FURSA HII YA KISWAHILI TUICHANGAMKIE

By , in Zote on . Tagged width:
LUGHA ya Kiswahili inazidi kukua na kupata
umaarufu kila uchao.
Lugha hiyo,
inazungumzwa na wakazi wa eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, baadhi ya maeneo ya Msumbiji na
Comoro, Zambia, Afrika Kusini, Namibia, Malawi, Zimbabwe, Somalia, Madagaska
na Oman, ambayo ni Asia.
Tanzania ndiyo
inayotambulika kwamba lugha ya Kiswahili inazungumzwa zaidi na ndiyo lugha ya
taifa, ingawa asili yake ni kibantu na ni lugha ya Kiafrika.
Kimsingi, ukiacha
nchi zingine jirani za Afrika Mashariki, raia wa nchi zingine wanakijua
Kiswahili, kwa sababu waliwahi kuishi nchini wakati wa vita vya kupigania
uhuru wa nchi zao kama Afrika Kusini na Zimbabwe.
Zingine kama Zambia,
DRC, Malawi, Comoro, Kiswahili kinatumika kwa sababu nchi hizo zina
mwingiliano mkubwa wa shughuli za kibiashara.
Licha ya Kiswahili kuwa lugha ya taifa nchini,
Tanzania haijachukua hatua za kutosha kuchangamkia fursa hiyo, kwa kuandaa
wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kwenda kuifundisha katika nchi zingine pamoja
na hitaji kubwa la wataalamu wa lugha hiyo katika nchi mbalimbali duniani.
Kwa mfano, Sudan Kusini imekuwa ikitangaza fursa
za wataalamu wa kwenda kufundisha Kiswahili.
Badala yake baadhi ya nchi hasa Kenya
imeichangamkia fursa hiyo na imekuwa ikichangamkia fursa za kutoa wataalamu wa
kufundisha Kiswahili katika nchi zingine.
Umuhimu wa Kiswahili unaendelea kuonekana kadiri
siku zinavyokwenda. 
Tayari Umoja wa Afrika (AU), umeshakiidhinisha
Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kutumika wakati wa vikao vyake.
Bunge la Afrika Mashariki (EALA), nalo limeanza
kuchukua hatua kuhakikisha kwamba vikao vyake vinaendeshwa kwa lugha ya
Kiswahili.
Hoja za wabunge ni kwamba, lugha hiyo
inazungumzwa na watu wengi katika ukanda huo, hivyo ni wakati mwafaka lugha
hiyo ikatumika.
Takwimu zinaonyesha kwamba, Kiswahili
kinazungumzwa Tanzania kwa asilimia 100, Kenya zaidi ya asilimia 80, Uganda
asilimia 50, Rwanda zaidi ya asilimia 50 na Burundi, nako ni zaidi ya asilimia
50.
Katika kuhakikisha kwamba lugha ya Kiswahili
inapewa kipaumbele, EALA imeshawasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya
mkataba kutaka Kiswahili kitumike katika Bunge hilo.
Kabla ya kukubaliwa, asilimia kubwa ya wabunge
wa Bunge hilo wamesikika wakipendekeza kuwasilishwa kwa muswada wa kuruhusu
matumizi ya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika bunge hilo, na kwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Niliwasikia wabunge kadhaa wakitoa kauli ambazo
zinadhihirisha jinsi gani lugha  hiyo ilivyo na umuhimu katika EALA.
Miongoni wa wabunge
hao ni
Adam Kimbisa wa
Tanzania Bara, ambaye alisema:
“Umefika wakati bunge
lipitishe muswada Kiswahili kiwe lugha rasmi katika bunge na Afrika
Mashariki.”
Naye Mariam Yahya
kutoka Zanzibar alinukuliwa akisema:
“Ni muhimu muswada
huo upiganiwe kwa nguvu zote ili lugha ya Kiswahili, itumike kwa nchi
wanachama na ndani ya bunge hili ili wananchi wanaofuatilia vikao wajue kwa
kina masuala yanayojadiliwa.”
Spika wa EALA, Daniel
Kidega, anaunga mkono Kiswahili kuwa lugha rasmi katika EAC, huku akiwataka
wabunge wenzake kuenzi lugha hiyo na kuifanya kuwa lugha ya kufanyia kazi
katika Jumuiya hiyo.
Kidega aliwaambia
wabunge wa EALA jijini Dar es Salaam, mapema mwaka huu kuwa lugha ya
Kiswahili ina umuhimu mkubwa kwa Jumuiya na kushauri kuwa kuna haja ya
kupitia katika Sheria ya Bunge hilo, ili kuhakikisha kuwa Kiswahili na
Kiingereza vinatumika ama kuzungumzwa kila mahali katika Afrika Mashariki.
Alisema kuna haja ya
kuhakikisha kuwa Kiswahili kinazungumzwa katika nchi zote za Afrika Mashariki
kwani ni lugha ya Afrika na wao kama Waafrika, hivyo zifanyike jitihada za
kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufanya kazi katika EAC.
Kauli za wabunge hao
wa EALA na spika wao, zinaonyesha wazi ni jinsi gani Kiswahili kilivyo na
umuhimu na jinsi gani kitakavyoendelea kuwa fursa muhimu ndani na nje ya
Tanzania.
Kiuhalisia EAC ni
eneo kubwa na lenye idadi kubwa ya watu ambao wanakosa fursa ya kuelewa mambo
ya msingi yanayowagusa yanapokuwa yakijadiliwa ndani ya EALA pale inapotumika
lugha ya Kiingereza, ambayo ni asilimia ndogo ya wananchi wanaielewa.
Kama huko nyuma
Watanzania hatukuiona fursa ya Kiswahili, kwa sasa itabidi turekebishe makosa
hayo na kuichangamkia.
Kuna mambo kadhaa
yanayoweza kufanyika yakiwamo kuitangaza lugha hiyo kimataifa kupitia katika
maonyesho ya biashara, mikutano mbalimbali ya kitaifa na ya kimataifa pamoja
na wataalamu wa lugha hiyo kuendelea kutoa machapisho mara kwa mara
yanayohimiza Kiswahili sanifu.
Mara kadhaa nimemuona
Rais John Magufuli akitumia Kiswahili wakati wa mikutano ya wakuu wa EAC.
Hiyo ndiyo njia pekee
ya kuitangaza lugha hiyo kama nilivyotangulia kueleza kwamba mikutano ya
kitaifa na kimataifa utumike kuitangaza lugha hiyo.
Takribani wiki mbili
zilizopita, nilimshuhudia Rais wa Mexico, Enrique Peña Nieto, akizungumza
lugha ya nchi yake alipokuwa akitoa hotuba yake alipotembelewa na mgombea
urais wa Marekani kupitia Chama cha Republican, Donald Trump, licha ya
kuielewa kwa ufasaha lugha ya Kiingereza.
Tunawashuhudia mara
kadhaa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, akitumia Kijerumani katika
mikutano mingi ya kimataifa, ingawa anakijua Kiingereza au Vladmir Putin wa
Urusi, anayezungumza lugha yake licha ya kukijua Kiingereza.
Viongozi wakuu wa
China an Ufaransa wanafanya hivyo hivyo.
Hii yote ni kuthamini
na kutangaza lugha zao.
Utaratibu huu
tutapaswa kuutumia kama kweli tumedhamiria kuikuza na kuitangaza lugha ya
Kiswahili.
Kadhalika, vyuo vyetu
vya elimu ya juu vinaweza kuweka utaratibu wa kuwataka wageni wanaojiunga
navyo kutakiwa kujifunza Kiswahili, kwa muda fulani kabla ya kuanza rasmi
kozi wanazotaka kusoma.
Nchi kama Urusi,
China wanao utaratibu huo, ambao lengo ni kutangaza lugha zao.
Kupitia utaratibu
huu, tutakitangaza Kiswahili duniani kote sambamba na Watanzania kupata fursa
ya kwenda kufundisha lugha hiyo ughaibuni.
Ifike mahali sasa
viongozi wengine wa serikali watumie lugha ya Kiswahili katika mkutano ya
kitaifa na kimataifa na watumishi wote wanaokwenda kuwakilisha serikali ya
Tanzania nchi za nje wakipewa ruhusa lazima wapewe pia waraka rasmi wa
kutumia na kukitangaza Kiswahili huko waendako.
Ziko jitihada kadhaa
ambazo zimeanza kuchukuliwa kwa ajili ya kukitangaza Kiswahili.
Kwa mfano, Serikali
imeshadokeza kwamba inatarajiwa kuanza kutumia Kiswahili katika mikutano yote
ya kimataifa itakayowakilishwa na viongozi wake baada kukamilisha kutuma
wataalamu watakaotafsiri lugha hiyo kwa watumiaji wa lugha nyingine duniani.
Ahadi hiyo ilitolewa
bungeni katika Mkutano wa Tatu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwamba vyuo
vikuu duniani kote vimeanza kufundisha Kiswahili, hivyo kuongeza mahitaji ya
wataalamu wa kufundisha lugha hiyo kutoka Tanzania.
Majaliwa alisema vyuo
vikuu nchini vinafundisha walimu wa lugha hiyo kukidhi mahitaji kwenye soko
la kimataifa, lakini pia serikali inajiandaa kupeleka nje wataalamu wa
kutafsiri Kiswahili.
Chama cha Wafanyakazi
wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, kimempongeza Waziri Mkuu kwa tamko hilo na kuishukuru Serikali ya
Awamu ya Tano kwa juhudi za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kuwa
ni tunu ya taifa.
Mwenyekiti THTU
Mlimani, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Salifius Mligo anasema wameona lugha
ya Kiswahili inavyozidi kukua kwa kasi barani Afrika, Afrika Mashariki na nje
ya Bara la Afrika.
Anatoa mfano wa Bunge
la Afrika kuwa linatumia lugha ya Kiswahili.
Anasema lugha hiyo
inafundishwa katika vyuo na shule za serikali na watu binafsi katika nchi
kadhaa ikiwamo Ghana, Libya, Zimbabwe, Namibia, Misri, Algeria, Afrika
Kusini, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.
Bara la Asia ni
China, Japan, Korea Kusini na India.
Ulaya ni Ujerumani,
Italia, Uholanzi, Uingereza, Sweden, Ufaransa na Austria. Kwa Amerika ya
Kaskazini ni Marekani na Canada.
Amerika ya Kusini ni
Mexico na Jamaika, na Australia ni katika miji ya Melbourne, Sydney na
Adelaide.
Ninakubaliana na
Mligo kwamba serikali inatakiwa kutoa waraka maalumu wa kurasimisha matumizi
rasmi ya Kiswahili katika taasisi zote za umma kutumia Kiswahili katika
mawasiliano yote na kuacha matumizi ya Kiingereza.
Kuna taarifa za kutia
moyo kwamba kuanzia Julai mwaka huu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaanza
kutumia lugha ya Kiswahili kuwasiliana katika vikao vyote isipokuwa
kufundishia darasani.
Machi mwaka huu,
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura,
amewataka watendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), kujitangaza na
kushiriki katika matukio ya kitaifa na kimataifa kuhamasisha matumizi ya lugha
ya Kiswahili ili kiweze kufahamika na kutumika na mataifa mengine.
Ni ubunifu, mbinu na
mikakati kama hiyo zitasaidia kuitangaza lugha ya Kiswahili kimataifa na
kuinufaisha Tanzania kwa ajira pamoja na kipato.
Tuichangamkie fursa
hii muhimu. CHANZO >>>>