CHANGAMOTO ZINAZOKUMBA CHAWAKAMA KATIKA MAKUZI YA LUGHA YA KISWAHILI NCHINI

By , in Kavazi on .

Chawakama

Simon Ekiru (kushoto), Mwenyekiti wa CHAWAKAMA-Kenya wa kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Bi Sabina Mokeira Afisa Mwenezaji wa CHAWAKAMA-Kenya kutoka CUEA na Bw Samuel Abesi, Katibu Mkuu wa CHAWAKAMA-Kenya kutoka Chuo Kikuu cha Laikipia walipohojiwa Nation Centre Januari 21, 2016. Picha/ANTHONY OMUYA

Na CHRIS ADUNGO

Kwa Muhtasari

Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) kina uwezo mdogo sana wa kujiendeshea nyingi za shughuli za kutetea Kiswahili.

CHAMA cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) kina uwezo mdogo sana wa kujiendeshea nyingi za shughuli za kutetea Kiswahili.

Ni dhahiri kwamba mapato ya chama hiki hutegemea michango ya wanafunzi ambao hawana uwezo mkubwa wa kifedha na mara nyingi wao hushindwa hata kuyaafikia malengo yao kutokana na uchechefu wa pesa.

Huenda hii ni mojawapo ya sababu kuu kwa chama kutokuwa na maendeleo ya kasi katika jitihada za kufikia viwango vya vyama na asasi nyinginezo maarufu zinazojishughulisha na kukipigia chapuo Kiswahili humu nchini.

Hii ni moja kati ya changamoto tele walizozisadiki vinara wa CHAWAKAMA katika mojawapo ya vikao vilivyowakutanisha na mwandishi wa makala haya mwishoni mwa 2015.

Utambulisho

Wakizielezea kadhia zao, Simon Ekiru (Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Moi), Sabina Mokeira (Afisa Mwenezi, Chuo Kikuu cha CUEA), Eric Juma (Mhariri Mkuu, Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga) na Samuel Abesi (Katibu Mkuu, Chuo Kikuu cha Laikipia) walisema kwamba jambo jingine linalopunguza kasi ya maendeleo ya CHAWAKAMA ni kutotambulika kwa chama katika vyombo husika vya serikali.

Kwa mfano hapa nchini, CHAWAKAMA hakitambuliwi na serikali kwa kuwa chama hakina usajili wa kudumu.

Chama kinaposajiliwa, kinapata utambulisho rasmi serikalini na hivyo kuwa rahisi kuendesha shughuli zake ikiwa ni pamoja na kuandaa hafla za kufanyia michango na pia kuomba msaada kutoka kwa vyombo vya serikali vinavyohusika katika kutukuza na kueneza Kiswahili.

Usajili

Nadhani viongozi wenyewe wa CHAWAKAMA hawajawa makini katika suala hili kwa kuwa kusajili chama hakuhitaji pesa nyingi! Na usajili si jambo kubwa la kusumbukia kiasi hicho kwa kuwa hata ada za wanachama zinatosha kuufanikisha.

Ningependa kuwashauri viongozi wa CHAWAKAMA humu nchini walichukulie kwa umakini sana suala hili, kwani chama kitakapotambulika serikalini hata vinara watakapokwenda kwenye kongamano katika nchi nyingine watatambuliwa na Ubalozi husika kwa kuiwakilisha nchi yao.

Teknohama

Changamoto nyingine katika chama hiki ni suala la kujitangaza. Chama hakijitangazi vya kutosha, watu wengi wakiwamo wataalamu na wasomi wa Kiswahili hawajui iwapo kuna CHAWAKAMA , na ni vyombo vya habari vichache sana vinavyojua kuhusu uwapo wa chama hiki.

La kutia moyo ni kwamba viongozi wa CHAWAKAMA wametambua kwamba katika enzi hizi za Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA), jukwaa bora na rahisi la kukitangaza chama ni mtandaoni.

Chama kina wavuti ambao kwa kweli utasaidia kukitangaza, na katika wavuti huo yawezekana kuwekwa makala na taarifa mbalimbali za chama ambazo zitawavutia wakereketwa, watetezi na wafia-lugha wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Kupitia kwa mtandao huo, wapenzi wa Kiswahili wanaweza kujisajilisha na kuwa wanachama kwa urahisi.

Kwa mfano, hivi sasa kuna Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) ambacho huwashirikisha walimu wote wa Kiswahili ulimwenguni.

Watu wanaweza kujisajili na chama hiki kupitia kwa mtandao, jambo ambalo lina nafuu zake. Japo wavuti ni kitu muhimu sana katika kukitangaza chama, ipo haja kwa mikakati mingine kubuniwa ili kuvumisha CHAWAKAMA zaidi.

Ilhamu

Mwamko mdogo wa vijana wengi wanaosomea taaluma za Kiswahili pia ni changamoto inayokikabili chama katika kukua kwacho.

Wengi wa vijana hawajawa na mshawasha wa kutosha kuhusu nafasi ya Kiswahili kama kiungo muhimu miongoni mwa watu wa Afrika Mashariki.

Wengi wanadhani kwamba Kiswahili ni cha watu duni ambao hawajasoma sana, watu wenye mitazamo iliyopitwa na wakati na kwa sababu hii hawaoni sababu ya kujishughulisha nacho.

Kongamano la 2012 lililofanyika nchini Burundi kwa mfano, lilitoa hamasa kubwa kwa vijana wa nchi hiyo kuhusu dhana ya umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kabla ya hapo, wengi wa wazawa wa Burundi na Rwanda waliamini kwamba Kiswahili si lugha ya kistaarabu kwa kuwa kilihusishwa na majambazi, wajanja na matapeli.

Japo hiyo ilikuwa ni hatua kubwa, cha kuvunja moyo ni kwamba baadhi ya vijana humu nchini wamekubali kutawaliwa na dhana kuwa lugha za kigeni ndizo zenye hadhi katika soko la ajira.

Kasumba

Kasumba inayowatawala ni kwamba ukijieleza kwa Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani au Kihispania kwa mfano, basi utaonekana msomi na mwenye kustahiki hadhi kubwa miongoni mwa wanajamii wengine. Lakini yule anayejishughulisha na Kiswahili yeye ataonekana kama ambaye kakosa jambo la msingi la kufanya! Mchakaramu!

Hali kama hii kwa kweli husikitisha sana. Ingawa hivyo, wanachawakama kwa upande mwingine pia hawatakiwi kukata tamaa kwa sababu wanajua kile wanachokifanya.

Wao wanaelewa vyema manufaa ya Kiswahili na hao wanaojaribu kuwavunja mioyo wanakuwa bado hawajaelewa kwa nini wanajishughulisha na Kiswahili. Kwa hivyo, la msingi ni kuwaelimisha na kuwaondolea hizo kasumba.

Kongamano la 11 la kimataifa lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kyambogo jijini Kampala, Uganda mwaka jana liliwashuhudia washiriki wakiazimia haja ya kukipa Kiswahili nguvu na uthabiti zaidi.

Kauli
Ingawa dhima kuu katika kongamano la leo katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki (CUEA) ni kulinganisha mitazamo ya matumizi ya Kiswahili katika taaluma za isimu, fasihi na tafsiri; wanafunzi, wasomi, wanahabari na wataalamu watapania kusisitiza nafasi ya Kiswahili katika ulimwengu wa sasa.

Kupitia kwa kauli “Taaluma ya Kiswahili na Maendeleo ya Jamii”, changamoto zitatolewa kwa watumiaji wa Kiswahili kujitahidi zaidi ili kuyakabili mawimbi ya mabadiliko ya TEKNOHAMA pamwe na kulipiga breki tatizo kubwa la kasumba.

Itakuwa muhimu sana iwapo wanachawakama wataamua kuuenzi utamaduni wao kwa vitendo.

Hamasa yao itakuwa na mvuto mkubwa sana kwa watu wengi. Wao hawakusukumwa na mtu yeyote kukichapukia Kiswahili lakini kwa kuona kwamba lugha hiyo ni chombo muhimu sana cha kuwaweka pamoja watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ndipo wakaamua kukiunda chama hiki.

Wekeza

Iwapo watu watazungumza lugha moja, wao wataona kwamba ni wamoja na hivyo kudumisha ushirikiano katika jamii.

Ipo haja kwa serikali za nchi wanachama wa CHAWAKAMA kuwekeza katika vikundi vyote vinavyojaribu kutumia Kiswahili kwa minajili ya kuwaunganisha wanajumuiya.

Kiswahili kinatambulika katika Katiba za Kenya na Tanzania kama lugha ya taifa na pia rasmi katika nchi hizo.

Na kama kweli serikali hizo zinataka Kiswahili kivie na kuendelea kujivunia hadhi hiyo, basi zinastahili kuuthamini mchango wa CHAWAKAMA katika kuendelza na kukuza lugha hiyo.

Yastahili viongozi wawe radhi kuwasaidia vijana hawa pindi wanapowaendea katika afisi zao na pia wao wenyewe waanzishe jitihada za maksudi katika kuchangia maendeleo ya Kiswahili.

Facebook Comments
Recommended articles