CHIMBUKO LA METHALI

By , in Fasihi Simulizi on . Tagged width:

Mitazamo mbalimbali imetolewa kuhusu chimbuko la methali miongoni mwake ikiwamo ifuatayo:

Miruka (1994) anasema methali hutokana na uzoefu wa maisha ya kila siku ya wanajamii na kwa kutumia methali wanajamii hao huwasilisha falsafa na msimamo wa maisha ya jamii yao. Akiunga mkono wazo la jamii kuwa chanzo cha methali,

Madumulla (1995) anasema Methali ziliibuka kutokana na uzoefu wa kila siku wa watu na pia kutokana na kuchunguza matukio ya maumbile (Tafsiri yangu).

Naye Nyembezi (1963) anaeleza kwamba methali huzuka kutoka vyanzo mbalimbali katika masimulizi ya jamii. Ziko methali ambazo zimetokana na masimulizi ya kimiujiza, ngano, na hadithi za kale. Ziko pia methali zilizotokana na matukio ya kweli ya kihistoria. Lakini Nyembezi (ametajwa) anasisitiza kwamba idadi kubwa ya methali chimbuko lake ni uzingatiaji wa tabia za binadamu na wanyama na pia vitu mbalimbali vilivyo katika mazingira. Tabia na maumbile yao hulinganishwa ili kupatanishwa na ukweli wa hali halisi.

Kutokana na hayo, ni dhahiri chimbuko kuu la methali ni jamii yenyewe na mazingira yanayoizunguka. Methali haiwezi ikazuka nje ya jamii. Methali isipochipuka kutokana na jamii inayohusika haitaeleweka kwa urahisi katika jamii ile. Kwanza kwa sababu haitakuwa ikihusisha mazingira yanayoeleweka kwa wanajamii na kwa kushindwa kufanya hivyo haitaweza pia kueleza ukweli unaotokana na hali halisi. Hivyo, kama asemavyo Mohamed (1974), methali ziliibuka tangu binadamu alipoanza kutumia lugha ili kukidhi mawasiliano na kueleza hisia zake za ndani na za jamii yake.