FASIHI, UANDISHI NA UCHAPISHAJI (7)

By , in Kavazi on .

SEHEMU YA PILI: UANDISHI

6. Udhibiti (Censorship) wa Fasihi na Uhuru wa Mwandishi wa Vitabu Tanzania

F.E.M.K. Senkoro
Utangulizi
Ushairi umechujuka mara tatu kutoka katika ukweli; kwa hiyo kuanzia sasa washairi wanapigwa marufuku katika Jamhuri yetu. 1
– Plato, The Republic.
Sheria inaniruhusu kuandika lakini kwa sharti moja kuwa niandike kwa mtindo usio wangu. Ninayo haki ya kuonyesha undani wa mambo, lakini nalazimishwa niuonyeshe undani huo kwa kupitia katika kauli isiyo yangu… Mimi ni mcheshi, lakini sheria inaniamrisha niandike bila mzaha wowote; mimi hupenda kusema mambo bila kuficha, lakini sheria hainitaki niandike hivyo.2
– Karl Marx, “Ueber die Neueste Preussische Zensurinstruktion”
Kila mtu ana uwezo wa kusema kwa uhuru kabisa; na maneno ya kila mtu sharti yasikilizwe hata kama mawazo ya mtu huyo yamepotoka kiasi gani au hayapendwi kiasi gani.3
– J.K. Nyerere, Uhuru na Maendeleo
Serikali ni chombo cha mabavu.4
– Lenin na Nyerere
Katika madondoo manne tuliyoyanakili, la kwanza ni la mdhibiti aliyekuwa na mamlaka ya kisiasa na kisheria katika jamii yake, na mamlaka haya yalimpa nyundo iliyomwezesha kupasua vichwa vya washairi ambao hawakufuata sheria na amri za tapo la uraslmi mkongwe lililokuwa limetawala Ughaibuni kwa wakati ule.5 Dondoo la pili ni kilio cha mwandishi dhidi ya udhibiti, kilio kinachodai haki na uhuru wa mwandishi kueleza kile anachotaka kukieleza na vile atakavyo kukieleza kitu hicho. La tatu ni tamko la mwanasiasa ambaye ni msanii vilevile. Huyu ni mtu wa karne ya 20 ambaye anasisitiza kinadharia kuhusu uhuru wa mtu kujieleza na kutoa mawazo yake; tamko ambalo linawekewa mipaka katika dondoo la nne lionyeshalo nguvu za serikali.
Katika madondoo haya tunaweza kupata picha iwakilishayo mjadala wa mada ya uhuru wa msanii. Mjadala huu umekuwepo hata kabla ya Masihi, nao unaendelea hadi leo. Ndani ya mjadala huu mmejikita suala la nafasi ya udhibiti katika uhuru wa msanii.
Katika makala haya tendo la udhibiti wa maandishi tutalichunguza na kuonyesha nafasi yake katika mifumo tofauti ya jamii, halafu hatimaye tutalihusisha na jamii ya Tanzania.
Udhibiti Katika Jamii Tofauti
Suala la udhibiti ni la kitabaka, kwani lilianza pale tu jamii ilipogawika katika matabaka mbalimbali ya watu. Ni vigumu basi, mathalani, kulihusisha suala hili najamii ya mwanzo ya mtu, jamii ya umajumui; kwani wakati huo wanajamii wote waliungana kupigana na mazingira ya kihasama yaliyokuwa yamewazunguka. Dunia ilikuwa haijapoa vizuri, minyama ya kidubwana ilirandaranda pote, na mtu wa wakati huo bado alitawaliwa na ujinga kuhusu mazingira yake. Nguvu zote hizi hazikumruhusu mtu huyu kuwa na jambo lolote lile, ikiwemo fasihi na sanaa kwa jumla, la kianasa, kwani nia yote ilielekezwa katika kujihami.
Jamii zilizofuatia hii ya ujima wa awali, za utumwa, umwinyi na baadaye ubepari zilikuwa za kitabaka. Sasa walikuwapo mabwana walioishi kwa damu na jasho la watumwa; mamwinyi walionenepeana kwa kazi zilizofanywa na watwana wasio na chochote ila nguvu zao; mabepari walionawiri kwa sulubu waliyoipata wafanyakazi.6
Kuanzia enzi za utumwa maandishi yalipovumbuliwa, fasihi andishi ya mwanzo ilikuwa ya wateule wachache tu wenye vyeo na vyao. Hao mabwana, mamwinyi na mabepari, walihakikisha kuwa kila mbinu hutumika, ikiwamo ya udhibiti wa maandishi, kuuendeleza na kuulinda utawala wao.
Ijapokuwa watumwa, watwana na wafanyakazi walikuwa na fasihi yao – ikiwemo fasihi simulizi – iliyoeleza hisia zao, majonzi yao, hasira zao na matumaini yao, mara nyingi hii ndiyo fasihi iliyoshambuliwa na rungu la mdhibiti. Ndiyo sababu hata katika historia twasoma jinsi ambavyo mabwana wafuga watumwa walifanya juu chini kuwatenganisha wale watumwa waliokuwa na utamaduni na lugha moja ili wasiweze kuungana na kueleza hali zao kwa kupitia katika lugha yao.
Kihistoria, mawazo yaliyohusu dini ndiyo yaliyokuwa lengo kuu la udhibiti wa mwanzo kwani wakati huo dini ilikuwa taasisi iliyoshikilia madaraka juu ya roho na miili ya watu; ilikuwa ndiyo kanisa na serikali kwa wakati huohuo. Ndiyo maana, kwa mfano, Socrates, katika mwaka wa 399 kabla ya Masihi, alihukumiwa kifo kutokana na “kuabudu miungu wa ajabuajabu na kuharibu mwenendo bora wa vijana.”7
Baada ya udhibiti wa kidini, udhibiti uliofuatia ulijikita katika mawazo ya kisiasa kutokana na kuzuka kwa serikali imara zilizokuwa kando ya taasisi ya dini; ndipo kesi za uhaini zilipoenea. Halafu, katika enzi za hivi karibuni udhibiti ulijielekeza zaidi katika mawazo yaliyohusiana na jazba na hisia za mtu, hasa maelezo ya tendo la kukutana kwa mwanamume na mwanamke pamoja na ya jinsi zao yalipohusika; ndipo masuala ya “vitabu vichafu” yalipojitokeza. Kila mbinu mpya za kupashana habari zilivyoibuka ndivyo udhibiti nao ulivyounda mbinu zake mpya. Hili lilihusu kugunduliwa kwa mashine za kuchapia, filamu, televisheni, redio, kuwapo kwa maktaba za jumuia, kutumika kwa vitabu vya kiada mashuleni, na kusambazwa kwa vitabu vya fasihi na magazeti ainaaina.
Huenda, katika hatua hii, swali litazuka: Je, kwa nini kuwe na udhibiti wa fasihi?
Jibu la moja kwa moja hapa ni kwamba kila kazi ya fasihi katika jamii ya kitabaka ni “mali” ya tabaka hili ama lile: kamwe hakuna fasihi iliyo mali ya “jamii” nzima isipokuwa tu katikajamii ya kiumajumui na katika ile ya kikomunisti. Fasihi ni mojawapo ya vyombo vya kiitikadi na tabaka tawala daima huhakikisha kuwa chombo hiki hutumiwa kuenezea itikadi zake. Pale fasihi inapojaribu kujitenga au kuipinga itikadi ya tabaka tawala inakumbana na rungu la mdhibiti.
Mfano mzuri wa udhibiti katika mfumo wa kibepari ni ule wa mshairi maarufu wa Marekani ya Kusini, Pablo Neruda, ambaye hapo mwanzo alikuwa akiandika mashairi yaliyosifu uzuri wa maua na machweo ya jua, utamu wa nyimbo zitokanazo na mtiririko wa maji ya mito na sauti nzuri za ndege, mvuto wa mandhari ya mpangano wa milima, na kadhalika. Maudhui haya yalisifiwa sana na wahakiki na vyombo vya habari vya kibepari. Lakini baada ya muda, Neruda alibadili mwelekeo wake wa maudhui akaanza kuandika utetezi wa mtu mnyonge wa tabaka la chini. Akieleza mabadihko haya, Neruda alisema “Dunia imebadilika, na ushairi wangu pamoja nayo.” Hapo walewale wahakiki waliomsifu sana mwanzoni sasa walimkashifu na kudai kuwa ushairi wake ulikuwa umepotoka; na kuwa Neruda alikuwa amechanganya ushairi na “siasa”, jambo ambalo ni mwiko kwa tabaka la kibepari.
Mfano huu unatuonyesha nyuso za udhibiti, hasa katika jamii ya kibepari, kuwa ni nyingi. Mathalani, udhibiti huweza kutekelezwa kwa kusifiwa kupita kiasi kwa kazi za fasihi zinazotekeleza matakwa ya tabaka tawala, kazi ambazo zinaeneza itikadi za kibwana na kuduwaza pamoja na kumdumaza mtu wa tabaka la chini ili asielewe hasa kiini cha unyonge wake, na asipiganie haki zake. Hapa fasihi na sanaa huhitajiwa imtenge msanii na uhalisi wa jamii yake, ijitenge na undani wa siri za mfumo wa kibepari. Ndiyo sababu kazi nyingi za fasihi tuzionazo leo katika jamii za kibepari zinajishughulisha zaidi na mambo kama vile mapenzi ya kibwege, upelelezi na ukachero unaowapumbaza wasomaji kwa mbinu mbalimbali za fani kama vile taharuki, msisitizo katika utamu wa lugha, na hata kuyapamba na kuyasifu mambo ya kibepari. Pale udhibiti usipoweza kutumika hivyo, hasa inapozuka kazi ya fasihi inayoenda kinyume na tabaka tawala, basi maguvu ya dola hutumika na kazi hiyo hupigwa marufuku, na hata wakati mwingine mwandishi wake huwekwa kizuizini.
Katika Afrika kuna mifano mingi ya udhibiti wa namna hiyo, na mzuri zaidi ni wa mwandishi maarufu wa Kenya, Ngugi wa Thiong’o, ambaye kazi zake, hasa ya Ngaahika Ndeenda8 ilimgonganisha na vyombo vya dola hadi akawekwa kizuizini. Ngugi, kwa kuanza kufichua siri za mfumo wa kibepari kwa watu wanyonge, aliliudhi tabaka tawala la jamii yake ambalo halikusita kutumia udhibiti na vyombo vyake vya mabavu.
Mifano mingine mizuri ya udhibiti wa maandishi na matumizi ya maguvu dhidi ya waandishi ni ya Afrika ya Kusini ambako leo hii waandishi wengi waliojaribu kupinga udhalimu na unyama wa siasa za kibaguzi, ama wamelazimika kuihama nchi yao kwa kuogopea maisha yao, au wamepiga potelea mbali na hata wengine kuishia vifungoni.
Hata hivyo, mfumo wa ubepari hautaendelea kuwapo daima dumu kwani tayari umejichimbia kaburi lake wenyewe. Mbinu mbalimbali, zikiwemo za migomo ya wafanyakazi, kuundwa kwa vyama vya kifanyakazi, pamoja na uhusiano mzuri’na ushirikiano wa matabaka ya kifanyakazi duniani, huimarisha tabaka hili ambalo hatimaye linachukua madaraka yote ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Jamii ya usoshalisti kamili na ya kikomunisti ni ya watu huru kabisa waliojikomboa katika nyanja zote za maisha, na katika jamii hii isiyo na matabakakinzani udhibiti hupoteza nguvu na umuhimu wake.
Kwa kifupi basi, mwandishi katika jamii ya kitabaka hana uhuru wowote ule nje ya mipaka aliyowekewa na tabaka tawala.
Udhibiti katika Jamii ya Tanzania
Udhibiti wa maandishi katika jamii ya Tanzania, sawa na ilivyokuwa katika jamii nyingi za Afrika, ulianza wakati wa majilio ya wakoloni.
Tangu enzi za Waarabu, Wajerumani hadi Waingereza, udhibiti huu ulionekana hata katika uteuzi wa vitabu vya kutafsiriwa vilivioeleza na kutukuza utamaduni wa kwao pamoja na “nguvu” walizokuwa nazo. Vitabu kama vile vya Mashimo ya Mfalme Suleiman, Allan Quarterman, Safari za Gulliver na Robinson Kruso viliteuliwa na kutumiwa mashuleni kwa malengo maalumu. Kwa mfano, katika Robinson Kruso mwanafunzi mtoto wa Kitanganyika alitakiwa azikiri nguvu za Mzungu mmoja mwenye uwezo wa kukitawala kisiwa peke yake na kuyamudu maisha bila matatizo. Haya yote yaliambatanishwa na itikadi na imani za dini ngeni walizolazimishwa Watanganyika kuzikubali na kuzitupilia mbali dini na imani zao za jadi. Ni dhahiri kwamba udhibiti usingeweza kuyakubali maandishi kama vile Manifesto ya Chama cha Kikomunisti9 cha Karl Marx na Engels kwani haya yangewaamsha watawaliwa. Hata vitabu vya historia vilivyosambazwa mashuleni nyakati hizi, mathalani cha Milango ya Historia au kile cha Fred Madjalanv (1963) A State of Emergency: The Full Story of the Maumau (Houghton Mifflin, Boston), ni vile vilivyopotosha ukweli wa historia ya mtu mweusi vikidai kuwa mtu huyo hakuwa na historia kabisa, au kuwa historia yake imejaa “maisha ya kishenzi yanayokaribia yale ya nyakati za kale za mawe10, maisha ambayo hayana mchango wowote wa thamani katika historia ya ustaarabu duniani.
Uhuru, mapinduzi ya Unguja, na Muungano wa Tanzanyika na Unguja na kutangazwa kwa Azimio la Arusha ni matukio muhimu ambayo yalishangiliwa sana na wananchi. Haya, hasa Azimio la Arusha, yaliumba matumaini makubwa mioyoni mwa wananchi wengi. Fasihi iliyojitokeza mara tu baada ya matukio haya ilijaa lelemama za hoihoi na vifijo vya kushangilia. Lakini pia matukio hayahaya yalisaidia kuzichonga kalamu za waandishi wa fasihi wa Tanzania ambao walifuatilia kwa makini utekelezaji au ukiukwaji wa maadili ya matukio hayo kama yalivyotangazwa na wanasiasa majukwaani.
Kati ya hao alikuwapo E. Kezilahabi ambaye aliandika riwaya ya Rosa Mistika (1971), miaka minne tu baada ya Azimio la Arusha. Kitabu hiki kilipigwa marufuku kisitumiwe mashuleni na hata kisiuzwe waziwazi madukani. Ilidaiwa na waliokipiga marufuku kuwa kilikiuka maadili ya “jamii” kwa kueleza mambo “ya aibu” kwa wazi. Sura ya kumi ndiyo hasa iliyotolewa kuwa mfano wa “uchafu” wa kitabu hiki. Udhibiti huu uliofanywa na Wizara ya Elimu ulizusha maswali mengi zaidi ya majibu. Wasomaji walianza kuuliza: Je, si kweli “uchafu” uelezwao katika Rosa Mistika umo ndani ya jamii ya Tanzania? Je upotofu na uongozi mbaya ambao unafichuliwa katika riwaya hii si upo kati yetu? Kwa baadhi ya wasomaji ilielekea kuwa suala la “uchafu” wa maelezo yatokeayo kitandani baina ya Mkuu wa Chuo na mwanafunzi wake lilitumika kama kisingizio tu cha kudhibiti ukweli wa masuala mengine nyeti yaliyowagusa viongozi wakiwakilishwa na watu kama vile Bwana Maendeleo Deogratius anayeshiriki katika kuwaharibu vijana.
Wakati huohuo, katika miaka ya 1975 na 1976 kamati ya chama cha TANU ilipitisha uamuzi wa kuvipiga marufuku vitabu vyote vya David G. Mailu11 wa Kenya, kitabu cha C. Mangua, A Tail in the Mouth12, na kile cha Mamuya cha Jando na Unyago (EAPH, Nairobi). Hivi vilielezwa kuwa ni vitabu vichafu ambavyo havikuzingatia maadili ya “jamii” kwani vilieleza “mambo ya aibu” kwa wazi kabisa bila kuficha. Udhibiti huu ulizusha majadiliano mengi sana magazetini hasa kuhusu maana hasa ya “vitabu vichafu”. Maswali yaliulizwa yakadai majibu: Je, mbona vitabu vyenye matusi zaidi kama vile Kama Sutra viliachwa viendelee kuuzwa madukani? Je, kuna uchafu gani katika kazi ya fasihi inayoonyesha uchu wa kinyama alio nao kiongozi fulani ambaye yu tayari kuhubiri kuhusu umuhimu wa malezi bora ya vijana wakati yeye mwenyewe ni mharibifu mkubwa wa vijana hao? Je, tuviweke wapi vitabu vinavyomlaghai na kumdanganya mtu mnyonge wa matabaka ya chini kuwa “wizi”, “ujambazi” na “umalaya” wake ni dhambi ambayo jawabu lake liko katika kuyaacha maovu hayo, la sivyo jawabu lingine ni mtutu wa bunduki, jela na kazi ngumu? Je, si katika mtazamo wa namna hii kuhusu matatizo ya mtu mnyonge umejificha uchafu zaidi ya ule uliodaiwa kuwa uko katika elimu ya biolojia na malezi bora ya Jando na Unyago?
Kwa kifupi, maswali mengi yalitaka kujua vigezo na vipengele vilivyotumiwa na wadhibiti wa maandishi tuliyoyaeleza. Utata wa vigezo hivyo ulijitokeza mara dufu wakati Mamuya alipoamua kuzitoa sura mbalimbali za Jando na Unyango katika vijitabu vidogovidogo ambavyo vichwa vyake vilivutia na kuonyesha “heshima” iliyotakiwa na wadhibiti. Hivi havikupigwa marufuku ijapokuwa maudhui yake yalikuwa yaleyale ya Jando na Unyago. Hili nalo lilizusha swali: Je, inawezekana kuwa udhibiti uliofanyika ulitokana na majalada na majina tu ya vitabu?
Udhibiti wa vitabu katika Tanzania si wa moja kwa moja kwani, kinyume na ule wa filamu, hauna bodi au kamati yoyote rasmi. Huu unatokea hapa na pale, na kwa namna tofautitofauti. Katika makala ya “Uhuru wa Mandhishi,” Walter Bgoya anatuonyesha njia moja ya udhibiti kwa kupitia kwa mchapishaji. Anasema:

Kwa sababu ni vigumu kwa viongozi kwenda kwa kila mkulima na mfanyakazi wapate maoni yake kuhusu maandishi fulani, ndio maana wanao sisi (wachapishaji) kama ndio wawakilishi wao. Wanatupa vyombo fulani na kutuambia tuwe wanaimla (dictators) wa sehemu zetu.

Ndiyo maana nisemapo mimi ni meneja wa TPH nina maana ya kwamba ni mwanaimla wa pale. Kama muswada wako hauafiklani na msimamo wangu ninaupiga zii! Kwisha.


(Bgoya, 1974: 18-22)

Swali linaweza kuibuka hapa kuhusu kauli hii ya Bgoya: Je, tuseme kuwa uhuru na haki za mwandishi wa vitabu katika Tanzania zimo mikononi mwa hao wanaimla? Kama wadhibiti hawa waliojiteua wenyewe ndio wenye mamlaka ya mwisho kuhusu uhuru na haki hizo, u wapi uhuru na haki aliyoisisitiza Nyerere, ya mtu kutoa mawazo yake na kusikilizwa hata kama mawazo hayo yamepotoka au hayapendwi kiasi gani?
Mfano mwingine mzuri wa udhibiti unaofanywa na wachapishaji ni ule wa kwenye magazeti. Mathalani, kuanzia miaka ya katikati ya 1970 ulitokea mjadala mkubwa kuhusu maana ya ushairi, hasa ushairi wa Kiswahili. Mhariri wa mashairi wa gazeti la Uhuru na Mzalendo alichapisha makala na mashairi mengi sana yaliyochangia katika mjadala huo; lakini kwa vile yeye aliamini kuhusu ushairi wa kirasimi uliosisitiza kuwa vina na mizani ni uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili, aliyatupa vikapuni mashairi yote yaliyoasi mwenendo wa kirasimi, hasa yale ambayo hayakufuata “sheria” za vina na mizani. Huu ulikuwa udhibiti ambao hata hivyo leo hii umepigwa vikumbo na nguvu za wakati kutokana na kuchapishwa na hata kukubaliwa katika mihtasari ya elimu kwa diwani mbalimbali za washairi wa kilimbwende na kihalisia walioasi minyororo ya sheria za kirasimi.
Kuchapishwa kwa hadithi fupi yenye msimamo mkali ya E. Kezilahabi, “Mayai Waziri wa Maradhi” katika gazeti la Chama la Mzalendo kulianza kuonyesha dalili za uhuru na haki alizosisitiza Nyerere. Hadithi hii ilichapishwa katika mfululizo wa sehemu tatu. Ni hadithi ambayo, sawa na riwaya na tamthilia za Kiswahili za kitashtiti, kejeli na dhihaka za miaka ya 1980, ilionyesha ubwege wa baadhi ya viongozi ambao bado wana mawazo duni ya kuwatumia wachawi ili wawasaidie kupata vyeo. Ni hadithi Uiyojaribu kutathmini maendeleo yaliyopatikana miaka kumi baada ya uhuru, maendeleo ambayo taswira yake ilionekana katika miili iliyokondeana ya mizuka ya watoto kumi, ukiwemo ule wa Ukombozi, mtoto wa Mayai, Waziri wa Maradhi, aliyekuwa kakonda zaidi ya wengine wote. Katika hadithi hii mwandishi anauliza maswali mengi kwa kutumia mbinu mbalimbali, hasa za taharuki, ndoto na maajabu mbalimbali, na mwishoni anatoa jibu tulikutalo katika tukio moja la vizuka hao.

Walipofika chumbani, Ukombozi alimwashiria babake asimame palepale mlangoni alipokuwa amefika. Alitii. Watoto walipanga vitabu walivyokuwa wamebeba chini karibu na ukuta. Walipomaliza, Ukombozi alipanda juu ya vitabu hivi akaifikia karatasi ya Baraza la Mawaziri. Ukombozi alichukua kalamu nyekundu kutoka ndani ya kijitabu cha katiba, akaanza kuweka alama x chini ya picha kadhaa, akabakiza moja. Karibu na karatasi hiihii kulikuwa na karatasi nyingine iliyokuwa na picha za Wabunge. Alikazana pia kuweka alama x chini ya picha hizi, hakubakiza hata moja…

Msomaji anaweza kushangaa kidogo kuona kuwa kazi ya namna hii ilichapishwa katika gazeti lisomwalo na mamilioni ya wananchi, na hili huweza kumhakikishia kuwa uhuru wa mwandishi upo mwingi mno Tanzania. Lakini sivyo ilivyokuwa. Baada ya sehemu mbili za mwanzo ambazo zilichapwa vizuri sana, na ambazo zilijaribu kuchora taswira iliyozoeleka ya upotofu na uongozi mbaya, sehemu ya tatu ya hadithi hiyo ambamo ndani yake mlikuwa na aya tuliyoidondoa, ilichapwa vibaya mno, aya zikachanganywachan ganywa ovyo na sentensi zikatupwatupwa huku na kule hadi ikawa vigumu kabisa kuupata ujumbe uliokusudiwa na mwandishi. Jambo hili, nionavyo mimi, lilionyesha udhibiti uliopitishiwa mlango wa nyuma. Dola haijali sana upotofu unapofichuliwa kwani wananchi wamekwishauzoea; lakini jawabu la upotofu huo linapopendekezwa, hasa kama ni la maangamizi ambayo wanakabidhiwa vijana wayafanye ili kuitakasa jamii, rungu la mdhibiti huinuliwa.
Aina nyingine ya udhibiti ambao unatokea ni ule unaohusu vitabu vya kiada vinavyotumiwa katika shule na vyuo vya elimu. Huu unao utata uleule wa vigezo vinavyotumika katika uteuzi wa vitabu hivyo. Kutokana na aina ya vitabu iliyozoweleka kuonekana katika mihtasari ya taasisi mbalimbali za elimu nchini, dalili zipo za kuwa maafisa wa elimu pamoja na kamati ya uteuzi wa vitabu hupendelea vile vinavyoimba nyimbo za ujamaa na kujitegemea zaidi ya vile vinavyochambua kiundani na hata wakati mwingine kuyakemea maovu yaliyopo katika jamii. Huu nao, basi, ni udhibiti wa aina yake ambao hatuna budi kuupatia nafasi katika mjadala wa uhuru wa mwandishi katika Tanzania
***
Si rahisi kuziorodhesha athari za udhibiti wa maandishi kwa waandishi wa vitabu vya fasihi Tanzania kwa kuwa, kama tulivyoonyesha, hakuna bodi au kamati maalumu ya udhibiH huo. Tuwezalo kubunia ni kuwa waandishi wenyewe wamekuwa na tabia ya udhibitinafsi wanapoandika kazi zao. Katika misingi hii tunaweza kueleza mabadiliko katika uandishi wa E. Kezilahabi ambaye katika Rosa Mistika alitumia mtindo wa kusema waziwazi bila kuficha, na katika kazi zake za hivi karibuni. labda kwa kujaribu kuukwepa udhibiti ulioikumba kazi yake ya mwanzo, kabadili mtindo, hasa katika riwaya zake fupi za Nagona (1987) na Mzingile.13 Katika riwaya hizo Kezilahabi anatumia visasili, taswira na ishara nzitonzito, maluwiluwi, ndoto na mbinu zingine za mficho wa kifani ijapokuwa kimsingi maudhui ya Rosa Mistika yanajitokeza humo pia.
Katika misingi hii hii tunaweza pia kusema kuwa udhibiti – nafsi umewafanya baadhi ya waandishi, mathalani Penina Muhando katika Hatia na Ndyanao Balisidya katika Shida(1975), waandike kazi nzuri sana ila zenye masuluhisho yanayoharibu uzuri huo. Cheja na Matika waamuapo kuwa jawabu la matatizo yao ni kurudi vijijini – jawabu ambalo huweza kuipotosha dhana nzima ya kijiji, hasa kijiji cha ujamaa, kuwa ni mlundikano wa wahuni, majambazi, wanyang’anyi na wote walioshindwa na maisha ya mjini – tunaliona jawabu hilo sawa na lile la ngonjera za Mnyampala zinazoibadili mioyo ya wasio wajamaa na kuifanya iwe ya kijamaa baada ya dakika tano za mjadala.
Hitimisho
Tuliyoyaeleza ni mawazo ya awali tu kuhusu suala la udhibiti na uhuru wa mwandishi wa vitabu Tanzania. Labda swali kubwa hapa ni, je, tuache udhibiti huu uendelee tu na kuwakubalia wanaimla waliokwisha kujitokeza waendelee na jukumu hili? Je, kuna haja ya kuwa na udhibiti wowote wa kazi za fasihi au tuwaachie wasomaji wenyewe waamue kuhusu lililo baya na lililo zuri kwao na kwa watoto wao? Iwapo ipo haja ya kuwa na udhibiti, udhibiti huo uwe wa aina gani, utumie vigezo na vipengele gani, na sifa gani zitumiwe katika uteuzi wa hao wadhibiti? Haya na mengine ya namna hii ni maswali muhimu kujibiwa ili isije ikatokea kama ilivyotokea miaka kadhaa nyuma, Bodi ya Ukaguzi wa Filamu Tanzania ilipoamua kuiondoa hotuba muhimu ya Mark Anthony kando ya maiti ya Juliasi Kaizari katika tamthilia ya Juliasi Kaizari ya Shakespeare!
Mwisho, labda jambo lingine ambalo tunaweza kulijadili ni sera ya vitabu ambayo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Utamaduni, Vijana na Michezo imeahidi kuitoa hivi karibuni: Je, sera hii iwe na nafasi gani katika suala zima la udhibiti na uhuru wa mwandishi wa vitabu Tanzania?
Tanbihi

1. Andiko la Plato la The Republic limekwisha kuchanishwa katika diwani nyingi, ikiwemo ya James Harry Smith na Edd Winfield Parks (wh.) (1967) The Great Critics: An Anthology of Literary Criticism, Norton, New York, uk. 6-24.

2. Kutoka katika O.B. Hardison, Jr. (1962), Modern Continental Literary Criticism. Appleton-Century-Crofts- New York uk 120
3. Nyerere (1968) Uhuru na Maendeleo, Government Printer. Dar es Salaam.
4. V.I. Lenin aliyasema haya katika insha yake ndefu, The State (1967), yakarudiwa na J.K. Nyerere katika baadhi ya hotuba zake.
5. Kwa maelezo zaidi kuhusu tapo hili na mengine ya fasihi za Ughaibuni na pia yale ya fasihi ya Kiswahili angalia F.E.M.K. Senkoro (1987).
6. k.h.j., Sura ya 1.
7. Kuhusu udhibiti uliofanywa na dini ni vizuri kusoma, kati ya vitabu vingi vinginevyo, James Hastings n.w. (wh.) (1910), hasa kur. 301 – 306; pia Juzuu la VII, Edinburgh: T. na T. Clark, 1914, hasa kurasa za 207 – 209.
8. Kitabu hiki kilichapishwa na Heinemann, London, 1982, na kutolewa kwa Kiingereza kwa jina la I Will Marry When I Want.
9. K. Marx na F. Engels (1967) Progress Publishers, Moscow.
10. Haya ni maneno ya Madjalany (1963) mwenyewe ambaye alisema: “Vita vya Mau Mau vilianza wakati Masetla wa kwanza wa kizungu walipowasili nchini kwa nia njema ya kupandikiza mwenendo wa maisha na mawazo mazuri ya kistaarabu kwa kundi la watu washenzi waliokuwa wakiishi maisha ya kishenzi yakaribiayo yale ya nyakati za kale za mawe…”
11. Hasa vile vya My Dear Bottle, After 4:30 na Troubles vilivyotolewa na Comb Book, Nairobi, miaka ya 1973, 1973 na 1974 kwa mfuatano.
12. Mangua (1972 East African Publishing House, Nairobi, pamoja na (1971) Son of Woman, East African Publishing House, Nairobi.
13. Kitatolewa na Educational Services Centre.
Bibliografia Teule
Arnold, S.H. (1976) “Film ni Tanzania – Part One: “Literary and Ideological Aspects” Umma, Vol. 6 No. 1, 21-55.
Balisiaya, Ndyanao (1975) Shida. Foundation Books, Nairobi.
Bgoya, Walter (1974) “Uhuru wa Mwandishi,” katika Zinduko 18-20
Cahn, Edomsond N. (1952) Social Meaning of Legal Concepts: An Annual Conference Conducted by New York University School of Law in Association with the Division of General Education. New York University School of Law, N.Y.
Frank, John Paul (1966) Obscenity, the Law and the English Teacher: Two Papers. Champaign. III., National Council of Teachers of English, Champaign – III.
Haight, Anne Lyon (1955) Banned Books: Informal Notes on Some Books BannedFor Various Reasons at Various Timesin Various Places. Allen and Unwin, London.
Hardison Jr., O.B. (1962) Modern Continental Literary’Criticism. Appleton, N.Y.
Hart, Harold H. (1971) Censorship: For and Against. Hart Pub. Co., N.Y.
Hastings, James N.W; (wh.) (1910) Encyclopaedia of Religion and Ethics. Vol. III, na Vol. VII, (1974), T and T. Clark, Edinburgh.
Hewitt, Cecil Rolph. (1969) Books in the Dock. Deutsch, London.
Hussein, Ebrahim N. (1978) “Ngugi: Ugumu wa Ukweli Anaousema,” Zinduko 3, 32 – 36.
Jennison, Peter S. (1963) Freedom To Read. Public Affairs Committee, New York.
Kandoro, S.A. (1974) “Uhuru wa Mwandishi,” Zinduko, 32 – 35.
Kezilahabi E. (1971) Rosa Mistika. EALB, Nairobi/Kampala/Dar es Salaam. (1987) Nagona. Educational Services Centre, Dar es Salaam. Mzingile. Kitatolewa na Educational Services Centre, Dar es Salaam.
Lenin, V.I. (1967) The State. Progress Publishers, Moscow.
Marx, Karl. (1962) “Ueber die neueste Preussische zensurinstruktion,” katika O.B. Hardison Jr, uk. 119-120.
Matteru, Bibi (1974) “Uhuru wa Mwandishi”, Zinduko, uk. 23-31.
Muhando, P. (1968) Hatia. East African Publishing House Nairobi.
Nyerere, J.K. (1968) Uhuru na Maendeleo. Govemment Printer, Dar es Salaam.
Plato (1967) The Republic, katika James Harry Smith na Edd Winfield Parks, (wh.), The Great Critics: An Anthology of Literary Criticism. Norton, N.Y. kur. 6-24.
Ringel, William E. (1970) Obscenity Law Today. Jamaica, Gould Publications, N.Y.
Senkoro, F.E.M.K. (1987) Fasihi na Jamii. Press and Publicity Centre, Dar es Salaam.
Smith, James Harry na Edd Winfield Parks, (wh.) (1967) The Great Critics: An Anthology of Literary Criticism. Norton, N.Y.
Soyinka, Wole (1970) The Man Died. Collins, London.
Swayze, Harold (1967) Political Control of Literature in the USSR: 1946-1959. Harvard University Press, Cambridge.
wa Thiong’o, Ngugi (Author) Detained: A Writer’s Prison Diary. Heinemann, London. (1983) The Barrel of the Pen. Africa World Press, Princeton, N.J.    ENDELEA HAPA>>>>>
Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!