FASIHI, UANDISHI NA UCHAPISHAJI (5)

By , in Kavazi on .
SEHEMU YA PILI: UANDISHI

4. Kiungo Dhaifu kati ya Mwandishi na Jamii*

C.S.L. Chachage
I
Mwito wa semina iwahusishao waandishi, wahakiki, wachapishaji, wachapaji, wauzaji vitabu, n.k., ni mwito wa kutafakari na kujifunza kutokana na historia ya majaribio yaliyofanywa nchini na kwingineko ya uendelezaji wa uandishi na usomaji. Mwito huu ni dalili wazi ya utambuzi wa umuhimu wa uandishi katika jamii zetu. Katika makala haya, mada ya “mwandishi na jamii” imefasiriwa kama uhusiano kati ya uandishi na usomaji. Hili ndilo suala litakalojadiliwa kwa ujumla, na mkazo utakuwa katika kujadili suala la wachapishaji na wauzaji vitabu kama kiungo kati ya uandishi na usomaji.
Sisi waandishi, wahakiki, wachapishaji, n.k., hatuishi nje ya dunia hii. Kwa hiyo swali la awali kuliko yote ni: kwa nini tunaandika? Ni dhahiri kwamba tunaandika ili kuwasiliana na kushirikiana na binadamu wenzetu. Tuandikapo, tunalaani yale yahuzunishayo na kuwashirikisha binadamu wengine katika yale yatufurahishayo. Nia ni kuufikia ukweli fulani katika jumuia zetu ambao umejificha katika njozi ya maisha mema – njozi ambayo mwanadamu amekuwa akiishi nayo tangu kuzuka kwake. Waandishi wengi pamoja na wachapishaji hudai, tena hadharani, kwamba tunautumikia umma wa watu wengi; kwamba tunaandika au tunachapisha kwa ajili ya watu tujinasibishao nao katika sudi zao njema na mikosi yao – wale wenye njaa. wakosao usingizi, kina Masalakulangwa wapiganao na manunda wala watu, na wanyonge kwa ujumla. Lakini wengi wa watu hao hawajui kusoma na kuandika. Hapa nchini kwetu, kwa mfano, asilimia 85 ya watu wanajua kusoma, idadi hasa ya wasomi ni asilimia 35. Hawa ni watu ambao wana tabia ya kusoma vitabu wakati wote. Kati ya hawa, karibu asilimia 2 wanajihusisha katika kusoma vitabu vya viwango mbalimbali. Hawa ni watu ambao wako katika vyuo vikuu vya mafunzo” (Ali 1987:2). Na ukweli ni kwamba, asilimia kubwa ya watu walio katika takwimu za wanaojua kusoma wamesharudia katika hali ya kutojua kusoma – karibu asilimia 65 au zaidi ya hiyo (Kamugisha 1987:10).
Waandishi wengi tunaandika dhidi ya upweke utukumbao sisi wenyewe binafsi, kadhalika na watu wengine. Kimsingi imani ni kwamba fasihi hutawanya maarifa, na kwa hiyo huathiri lugha na tabia za wasomaji. Fasihi inatufanya tuzitambue nafsi zetu kama jumuia. Hivyo basi, awali ya yote, ya msingi kuzingatia ni masuala muhimu ya kihistoria, mahitaji ya kiutamaduni na hatua tuliyopo kijamii na kisiasa katika uandishi, uhakiki, uchapishaji, n.k. Labda tulichunguze suala hili kwanza.
Tunaishi chini ya anga la dunia hiikama waandishi, wahakiki, wachapishaji, n.k. Ajali na neema yetu ni kuishi katika bara lililojaa mazonge na madhila tele – Afrika. Tunaishi katika enzi ambayo mataifa makubwa na mashirika yao yanatoa kanuni za maisha kwa dunia nzima, na mbinu mpya za mahusiano zimebuniwa ambazo zimeyaimarisha zaidi mahusiano tuliyoyakataa miaka ya 1960. Mbinu hizo zimejitokeza katika sura mbalimbaliza wazi kabisa na zilizojigubika Uafrika, au hata usoshalisti wa rangi mbalimbali. Hizi ni enzi ambapo tumeshuhudia kuanguka kitakotako kwa majaribio ya ujenzi wa jamii zenye ubinadamu, haki na ukomavu wa kiuchumi; majaribio yaliyofanywa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa kwa kisingizio cha kulinda umoja wa taifa.
Hizi ni enzi za matatizo makubwa ya kiuchumi; enzi ambazo matatizo ya jamii za kitabaka ni maradufu katika nchi zetu kuliko yalivyo katika nchi zilizokomaa kibepari. Tunu ya nchi yetu ni umaskini wa kukithiri wakati asilimia 6 ya wakazi wa dunia inatafuna pasi kificho wala aibu karibu utajiri wote uzalishwao na dunia nzima. Na jabari liwatenganishalo akina Shailoki na akina Lazaro linazidi kukua Kama mgomba, huku mbinu za kulikomaza zaidi zikiimarishwa kila siku. Katika baadhi ya nchi za Kiafrika, ule umahiri wa jadi wa wanasiasa wa udanganyifu, ulaghai, ulimi mwepesi, cheko za fisi, n.k., haufui dafu tena; haupo kabisa na unaonekana ni wa kishenzi. Badala yake, mabavu ndiyo yatumikayo na “watemi wa kisasa” kuidumisha hii mifumo isiyoisha kuwalaza watu matumpo matupu. Na ukweli ni kwamba, mifumo hii ya nchi nyingi za Kiafrika haiwezi kuiinusum bila kutumia mabavu ya aina hii au ile. Uhuru wa biashara tuusikiao ukiimbwa kila uchao maana yake kihalisi ni kuongeza matatizo ya kiuchumi na kupunguza na kufutilia mbali uhuru na uwezo wa watu kujiamulia mambo yao, kwa visingizio vya ukosefu wa fedha za kigeni, huku fedha hizohizo zikosekanazo zikitumika kukuza na kuimarisha teknolojia ya kutishia watu ili kuua hisia zao na uwezo wao wa kufikiri.
Sisi sote tumeshuhudia kupotea kwa njozi za kujenga ulimwengu wa jumuia huru na ufalme wa haki; ulimwengu ulioukana mfumo usababishao njaa. Badala yake wimbo tuusikiao katika vyombo vya habori na mikutanoni ni: “Matatizo yaikumbayo Afrika.” Mnamo mwaka 1984 ilitangazwa kwamba zaidi ya watu milioni 150 walikuwa na matatizo makubwa ya njaa, utapiamlo na ukosefu mkubwa wa maji safi (UN 1984:5). Si hivyo tu, kumekuwa na ongezeko kubwa la uhasama ndani na miongoni mwa nchi za Kiafrika badi kufikia vita (k.m. Chad, Libya, Zaire, Sudan, Ethiopia, Uganda, Angola, n.k.). Kila mtu anaweweseka: Nini kimeisibu Afrika? Vipi mtu anaweza kuelewa bara hili? Vipi mabadiliko yanaweza kutokea? Kwa nini Afrika inakwenda kombo?
Katika hali ya mazonge kama hayo, kukosa mawasiliano ni sawa na kujichimbia kaburi. Fasihi, katika historia ya binadamu, imekuwa njia mojawapo muhimu sana katika mawasiliano. Mwandishi aandikapo anawasiliana. Na ndiyo sababu Sheikh Shabaan bin Robert (1966a:31) enzi zake aliimba:
Wajibu upasao, wimbo nakujulisha
Kuwa nataka leo, mbali kukusafirisha
Kwa watu wakupendao, uishi mapya maisha
Na kwa wakuchukiao, ubora wako fundisha.
Wawezeshao urushaji wa “wimbo” ni wachapishaji na wauzaji vitabu. Si rahisi kuzungumzia uhusiano wa mwandishi/fasihi na jamii katika enzi hizi bila kuwataja hao ambao ni daraja au kiungo cha nitu hivyo viwili. Kwa bahati mbaya, wachapishaji wamekuwa dhaifu, na natuna budi kuwachambua. Hapa, nia ni kukosoana na wala si kulaumiana.
II
Kilio cha wachapishaji na wauza vitabu nchini na Afrika kwa ujumla kimehusu tatizo la akosefu wa soko na ukosefu wa wasomaji. Katika mikutano ya wachapishaji iliyofanyika Ife, Nigeria (1973); Accra, Ghana (1968); Arusha (1984); na Dar es Salaam (1987) Tanzania, wachapishaji wamekuwa wakidai kwamba kati ya matatizo makubwa Afrika ni kutokuwepo kwa tabia ya usomaji miongoni mwa watu. Imekuwa ikidaiwa kwamba Waafrika wanasoma kwa mahitaji maalum kama vile kupata shahada ili kupata kazi au kupanda cheo. Kadhalika, imekuwa ikidaiwa kwamba mazingira ya Kiafrika ni kikwazo kikubwa cha ukuaji wa tabia za usomaji kutokana na kutawaliwa na utamaduni wa fasihi simulizi, uhaba wa mapato ya kifedha, na matatizo ya kutojua lugha zitumikazo katika fasihi – andishi (Development Dialogue 1984 (1-2); Oluwasanmi, n.w., 1975).
Madai kama hayo hayatofautiani kabisa’ na madai yaliyotolewa na Wazungu enzi za ukoloni kuhusu Waafrika, isipokuwa wayatoayo sasa ni Waafrika wenzetu – ambao huenda wanaishi katika mazingira tofauti, wanazifahamu lugha zitumikazo katika fasihi – andishi, na kadhalika hawana uhaba wa vipato. Kabla hatujajadili zaidi suala hili, itakuwa bora kama tutajikumbusha kwa kifupi historia ya uchapishaji na usomaji nchini.
Uchapishaji kwa ajili ya wasomaji wa jumla wa Kiafrika hapa nchini, ulianza kuzingatiwa na serikali ya kikoloni baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Hili lilisababishwa na madai ya Waafrika ya elimu na maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia. Kutokana na vuguvugu hilo, Erica Fiah, na chama chake cha wafanya biashara, alikuwa ameanzisha gazeti la kwanza huru la Waafrika mnamo mwaka 1937 ambalo likiitwa Kwetu. Sheikh Shaaban bin Robert (1966b) alilalamika sana kuhusu unyonyaji wa wachapishaji, walivyopoteza au kukataa miswada yake, na hatimaye alifanya majaribio ya kuanzisha ushirika wa kuchapisha – Tanga Art and Literature. Kilio cha Sheikh Shaaban bin Robert kilikuwa: “Mwandishi si mtu wa ajabu awezaye kuishi kwa kula hewa na kunywa ukungu. Ni mtu wa desturi ambaye, kama watu wengine wa desturi hafarijiwi na hasara.” (Shaaban Robert 1966b:82).
Vuguvugu la Waafrika lilifanya Ofisi ya Bwana Makoloni huko London kumtuma Bibi E. Huxley kuja Afrika Mashariki mwaka 1945, kutazama hali ya uchapishaji na usambazaji vitabu, na kutoa maoni. Matokeo yake yakawa kuanzishwa kwa East African Literature Bureau mwaka 1947. Shughuli za uchapishaji zilipamba moto zaidi nchini miaka ya 1950 kutokana na uvamizi wa mashirika ya uchapishaji ya kimataifa yaliyoigundua fursa iliyokuwa imejitokeza kutokana na mabadiliko ya kisiasa yaliyobashiri ushindi wa Waafrika wakati wowote ule.
Hata hivyo, hali haikuwa imebadilika sana. Kwa kifupi, uchapishaji wa vitabu vya wasomaji wa jumla enzi za ukoloni – kama tukitoa mashirika ya kidini – ulifanywa na mashirika ya watu binafsi. Kenya ilikuwa na mashirika hayo mengi zaidi kuliko nchi zingine za Afrika Mashariki kutokana na uchumi wake wa kisetla, maana wasomaji wengi walikuwa masetla na maofisa wa kikoloni. Kulikuwa na wachapishaji 18 Afrika Mashariki waliojitokeza nyakati tofautitofauti kati ya mwaka 1899 na 1940 (Mulokozi 1983: 131).
Kufikia mwaka 1945 kulikuwa na wafanyakazi 75 tu waliokuwa wameajiriwa katika mitambo ya uchapaji (Coulson 1982: 72). Kufikia miaka ya 1950 uchapishaji wa vitabu ulifanywa na Wamishenari au mashirika ya nje kama vile Sheldom Press, Longman, Oxford University Press, Nelson, Witwatersrand University Press na MacMillan & Co. Wengi wa wachapishaji hawa walishughulikia vitabu vya mashule, ambavyo kiitikadi vilionyesha utukufu wa Mzungu na kumdhalilisha Mwafrika. Hivi ni pamoja na tafsiri kama, Mashimo ya Mfalme Suleiman, Allan Quartermain, Kisiwa Chenye Hazina, Roblnson Kruso, n.k. Kadhalika yalichapishwa masimulizi ya Waarabu na fasihi simulizi iliyorandana kimaudhui na tafsiri zilizotajwa.
Kama ilivyokwishagusiwa, miaka ya 1950 ilishuhudia kupanuka kwa shughuli za uchapishaji kutokana na uvamizi wa mashirika ya kuhodhi.ya nje. Madai ya Waafrika yalibainisha kinagaubaga kwamba kungekuwa na upanuzi mkubwa wa sekta ya elimu. Mashirika hayo yalifungua ofisi au hata matawi hapa nchini, na baadhi yake – kama MacMillan – yaliweza hata kuingia katika mikataba na serikali baada ya uhuru.
Imeshadhihirishwa na baadhi ya wataalamu kwamba Watanganyika walikuwa na ari kubwa sana ya kusoma na kujiendeleza baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Japokuwa asilimia ya wasiojua kusoma Dar es Salaam ilikuwa 59 kwa wanaume na 88 kwa wanawake mwishoni mwa miaka ya 1950, ari ya kupata habari ilikuwa kubwa sana. Kwa kawaida, machapisho ya serikali hayakuaminika kwa watu katika miaka hiyo, kwani mara kwa mara yalitumika kwa ajili ya propaganda, na fani yale ilikuwa si ya kupendeza kwa wasomaji. Watu wengi wenye mwamko walisoma magazeti kama Sauti ya TANU, Zuhra na Mwafrika (Scotton 1978:11). Watu wengi wajuao kusoma na hata wale wasiojua walipenda kupata habari. Wasiojua kusoma walikuwa wakiyanunua magazeti hayo, au fasmi nyingine waliyoithamini, na kuwaomba wanaojua kusoma wawasomee.
La kushangaza ni kwamba, mara tu baada ya uhuru, ilianza kudaiwa kwamba kumekosekana tabia ya usomaji miongoni mwa Watanzania! Kipindi ambacho madai hayo yanatokea, pia ni kipindi kilichoshuhudia upoteaji wa magazeti na majarida, moja baada ya jingine, ambayo yalikuwa yakichapishwa kitaifa na kiwilaya kwa Kiswahili na lugha za kienyeji. Fikra hii ya kudhania kuwa hakuna tabia ya usomaji inatokana na mtazamo wa kiitikadi wa viongozi wa mapambano ya uhuru ambao unaakisi mahusiano halisi ya kijamii. Wakati wa kugombea uhuru, viongozi wa mapambano wasomi na wakwasi wa Kiafrika ndio hasa waliotaka ongezeko la elimu na ujenzi wa uchumi na teknolojia ya kisasa. Ijapokuwa mapambano dhidi ya ukoloni yalifanikiwa kwa sababu ya uasi wa wafanyakazi na wakulima, imedhihirishwa na baadhi ya wanahistoria kwamba hawa viongozi hawakukubaliana kwa kila hali na matakwa ya Umma; ilikuwa ni katika mambo fulanifulani tu. Kilichowaunganisha ni dai la uhuru tu.
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, L. Cliffe alijaribu kuonyesha kuwa palikuwa na uhusiano kati ya kuzuka kwa madai ya uhuru ya viongozi waliodai usawa wa mataifa yote, maendeleo katika elimu na uchumi, na madai ya wakulima waliopambana na mifumo ya mabavu ya ubadilishaji wa mitindo ya kilimo na ufugaji Uluguru, Meru, Usambara, Iringa, Usukuma, Uzaramo, n.k. Mnamo miaka ya 1970, Cliffe huyohuyo alilipinga dai hilo: ushahidi wa kihistoria ulidhihirisha kwamba labda viongozi wa harakati za uhuru walikuwa na matakwa tofauti na yale ya umma wa wafanyakazi na wakulima. Kufuatana na Cliffe, vipi mtazamo wa viongozi, hata baada ya Azimio la Arusha, uwaone watu wa vijijini pamoja na wafugaji kama Wamasai kuwa ni watu waliotawaliwa na ukale na wasiopenda mabadiliko? Haikuyumkinika vipi msimamo huu uwe sahihi (Cliffe 1972:23).
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitatu (1961 – 64) uliotayarishwa na Benki ya Dunia na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (1964 – 1969) ilitawaliwa na maoni kwamba wakulima ni watu walio nyuma kimaendeleo, wapendao ukate, wasiopenda mabadiliko, wajinga na kwa ujumla duni (k.h.j: 161). Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulisisitiza suala la kuwabadili watu wenye kushikilia ukale wenye madhara ili kuleta maendeleo. Ilidaiwa kwamba kulikuwa na haja wakulima wabadilishe fikra zao na kama hawakufanya hivyo ilibidi walazimishwe.
Ikumbukwe kwamba hata Wazungu walikuwa na mtazamo kama huo kuhusu Waafrika – kwamba ni washenzi, waabuduo ukale, wasiopenda mabadiliko, wajinga, washirikina, wavivu, n.k. Ustaarabu, kufuatana na walivyouelewa wao, ulimaanisha watu kubadili fikra zao na kuchukua zile za “kisasa”. Viongozi wa mapambano ya uhuru, inavyoelekea, waliyatumia kwa shabaha zao wenyewe mapambano ya wakulima na wafanyakazi, japo walikuwa na tofauti nao. Kulikuwa na nyakati ambapo viongozi hao waliyakana mapambano ya watu wa kawaida. Hivyo ndivyo ilivyotokea Usambara, Usukuma, na Iringa. Mambo haya yalijitokeza wazi baada ya ushindi wa uchunguzi wa mwaka 1958/59. Wasukuma walidaiwa na viongozi kuchukulia mambo kistaarabu; kadhalika wafanyakazi wa Mwadui, Posta, Reli, Mkonge, n.k., hawakuungwa mkono na viongozi wa siasa kama ilivyokuwa awali kabla ya uchaguzi. Viongozi walidai kwamba kilichokuwa muhimu baada ya uhuru ni mapambano dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi. Vita dhidi ya maadui hawa vilihitaji umoja na siyo utengano katika jamii.
Ukweli ni kwamba mtazamo wa Kizungu ndio uliohusisha ujinga na umaskini. Imani kwamba umaskini unatokana na ujinga ni tafsiri ya Kizungu ya tatizo ambalo misingi yake imo katika mahusiano yaliyopo (Fuglesang 1984 (1 – 2):45). Hata Azimio la Arusha halikuubadili msimamo huo wa “usasa”. Hili linajitokeza wazi katika mahusiano halisi ya kijamii, na humo ndimo inabidi tuchunguze ili kuulewa mwelekeo wa masuala ya elimu, uandishi, uchapishaji, uuzaji vitabu na usomaji hapa nchini baada ya uhuru.
III
Ni kweli kwamba nchi yetu ina njaa ya vitabu Hili linakubalika na watu wengi hata wale wanaolalamika kwamba hakuna tabia za usomaii. Mashule na vyuo ndiyo masoko yategemewayo na mashirika mengi ya uchapishaji na maduka ya vitabu. Kutokana na “matatizo ya kiuchumi” hata hayo masoko yameshindwa kununua vitabu, japo kihitajikacho si fedha za kigeni, na kodi ya maendeleo inalipwa na wananchi. Hii ndiyo sababu ambayo imefanya mashirika mengi ya kigeni kuhama na kubakiza ofisi ndogondogo nchini, ambazo kazi yake ni kuvizia kile ambacho Wizara ya Elimu inaweza ikazipa zifanye.
Tangu tupate uhuru, mashirika ya uchapishaji na maduka ya vitabu yameshughulika zaidi na vitabu vya mashule na masomo kwa ujumla katika ngazi mbalimbali kama njia pekee na rahisi kuishi. Hadi mwishoni mwa miaka ya 1970, kwa mfano, Meneja Mkuu wa Tanzania Publishing House aliamini kwamba soko kubwa la vitabu ni Wizara ya Elimu, hasa shule za msingi (Bgoya 1978:4). Ni hali hii iliyomfanya Topan (1971:30) kufikia uamuzi kwamba ielekeavyo, uchapishaji wa fasihi ya Kiswahili daima umeamuliwa na mahitaji ya shule. Mara nyingi wachapishaji wamesita kuchapisha fasihi ambayo haiwezi kuingizwa katika shule kama kitabu cha kiada au ziada kwa kuwa shdle ndilo soko kubwa.
Wachapishaji hawakuitegemea sekta ya elimu ili kupata riziki tu, bali pia walitaka kujihusisha na mahitaji ya kisiasa na kiuchumi. Kwani mbali na vitabu vya shule, vitabu vingine vilikuwa vya kufundisha watu kutumia maksai, jinsi ya kufanya mikutano vijijini, n.k., au vita kama Fimbo ya Mnyonge ambavyo ni propaganda tupu.
Wachapishaji na wauza vitabu wamekuwa wakifanya shughuli zao kwa kuzingatia malengo ya kisiasa. Nao wamekuwa wakishiriki katika kuleta “usasa”. Na ni kutokana na hali hiyo, ndiyo sababu wakaishia kutegemea masoko ya kiasasi ambayo pia yalirahisisha biashara. Mashirika ya nje nayo yaliishi maisha ya namna hiyo, yakichapisha asilimia kubwa ya vitabu vya taaluma, pamoja na vile vilivyoandikwa na Watanzania. Imekadiriwa kwamba katika nchi za Kiafrika zilizotawaliwa na Mwingereza, asilimia 80 hadi 95 ya vitabu vilivyochapishwa ni kwa ajili ya shule (Fedin 1984: 100). Hata mgogoro kati ya mashirika ya uchapishaji ya nchini na mashirika ya nchi za nje ambao umekuwepo kwa muda mrefu umekuwa ni ugomvi wa kung’ang’ania soko – Wizara ya Elimu – wala si ugomvi wa mashindano ya kuimarisha na kuinua hali ya jamii kitamaduni.
Wachapishaji na wauza vitabu wametawaliwa na imani ionayo kwamba elimu ni chombo cha kuleta ‘maendeleo’. Kutokana na imani hii, kumekuwa na kutozingatia kabisa mahitaji ya ujumla ya kiutamaduni ya wasomaji wa kawaida; badala yake kumekuwako kuzingatia mahitaji ya kisasa na kiasasi. Kutokana na hali hii, imebidi ama wasomaji wa kawaida wavumilie kusoma hivyo vitabu vya elimu na kujiendeleza, au wasisome kabisa. “Tatizo la msingi la shughuli za uchapishaji ni ukosefu wa soko,” aliandika Meneja Mkuu wa Tanzania Publishing House mwaka 1978. Aliendelea:

Kimsingi, kitabu ni kitu kitumikacho na watu ambao wamefikia ngazi fulaniya elimu na utamaduni. Kama uchapishaji kwa ajili ya mashule utaondolewa, wachapisbaji watabakia na watu wachache sana wanaorahamu thamani ya vitabu na ambao wana uwezo wa kifedha wa kuvinunua. Kwa sababu watu wengi nchini hawajui kusoma, au wanajua kidogo, soko la vitabu kimsingi ni mashule na vyuo, ndio watumiali wakubwa wa vitabu na ndio sababu wachapishaji wanazielekeza programu zao kwenye mahitaji ya asasi za umma. (Bgoya m.y.k.: 2. Tafsiri na mkazo ni wangu).

Haikuishia hapo. Aliendelea: kwa sababu ya uwezo mdogo wa kusoma; kwa sababu utamaduni wa wakulima ni wa fasihi simulizi na siyo fasihi – andishi (kutokuwepo tabia za usomaji), na kwa sababu uchumi wao ni wa kujipatia riziki tu – hauruhusu mtu kubaki na akiba ya fedha wala kupata tamaa ya kununua vitabu; ndiyo maana wachapishaji wamekuwa wakitegemea asasi za elimu (k.h.j.: 4).
Kwa ufupi, hii ndiyo athari ya imani za “usasa” miongoni mwa wachapishaji na wauza vitabu. Hata waandishi wengi wameingia katika mtego huo. Matokeo yake katika miaka ya 1960-70 kumefurika fasihi ya Kiswahili yenye mfumo wa vitabu vya shule na vyuo kimaudhui na kifani. Wachapishaji walisita kuchapisha kazi ambazo hazina manufaa madarasani (Topan m.y.k.). Labdajambo lililokuwa baya zaidi ambalo liliuimarisha mtindo huu wa uchapishaji ni upigwaji marufuku wa vitabu kama vile Rosa Mistika (E. Kezihabi), Jando na Unyango (S.A. Mamuya), n.k. Ni jambo la kusikitisha sana kuona nchi haina hata fasihi ya watoto.
Haikusudiwi ieleweke kwamba wachapishaji wameendelea na mtindo huo bila kubadilika, la hasha! Kufikia mwaka 1984, Meneja Mkuu wa TPH alifikia uamuzi kwamba TPH imeweza kuishi miaka yote hii kwa sababu tu ya wasomaji wa jumla, wa kawaida, wafanyakazi na wakulima (Bgoya 1984: (1-2): 90-1). Huu utambuzi ulifanyika baada ya kupat» uzoefu, kutokana na kushindwa kuiuzia vitabu Wizara ya Elimu, na majaribio ya kufanya maonyesho ya vitabu Sokoni Kariakoo, Bukoba na Zanzibar (k.h.j). Katika maonyesho hayo iligundulika kwamba wakulima na wafanyalcazi ndilo soko kubwa la vitabu na wala siyo wasomi ambao hawasomi vitabu baada ya kutwaa vyeti. Kadhalika, iligundnlika kwamba vitabu vya upelelezi na mapenzi ambavyo vinauzwa sana mitaani sivyo vipendwavyo hasa; vinavyopendwa ni vile vmavyoainisha mahitaji ya kitamaduni ya watu wenyewe, k.m., Kuli, Njozi Iliyopotea na hata Kamusi ya Wanyama.
Ukweli ni kwamba kuna tatizo kubwa la kutathmini wingi wa vitabu viuzwayo au vichapishwavyo. Kwa kawaida mambo hayo wachapishaji huyafanya siri, isipokuwa pale watangazapo vitabu ili vinunuliwe. Usemi kama “toleo la tano”, n.k., hauna maana yoyote, kwani hautoi idadi na nakala zilizochapwa. Au maneno kama “msomaji yeyote mwenye akili hatokosa kukisoma kitabu hiki!” yawekwayo jaladani, hayana maana yoyote. Msemo huo hutolewa kuvutia wasomaji. Lakini mchapishaji wa vitabu ajikosoapo na kukiri kile ambacho hakutilia maanani awali, yabidi tuamini akisemacho. Bila shaka huo msimamo wa TPH wa miaka ya 1980 una ukweli mkubwa.
Kinachojidhihirisha hapa lu ukweli kwamba kutegemea asasi mbalimbali kama masoko, badala ya kutafiti na kuchunguzi matakwa ya kijamii ya kitamaduni, ni jambo ambalo linaweza kuua kabisa fasihi na uandishi. Kisingizio kilichotumika siku zote ni elimu, maendeleo na ‘usasa’. Na sote tumeshuhudia hiyo elimu ikizidi kuanguka mwaka hadi mwaka, na ‘maendeleo’ kutufikisha katika matatizo ya kiuchumi, huku ‘usasa’ ukitufanya tuwadharau na kuwakashifu watu wa kawaida. Hata maduka ya vitabu yamekataa au kushindwa kabisa kusambaza vitabu ambavyo si vya shule na masomo ya kujiendeleza. Kwao hili limerahisisha uuzaji. Matokeo yake ni uvamizi wa kinduli katika shughuli za vitabu wa watu ambao hawana mapenzi na utamaduni au hata vitabu, wale ambao nia yao ni kupata utajiri wa harakaharaka. Mashirika ya uchapishaji na wauza vitabu wamekuwa wakifanya shughuli zao kama watoto wa sbule wasiokubali kusoma au kufanya chochote ambacho hakitatokea kwenye mtihani. Lakini maisha si shule wala madarasa tu (Oduyoye 1975:215) na ndiyo sababu binadamu haishi kwa mkate tu.
Uchapishaji na utawanyaji vitabu ni shughuli tofauti na utengenezaji na uuzaji wa sukari au dawa ya meno. Unahitaji maarifa, na ujuzi, badala ya kusingizia kwamba “watu hawasomi” na kuazima kisisisi msamiati wa kikoloni kisha kuwapachika watu wa kawaida. Vitabu si shughuli ya watu wenye papara ya kupata faida, ni kazi ya watu wenye uwezo wa kuzingatia kithabiti suala la mawasiliano miongoni mwa watu. Kuna haja ya kutafiti historia ya maandishi hapa nchini, ukuaji wake, matatizo ya wasomaji, fani za maandishi mbalimbali, na kujua zipi zinazowapedeza wasomaji.
Katika semina ya walimu wa historia mwaka 1983, kuna maswali yaliyoulizwa ambayo nadhani ni muhimu hata waandishi, wahakiki, na wachapishaji wajiulize. Hayo ni: kiasi gani cha maarifa tumekwishasambaza miongoni mwa umma mkubwa wa watu tudaio hadharani kwamba tunautumikia? Hayo maarifa ni ufafanuzi, mkusanyiko na matengenezo ya utaratibu wa mawazo ‘yaliyotawanyika’ ya umma wa Waafrika? Je, tunafikiria kwamba asilimia 75 ya Waafrika walio chini ya miaka 25 ndio hasa waundaji wa historia ya Afrika na siyo mtaji wa ndani na nje? Je, ufafanuzi wa hayo maarifa unaainisha hali yakinifu za kijamii za harakati za watu katika mapambano yao ya kuyabadili mazingira na nafsi zao? Je, tumeshakoma kuwaona watu wa kawaida kuwa ni wajinga, au wasiojua chochote kuhusu sayansi? Na, je, tumekuwa wepesi wa kujifunza kwa unyenyekevu? (Wamba dia Wamba 1983: 1 – 2).
Haya maswali ni muhimu hata kwetu kwa sababu wengi wetu tunadai kwamba tunatumikia maslahi ya umma – “Naandika kwa ajili ya wananchi!” “Nachapisha kwa ajili ya umma!” “Nawauzia vitabu wananchi!” n.k. Ukweli ni kwamba wakati utafika ambapo kila mmoja wetu atalazimika kuyajibu maswali hayo. Ni kwa kujiuliza maswali hayo ndipo tunaweza kukiimarisha kiungo hiki muhimu kati ya uandishi na jamii.
Bibliografia
Ali, Fatma Said (1987) “Hotuba ya Ufunguzi wa Semina Kuhusu Dhima ya Mchapishaji Iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii Utamaduni, Vijana na Michezo”, EAP, Dar es Salaam.
Bgoya, E. (1978) “Rationalization of the Publishing and Printing Industry”, Dar es Salaam. (1984) “Autonomous Publishing in Africa: The Present Situation”, katika Development Dialogue, 1 – 2.
Coulson, A. (1982) Tanzania: A Political Economy, Clarendon Press, Oxford.
Development Dialogue (1984) (1 – 2) Dag Hammarskjord Foundation, Uppsala.
Fuglesang, A. (1984) (1 – 2) “The Myth of Peoples’ Ignorance” katika Development Dialogue, k.h.j.
Hughes, B. (t.h.) “Library and Books Profile in Tanzania” Bntish Council Library Report, Dar es Salaam.
Kamugisha, T.A.R. (1987) “Developing Indigenous Publishing in Tanzania”, IFM, Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1983) “Maendeleo na Matatizo ya Uchapishaji wa Vitabu vya Kiswahili” katika Makala ya Semina Juzuu II. Uandishi na Uchapishaji, TUKI, Chuo Kikuu, Dar es Salaam.
Oduyoye, M. (1975) “The Role of Christian Publishing ni Africa Today” katika Oluwasanmi n.w. (Wh.) Publishing in in Africa in the Seventies.
Oluwasanmi, E., Maclean, E.E. & Zell, H. (1975) (Wh.) Publishing in Africa in the Seventies, University of Ife Press, Ife.
Robert, Shaaban (1966a) Pambo la Lugha, Oxford University Press, Nairobi.
Robert, Shaaban (1966b) Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, Nelson, Nairobi.
Scotton, J.F. (1978) “Tanganyika African Press (1937) – 1960)” katikay African Studies Review XVI: April 1978.
Topan, F. (1971) “Swahili Literature Plays Major Social Role” katika Africa Report Vol. 16, 2, February 1971.
UN Economic and Social Council Report (1984) “Critical Economic Situation in Africa”, Second Regular Session, April 1984.
Wamba dia Wamba, E. (1983) “History of Neo-Colonialism or Neo Colonialist History? Self Determination and History ni Africa,” Department of History, University of Dar es Salaam.    ENDELEA HAPA>>>>>>>
Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!