kifasihi zinabeba dhamira zinazoshabihiana sana zikiongozwa na;

 •  Mapenzi
 •  Uongozi mbaya
 •  Usaliti
 •  Siasa
 •  Mila na desturi
 •  Ujenzi wa jamii mpya
 •  Rushwa
 •  Matumizi mabaya ya vyombo vya dola (jeshi)
 •  Matabaka

Ebu tuchunguze dhamira hizi ndani ya baadhi ya kazi za kifasihi zenye ladha ya utandawazi.

Makuadi wa Soko Huria 

Hii ni riwaya iliyoandikwa na Chachage. Inatoa taswira ya mapambano dhidi ya ukoloni na baadaye dhidi ya baadhi ya watu walioteka nyara uhuru wa wengi na kushirikiana na wageni kupora rasilimali ya nchi kwa kisingizio cha sokohuria.

Riwaya hii pia inaweka bayana uozo na udhalimu uliofichwa katika mfumo wa sokohuria, kama vile: Tamaa ya pesa, ubinafsi na ukandamizaji, rushwa na utapeli.

Hata hivyo kwa upande mwingine, riwaya hii inaleta matumaini kwa kuwa inaonesha watu wasivyokubali kukandamizwa na wasivyokata tama katika kujitafutia haki zao.

Mwandishi anafikisha ujumbe kupitia vipengele mbalimbali vya kifasihi kikiwemo cha wahusika.

Wahusika hao ni kama vile:

Japhet Lupacho

 • Kuadi na msaliti aliyeacha uzalendo na kukubali kuvaa joho la ubaraka na ubarakala wa wawekezaji.

Mbunge Luhaba

 • Nikiwakilishi cha viongozi wa juu wanaowakandamiza wananchi.

Binti Wenga

 • Anatetea haki za nchi hasa kupinga tabia ya ubinasfi kwa viongozi.

Miraji na Mrisho

 • Wazee wa rufiji wenyekupinga unyonyaji na kutetea haki za wanyonge.

Wahusika wengine ni pamoja na Janga Mjuba, Fidelis Mumi, Msakapanofu, Salama, Sifuni na Oscar Mayowe

Msomi Aliyebinafsishwa

Hii ni riwaya iliyoandikwa na Nyambari Nyangwine mwaka 2012. Riwaya hii inazungumzia matatatizo mbalimbali yanayoikumba jamii kutokana na suala la utandawazi. Kikubwa ni ubinafsishaji na uwekezaji.

Wahusika

 • Mama Msagane
 • Entakana
 • Nyagichuro

Mabepari wa Bongo

Hii ni tamthilia iliyoandikwa na Frowin Paul Nyoni mwaka 2007. Nayo inazungumzia matatizo mbalimbali yaletwayo na wachache hasa waliopewa dhamana ya uongozi. Suala la uwekezaji nalo limejitokeza kwa kiasi kikubwa na athari zake pia zimeainishwa.

Wahusika

 • Mc Kilevi
 • Mke 1, 2, 3, 4
 • Mtoto 1, 2
 • Wawekezaji
 • Bibi Mtamba hadithi n.k

Wasakatonge

Hii ni diwani iliyoandikwa na Muhammed Seif Khatib mwaka 2003. Inabainisha uozo ndani ya jamii na harufu ya uozo huo inayoleta madhara makubwa kwa wanyonge. Ni sauti inayowatetea wavujajasho ambao hudharauliwa na kuonewa. Na chanzo cha uozo wote huo ni huyuhuyu anayeitwa utandawazi

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!