FAHAMU MAANA ZA MANENO HAYA

NENO MAANA ZAKE
1 Cheche

1. Kipande kidogo cha kitu kilicholengwa k.v. muhogo.

2. chembechembe za moto zinazoruka.

‘Cheche ya moto’

‘Cheche ya umeme’

3. samaki mwenye mwili wenye miba yenye sumu.

4. dhima inayochukuliwa na zaidi ya mtu mmoja.

2 Pakacha

1. kikapu kilichosukwa kwa makuti ya mnazi.

2. mtu mwongo.

3 Zinduna

1. mojawapo ya dawa kama sandarusi inayopatikana pwani.

Sandarusi >>>> utomvu wa msandarusi ambao hutumika kutengenezea gundi.

4 Ambari

1. kitu kama vile nta ngumu, kinachonukia, chenye rangi ya hudhurungi, kinachotokana na nyangumi baharini.

2. Huliwa ili kunenepesha na kuongeza nguvu.

 

5 Kustahi

1. Kuwekea heshima; wekea adabu.

2. jali, heshimu, tukuza

6 Ukuukuu

1. uzee wa kitu.

2. Uchakavu

7 Kugema

1. mteremko mkali, agh. katika kingo za mto.

2. chanja au kata tunda au magome ya mti ili kupata utomvu au maji.

8 Mung’unye 1. boga dogo, refu na jembamba lililo jeupe ndani na likikauka hutengenezwa kibuyu.
9 Mkwezi 1. mtu anayefanya kazi ya kupanda miti, agh. minazi, na kuangua nazi.
10 Chua

1. sugua kwa nguvu kwa mkono au kwa kitu kingine.

‘Chua miguu’

2. kanda au singa.

‘Chua mkono’

3. danganya mtu kwa maneno mazuri.

11 Aula

1. kazi au mipango inayopewa umuhimu wa kwanza kushughulikiwa.

2. kipaumbele

12 Panzi

1. mdudu wa jamii ya nzige, mwenye umbo refu, meno meusi mawili, mbawa nne na miguu sita na kati ya hiyo miwili ni mikubwa zaidi na hutumika kwa kurukia na kujihami.

2. samaki mdogo ambaye mapezi yake hutumika kama mbawa na humwezesha kuruka kutoka majini.

13 Ufito

1. kipande cha mti au chuma kirefu na chembamba ambacho hutumiwa kujengea nyumba.

2. ada inayotolewa na kupewa mwalimu wakati mwanafunzi anapoingia chuoni.

14 Nuksi 1. Nuhusi, ukuba, mkosi, ndegembaya, kisirani, kunusi, baa,feli
15 Uzushi

1. hali ya kuzua mambo.

2.maneno yasiyo ya kweli.

16 Tanga

1. kitambaa kikubwa kinachokingamishwa kwenye mlingoti wa chombo k.v. jahazi, kuteka upepo na kukiwezesha chombo kwenda.

2. mkusanyiko wa watu kwenye nyumba iliyofikwa na msiba ili kuomboleza na kuwaliwaza wafiwa kwa siku tatu au zaidi baada ya kuzika.

3. enda huku na huku.

17 Kimako 1. sauti ya mshangao au kustaajabu.
18 Sogi 1. mifuko miwili anayobebeshwa punda, mmoja kila upande, ambayo hutumiwa kubebea mizigo.
19 Tungi 1. chombo cha kioo chenye umbo la duara na uwazi chini na juu kinachotumiwa katika taa k.v. ya karabai au kandili.
20 Mwanga

1. mtu afanyaye mazingaombwe ya uchawi usiku.

2. mtu anayetembea usiku badala ya kulala.

3. nuru ya k.v. mchana, taa au jua.

21 Kochi 1. Kiti kirefu chenye springi au sponji ambacho kina sehemu ya kuegemea na kuwekea mikono.
22  Chane, kichane

1. shada moja la mkungu wa ndizi; kifungu cha ndizi kutoka katika mkungu.

2. nunu za ukindu au miyaa baada ya kuchanwa ili zisukwe ukili.

23 Lele 1. uimbaji wa kuanzia ngoma; nyimbo za kuchangamshachangamsha kabla ya ngoma kuanza.
24 Mwapiza

1. ombea mtu maovu.

2. laani, duia

25 Mrama

kwa upandeupande; kwa msepetuko; isivyo.

‘Chombo kinakwenda mrama’

26 Twambe

1. Sema, eleza, dhukuru, nena

2. Sengenya, teta

 

27 Harabu

1. mtu mharibu.

2. kitu kiharibifu.

28 Mwigo

1. tendo la kufuatisha jambo lililofanywa na mwingine.

2. namna ya uigaji.

3.  aina ya njiwa mkubwa anayedhaniwa kuwa anaweza kutabiri juu ya matokeo ya safari.

29 Mkungu

1. mti unaozaa kungu ambazo ndani ya kokwa zake mna badamu.

2. sehemu ya mgomba yenye ndizi.

3. chombo cha udongo kinachofanana na bakuli.

4. mfuniko wa chungu uliotengenezwa kwa udongo.

30 Tabibu

1. Mtu mwenye ujuzi wa kutibu.

2. Mganga, daktari

31 Kundule Hutumiwa kumaanisha sehemu ya nyuma ya nyani ambayo huwa haioni na hivyo huwacheka wenzake.
32 Jihadi · Kidini
1. tendo la Mwislamu kufanya juhudi na kujitolea kwa nafsi yake au mali yake katika kutimiza amri za Mungu na kuzieneza.2. vita wanavyopigana Waislamu kutetea dini yao.
33 Urimbo/ulimbo ·utomvu mzito unaonata kama wa mfenesi, agh. hutumiwa kutegea ndege au nzi.
34 Pwagu ·mtu anayejulikana kuwa anatumia hila na nguvu katika kudanganya wenziwe ili apate mahitaji yake.
35 Pwaguzi

mwizi wa daraja ya juu kuliko pwagu.

‘Leo pwagu na pwaguzi wamekutana’

36 Simbiko tendo la kusimbika.
37 Simbika funga au tatiza uzi kwenye shina la ndoana ili iweze kuunganishwa na mshipi.
38 Kata

1. pitisha kitu chenye makali k.v. kisu au makasi kwenye kitu ili kukigawanya katika visehemu.

‘Kata kitambaa’

2. ondoa sehemu ya kitu; tenga sehemu katika kitu; kata mkono; kata tawi; kata mshahara.

39 Tonga

1. tunda la jamii ya bungo lakini kubwa kidogo, lenye ganda gumu la rangi ya njano iliyofifia.

2. ukubwa wa nazi au dafu.

40 Tuwi ·Kimiminika kitokanacho na nazi kitumiwacho kupikia kama mafuta
41 Mbazi ·ni hadithi fupi yenye mafunzo na itolewayo kama kielelezo wakati wa kumkanya au kumwelekeza mtu
42 Mashuzi ·hewa itokayo kwa nguvu kwenye tupu ya nyuma.
43 Aanguaye huanguliwa ·hii ni methali itumiwayo kuonesha kuwa kila atendaye jambo baya kwa mwingine naye hupatwana jambo kama hilo
44 Nduwari ·samaki mwenye mwiro mrefu unaotangulia mdomo wake.
45 Jitihada ·bidii, juhudi, idili, hima, kasi
46 Kudura ·nguvu au uwezo wa Mungu, majaaliwa
47 Kuchamba

1. osha utupu baada ya kwenda chooni.

2. toa maneno mabaya.

3. tukana, shambulia, tusi, sibabi, subu

48 Mchongoma ·mti wenye miba na majani madogo madogo, agh. hupandwa kuwa ni uzio au mpaka wa shamba.
49 Usambe ·Usiseme
50 Kutu

utando mwekundu unaotokea juu ya chuma kikipata maji.

‘Chuma kimepata/kimeshika kutu’

51 Kuvunda

1. kuwa katika hali ya kuchachuka hadi kufikia kiasi cha kutoa ukungu.

2. toa harufu mbaya ya kuoza.

52 Rubani mtu anayeendesha na kuongoza chombo k.v. ndege.
53 Mkoma

1. mti jamii ya mkoche.

2. mtu mwenye ugonjwa wa ukoma.

3. Mchawi au muuaji; mtu anayegandamiza watu.

54 Sanda

1. nguo nyepesi, agh. nyeupe, anayovishwa maiti na kuzikwa nayo.

2. fedha anazotoa mtu kumpa jamaa yake mfiwa ili kumsaidia katika gharama za mazishi.

55 Rambirambi

salamu za kuonyesha masikitiko kwa maafa yaliyomfika mtu.

‘Peleka rambirambi’

56 Maafuu mtu anayestahiki kusamehewa makosa anayofanya kwa sababu ya hali yake k.v. mwendawazimu au mgonjwa.
57 Fahali/Mafahali

1. ng’ombe dume; dume la mnyama.

2. mtu shujaa.

3. -enye nguvu.

58 Ukingoni

·panapoishia kitu.

·Visawe;

·ubigoubigo, chambochambo, mleoleo, ombe

59 Mbiu

1. pembe ya mnyama itumikayo kuwaita watu au kama ala ya kuchezea ngoma.

2. sauti itokayo kwenye pembe.

3. wito.

60 Mgambo ·mkutano, agh. unaozungumzia mambo ya busara au ya wazee.
61 Mchakacho ·sauti ya majani makavu inayotokea wakati k.v. yanapokanyagwa.
62 Mpemba ·aina ya muhogo ambao ni laini na huiva kwa haraka.
63 Kauri

·gome la konokono mdogo wa baharini ambalo hutumika katika uganga na kwenye mapambo, na zamani zilitumika kama fedha.

·-visawe

·simbi, kete, dondo

64 Mvunguni ·sehemu wazi iliyo chini ya kitu k.v. kitanda au meza.
65 Unda

1. fanyiza, tengeneza au jenga, hasa kitu cha mbao au chuma.

2. Pakua asali kutoka katika mzinga wa nyuki.

66 Kuneni ·Usemaji wa jambo fulani
67 Nundu

1. sehemu ya mnyama k.v. ng’ombe au ngamia iliyotokeza mgongoni.

2. mnyama mdogo kama panya arukaye, anayekula matunda na wadudu, mwenye tabia ya kujificha mahali penye gizagiza mchana na huonekana usiku.

68 Chambo

1. kitu, agh. mdudu, nyama, n.k. kinachowekwa katika ndoana au mtego ili samaki au wanyama wakile na wanaswe.

2. kitu au mtu anayefanywa kuwa ndiye sababu au njia ya kupatia haja.

69 Nyenzo

vifaa vya kufanyia shughuli fulani.

‘Nishati ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya binadamu’

70 Mtumi

1. mtawala wa kijadi.

2. mtu mwenye nguvu na hodari kwa kupiga wenziwe.

71 Kunga ·mambo ya siri ambayo hayafai kusikika ovyoovyo.
72 Changa

1. toa kitu au fedha ili kukusanya kwa makusudi fulani.

‘Changa fedha’

2. changanya karata.

3. umwa viungoni au mishipani kama mgonjwa wa baridi yabisi.

4. -siokomaa k.v. tunda.

‘Embe changa’

5. -siopevuka.

‘Mimba changa’

‘Mtoto mchanga’

73 Vumbika ·funika au fukia matunda katika vumbi, majani au udongo kwa muda fulani ili yapate kuiva.
74 Asili

1. mwanzo wa mtu au kitu.

2. tabia ya mtu aliyozaliwa nayo

3. kiini cha jambo; kitu cha awali.

‘Mali ya asili’

75 Mtovu

mtu asiye na k.v. adabu.

‘Mtovu wa adabu’

76 Uzushi

1. hali ya kuzua mambo.

2. maneno yasiyo ya kweli.

 

S/N METHALI MAANA
1 Mwenye kelele hana neno. Mtu mwenye kelele na fujo nyingi huwa hana madhara
2 Mwenye kovu usidhani kapowa. ·        Kovu: alama ya kidonda au jeraha lililopona.

·        Mwenye alama ya kidonda kilichopoa usimfikirie kuwa ndiyo amepoa kabisa kabisa

3 Mwenye kubebwa hujikaza. ·        Kujikaza – vumilia, himili, stahimili, zinda

·        Kila mwenye kusaidiwa huonesha juhudi

4 Mwenye kuchinja hachelei kuchuna ·        Hachelei – haogopi

·        Kuchuna- kuondoa ngozi

·        Usitegemee huruma kwa aliyekutenda ubaya

5 Mwili wa mwenzio ni kando ya mwilio. ·        Maumivu ya mwenzio hayawezi kuwa sawia kwako
6 Mzazi haachi ujusi. ·        Mzazi hakosi kuwa na harufu ya uzazi (harufu anukayo mwanamke baada ya kujifungua)

·         Ujusi – 1. hali ya kutokuwa safi ambayo mwanamke huwa nayo, agh. kwa siku arubaini baada ya kujifungua.

·         2. harufu anukayo mwanamke baada ya kujifungua.

7 Mzigo Wa mwenzio ni kanda Ia usufi. ·        Mzigo wa mwenzio wauona mwepesi kama mfuko wa sufi

·        Usufi – uzi mweupe laini unaotokana na tunda la msufi.

8 Mzika pembe ndiye mzua pembe. ·        Mfichua siri siku zote huwa ni yule mwenye kuifahamu siri hiyo
9 Mzungu Wa kula hafundishwi mwana. ·        Mtoto huwa hafundishwi adabu ya kula, hujifunza kupitia jamii na makuzi yake.

·        Mzungu – mafundisho wapewayo wari jandoni au unyagoni.

10 Nahodha wengi, chombo huenda mrama. ·        ujuaji wa wengi huharibu jambo

·        mrama –

·        nahodha –

11 Natuone ndipo tuambe, kusikia Si kuona. ·        Tuone kwa macho yetu ndipo tuseme, kwani jambo la kusikia si la kushuhudia kwa macho
12 Nazi mbovu harabu ya nzima. ·        Nazi moja iliyo mbovu yaweza kuharibu nazi nzima zilizomo guniani

·        Harabu – mtu mharibu./ kitu kiharibifu.

13 Ndege mwigo hana mazowea. ·        Kuiga ya kigeni hupoteza asili ya mtu
14 Ndevu sio shani, hata beberu anazo. ·        Ndevu hazimpi mtu heshima kama hanayo

·        Shani – jambo au kitu kinachoshangaza na ambacho si kawaida yake kutukia.

15 Ndugu chungu, jirani mkungu. ·        Ndugu ni wa muhimu kuliko jirani, ndugu ni sawa na chungu na jirani ni mfuniko (mkungu)

·        Chungu – chombo kilichofinyangwa kwa udongo na kitumiwacho kwa kupikia.

·        Mkungu – mfuniko wa chungu uliotengenezwa kwa udongo.

16 Ndugu mui afadhali kuwa naye. ·        Ndugu ni bora hata akiwa muuaji

·        Mui – mwovu

17 Ngoma ya kitoto, haikeshi. ·        Jambo lisilo na maana halidumu

·        Ngoma – mchezo wa kufuata mdundo wa ala hiyo.

18 Ng’ombe haelemewi na nunduye. ·        Kila mtu hubeba mzigo anaoumudu, usione kalemewa hali amebeba mwenyewe

·        Nundu – sehemu ya mnyama k.v. ng’ombe au ngamia iliyotokeza mgongoni.

19 Nimekula asali udogoni, utamu ungali gegoni. ·        Mambo mazuri huacha kumbukumbu muda mrefu
20 Nimekupaka wanja, wewe wanipaka pilipili. ·        Umtendeaye mema aweza kukutendea ubaya
21 Nyumba usiyolala ndani huijui ila yake. ·        Mahali kama si pako huwezi kujua shida yake

·        Ila – shida,adha,madhila

22 Ondoa dari uwezeke paa ·        Fanya maamuzi magumu ili kujitoa kwenye aibu au shida fulani

·        Dari – sakafu ya juu ya nyumba, agh. iliyo juu ya ukuta wa nyumba lakini chini ya paa.

·        Paa – sehemu ya juu inayofunika nyumba.

23 Pele hupewa msi kucha. ·        Mtu asiyehitaji jambo ndiye hupewa
24 Pema usijapo pema; ukipema Si pema tena. ·        Mahali huwa salama kabla hujapafika
25 Penye urembo ndipo penye ulimbo. ·        Mvuto ndio unaonasa wengi

·        Ulimbo – utomvu mzito unaonata kama wa mfenesi, agh. hutumiwa kutegea ndege au nzi.

26 Pwagu hupata pwaguzi. ·        kila mbabe huwa ana mbabe wake

·        pwagu – mtu anayejulikana kuwa anatumia hila na nguvu katika kudanganya wenziwe ili apate mahitaji yake.

·        pwaguzi – mwizi wa daraja ya juu kuliko pwagu.

27 Sahani iliyofunikwa, kilichomo kimesitirika. ·        Thamani ya vitu ipo kwenye kutojua undani wake

·        Sitirika – ficha jambo au kitu cha aibu ili kisionekane; ficha aibu.

28 Sahau ni dawa ya Waja. ·        Kusahau humsaidia kila mja wa Mungu
29 Samaki mpinde angali mbichi. ·        Kosa hurekebishwa lingali dogo, likiwa kubwa huweza lisirekebishike
30 Msishukuru mja, hamshukuru Molawe. ·        Asiye na shukrani hashukuru kwa lolote
31 Msitukane wagema na ulevi ungalipo. ·        Tusiwadharau wale tunaowahitaji kutusaidia
32 Msitukane wakunga na uzazi ungalipo. ·        Tusiwadharau wale tunaowahitaji kutusaidia
33 Mstahimilivu hula mbivu. ·        Kila mwenye kuvumilia hakosi kufanikiwa
34 Mtaka cha mvunguni sharti ainame. ·        Ukitaka mafanikio lazima uwe tayari kuvumilia adha zote
35 Mtaka nyingi nasaba hupata mwingi msiba. ·        Mtu anayependa mambo makubwa hupatwa na madhara mengi

·        Nasaba – uhusiano wa kizazi baina ya watu; uhusiano kutoka katika mlango au ukoo mmoja.

36 Mtaka unda haneni. ·        Mwenye kujua jambo hasemi hufanya moja kwa moja

·        Unda – fanyiza, tengeneza au jenga, hasa kitu cha mbao au chuma.

·        pakua asali kutoka katika mzinga wa nyuki.

37 Mtaka uzuri hudhurika. ·        Ukitaka jambo zuri sharti ukubaliane na matokeo yake
38 Mtegemea nundu haachi kunona ·        Mtegemea tajiri au mjuzi fulani daima hakosi kufaidika
39 Mtego bila ya chambo, haunasi ·        Hutumika kuwatahadharisha watu ambao hukosa kujiandaa kabla ya kufanya jambo kwamba huenda wasifanikiwe.
40 Mteuzi heshi tamaa. ·        Mtu anayepata nafasi za upendeleo huwa haishi kutamani nafasi kubwa zaidi
41 Mti hauwendi ila kwa nyenzo. ·        Mafanikio huhitaji maarifa Zaidi na sio nguvu
42 Mtondoo haufi maji. ·        Mwenye uzoefu na kazi yake hawezi kuiogopa

·        Mtondoo – mti mkubwa ambao hutoa mbao zinazotumika kutengenezea madau na vyombo vingine vya uvuvi.

43 Mtu hakatai mwito, hukataa aitiwalo. ·        Unapoitwa tii japo utakaloelezwa si muafaka kwako
44 Mtumi wa kunga haambiwi maana. ·        Asiyefahamu umuhimu wa jambo haambiwi

·        Kunga – mambo ya siri ambayo hayafai kusikika ovyoovyo.

45 Mtumikie kafiri upate mradi wako. ·        Fanya sehemu yako ili maisha yako yasonge

·         Kafiri –

·         1. Kidini
mtu anayesema au kufanya jambo ambalo ni kinyume na mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

·         2. Kidini
mtu anayekanusha neema na maamrisho ya Mwenyezi Mungu au asiyetii sheria zake.

·         3. Kidini
mtu anayefuata dini isiyokuwa Uislamu.

·

46 Mtupa jongoo hutupa na mti wake. ·        Aliyekusahau husaua kila kitu chako

·        Jongoo – mdudu mweusi au wa kikahawia mwenye miguu mingi sana.

47 Muhitaji khanithi walau kana rijaali. ·        Mwenye shida hana hiyari

·         Hanithi –

·         1. mtu asiyesimika.

·         2. mtu mpumbavu.

·         3. mwanamke asiyepata hisi wakati wa kuingiliana.

 

·        Rijali – mwanamume mwenye nguvu za kiume.

48 Mungu si athumani ·        Mungu hatendi kama binadamu watakavyo
49 Muuza sanda, mauti kwake harusi. ·        Aliyezoea shida huziona za kawaida
50 Mvua nguo, huchutama. ·        Ukifanya ukagundua umekosea unapaswa kuwa mtulivu sio kulazimisha iwe

·        Chutama – chuchumaa

51 Mvumbika changa hula mbovu. ·        Asiyetia bidii hupata mafanikio haba
52 Mvumbika pevu hula mbivu na mvumbika changa hula mbovu. ·        Kila mtu huvuna kile akipandacho
53 Mvungu mkeka. ·        Ukiridhika kila kitu utakiona kiko sahihi
54 Mwacha asili ni mtumwa. ·        Asiyekubali asili yake huwa ni mtumwa wa asili ya wengine
55 Mwamba na wako hukutuma umwambiye. ·        Amsemaye mtu mbele yako anakutuma ukamwambie asemwaye

·        Mwamba – mtu mwenye nguvu na hutumia mabavu.

56 Mwamini Mungu si mtovu. ·        Mwenye kumwamini mungu hapungukiwi jambo
57 Mwana maji wa kwale kufa maji mazowea. ·        Kwa mzoefu kupata ajali ni jambo la kawaida
58 Mwana wa kuku hafunzwi kuchakura. ·        Shida ndiyo humfunza mtu kujitafutia maisha ya kujikimu

·        Kuchakura – tafuta kwa kupekuapekua vitu vya juu ili kupata kilicho chini.

59 Mwana wa mtu ni kizushi, akizuka, zuka naye. ·        Mtoto wa mwenzio si sawa na wako kaa naye kwa uangalifu

·        Kizushi – hali ya kuzua mambo.

60 Mwanga mpe mtoto kulea. ·        Mtu mbaya mkabidhi jambo jema alifanye
61 Mwanzo kokochi mwisho nazi. ·        Kila jambo huwa na chanzo chake
62 Mwanzo wa chanzo ni chane mbili. ·        Mwanzo wa jambo lolote huwa na alama yake
63 Mwanzo wa ngoma ni lele. ·        Kila jambo lina mwanzo wake

·        Lele – uimbaji wa kuanzia ngoma; nyimbo za kuchangamshachangamsha kabla ya ngoma kuanza.

64 Mwapiza la nje hupata la ndani. ·        Mwenye kulaani wengine hurudiwa na laana hiyo pia
65 Mwekaji kisasi haambiwi mwerevu. ·        Mwenye kulipiza kisasi si muungwana

·        Kisasi – nia au kusudio la kulipiza ubaya aliofanyiwa mtu.