KATEGORIA ZA KILEKSIKA

By , in Shahada on . Tagged width:
Kategoria ya kileksika ndilo
kundi la kwanza la kisemantiki ambapo vitu vyote vilivyo katika ulimwengu,
vinavyoonekana na visivyoonekana hupewa majina ya kidhahania kimakundi. Makundi
hayo si ya ubia bali hutegemea jamii-lugha, utamaduni wao na mazingira yao.
Uainishaji wa vitu kimakundi hutokea bila kufahamu, kufikiri au kupanga. Hali
ya ufahamu hutokea panapozuka utata.
Rosch (1975) anaziita kategoria
hizi za kisemantiki kategoria tambuzi. Kategoria hizi hupangwa na watumiaji wa
lugha kutegemea tajiriba zao, imani na mazoea ya  jamii au kundi fulani la kijamii, na jinsi
wanavyouona ulimwengu wao bila shaka itadhihirika kutokana na kategoria tofauti
tofauti za kisemantiki. Kila kategoria huwa na kielelezo chenye sifa mahususi,
na chochote kinachokiuka sifa za kundi hubainika kimaelezo na kuwekwa katika kundi
lingine.
Kwa mfano, kasuku anaweza
kutumika kama kielelezo cha ndege ilhali popo ambaye ana sifa za ndege vilevile
hutofautishwa na ndege kwa vile baadhi ya sifa zake ni tofauti na zile za ndege
wengine.
Mbinu nyingine ya uainishaji ni
ile iliyotumiwa na Voegelin (2006) na inazigawa kategoria za kisemantiki kwa
matapo manne. Matapo hayo ni pamoja na 1) sura ya nchi pamoja na vitu na viumbe
vilivyomo, 2) tabia na shughuli za watu, 3) shughuli za kiakili pamoja na
hisia, jazba na maadili na, 4) watu na mahusiano kati yao. Katika kujumlisha
matapo haya ya kusemantiki, Voegelin (Aprili 2006) katika makala ya AIATSIS
anayaita makundi ya kisemantiki ambayo ni pamoja na nomino, vivumishi, vitenzi,
na mengineyo anuwai yanayotoa maana msingi za dhana mbalimbali. Kategoria za
kisemantiki zimerejelewa kama kategoria za kisintaksia na na kisemantiki na
Bennet (2000).
Mbinu nyingine inayotumiwa
kuainisha kategoria za kileksika ni ile inayoyagawa maneno ya lugha kwa makundi
mawili makuu. Makundi hayo ni maneno makuu na maneno ya kimatumizi. Kundi la
kwanza lina maneno mengi mno, na kila neno huwa na sura mbalimbali kutegemea
jinsi linavyobainika kiuamilifu katika tungo.
Sura hizo zinatokana na
uambishaji wa maneno hayo. Kundi la pili lina maneno machache, na maneno hayo
huwa hayabadilikibadiliki (Crystal, 2003).
Maneno katika lugha hugawanywa
katika sehemu mbalimbali kutegemea matumizi yayo katika upatanisho wa kisarufi.
Migao hiyo ndiyo huitwa aina za maneno. Kila lugha ina maneno mengi yanayotumika
katika mawasiliano ya kawaida na yale yanayotumika katika miktadha na taaluma
maalum, na uianishaji huo hutegemea maana au semantiki, maumbo ya maneno hayo
au mofolojia yao pamoja na uamilifu wa maneno hayo kwenye tungo, (Kapinga, 1983;
Mgullu, 1999).
Nyanja za kileksika ndizo
huorodheshwa kwenye makamusi ya lugha na maana za kila neno kuelezewa. Pamoja
na maana msingi ya neno, matumizi yake pia huelezwa pamoja na jinsi neno hilo
hubainika kimatumizi. Kando na matumizi yake, maneno huelezwa kama ni ya umoja au
wingi, miktadha yanamotumika pamoja na makundi yao. Katika ufundishaji wa
sarufi, maana msingi za maneno husisitizwa pamoja na taratibu za upanganji wa
maneno hayo kenye tungo ili
maana ziweze kufasiriwa kwa
urahisi.
Kategoria za kileskika zimeelezwa
kama aina za maneno katika lugha za Kiswahili na Ekegusii (Whiteley, 1956 ;
Massamba na wenzake, 1999 ; Habwe na Karanja 2004). Katika lugha ya Kiswahili
maneno yameainishwa kwa makundi manane  makuu
ambayo ni nomino, viwakilishi, vivumishi, vitenzi, vielezi, viunganishi, vihusishi
na vihisishi. Majina ya makundi hayo yanatokana na uamilifu wayo katika
sintaksia. Katika lugha ya Ekegusii makundi yaliyotambuliwa na Whiteley (1956)
ni pamoja na nomino, viwakilishi, vivumishi, vitenzi, vielezi, viunganishi, vihusishi
na vihisishi. Taratibu hizi za uainishaji wa maneno katika lugha hizi mbili
unaelekea kushabihiana kwa sababu lugha hizi zote ni za Kibantu na muundo wake
wa kisintaksia unashabihiana sana.
Utafiti huu utachunguza kategoria mbili za kileksika ambazo
ni nomino na vitenzi. Nomino ni maneno yanayotajia vitu, watu, hali na mahali.
Kuna aina mbalimbali za nomino, (Mgullu, 1999 ; Habwe na Karanja 2004). Katika
lugha za Kiswahili na Ekegusii, nomino zina mshabaha mkubwa kimaana na
kiothografia, hasa ikizingatiwa kuwa hizi zote ni lugha za Kibantu.
Mifano ya nomino ni :
Kiswahili         Ekegusii
Mtu                 Omonto
Nyumba          enyomba
Utamu              obwansu
Kuku               engoko
Maji                 amache
Munyu             omonyo
Maneno haya yana maana mahususi
zinazoeleweka yanapoelezwa bila miktadha ya kimazungumzo. Tofauti na maana
msingi za maneno haya, neno linapowekwa kwenye muktadha kimazungumzo linapata
maana nyingine, kwa mfano:
3. Mainye n’achete enyomba yaye.
Mainye anaipenda nyumba yake.
Kando na maana msingi ya nyumba, nomino hiyo inapata maana
nyingine ambayo
inadhihirika kiusemi kwamba:
Mainye anaipenda familia yake
Mazungumzo yanaliwezesha neno ‘nyumba’ kusimba maana nyingine
tofauti na uwazi na hivyo kuzua umaanisho wa familia.
Vitenzi ni maneno yanayoeleza mambo yanayotendeka. Massamba (2004)
anaeleza kitenzi kama ‘Kipashio kinachotoa taarifa kuhusu tendo linalofanyika, lililofanyika
au litakalofanyika.’ Lugha zote zina maneno ya kutajia vitendo.
Lugha za Kiswahili na Ekegusii zina vitenzi vingi ambavyo
hubainisha mlingano wa kimuundo.
Mifano ya vitenzi katika lugha hizi ni:
Kiswahili         Ekegusii
Amka
booka
Funga              sieka
Toka                sooka
Angalia
rigereria
Lala
raara
Maana msingi za vitenzi hivi
katika lugha hizi ni mahususi. Hata hivyo, kimazungumzo vitenzi hivi huweza
kupata maana nyingine tofauti na maana za kileksika, na maana hizo zinaweza
kufikiwa na msikilizaji kwa kutumia mbinu ya ufaafu katika miktadha maalum, kwa
mfano, mtu akisema;
4. Tom nere osieka
    Tom ndiye alifunga

Uwazi wa kauli hii ni kwamba Tom
ndiye alifunga (pengine mlango) lakini umaanisho wake katika mazungumzo ukawa
unaelekea kwenye ile hali ya kuwa wa mwisho katika mashindano fulani. Washiriki
wa mazungumzo haya ni lazima wawe katika hali sawa ya kimawazo ili kupata maana
ya kile kilichomaanishwa ingawa hakikusemwa kwa kutumia mbinu za uhusiano.
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!