CHANGAMOTO ZA TAFSIRI ZINAZOSABABISHWA NA TOFAUTI ZA KITAMADUNI

By , in TAFSIRI/UKALIMANI on .

CHANGAMOTO ZA TAFSIRI ZINAZOSABABISHWA NA TOFAUTI ZA KITAMADUNI

Kila jamii ina utamaduni wake. Tamaduni hizi hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. Jamii tofauti tofauti huwa na mitazamo tofauti kuhusu mambo na dhana tofauti na hali hii ni kulingana na itikadi, imani, mila na desturi za jamii husika. Lugha ni mfano wa dhana ambayo imemilikiwa, imefungamanishwa na kuzaliwa kutoka utamaduni fulani. Hii inamaanisha kuwa ili mtu kuelewa lugha fulani na dhana zinazohusishwa na hiyo lugha, itabidi awe mzawa wa utamaduni husika ama awe na tajiriba ya utamaduni huo. Hivyo,utamaduni umekuwa changamoto katika shughuli ya kutafsiri. Hebu tuzingatie mifano ifuatayo:

Aina za Vyakula vya Kitamaduni katika Jamii ya Wamaasai.

i) Madida – Aina ya chakula, kati ya ugali na uji, hupikwa kwa kutumia unga wa mahindi, huongezwa ladha kwa chumvi kidogo, sukari na mafuta.

ii) Munono – Aina ya chakula ambacho huundwa kwa nyama ya mbuzi au kondoo.

Hukatwakatwa vipande vidogo sana kisha hukaushwa kwa kukaangwa na mafuta na kisha kuchanganywa na damu.

iii) Orketutu – Aina ya ugali mgumu sana, hukaushwa hadi kuwa chenga chenga, huongezwa mafuta na chumvi. Huliwa pamoja na chai wakati wa kiangazi wakati ambapo maziwa yameadimika.

iv) Orpurda – Aina ya nyama haswa ya mbuzi au kondoo. Huandaliwa kwa kukaangwa kwenye mafuta mengi hadi kukauka. Nyama zenyewe huachwa kupoa na kushikamana na mafuta. Huweza kuhifadhiwa kwenye mafuta hadi mwezi mmoja. Huliwa haswa na akina mama waliojifungua na vijana waliopashwa tohara. Itakuwa vigumu kutafsiri aina hii ya vyakula katika lugha ya Kiswahili kwa sababu hamna visawe vyake katika Kiswahili. Majina kama haya ya aina ya vyakula ambavyo vimejikita katika utamaduni wa jamii ya Wamaasai huleta changamoto kwa mtafsiri anapotaka kutafsiri kutoka Kimaasai hadi Kiswahili.Vile vile kuna vyakula ambavyo si maarufu miongoni mwa jamii ya Wamaasai na ambavyo ni maarufu katika jamii zingine na hurejelewa kwa Kiswahili. Mifano ni kama:

i) Pilau

ii) Biriani

iii) Makande

iv) Viazi karai

v) Mshikaki

Vyakula hivi havina visawe vyake katika lugha ya Kimaasai na pia havina mashikilio katika utamaduni wa Kimaasai. Hivyochangamoto huzuka katika kutafsiri majina haya ya vyakula kutoka Kiswahili hadi Kimaasai.

Hali ya Kubadilishana au Kuzawadiana Kuimarisha Uhusiano katika Jamii.

Katika jamii ya Wamaasai kuna hali ambapo watu hutoa zawadi haswa wanyama. Hii ni ishara ya kudumisha uhusiano mwema na urafiki. Kuna majina ambayo hutumika kurejelea jinsi watu huitana kutegemea mtu alizawadiwa mnyama gani.

Kama mtu amezawadiwa mnyama fulani basi mtu huyo atamwita aliyemzawadia kwa jina fulani. Aliyetoa zawadi ya mnyama fulani pia atamwita aliyempa zawadi kwa jina hilo hilo.Kwa mfano katika jamii hii, utasikia watu wakiitana:

i) Pasikiria- ni zawadi ya punda

ii) Esupen – zawadi ya mbuzi wa kike ambaye hajazaa.

iii) Pakishu – ng‘ombe ametolewa kama zawadi.

iv) Pakuo – mwanambuzi ametolewa kama zawadi.

v) Pakine – mbuzi wa kike aliyezaa ametolewa kama zawadi.

vi) Paker – kondoo wa kike ametolewa kama zawadi.

vii) Pakiteng‘ – fahali ametolewa kama zawadi.

viii) Paashe – ndama ametolewa kama zawadi.

Mtu aliyetoa zawadi na aliyepokea zawadi huitana kwa majina hayo tuliyoorodhesha. Itakuwa ni changamoto kutafsiri majina kama haya kutoka Kimaasai hadi Kiswahili kwa sababu hayana visawe na pia hayaingiani na utamaduni wa Kiswahili. Kama mtafsiri hatoki katika utamaduni wa Kimaasai au hana tajiriba ya utamaduni huu, itakuwa ni changamoto kwake kutafsiri majina au maneno hayo ya Kimaasai hadi Kiswahili.

Majina ya Kurejelea Wapendwa

Katika jamii ya Wamaasai, kuna majina ambayo wazee na wanawake walio na umri mkubwa hutumia kuwaitia watoto wao, wajukuu wao na watu wa umri mdogo katika jamii. Jambo hili hufanyika ili kuonyesha upendo kutoka kwa wazee na wanawake wakongwe na kuwapa shime watoto wao na kizazi kichanga. Tuangalie baadhi ya majina ambayo hutumika: Kimaasai Kiswahili

  1. Osikiria lai: Punda wangu
  2. Enkoshoke ai: Tumbo langu
  • Enkutuk ai: Mdomo wangu
  1. Enkaji e yieyio: Nyumba ya mama
  2. Enkaina ai: Mkono wangu
  3. Nkonyek ainei: Macho yangu
  • Enkeju ai: Mguu wangu
  • Enkarna ai: Jina langu
  1. Enkiteng ai: Ng‘ombe wangu

Ingawaje majina haya ya Kimaasai yana visawe katika lugha ya Kiswahili, yana maana tofauti kando na maana yake yakimsingi iliyozoeleka. Majina yaliyotumika katika kuwarejelea wapendwa ni majina ya wanyama na majina ya sehemu za mwili. Majina haya hayarejelei wanyama au sehemu za mwili, bali yanasisitiza upendo na ile hali ya mshikamano katika jamii.

Kwa hivyo, iwapo mtafsiri hana uelewa wa utamaduni huu wa Kimaasai, anapotafsiri majina haya hadi Kiswahili basi atasababisha upotovu wa maana na kutatiza mawasiliano.

Aina za Mavazi na Mapambo

Kama ilivyo katika tamaduni zingine, jamii ya Wamaasai ina aina ya mavazi na mapambo kulingana na utamaduni wao. Mavazi kama haya na aina mbalimbali ya mapambo hurejelewa kwa majina maalum. Tuangalie baadhi ya majina yanayorejelea aina ya mavazi na mapambo:

i) Elokesena – vazi la kina mama la kuvaliwa chini – aina ya sketi ya shuka.

ii) Enchoriba – aina ya vazi la ngozi nyororo ambalo huvaliwa na wazee.

iii) Enkarewa – aina yapambo lililotengezwa kwa shanga na ngozi. Huvaliwa shingoni na huning‘inia hadi miguuni. Huvaliwa na akina mama na wasichana.

iv) Enkatar – aina yapambo amblo hutengenezwa kwa kutumia nyaya nyembamba na shanga na ambazo huvaliwa kwa kuviringishwa miguuni.

v) Orkatar – aina ya pambo ambalo hutengenezwa kwa kutumia waya nyembamba na shanga. Huvaliwa shuingoni na wanawake kwa waume.

vi) Enkirina – aina ya bangili ambayo hutengenezwa kwa kutumia aina fulani ya mpira au ngozi na shanga. Huvaliwa mkononi kama pambo.

vii) Enkishili – aina ya pambo la bibi harusi ambalo hutengezwa kwa ngozi na shanga na huvaliwa kichwani.

viii) Orkeliai – aina ya pambo, hutengenezwa kwa shanga, ngozi au mipira. Huvaliwa shingoni na wanaume na wanawake.

ix) Imuna – pambo ambalo hutengezwa Kwa shanga na waya ambalo huvaliwa masikioni na wazee na wanawake.

x) Enkitati – aina ya mshipi mpana uliotengezwa kwa ngozi ya ng‘ombe. Huvaliwa na wanawake.

Mavazi haya na mapambo yana majina maalum kulingana na utamaduni wa Wamaasai. Ni vigumu kupata visawe vya majina haya katika lugha ya Kiswahili. Kuelezea majina haya kutoka lugha ya Kimaasai hadi Kiswahili, itabidi mtafsiri awe na ujuzi wa kitamaduni ya Wamaasai ama awe ametoka katika jamii hii. Hali hii inapelekea kuwa na changamoto katika kutafsiri.Vile vile kuna mavazi ambayo si maarufu katika jamii ya Wamaasai na ambayo hurejelewa kwa majina ya Kiswahili. Mifano ni pamoja na:

i) Kanzu

ii) Kitenge

iii) Kikoi

iv) Rinda

v) Kizibao

vi) Kabuti

vii) Kaptula

viii) Surupwenye

ix) Buibui

x) Kanchiri

Ni changamoto kwa mtafsiri kutafsiri na kuelezea majina kama haya kutoka Kiswahili hadi

Kimaasai kwa sababu hamna visawe vyake katika lugha ya Kimaasai na vile vile hayashikamani na utamaduni wa Kimaasai.

Dhana ya Ekolojia

Ekolojia hurejelea suala la tabia za kijiografia, mazingira, tabia nchi, hali ya hewa na kadhalika.

Tabia na hali kama hizi kwa kawaida zinaweza kutofautiana kati ya utamaduni wa jamii moja na

jamii nyingine. Kwa mfano tuzingatie aina zifuatazo za mandhari:

i) Ufuo / ufuko (wa bahari)

ii) Theluji

iii) Volkano

Mandhari kama haya hayapatikani au hayahusiki moja kwa moja na utamaduni wa jamii ya Wamaasai. Kuleta dhana kama hizi kutoka lugha ya Kiswahili hadi lugha ya Kimaasai itakuwa ni changamoto kwa mtafsiri wa Kiswahili kutafsiri hadi Kimaasai.Vile vile, tunapoangazia mazingira fulani tunapata, kwa mfano, mimea fulani ambayo inahusishwa na tamaduni za jamii fulani. Kwa mfano:

i) Mnazi

ii) Mparachichi

iii) Muarobaini

iv) Makuti

Majina haya ambayo yanarejelea aina ya mimea, ni maarufu miongoni mwa Waswahili wanaoishi mwambao wa pwani. Majina haya ambayo yamerejelewa katika lugha ya Kiswahili yanaleta changamoto yanapotafsiriwa hadi lugha ya Kimaasai. Sababu kuu ya changamoto hizi ni kwamba mimea hii haihusiani na utamaduni wa Kimaasai.

Rika na Umri katika Jamii

Katika utamaduni wa jamii ya Wamaasai kuna swala la rika na umri ambayo hupewa kipaumbele na kuheshimiwa. Katika jamii hii kuna majina ambayo hurejelewa kutofautisha makundi mbali mbali katika jamii. Makundi haya hujumuishwa kulingana na umri na wakati (mwaka) ambapo mwanamume alipashwa tohara. Majina haya hivyo husimamia watu katika jamii na ambao ni wa rika moja kwa misingi ya kiumri na wakati wa kupashwa tohara. Rika hizi hubuniwa kila baada ya miaka kumi hadi miaka kumi na tano. Baadhi ya rika hizi katika jamii hii husika ni pamoja na:

i) Ilterito

ii) Ilnyangusi

iii) Iseuri

iv) Irambauni

v) Irkishili

vi) Irmeshuki

Ili mtafsiri aweze kutafsiri ama kuelezea makundi haya kutoka lugha ya Kimaasai hadi lugha ya Kiswahili, itabidi mtafsiri awe na uelewa wa utamaduni huu. Hii ni changamoto katika kutafsiri kutoka Kimaasai hadi Kiswahili.

Koo au Mbari katika Jamii

Katika jamii hii ya Wamaasai kuna majina maalum ambayo yanatumiwa kurejelea ukoo au mbari fulani .Koo hizi ni familia pana zinazounda jamii moja ya Wamaasai. Walio katika ukoo mmoja hueshimiana sana, huonana kama ndugu na hawawezi kuoana. Mifano ya koo au mbari hizi ni pamoja na:

i) Ilmakesen

ii) Ilmolelian

iii) Ilukumai

iv) Iltaarosero

v) Ilkerin – ingishu

vi) Ilmeponi.

Majina haya ya Kimaasai ambayo yanarejelea koo au mbari, hayana visawe vyake katika lugha ya Kiswahili. Dhana kama hii ya koo ama mbari inapojitokeza katika kutafsiri Kimaasai hadi Kiswahili inazua changamoto. Changamoto yenyewe inasababishwa na tofauti za kitamaduni baina ya lugha ya Kimaasai na Kiswahili.

Uvumbuzi wa Kisayansi na Teknolojia

Uvumbuzi na ubunifu wa kisayansi na teknolojia umeathiri sana utamaduni wa lugha hasa katika mataifa ya nchi zinazoendelea. Utamaduni wa nchi zilizoendelea umepitishwa hadi katika tamaduni zingine. Hali hii husababisha wanaotafsiri kushindwa kupata visawe mwafaka kwa baadhi ya maneno katika utamaduni wa nchi zilizoendelea. Lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya mawasiliano katika maeneo yetu ya utafiti pia imeathiriwa na kuishia kutohoa maneno kama hayo kutoka lugha husika ya mataifa yalioendelea na kuyarekebisha tu kisarufi na kimatamshi. Inakuwa ni changamoto kutafsiri maneno kama haya kutoka Kiswahili ( maneno yaliyotoholewa) hadi lugha ya Kimaasai.

Kwa mfano:

 

Kiswahili                                           Kimaasai

i) Redio                                               _________

ii) Kemikali                                        _________

iii) Dijitali                                            _________

iv) Telefaksi                                         _________

v) Hadiwea                                          _________

vi) Softiwea                                          _________

vii) Kamera                                           _________

viii) Maikrowevu                                   _________

ix) Dekoda                                              __________

x) Memori (kadi)                                   __________

Imani kama Changamoto katika Kutafsiri

Utamaduni wa Waswahili umeathiriwa kwa kiasi fulani na utamaduni wa lugha ya Kiarabu ambayo waumini wake wengi ni Waislamu. Kuna majina mengi ambayo yanarejelewa katika lugha ya Kiswahili ambayo yamejikita katika imani ya Kiislamu. Inakuwa ni vigumu kutafsiri majina kama haya kutoka Kiswahili hadi Kimaasai kwasababu hamna visawe vyake katika lugha ya Kimaasai. Changamoto hii inaletwa na tofauti kubwa iliyoko ya utamaduni unaofungamanisha imani na itikadi. Hivyo panazuka changamoto katika kutafsiri maneno au majina yafuatayo kutoka Kiswahili hadi Kimaasai:

i) Kadhi

ii) Hijabu

iii) Mikabu

iv) Sheikh

v) Muktadh

Semi kama Changamoto katika Kutafsiri

Semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye lugha ya mafumbo ambazo hukusudia kuleta mafunzo kwa jamii husika. Semi ni moja wapo ya vipengele vigumu katika kufanyia kazi ya kutafsiri. Hii inasababishwa na tofauti kati ya utamaduni wa jamii moja na nyingine.

Semi hizi zinaweza zikatumika katika jamii moja na jamii nyingine zisitumike semi hizo. Kwa hivyo itakuwa changamoto kutafsiri semi za Kiswahili zifuatazo hadi lugha ya Kimaasai:

 Methali

i) Ndondondo si chururu, chururu si ndondondo.

ii) Kupanda mchongoma, kushuka ndio ngoma.

iii) Afadhali wahed shika, kuliko kenda nenda rudi.

Nahau

i) Mkono mrefu (mwizi)

ii) Zunguka mbuyu (toa rushwa)

iii) Kupata jiko (kuoa)

iv) Piga maji (kunywa pombe)

v) Ramba kisogo (kusengenya)

 Misimu

i) Amenitoanisha (nimempa fedha)

ii) Mpango wa kando (kutoka nje ya ndoa)

iii) Amejaa upepo (amekasirika)

iv) Mambo ni London (maisha ya juu)

Vitendawili

i) Kuku wangu anatagia mibani (nanasi)

ii) Popo mbili zavuka mto (macho)

iii) Parrr hadi Meka (utelezi)

iv) Mwaarabu mweupe husimama kwa mguu mmoja ( uyoga)

Misemo

i) Mtu ni afya ( kuzingatia usafi)

ii) Maji ni uhai (kulinda vyanzo vya maji)

iii) Miti ni mali (kulinda misitu au kuhifadhi mazingira)

iv) Mtoto ni mamake (malezi bora)

Dhana nyingine za Kitamaduni ambazo Hutatiza Tafsiri

(i) Dhana ya Utajiri

Kulingana na utamaduni wa Kimaasai, utajiri huhusishwa na wanaume pekee. Mwanamume anayehesabiwa kuwa tajiri anaangaliwa kwa misingi ya idadi ya wake aliyooa, idadi ya mifugo aliyonao na ukubwa na idadi ya mashamba aliyonayo. Hivyo hata ikiwa mtu ana fedha nyingi, kazi ya kifahari na mijengo, kama hana mifugo na wake wengi, kulingana na utamaduni wa kimaasai, mtu kama huyo ni fukara. Suala la utajiri hivyo, linapotafsiriwa kutoka Kiswahili hadi Kimaasai kwa misingi ya jinsi utajiri unavyoeleweka katika misingi ya Kiswahili, basi patakuwa na upotovu wa maana.

ii) Dhana ya Jinsia.

Katika utamaduni wa Kimaaasai, mwanamke huhesabiwa au huchukuliwa kama mtoto. Katika lugha ya Kimaasai neno‗Enkerai‘ – hurejelea mtoto, na katika muktadha mwingine, mwanamke au mke. Hivyo, katika hali ya kujuliana hali ama salamu, maneno yafuatayo hutumiwa: kejaa enkerai ( habari ya watoto), ambapo kauli hii inamaanisha habari ya familia, yaani mke na watoto. Kauli kama hii inazua changamoto katika kutafsiri kutoka Kimaasai hadi Kiswahili.

Iwapo mtafsiri haelewi utamaduni huu wa Kimaasai basi anaweza kutafsiri visivyo kutoka Kimaasai hadi Kiswahili.

HITIMISHO

Katika sehemu hii zimeangaliwa changamoto zinazoibuka katika kutafsiri Kiswahili katika muktadha wa wingilugha.Tumeangazia chagamoto hizo wakati ambapo tafsiri inapotekelezwa kutoka Kimaasai (lugha ambayo tumetumia kuwakilisha lugha nyingine katika muktadha wa wingilugha) hadi Kiswahili na vile vile kutoka lugha ya Kiswahili hadi Kimaasai.Tumeweza kubainisha tofauti ambazo zinatofautisha lugha ya Kiswahili na ya Kimaasai.Tumebainisha jinsi tamaduni za lugha hizi mbili zinavyotofautiana katika maeneo yafuatayo: Mavazi na mapambo, aina za vyakula,dhana ya rika katika jamii, dhana ya koo/mbari katika jamii,majina ya kurejelea wapendwa katika jamii kwa kurejelea Wamaasai na Waswahili.

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!