KATIKA KAMUSI LEO ‘Wanahabari wanavyobananga lugha’

By , in Kamusi on .

No photo description available.

Na. Majid Mswahili

Karibu katika KAMUSI leo.

KAMUSINI tunaangazia namna baadhi ya Wanahabari wanavyobananga lugha ya Kiswahili. Kwanza ifahamike dhahiri kuwa lengo la makala haya ni kuchagiza matumizi ya Kiswahili sanifu ikiwa ni pamoja na kusahihisha makosa ya matumizi ya Lugha na hasa yanayofanywa na Wanahabari wa vyombo vyote.

Kwa nini kwa wanahabari ? Ni kwa sababu vyombo vya habari vina nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya jamii. Kwa hiyo, vinaweza kuwa mwalimu mzuri au mbaya kwa jamii ndani ya muda mfupi.

Kwa hiyo, makala ya Kamusi hayana chuki na chombo chochote chenye kutumia Kiswahili. Hata hivyo, wapo Wanahabari kwa makusudi au kwa ujinga wanafanya makosa lukuki wanapotekeleza majukumu yao.

Inashangaza kuona namna Watangazi/ Waandishi wa vyombo vya Idhaa za Kiswahili walivyo weledi wa Kiingereza wakati Kiswahili ndiyo lugha ya kupashia habari hawana ujuzi nacho au wanakibeza tu kwa makusudi. Hivyo wanatumikia Kiswahili kilichochapwaa kabisa.

Baadhi ya Wanahabari machale hudhani kuwa ikiwa watasema Kiingereza katika vipindi vyao basi wataonekana wana akili au wana ujuzi mkubwa juu ya kazi zao. Hiki ni kinyumbe cha mambo.

Uchunguzi uliofanywa na makala ya KAMUSI umebaini kuwa Waswahili wengi wanafuatilia vyombo vya habari vya nje vya Idhaa za Kiswahili kama BBC, DW, VoA kwa kuvitaja vichache. Ingawa navyo havipo salama sana katika usanifu wa lugha lakini vyombo hivyo vya nje vinaonesha bidii za wazi kwa kutumia Kiswahili Fasaha.

Ufasaha wao lugha hasa uteuzi bora wa msamiati katika matangazo yao huwafanya Waswahili wengi kufuatilia matangazo ya vyombo hivyo kwa raghba kubwa.

Hata hivyo , hapa nyumbani vipo vyombo vya habari vituamiavyo lugha kwa ufasaha kiasi na kujipambanua kwa kipekee. Baadhi ya vyombo hivyo ni runinga ya Imani- Morogoro na redio Imani ya huko huko, ITV/ Redio One ya Dar es Salaam, TBC taifa, Azamtv/ U FM ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, vyombo vilivyotajwa hapo juu bado vina changamoto za lugha lakini kama ilivyosemwa vyombo hivyo vina nafuu kwa kiasi fulani ikilinganishwa na vingi visivyokuwa katika orodha hiyo.

Aidha, vipo vyombo vya habari vya ovyo/ hovyo sana kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili. Hivi ni vile uongozi na watangazaji wake hawaoni soni wala hawajali kuhusu lugha ya Kiswahili. Wao wanaamua kutumia neno lolote tu, katika muktadha wowote , namna yoyote na kivyovyote. Vyombo hivi ni hovyo sana na ni vingi hapa Afrika Mashariki.

Bila shaka wafuatiliaji wa makala haya ya KAMUSI wanaweza kuviorodhesha hapo chini kimoja baada ya kingine. ( Tunaomba uorodheshe vyombo vya ovyo/ hovyo katika mutumizi usanifu ya Kiswahili unavyovijua wewe).

KAMUSI ilifanya uchunguzi zaidi wa uwandani kuhusu sababu za vyombo vya habari kubananga lugha kwa kiasi kikubwa. Baadhi ya sababu ya ubanangaji huo ni pamoja na : Mosi, baadhi ya vyombo hivyo kuwaajiri machale badala ya Wanahabari, pili, Uongozi wa vyombo hivyo kutoweka mkazo katika lugha ya Kiswahili, tatu, vyombo vingi vya nyumbani kutokuwa na kamusi ,

Sababu nyingine ni pamoja na : nne, vyombo karibu vyote kutokuwa na wataalam wa Kiswahili katika madawati ya Habari na vyumba vya habari, tano, Baraza la Kiswahili la Taifa ( BAKITA) kutokuwa na meno makali ya kutoa adhabu kwa wabanangaji wanaotajwa, sita , watangazaji kuwa ushamba , kasumba , kukosa uzalendo na uchache wa mawazo ya Kimajumui wa Kiafrika.

Mathalani, baadhi ya Wanahabari wanaohusikika wakieleza kwa mfano, ,( i) Watu wawili wameweza kufa, (ii) Timu ya Yanga imeweza kufungwa katika mchezo wa mwisho ligi mabao mawili na Azam.Haya ni baadhi tu ya makosa.

Yaani mwanadamu aliyetoka nyumbani kwake kwa azama ya kutarazaki kwa mkosi tu akagongwa na motokali kisha kupoteza maisha. Ati mtu huyo anatajwa kuwa ameweza kufa kama vile mtu huyo alikuwa akitafuta kufa na amefanikiwa kufa huko.

Na huo mfano wa pili, kwanza haupendezi masikioni mwa Yanga wenyewe lakini si kweli kwamba yanga iliingia uwanjani ili kupoteza mchezo ule dhidi ya kikosi cha Azam. Basi tu Mipango si matumizi na mchezo wenyewe umechezwa wakati watu wakiwa na swaumu! Shubamiti!

KAMUSI inatoa wito kwa jamii ya Wanahabari kujitahidi kukifahamu vema Kiswahili na kukitumia kwa ufasaha. Makala ya KAMUSI ipo tayari kusaidia wanahabari katika kujifunza lugha Kwa nadharia na vitendo. Chombo chochote chenye utashi na lugha kinaweza kuwasiliana na uongozi wa kamusi ili kushirikiana katika kutoa mafunzo ya kunoa ubongo ili kujijengea uwezo wa matumizi sanifu ya Kiswahili chanana.

” Lugha ndiyo Utambulisho wa Utamaduni wa mtu, Fikra sahihi hufumbatwa na lugha sahihi”

Majid Mswahili
#Bwanakamusi
Mchambuzi wa Lugha, Fasihi , Fasaha ya Kiswahili.

Usithubutu Kupitwa na Makala haya ya KAMUSI. ( Imahaririwa tahajia)

Tuandikie: majidkiswahili@gmail.com Au +255 715 83 84 80.

KAMUSI imeletwa kwenu kwa hisani ya Utu- Tanzania na Culture Link Africa Ltd na Kamusi Pevu ya Kiswahili

Facebook Comments
Donate
Recommended articles