DHANA ZA USHUJAA NA SHUJAA KATIKA NGANO ZA MOTIFU ZA SAFARI NA MSAKO

By , in Kavazi on .

Dhana za Ushujaa wa Shujaa kwa Jumla

Raglan (1979) ameelezea mikondo, namna na ruwaza
ishirini na mbili ambazo ushujaa wa shujaa hutokea kwa tamaduni zote za
ulimwengu. Kutokana na ruwaza ishirini na mbili zilizoelezwa na Raglan (1979)
na namna za ushujaa wa shujaa unavyojitokeza katika jamii na tamaduni
mbalimbali ulimwenguni. Utafiti huu umenufaika kwa kubaini nduni bainifu za
shujaa kwa jumla na nduni hizi zilizobainishwa na Raglan zilisaidia utafiti huu
kulinganisha na kulinganua sifa za shujaa wa Waikizu na mashujaa wengine.
Raglan (1979) anaonesha majina ya mashujaa kama
Yesu, Musa, Sunjata/Sundiata Simba-Mfalme wa Mali ya zamani, Mithradates VI wa
Pontus, Krishna, Romulus, Mfalme Arthur, Perseus, Watu Gunung wa Java,
Heracles, Mohammad, Beowulf, Buddha, Czar Nicholas II, Zeus, Nyikang, a
Cult-hero of the Shiluk tribe of the upper Nile, Achilles, Odysseus na Harry
Potter. Anaonesha mikondo na nduni za kila shujaa na namna za ushujaa wa
mashujaa hawa wote. Hapa, Raglan ameonesha kwa undani namna ambavyo sifa za
mashujaa hawa zinafanana kwa kiasi kikubwa, tofauti zao ni ndogo sana. Hii
ilisaidia utafiti huu kumbainisha shujaa wa Waikizu na mashujaa wa namna yake
katika utafiti huu.
Raglan (1979)
hakuishia hapo, ameonesha ushujaa wa mashujaa wanawake. Ameonesha sifa za
mashujaa wa kike na amebainisha sifa zao ambazo zinafanana na sifa za mashujaa
wanaume kama alivyozibainisha. Na amewataja baadhi ya mashujaa wa kike/wanawake
kama Leia/malikia Leah (nyota wa vita), Guinivere, Tori Amos, Cleopatra VII,
Merie de Medici, Penlope, Helen of Troy, Malikia Diana, Nefertiti 1, Nefetiti
2, Iren of Athens, Susan B. Antony, Hellen Killer, Harriet Tubman, Sacagawea,
Semiramis, Malkia wa Assyria, Antigone, Jane Addams, shujaa katika Shakespear
na Joan of Arc. Aidha Raglan anamueleza Joan of Arc kama shujaa, anasema
aliondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka kumi na tatu kwenda katika ufalme wa Ufaransa,
alikuwa askari, alikamatwa na Waingereza na kuuwawa, alifia kileleni mwa kilima
kidogo, mwili wake haukuzikwa. Aidha akimuelezea shujaa Cleopatra VII anasema,
Cleopatra alikuwa Malikia wa Kimacedonia aliyeongoza Alexandria. Anaeleza
kwamba Cleopatra kamwe hawezi kusahaulika kwa ushujaa wake. Hii ilisaidia
utafiti huu kubainisha kama jamii za Waikizu, Wabondei na Wazanzibari zina
mashujaa wa kike.
Utafiti huu
umenufaika sana na kazi ya Raglan kutokana na ukweli kwamba umemsaidia mtafiti
kubaini nduni bainifu za shujaa kwa jumla. Hata hivyo, utafiti wa Raglan ni wa
jumla sana na hausaidii kutatua tatizo lishughulikiwalo na utafiti huu, kwani
alijikita zaidi katika tamthiliya na hadithi kwa jumla. Aidha, Raglan
alishughulikia suala la ushujaa katika muktadha mpana zaidi wa kilimwengu.
Utafiti huu wa sasa ulifanywa kwa kuzingatia jamii mahsusi ili kuchunguza na
kubainisha nduni bainifu za ushujaa wa shujaa wa Waikizu, Wazanzibari na
Wabondei, kulinganisha na kulinganua ushujaa wa mashujaa hawa na kubainisha
sababu za tofauti za ushujaa wao. Aidha, utafiti huu umejikita katika utanzu wa
ngano hasa ngano za motifu za safari na msako kukidhi malengo ya utafiti huu.
Jambo ambalo halikugusiwa kabisa na Raglan, hakugusia ngano za motifu za safari
na msako.
Dundes (1965)
ameorothesha hadithi za Aeneas, Auther, Buddha, Romulus, Daudi, Scegfried,
Musa, Odysceus na Perseus, na ameelezea kaida na ruwaza ishirini na mbili za
shujaa. Anasema, kwa kawaida, maisha ya shujaa yeyote hujumuisha sifa nyingi,
lakini sio zote kati ya sifa zote ishiri na mbili za shujaa. Dundes
amelinganisha sifa hizi na maisha ya Yesu. Amebaini kwamba maisha ya Yesu
yamejumuisha takribani sifa ishirini na mbili zote za shujaa kwamba; mama yake
ni bikra toka familia ya kifalme, baba yake ni mfalme, baba yake na mama yake
wanauhusiano wa kinasaba, kuzaliwa kwake hakukuwa kwa kawaida (inasemekana mama
yake alibeba mimba kwa uwezo wa roho mtakatifu), inasemekana alikuwa mwana wa
Mungu, jaribio la kutaka kumuua shujaa huyu akiwa mtoto lilifanyika, alipaa
kwenda mbinguni, alipelekwa uhamishoni nchi ya mbali, hakuna tarifa
zinazofahamika kuhusu utoto wake, alirudi toka nchi ya uhamishoni, alimshinda
mfalme, alikuwa mfalme, alifundisha na kuacha sheria kwa waumini wake, alikufa
kifo kisicho cha kawaida, alipoteza hali yake ya utukufu, alifia kileleni
mlimani,  mlima Golgota, hakurithiwa na
mwanae, mwili wake haukuzikwa na makumbusho ya sehemu aliposulubiwa ililijengwa
kama kumbukumbu yake.
Johnson (2008)
na (2009) akieleza dhana ya shujaa na ushujaa ametoa mifano ya wanaume na
wanawake mashujaa kutoka kila kizazi, kazi na kutoka kila kona ya dunia kama
asemavyo mwenyewe, na anatoa rai kwa wale wanaodhani kwamba dunia hii haina
mashujaa kabisa waweze kusoma katika uga huu ili wapate maarifa. Anaonesha
mashujaa kuanzia kwa Alexander the Great na Julius Caesar mpaka kwa Churchill
na de Gaulle na wengine anaowaeleza ni pamoja na; Samsoni, Judith, Deborah,
Henry V, Joan of Arc, Elizabert I, Walter Raleigh, George Washington, the Duke
of Wellington, Lord Nelson, Emily Dickso, Abraham Lincoln, Robert E. Lee, Pope
John Paul II, Alexander, Julius Caesar, Thomas More, Lady Jane Grey, Malikia
Mary wa Scots, Charles de Gaullle na Margaret Thatcher.
Freser (1922) na
(1976) anaonesha suala la ushujaa na msigano uliopo katika suala la sihiri,
dini na sayansi. Anasema vina athari kubwa sana kisaikolojia, kifasihi na
kijamii katika akili ya mwanadamu. Na anasema, uhusiano uliopo baina ya dini na
sihiri kiimani vinafanana. Anazidi kueleza chanzo cha dini yenyewe ilivyo,
waweza kuwa na sababu za kuchunguza uhusiano wake na sihiri. Na anaeleza kuwa
dini na sihiri vyote vimejijenga katika dhana ya utoaji kafara, anaonesha
mifano ya nchi kama Misri ya kale, India ya kale, Ugiriki na Italia ni nchi
ambazo ziliamini miujiza na kafara, na anasema wafalme wa zamani walikuwa pia
makuhani. Anasema, katika jamii za zamani muda wote wafalme walikuwa ni watu wa
miujiza/sihiri na pia walikuwa makuhani, kwa mfano mfalme wa Madagascar alikuwa
kuhani. Anasisitiza kwamba miujiza/sihiri ni sanaa, sio sayansi.
Bowra (1964)
anaonekana kutomtambua shujaa wa kiafrika wala uwepo wa tendi za kiafrika. Hii
ni kutokana na mtazamo wake kwamba, sihiri/uchawi ni maudhi na si ushujaa.
Anaendelea kufafanua kuwa, tendi simulizi ziwekazo msisitizo mkubwa katika
nguvu za kisihiri haziwezi kufasiliwa kama tendi za kishujaa, kwa sababu badala
ya kutumia sifa halisi pamoja na vipaji alivyonavyo binadamu, zinatumia uwezo
usiokuwa wa kibinadamu. Pia anadai kuwa, katika tendi za kiafrika mashujaa hawatumii
nguvu zao za asili na vipaji vyao walivyojaliwa kutatua matatizo na kutekeleza
majukumu mbalimbali ya kijamii, badala yake wanategemea sana nguvu za
kichawi/sihiri kiasi kwamba wanapoteza uhuru wa kufanya mambo kwa matakwa yao
kwa sababu wamekuwa watiifu kwa nguvu za kichawi ambazo si nguvu za shujaa wa
tendi. Katika kusisita hilo, anaona kwamba tendi za kishujaa zinapaswa kuwa na
mtazamo wa kimagharibi kwa kuwa zinamchora binadamu halisi pamoja na sifa zake
asilia kama vile nguvu, ujasiri, ustahimilivu na uwezo wa kuamua. Mtaalamu huyu
anaonekana kubeza mashujaa wa tendi za kiafrika kwa kusema kwamba, katika tendi
za kiafrika shujaa wa kweli ni yule mwenye uwezo wa kutumia nguvu zisizo za
kibinadamu tu katika kufanya matendo yasiyo ya kawaida.
Finnegan (1970)
katika utafiti wake kuhusu tendi za kiafrika anaathiriwa sana na mawazo ya
kimagharibi kuhusu shujaa wa tendi anavyopaswa kuwa. Anataka shujaa wa Ulaya
afanane na shujaa wa Afrika, kitu ambacho hakiwezekani kutokana na tofauti za
kijiografia, kiutamaduni, kihistoria na hata kiteknolojia. Hivyo, mtazamo wa
Finnegan na Bowra kuhusu kutokuwepo kwa shujaa wa tendi za kiafrika hauna
mashiko hata kidogo, kwani huu ni mtazamo finyu na wenye mawazo mgando.
Tofauti na
wataalam tuliowaona, Ayivor (1997) anakiri kwamba, nguvu za sihiri kwa shujaa
ndizo zinazozipa upekee wa kishujaa tendi za kiafrika. Hivyo, huyu anakiri
kwamba, Afrika ina mashujaa wa tendi ambao ni tofauti na mashujaa wa tendi za
Ulaya.
Idowu (1973)
kama alivyorejelewa na Deme (2007) anaona kwamba mashujaa wa kiafrika hutumia
nguvu za kichawi na za majini katika kukabiliana na matatizo mbalimbali katika
jamii zao. Anasema, Sundiata amefaulu kushinda nguvu za kichawi za Kita Mansa
kutokana na msaada wa jini, vinginevyo asingeweza kushinda guvu za kichawi za
Kita Mansa.
Seydou (1983)
katika makala yake alichunguza tendi za kiafrika, Afrika ya magharibi na Afrika
ya kati. Akang’amua kwamba, katika Afrika kuna tendi simulizi ambazo
hutofautiana sana na tendi andishi kwani zenyewe hutumia ala za muziki n.k.
Vilevile aliona kuwa, kazi nyingi za waandishi wa tendi za kiafrika
wameziegemeza katika historia na visasili. Pia anatambua uwepo wa shujaa wa
tendi za kiafrika na anaona kuwa, matendo ya shujaa na uwezo alionao ni
kielelezo cha sifa binafsi na nguvu zake za kichawi humsaidia na huzitumia
katika matukio maalum.
Mulokozi (1999)
anasema, kutokutambulika kwa tendi za kiafrika kulikosisitizwa na Finnegan,
Knappert na wenzake kuliwatia hamasa watafiti wengi wa kiafrika katika
kuchunguza tendi za makabila yao kwa lengo la kupinga madai ya wanazuoni wa
kimagharibi. Matokeo ya utafiti wao kuhusu shujaa wa tendi za kiafrika,
walisema; shujaa wa tendi za kiafrika kwa kawaida huwa na sifa zifuatazo;
Nguvu: nguvu za kimwili (yaani ubabe na mabavu); nguvu za kiume na kidume,
yaani urijali; nguvu za kiakili; nguvu za kivita; Uganga au nguvu za sihiri; na
Mshikamano na kundi au jumuiya fulani inayomuunga mkono. Aidha Mulokozi
anamrejelea na kueleza kwa kina kuhusu shujaa Fumo Liyongo na Yesu/Emanuel na
kuonesha sifa zao, ufanano wao na tofauti za mashujaa hawa wawili. Alionesha
taswira ya vifo vya mashujaa hawa, anasema dhana ya usaliti imejitokeza sana
katika kazi za kifasihi na inaonekana ni silaha ya kumwangusha shujaa kwa
mfano; Lwanda Magere, Samsoni, Yesu na Fumo Liyongo. Anasema dhana hii ya usaliti ina sura mbili, yaani
faida na hasara. Faida, ni anayenufaika baada ya usaliti na hasara ni
anayeathirika baada ya usaliti. Anabainisha kwamba, kifo cha shujaa pamoja na
usaliti vinatupatia motifu ya dhambi na motifu ya mapatilizo. Pia, akionesha
tofauti za mashujaa hawa anasema shujaa Yesu baada ya kufa alifufuka, alipaa
kwenda mbinguni, hakuoa, aliponya wagonjwa kwa nguvu za roho mtakatifu sifa
ambazo zinamtofautisha kabisa shujaa Yesu na mashujaa wengine. Shujaa Fumo
Liyongo baada ya kufa hakufufuka, hakupaa kwenda mbinguni, alioa mke na alikuwa
na mtoto wa kiume, alitumia nguvu za sihiri, ana nguvu za kirijali, hadhuriki
kwa chochote isipokuwa kudungwa sindano ya shaba kitovuni, aliishi Pate na Ozi
pwani ya kaskazini mwa Kenya kwenye karne ya 14 au kabla. Katika kufanana kwa
mashujaa hawa anasema, wote walisalitiwa na watu wao wa karibu.
Mulokozi (1996) ameeleza kuwa, mashujaa wa utendi
wa Kiswahili ni wa aina tatu; moja ni mashujaa wa kijadi wa kiafrika kwa mfano,
Fumo Liyongo katika utendi wa Fumo Liyongo (Mohamed Kijumwa, 1913) na Abushiri
bin Salim katika utendi wa vita vya Wadachi kutamalaki Mrima (Hemed Abdallah K,
1895), pili ni mashujaa wa kidini, hasa mtume Muhamadi na maswahaba wake, kama
Ras ‘Ighuli, na tatu ni mashujaa wa kubuni kwa mfano, Tajiri katika Utendi wa Masahibu. Mulokozi pia
ameeleza kuhusu shujaa Emanuel katika Biblia akihusishwa na shujaa wa
kihistoria na wa kijadi. Mwanamalundi pia ni shujaa wa kijadi.
Okpewho (1979) kama alivyorejelewa na Deme (2007)
anasema kwamba, uchawi/sihiri humfanya shujaa asishindwe na maadui wake.
Anatumia utendi wa Sundiata katika
kuthibitisha hilo kwamba, shujaa Sundiata alimshinda Soumaoro kutokana na ama
nguvu za kichawi ama kwa ushiriki baina ya nguvu zake na nguvu za kishirikina.
Akiendelea kueleza dhana ya ushujaa, Okpewho anasema, shujaa anaondoka
nyumbani, anakwenda kutafuta kitu fulani, anakipata, na kuishia kumuoa malikia
na kuwa mfalme. Hii ni moja ya sehemu kubwa na ya hakika ya ruwaza na sifa za
shujaa.
Kunene (1971), akionesha dhana ya ushujaa na
shujaa wa Kiafrika kwa kuirejelea jamii ya Wasotho anasema, jamii ilitamani
ubora wa mashujaa wao wa kitamaduni kama mfano kwao. Hii namna ya kuelezea
tabia, huu mchakato uko katika jamii za kiafrika kwa mfano katika jamii ya
Wasotho, kama Kunene alivyothibitisha. Kwa mifano, watu ambao wako tayari
kupoteza uhai wao kuliko kupoteza heshima yao. Katika maisha ya Wasotho katika
namna zote za mazingira hatarishi na yenye wanyama wengi wakali, kama vile
simba, imani ya jamii ya Wasotho inatia hamasa na kutamanisha watu ambao sio tu
wawe na jitihada bali pia wawe na nguvu na kuwa kitu kimoja kwa manufaa na
mustakabali wa taifa lao. Anaendelea kueleza kuwa, kama ilivyodhihirika wazi
katika ushairi wa Wasotho, tamaduni za mababu zao walivyo hatarisha maisha yao
na uhai wao hata kufa, muda mwingine haikuwa ni kwa sababu tu inawezekana,
lakini ilikuwa ni kwa matakwa yao kujipatia heshima wao wenyewe na kwa jamii
yao.
William (1986), anaeleza usuli wa Son-Jara kwamba
Sundiata ni shujaa wa kiutamaduni wa makabila ya Afrika Magharibi hasa yale
yenye kuzungumza lugha ya Kimande: Wa-Bambara, Wa-Khasonke, Wa-Susu, Wa-Jula,
Wa-Wangara, Wa-soninka, Wa-Mandika na Wa-Mandenke. Watu hawa huishi katika
nchi za Gambia, Ghana, Guinea-Conakry, Ivory Coast, Liberia, Mali, Mauritania,
Niger, Senegal, Siera Leone, na Upper Volta. Tendi na mazira ya Sundiata
hupatikana katika nchi hizo. Hivyo huyu ni shujaa muhimu wa kimataifa; Wanahistoria wanamchukulia ni mwanzilishi
wa himaya ya Mali. Hivyo, anaonesha utendi wa Son-Jara ni utendi wa kihistoria
unaohusu maisha yake kabla na baada ya kuzaliwa na vikwazo anavyopitia hadi
kutawala kwake. Baba yake Fatta Magan alikuwa mtawala wa mali. Alitabiriwa
atamuoa mke wa pili mwenye sura mbaya aitwaye Suguluni Konde, naye atamzalia
mtoto wa kiume atakayekuwa mtawala mrithi wake. Wake zake wote wanapata ujauzito
na wanajifungua siku moja.
Dankaran Tuman na Sun-Jara wanazaliwa na hapo
ndipo matatizo yanaanzia baada ya Son-Jara kutambuliwa na baba yake ndiye
mzaliwa wa kwanza na atakuwa mrithi wake. Taarifa iliyomsononesha Suman Berete
mama yake Dankaran, hivyo aliomba kwa miungu hali iliyosababisha Son-Jara
asitembee kwa miaka tisa. Son-Jara anatembea kwa msaada wa jini na kafara. Baada
ya Fatta Magan kufariki Dankaran na mama yake wanatumia uchawi ili Dankaran awe
mrithi wa baba yake. Hali iliyoleta mgogoro na kusababisha Son-Jara na mama
yake kuondoka Manden na kwenda kukaa uhamishoni, Mema kwa muda wa miaka saba.
Hapa wanasema; ‘‘kukaa hakutatui tatizo
kusafiri kunatatua tatizo’’
  Son-Jara
akiwa uhamishoni, Sumamuru alipambana na Dankaran na kumshinda hivyo, Sumamuru
akatawala himaya ya Manden. Son-Jara anapata taarifa hii na kuamua kurudi
Manden na kupambana na Sumamuru ila alishindwa. Kushindwa kwa Son-Jara
kulisababisha dada yake Sugulun Kulunkan kumsaidia kwa kufanya hila ya kuolewa
na Sumamuru ili ajue siri ya nguvu zake; alibaini iko kwenye nyumba yake.
Matokeo ya hila hiyo ni kufanikiwa kujua siri. Alimpa kaka yake na kumwezesha
kumshinda adui yake. Hapa imebainika dhana ya ujenzi wa motifu za safari na
msako imejitokeza, dhana ya sihiri na usaliti na dhana ya vikwazo kwa shujaa na
kuvishinda vikwazo hivyo.
Mbogo, (2011), katika Sundiata ametumia mtindo wa
Kiaristotle ambapo shujaa huishia katika anguko. Sundiata wa tamthiliya
hii hapewi nafasi kufurahia ushindi wake. Shangwe za ushindi zinageuka kuwa
maombolezo ya kifo chake. Sundiata- kadhulumiwa urithi wake; anapoupata tu
anapoteza maisha yake! Tunabaki tukijiuliza: Je, kwa nini mtunzi kamuua
Sundiata? Labda anataka kututahadharisha kuhusu ubatili wa ulimwengu. Kama
hivyo ndivyo mtunzi atakuwa ametuingiza katika falsafa ya Al-Inkishafi kuwa
raha na furaha za ulimwengu ni ghururi na ghiliba tupu. Au pengine mtunzi anataka tu kutoa ujumbe ulio dhahiri kwa ma­Sundiata
wa enzi zetu: Ma- “Baba wa Taifa,” ma ‘‘mama wa Taifa,’’ ma ‘‘Bibi wa
Taifa,’’ ma ‘‘Babu wa Taifa,’’ma- “Rais wa Maisha,” ma- “Amiri
Jeshi Wakuu,” kwamba vituko vyao ni mbio za sakafuni tu ambazo zitaishia
ukingoni?
Hallet (1970) Jackson
(1970) Levtzion (1985) Niane (1965) wanasema kuwa, Sundiata wa historia
alipigana, akashinda, akaasisi himaya ya Mali na kuitawala kwa miaka mingi
(kama 1230 – 1255 BK), na kuleta amani na ustawi. Sundiata wa tendi vilevile
alifanikiwa kushika madaraka na utawala baada ya kumshinda Sumaoro (Sumanguru
/Sumamuru), mfalme wa Susu. Yeye pia aliishi na kuyafaidi matunda ya juhudi
yake, akatawala kwa haki na hekima na kuiendeleza nchi yake. Hawa ni mashujaa
wenye sifa moja kuu; Sifa ya kuwa Waasisi au Waanzilishi. Hawa ni waanzilishi
wa mfumo na mtindo mpya wa maisha ya jamii na pengine ni waasisi wa mataifa
mapya na dola mpya ambazo hazikuwapo kabla. Kiulimwengu, tunaweza
kuwalinganisha na watu kama Vainamoinen/Mwanamwini (Finland), Mfalme Arthur
(Uingereza), Buddha (India), Yesu Kristo, Mtume Muhamadi, Musa (Uyahudi),
Napoleon (Ufaransa), Martin Luther (Udachi), Chaka (Afrika Kusini), V. I. Lenin
(Urusi), na Mao Tse­Tung (China). Hawa ni watu ambao maisha na matendo yao
yaliubadilisha mwelekeo wa jamii zao na wa ulimwengu kwa jumla.
Aidha, Tamthiliya na
Tendi zingine zinazomhusu Sundiata hazisawiri Sundiata wa historia, bali
Sundiata wa kisanaa na kimapokeo. Huyu ni Sundiata ambaye maisha yake
yamerembwa ili kukidhi haja za ruwaza (pattern)
fulani, itikadi, na mtazamo fulani kuhusu maisha. Ni shujaa wa kiutendi kama
walivyo Liyongo, Yesu, Seyyidna Ali, Roland (Ufaransa), Akile (Uyunani), Musa,
Ozidi (Wa-Ijaw wa Nigeria) na mashujaa wengine wa tendi mashuhuri duniani.
(Hallet, 1970 ; Jackson, 1970; Levtzion, 1985; Niane, 1965).
Mbele (2006) akionesha nafasi ya wanawake katika
tendi za Kiafrika, anaonesha mchango mkubwa wa wahusika wanawake katika tendi
za kiafrika hasa katika dhana ya ushujaa lakini wasomi wameshindwa kuonesha na
kutambua ushujaa wao; wameweka msisitizo na kumtazama zaidi shujaa mwanaume kwa
jicho pevu na kumsahau mwanamke na kufanya dhana ya ushujaa kuonekana katika
mtazamo dume. Hivyo Mbele anaona kuna haja kuangalia dhana ya ushujaa wa
mwanamke kwa kuchunguza sanaa jadiya kwa kuangalia kwamba hata tendi zina
uhusiano na  utanzu huu wa ngano.
Njozi (1998), akionesha ushujaa wa Yesu anasema,
alitenda miujiza ambayo hakuna awaye yeyote amewahi kuitenda kama kutembea juu
ya maji, kutuliza mawimbi, kuponya vipofu, kufufua wafu kwa kutamka tu.
Historia inaonesha Afrika imekuwa na mashujaa
mbalimbali tangu zama za kale na hata kipindi cha wakoloni. Baadhi ya mashujaa
wa Afrika na wa kihistoria ni pamoja na Dedan Kimath Waciuri (Kenya), Chaka
Zuru, Stive Bike, Nelson Mandela/Madiba (Afrika Kusini), Mkwavinyika/Mkwawa,
Nyerere (Tanzania) Nkwame Nkurumah (Ghana), Patric Lumumba (Kongo). Ushujaa wao
hubainika kutokana na matendo waliyofanya kwa jamii zao katika kutatua matatizo
yao.
Aidha, Kirikuu ni utendi ulioandikwa na Michael
Ocelot mwaka 1998. Utendi huu unatokana na simulizi za kijadi za watu wa Afrika
Magharibi, zijulikanazo kama hadithi za kingano. Lengo la mtunzi huyu ni kuleta
mabadiliko ya kifikra miongoni mwa wanajamii kama mila na imani potofu.
Wanakijiji wote waliamini kwamba, matatizo yote ya kijiji chao yanatokana na
uchawi wa mwanamama Karaba. Kirikuu anayaona matatizo hayo hata kabla
hajazaliwa. Tatizo kubwa linalomkabili Kirikuu na jamii yake ni uhaba wa maji.
Kirikuu anang’amua chanzo cha tatizo na anafanikiwa kutatua tatizo hilo kwa
kuliuwa dubwana lililokuwa linazuia maji. Tatizo jingine aliloling’amua Kirikuu
ni uonevu uliokithiri katika kijiji chao. Mchawi Karaba kwa kutumia nguvu zake
za kichawi anawateka watoto, lakini Kirikuu anafaulu kuwaokoa na kuishia kumuoa
mchawi karaba, na karaba anaacha kabisa uchawi. Baada ya Kirikuu kugundua
sababu zinazomfanya mchawi Karaba kuwa katili, alitafuta mbinu ya kuweza
kutatua tatizo hilo Karaba anaacha uchawi. Kutokana na mambo aliyoyafanya
Kirikou kwa jamii yake ni wazi kwamba, Kirikuu anastahili kuitwa shujaa wa
jamii hiyo.
Biebuyck & Mateene (1969) wanaeleza utendi wa
Mwindo wa jamii za Nyanga, ziishizo katika misitu minene ya Kongo. Huyu ni
mfano wa mashujaa waliowahi kutokea katika jamii hii. Mfalme She-Mwindo anatoa
amri kuwa yeyote atakaye zaa mtoto wa kiume, mtoto huyo lazima auwawe. Mke wa
mfalme anabeba mimba ya mtoto wa kiume, anaanza kuongea akiwa tumboni na kujua
kuwa babaye anataka kumuua. Anazaliwa anatembea na kuongea. Kuzaliwa kwake
kunaonesha Mwindo atakuwa ni wa pekee katika jamii. Baba yake Mfalme She-Mwindo
anashangaa anamrushia mkuki kumuua. Mwindo anauzuia na kuuvunja vipande viwili.
Mfalme anashangaa na kupiga kelele; mtoto huyu ni wa namna gani? Anaagiza
Mwindo azikwe akiwa hai, anazikwa, lakini kesho yake wanamwona Mwindo akiwa
hai. Mfalme anakasirika na kuagiza atiwe kwenye pipa kisha atupwe mtoni,
anatupwa mtoni lakini anatoka mtoni na kuliacha lile pipa ufukweni.
Mwindo aliamua kwenda kuishi kwa shangazi yake
kijiji cha ng’ambo ya mto. Alipokuwa akirudi kwao akiwa anapambana na mfalme
She-Mwindo, Mwindo akafanya miujiza yake, ghafla radi ikatuma mshale wake na
kuwachoma wanaume wote wa Tubondo wakafa wote kasoro mfalme She-Mwindo na
shangazi yake Mwindo. Shangazi yake alisikitika, akamwambia Mwindo, ‘‘umekuja
kupigana na baba yako, tazama sasa mjomba wako na watu wetu wote pamoja na watu
wa baba yako wamekufa’’. Baada ya Mwindo kuona watu wote wamekufa, akazungusha
konga yake na kumgusa mmoja mmoja akisema; ‘‘mwanzo ulilala, sasa amka’’ wote
wakafufuka. Wakashangilia wakisema; ni nani mtu mkubwa ni Mwindo! Nini mtu
yeyote aweza fanya kumpinga?’’. Hivyo ushujaa wa shujaa Mwindo unabainika
kutokana na kupambana na matatizo yote yaliyomkabili na kuyashinda. Katika
kuyakabili haya, Mwindo anaonesha utofauti wake na watu wengine katika jamii.
Utofauti huu ndio uaomfanya atambulike kama shujaa. Hii ni ishara tosha kuwa,
Mwindo alikuwa na nguvu za kipekee zipitazo wanajamii wote, yaani nguvu za
sihiri, yaani nguvu alizonazo shujaa zisizoweza kuelezeka katika mtazamo wa
kisayansi.
Njogu na
Chimerah (1999) wakielezea utanzu wa utendi wanasema, tendi ni hadithi
zinazohusu ushujaa. Wahusika wake wakuu ni mashujaa wa Kitaifa, na hustahiwa
sana. Wakiendelea kuelezea dhana ya shujaa wa utendi wanasema aghalabu mashujaa
wa utendi huwa na wapinzani wao/majahili. Mashujaa hawa wa tendi huwa ni watu
wema na hupigania haki za kila mtu hasa wanyonge. Wakinzani wao huwa hawajali
kamwe maslahi ya watu wengine na, aghalabu, huwa ni wakandamizaji, makatili na
wenyekuelemea ubinafsi. Hivyo basi, mara nyingi mapambano ya mwisho katika
tendi huwa ni baina ya jagina/shujaa na jahili, ambapo jahili hushindwa na
kuuwawa. Wakiendelea kueleza, wanasema kwamba hata hivyo, si tendi zote
ziishiazo na kuuwawa kwa jagina. Ziko tendi kadhaa za jamii nyingi ulimwenguni,
zinazoishia na kuangamia kwa shujaa/jagina. Tendi za namna hii huitwa tanzia na
hupendwa na hustahiwa zaidi na wenyewe kuliko mighani za kimelodrama, ambapo
jagina anaibuka mshindi. Vilevile, katika tendi zingine shujaa/jagina huwa hana
mpinzani wake/jahili wa moja kwa moja, bali hupambana na kundi zima la watu
waovu, au hata taifa zima ovu. Katika tendi za aina hii, shujaa anaweza ashinde
au ashindwe. Akishinda anatawazwa na kuwa mfalme. Mfano ni Samsoni na Delila (Uyahudi), Herakili (Ugiriki), Musa katika safari ya Waisrael (Uyahudi), Lwanda
Magere (Kenya), Julias Kaizari (Italia), Sundiata (Afrika Magharibi), Shaka wa
Kwazulu (Afrika Kusini), Fumo Liyongo (Wa Uswahilini/Kenya), Goliati na Daudi
(Uyahudi) na Mfalme Edipodi (Ugiriki).
 Wakiendelea kueleza hoja hii ya ushujaa
wanasema, Mashujaa takribani wote katika tendi za watu wa mataifa mbalimbali
ulimwenguni kote huwa wana sifa moja usikawaida. Jambo la kwanza, mashujaa huwa na
uwezo ambao si wa kibinadamu, na usio wa kawaida. Hawauliki. Mtu mmoja huwa ni
kama jeshi na zaidi ya jeshi. Licha ya maajabu haya yote ya uwezo wake, shujaa
huwa ana unyonge mmoja, bado ni binadamu tu, na hufa, tena kwa urahisi sana;
bila kuhitaji jeshi. Shujaa huweza akauwawa na mtu mnyonge sana, au hata mtoto
mdogo. Vipi? ‘‘Kwa kuijua siri’’. Mtu anayeweza kuitambua siri ya jinsi shujaa
anavyoweza kuulika, basi mtu huyo huweza, ama yeye mwenyewe au kwa njia ya
kuwafichulia siri hiyo adui za shujaa, husababisha kifo cha shujaa. Katika
tendi nyingi mashujaa husalitiwa na akraba zao wenyewe; watu ambao yeye shujaa
hata hawezi kuwashuku kamwe. Watu hawa mara zote huwa wamefichuliwa siri na
shujaa mwenyewe, bila hata kushuku kwamba watu hao, wanaweza kumgeuka. Mfano ni
Samsoni anapatoa siri ya kunyoa nywele kwa Delila hatimaye ananyolewa na
kuuwawa, Lwanda Magere anatoa siri ya kivuli
chake kwa mkewe mdogo wa Kilang’o, hatimaye Walang’o wanapiga kivuli chake
na kumuuwa, na Fumo liyongo anatoa siri ya kuchomwa sindano ya shaba kitovuni kwa mwanaye na hatimaye mwanaye
anamchoma sindano kwenye kitovu anakufa, ingawa Liyongo alibaini madhumuni ya
mwanaye ya kutaka kumsaliti na kumuuwa na akamwambia wazi kwamba, ‘‘umekuja
kunisaliti’’. Zipo tendi chache ambazo ni tofauti kidogo na tendi nyinginezo,
hasa kuhusu nguvu za  jagina/shujaa.
Katika tendi hizi shujaa huwa ni mtu dhaifu sana akilinganishwa hata na watu wa
kawaida, licha ya majahili wenye miguvu isiyo ya kawaida. Kinyume na
inavyotarajiwa, Vishujaa hivi vinyonge havishindwi. Mara zote huwa vinamudu
kuyasambaratisha majahili yenye nguvu kuvishinda. Katika jamii nyingi za
Kiafrika, shujaa wa aina hii hakosekani. Mfano
Nyanje katika masimulizi ya Kimijikenda. Daudi anajulikana kwa kumpatiliza
Goliati wa Gathi. Tendi za aina hii ndizo nyingi katika mataifa yote ya
ulimwengu. Njogu na Chimerah (1999).
Mtandao
wa Kilimwengu wa Google ukifafanua dhana ya ushujaa katika muktadha wa kisasa
inaeleza ni kufanya jambo zaidi ya matarajio. Mashujaa katika muktadha huu ni
kama baba au mama wanaochukua jukumu la kumuwezesha mtoto kuishi, daktari
anayeokoa maisha ya wagonjwa, askari anayekwenda kupigana vitani kulinda uhuru
wa watu, wachungaji makanisani nao ni mashujaa na mtu anaetoa pesa kumsaidia
mtu mwingine naye ni shujaa.
Hoja za wataalamu hawa zimetoa mwanga katika
utafiti huu, na kubaini kwamba ni dhahiri kwamba ushujaa wa shujaa hujibainisha
kutokana na namna shujaa anavyoisaidia jamii yake, hasa nyakati za matatizo.
Katika hizi ndipo mashujaa wengi hutumia akili zao, vipaji vyao na hata kujitoa
muhanga. Pia wengine hutumia hata nguvu za kichawi na sihiri katika kuhakikisha
kwamba, jamii yake inabaki salama wakati wote. Kutokana na hoja za wataalamu
hawa utafiti huu umebaini kwamba kitu cha pekee ambacho humfanya shujaa
aonekane ni mtu wa pekee katika ufumbuzi wa matatizo ni sihiri, yaani nguvu
alizonazo shujaa zisizoweza kuelezeka katika mtazamo wa kisayansi. Mbali na
mafanikio makubwa ya hoja za wataalamu hawa kwa utafiti huu, wataalamu hawa
wote walitafiti juu ya ushujaa na mashujaa wa tendi, hawakugusia kabisa utanzu
wa ngano; ndio sababu utafiti huu unaona kuna haja ya kutafiti juu ya ushujaa
wa shujaa wa motifu za safari na msako katika ngano, hususani ngano zenye
motifu za safari na msako ambazo wahusika wake wakuu ni mashujaa ili kubaini
uhusiano wa mashujaa hawa wa tendi na wa ngano.

Dhana ya Ushujaa wa
Shujaa wa Waikizu

Baadhi ya wataalamu waliotafiti dhana ya ushujaa
wa Kii-kizu ni pamoja na Nyamsenda (2012), Marwa (1982) na Shetler (2001). Akielezea
dhana ya ushujaa wa Kiikizu Nyamsenda (2012) anasema dhana ya taswira ya
ushujaa wa Waikizu imejengeka katika kuuwa wanyama wakali kama simba na chui. Shujaa ni lazima aende safari ya mbali
kwenda porini apambane na simba au chui na kumuua. Mara nyingi ushujaa wa Waikizu
huwa ni kwa mustakabali wa jamii nzima ya Ikizu, na mara chache sana ushujaa
wao huwa kwa manufaa ya shujaa mwenyewe binafsi na familia yake hasa katika
ngano zao. Na zaidi shujaa wa Waikizu huwa hapewi msaada wowote na mtu au kitu
chochote, hupambana peke yake mpaka mwisho, kulingana na falsafa yao ya
ushujaa. Muda wote huwa ni shujaa wa masafa marefu. Koponen (1988) anataja
baadhi ya wanyama hatari katika jamii za jadi kuwa ni simba, chui na tembo
ambao walitishia uhai wa watu na mali zao. Chui hawa walikuwa na tabia ya
kuvamia wanyama kama mbuzi na ng’ombe na kuwala. Wakati mwingine waliwaua au
kuwajeruhi hata watu. Hivyo, chui katika jamii za jadi aliogopwa sana. Hapa
imebainika hoja ya Koponen inaendana na dhana ya Waikizu ya ushujaa katika
kuuwa wanyama hatarishi.
Katika muktadha wa wanawake, katika jamii ya
Waikizu, ushujaa wa mwanamke ni katika uzazi, ambapo mwanamke akijifungua bila
kulia wala kuogopa, na asiuwe mtoto kwa uoga wakati wa kujifungua/kubhunza. Hivyo, kwa Waikizu suala la
ushujaa ni kwa wanawake na wanaume. Suala ambalo limebainika hata katika jamii
mbalimbali za Ulimwengu. Kama ilivyobainishwa na Raglan (1976). Aidha, ushujaa
kwa Waikizu hubainika pia katika utawala wao, ambapo watawala wote katika
Ikizu, kuanzia watemi mpaka wahimayyi,
ili uwe na wadhifa wowote katika Ikizu ni lazima mtu huyo awe shujaa mwenye
sifa zote za ushujaa. Toka mwanzo katika jamii ya Waikizu watemi/machifu
walikuwa ni wanawake pekee, kutokana na sifa yao ya ziada ya ushujaa ya kuleta
mvua/abhagemba. Akiendelea kuelezea
dhana ya ushujaa wa Kii-kizu Nyamsenda anaeleza kwamba, ushujaa wa Waikizu
huambatana na ujigambi/etambo na
nyimbo katika mchezo wao wa ushujaa na kishujaa/ekesa. Mchezo huu wa ushujaa huwajumuisha mashujaa wote wanawake na
wanaume. Shetler (2001) anaunga mkono hoja hizi. Songoyi (1990) anabainisha
kwamba kadri mtu alivyokuwa na nyumba yenye watoto wengi ndivyo alivyoheshimika
na kuonekana tajiri. Hivyo, jamii za jadi ziliuona uanaume kuwa mali kwani ndio
chanzo cha utajiri. Sitiari hii inabeba falsafa ya uzazi katika jamii za jadi
za Kiafrika. Campbell (1973) anaeleza katika jamii za wafugaji ushujaa ulikuwa
katika nguvu za kupambana na wanyama wakali na katika jamii za wakulima,
ushujaa ulikuwa ni katika rutuba na uzalishaji zaidi wa mazao. Hoja hii ni sawa
na Nyamsenda (2012) anapoeleza jinsi watemi wa Ikizu walivyotakiwa kuleta mvua
kwa wingi katika vipindi vyote, hata vya kiangazi, kwaajili ya uzalishaji wenye
tija kwa jamii.
Marwa (1983), akieleza dhana ya ushujaa wa Waikizu
anamrejelea ushujaa na ushupavu wa chifu Makongoro wa Ikizu kijamii, kisiasa,
kiutawala na kiutamaduni, kwamba ni mtu mbaye hakuwaogopa hata wazungu katika
utawala wa kikoloni na aliungana na mwalimu Nyerere katika harakati za kuleta
ukombozi wa Watanganyika.

Dhana ya Ushujaa wa
Shujaa wa Wabondei na Wazanzibari

Kulingana na Kiango (1974), aliyefanya utafiti wa
kukusanya ngano za Wabondei akiwa na kusudi la kuthibitisha kwamba, katika
jamii ya Wabondei kuna shujaa wa motifu ya safari katika ngano za jamii hiyo. Kiango
amebainisha kuwa katika jamii ya Wabondei shujaa anaweza kuwa mwanamke au
mwanaume, mkubwa au mdogo, mtoto au kijana. Japo dhana ya ushujaa wa Wabondei
imejengwa zaidi katika uzuri wa sura ya mtu/urembo. Hivyo basi, Kiango
anaonesha mahasidi wa shujaa humuonea wivu shujaa kwa uzuri wake na kupanga
maangamizi juu yake. Katika muktadha mwingine, Kiango ameonesha safari ya
shujaa huanza baada ya kifo cha wazazi ambapo safari ya shujaa huwa ni ya
kulazimishwa, ambapo shujaa huondoka nyumbani na kwenda katika mazingira ya
kubahatisha. Sababu hasa ya safari hii ya shujaa huwa ni ugonvi wa kugombania
mali/urithi. Kulingana na ngano alizokusanya Kiango, mara zote ushujaa wa
shujaa wa motifu ya safari huwa ni kwa manufaa ya shujaa mwenyewe binafsi na si
kwa manufaa ya jamii yake. Na kwa mujibu wake shujaa ni lazima apate msaada
toka kwa ndugu wa karibu au toka kwa joka au kitu chochote. Mara nyingi shujaa
huwa wa masafa mafupi. Ni mara chache shujaa huwa wa masafa marefu. Mara nyingi
shujaa hupelekwa sehemu ya maangamizi na mahasidi wake bila yeye kujua na
kurudishwa nyumbani na watu waliomuokoa.
Senkoro (1997), kwa mujibu wa utafiti wake,
alionesha umuhimu wa safari katika ngano za motifu ya safari katika ngano za
Wazanzibari. Kulingana na ngano alizokusanya, shujaa ni lazima asafiri kutoka
nyumbani au kwa kufahamu au kwa kutofahamu. Shujaa hupambana mwenyewe mara
nyingine hupata msaada kutoka kwa dege, mtu, kwa wazazi au kitu chochote,
shujaa huwa na busara na hekima. Shujaa huweza kuwa wa masafa marefu au masafa
mafupi.

 

[1]
Tazama Biblia takatifu Waamuzi 13:1-23, 14:1

 

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!