CHANGAMOTO ZA KITAMADUNI KATI YA LUGHA CHANZI NA LUGHA LENGWA KATIKA TAFSIRI

By , in TAFSIRI/UKALIMANI on .
Makala hii inasehemu kuu tatu: sehemu ya kwanza ni
fasili ya tafsiri, utamaduni na vipengele vya kiisimu ambavyo vinaleta
changamoto katika mchakato wa kutafsiri. Sehemu ya pili ni vipengele vya
kiutamaduni vinavyosababisha changamoto katika shughuli ya kutafsiri. Sehemu ya
tatu ni hitimisho.

 

Wataalamu mbalimbali wanaeleza tafsiri kama
ifuatavyo:
Newmark (1988) na Mwansoko na wenzake (2006) wanaelekena sana katika fasili zao
ambapo wanaeleza kuwa: tafsiri ni zoezi la kuhawilisha mawazo au maneno ya
lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Kwa upande wa Nida na Taber  (1969)
wanatofautiana kidogo na mawazo ya wataalamu wenzake kwa kutueleza kuwa:
kutafsiri hujumuisha kuzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe
asilia vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi kimaana na
kimtindo.
Kutokana fasili za wataalamu hawa tunaweza kutoa maana ya tafsiri kuwa: ni
uhawilishaji wa mawazo yaleyale yaliyoandikwa katika matini chanzi kuyapeleka
katika matini lengwa.
Pia maana ya utamaduni imefasiliwa na wataalamu kama ifuatavyo:
Newmark (1988) anaeleza kuwa: utamaduni ni mkusanyiko wa mila na desturi zote
za jamii inayotumia lugha mahususi kama njia yake ya mawasiliano.
Ruhumbika (1978:261) anatofautiana na mawazo ya Newmark kueleza utamaduni kwa
kupinga kwamba utamaduni wa binadamu si mila na desturi zake na mambo ya yake
tu. Bali utamaduni ni jumla ya juhudi zote za jamii fulani katika kila
kipengele cha maisha, katika umma wake, katika filosofia zake za maisha, mfumo
wa sheria zake, mbinu zake za ulinzi na usalama wa nchi, taratibu za kuelimisha
raia zake, taratibu zake za mgawanyo wa kazi za uzalishaji mali na mifumo ya
ugawaji wa matunda ya kazi hizo na juhudi za kuiwezesha jamii isonge mbele.
Kwa upande wa tofauti za kiisimu ambazo ni changamoto katika shughuli ya
kutafsiri hujidhihirisha katika vipengele vikuu vinne yaani maumbo sauti,
maumbo ya maneno, miundo ya sentensi pamoja na maana.

Baada
ya kueleza fasili ya tafsiri  na utamaduni pamoja na
kuainisha  vipengele vya kiisimu ambavyo ni changamoto katika
tafsiri. Tuangalie sehemu ya pili ambayo ni tofauti za kiutamaduni ni
changamoto kwa wafasiri wote katika shughuli nzima ya tafsiri. Vipengele
vya kiutamaduni vinavyosababisha changamoto hizo zimebainishwa na wataalamu
kama ifuatavyo,

Nida
(1964) akinukuliwa na Mwansoko na wenzake (2006:31) na Newmark (1988:95) visawe
vya utamaduni wamevibainisha katika makundi matano yaani: ekolojia,
violwa, mila na desturi, siasa na dini.
 Licha ya wataalamu hawa
kubainisha katika makundi matano kwa ujumla tumeweza kubaini kwamba kipengele
cha kisiasa kinajitegemea hakiwezi kuingizwa katika utamaduni na kipengele cha
dini nacho kinaingia katika kipengele cha mila na desturi. Hivyo kutokana na
mawazo haya vipengele vya kiutamaduni tumevibainisha katika makundi manne yaani:
ekolojia, violwa na mila na desturi pamoja na semi kwa mujibu wa mawazo yetu
Tukianza kueleza kipengele kimoja hadi kingine namna vilivyo na changamoto
katika tafsiri kwa mfasiri au wafasiri.
Ekolojia: suala la tabia za kijiografia kwa kawaida zinaweza
kutofautiana kati ya utamaduni wa jamii moja na nyingine. Hivyo kwa mfasiri ni
ugumu sana kupata visawe mwafaka kwa maneno husika. Mfano lugha ya Kiswahili
huzungumzwa zaidi katika nchi za joto hususani za Afrika Mashariki ambapo
tunabainisha misimu minne ya mwaka yaanikiangazi, vuli, masika na kipupwe.
Lakini Kiingereza huzungumzwa nchi za baridi hususani Uingereza wao hubainisha
misimu minne pia ya mwaka summer, autumn, winter na spring. Lakini
kwa waingereza:
 Summer ni kiangazi (lakini
joto la kiangazi ni kali zaidi ya lile la
Summer wanalolifahamu
Waswahili)
Winter-kipupwe (lakini
baridi ya winter kwa Waingereza ni kali
zaidi ya ile ya baridi
ya kipupwe wanayoifahamu Waswahili)
Pia kuna michezo ambayo hufanyika sehemu zenye baridi ambayo kwa kawaida
haiwezi kufanyika  nchi za joto kama hizi za Afrika Mashariki. Kwa
mfano:
Skate-sketi (mchezo wa kusketi).
Ski-
skii (mchezo wa kuskii).
Hivyo kwa mfasiri itamwia vigumu sana kupata visawe sahihi hususani
anapofasiri matini ya kiingereza kuzipeleka Kiswahili. Kwa sababu vipindi kama
hivyo hatuna na michezo hiyo haipo kwa hiyo kupata kisawe mwafaka kwa neno
husika ni vigumu.
Violwa: kuhususha suala la uvumbuzi wa kisayansi na teknolojia
kuingizwa katika nchi zetu zinazoendelea. Uvumbuzi na ubunifu huu umeathiri
sana utamaduni wa lugha yetu ya Kiswahili na kusababisha wafasiri kushindwa
kupata visawe mwafaka kwa baadhi ya maneno katika lugha ya Kiswahili. Badala
yake kinachofanyika ni kutohoa maneno hayo kutoka katika lugha ya Kiingereza
kwa kuyafanyia tu marekebisho ya kisarufi yanapoingizwa katika lugha yetu yaani
ya kimatamshi na kimaumbo. Kwa mfano:
Kiingereza            Kiswahili
Radio                    redio
Chemical               chemikali
Telefax                  telefaksi,
Digital                  
digitali
Software              softiwea
Hardware          hadiwea

Mila
na desturi:
 tofauti hizi inaweza
kujidhihirisha kupitia ulaji, vinywaji, mavazi na imani (dini) baina ya
utamaduni wa jamii moja na jamii nyingine. Hivyo basi tofauti hizo ni
changamoto kubwa sana kwa mfasiri au kwa wafasiri wakati wa kutafsiri. Tukianza
na:
Ulaji: utamaduni wa Waswahili wanamilo mikuu mitatu tu yaani kifungua
kinywa, chakula cha mchana na chakula cha jioni
. Lakini Waingereza wao
wanamilo mikuu mitano yaanibreakfast, lunch, high tea, dinner na supper.
Kwa hiyo kwa mfasiri wa Kiswahili high teaambayoni chai nzito kwa
kawaida ambayo hunywewa 11-12 jioni itampa ugumu kuifasiri. Kwani katika
utamaduni wetu wa Waswahili hatuna chai ambayo watu wanakunywa wakati huu.
Hata supper mlo wa usiku kwa kawaida mwepesi pia itamwia
vigumu sana kwa wafasiri kupata visawe kwa sababu katika utamaduni wetu hatuna
chakula ambacho huwa kinaliwa wakati huu.
Pia hata Wafaransa wanamlo ambao huliwa kabla ya “Lunch” uitwao “Appacative” mlo
huu kwa utamaduni wa Waswahili haupo hivyo kwa mfasiri ni vigumu sana kupata
kisawe chake kitakachofanyika ni kutumia mbinu ya ufafanuzi kuwafanya hadhira
lengwa kuelewa nini kinachomaanishwa.
Hata upande wa matini za Kiswahili ambapo mfasiri anapofasiri matini ya
Kiswahili kuipeleka katika lugha ya Kiingereza atashindwa kufasiri maneno ya
vyakula kama vile:ugali na kande kwa sababu katika
utamaduni wa Waingereza hakuna vyakula hivi atakachofanya mfasiri ni kutumia
mbinu ya kuhawilisha maneno kama yalivyo kuyapeleka katika lugha lengwa au
kutumia mbinu ya ufafanuzi.
Vinywaji: kwa upande wa vinywaji baridi vinavyonywewa katika utamaduni wa
Waingereza vimekosa visawe katika utamaduni wetu wa Waswahili. Kwa hiyo kwa
wafasiri ni changamoto kinachofanyika yanatoholewa na kufanyiwa mabadiliko ya
kisarufi hususani ya kimatamshi na kimaumbo.
Kwa mfano:
Cognac-konyagi, Whisky-wiski, Beer -bia .
Pia kwa matini ya Kiswahili kuipeleka Kiingereza kuna baadhi ya vinywaji
vinavyopatikana katika utamaduni wa Waswahili lakini utamaduni wa Waingereza
havipo.
Kwa mfano:
Ulanzi, Mbege, Chibuku,
Gongo

Kwa
hiyo upande wa mfasiri ni vigumu sana kupata visawe kwa maneno haya. Mfasiri
anakichofanya ni kutumia mbinu ya kuyahawilisha kama yalivyo kuyapeleka katika
matini lengwa.
Mavazi: upande wa mavazi ni changamoto vilevile kwa wafasiri wote hususani pale
unapokutana na mavazi ambayo asilia yake ni utamaduni fulani mfano yale ya
Waingereza ambayo yanatengenezwa katika nchi yao. Suala hili linajidhihirisha
katika jamii zetu za Waswahili mavazi mengi yanatoka nchi za Magharibi.
Kinachofanyika yanatoholewa na kuyafanyia mbadiliko kidogo ya kisarufi ambayo
kama vile ya  kimatamshi na kimaumbo.
Kwa mfano:
Skirts-sketi, Jeans-jinsi, Pullovers-pulova
Pia kwa mavazi ambayo kwa asili hutengenezwa katika nchi zetu vigumu sana
kupata visawe yakitumika katika matini za Kiswahili wakati wa kutafsiri, kwa
sababu nguo hizi zipo tu katika utamaduni wetu wa Waswahili. Utamaduni wa nchi
za wenzetu hazivaliwe na hazitengenezwi. Kwa hiyo wafasiri wanachokifanya ni
kuyahawilisha kama yalivyo wakati wa kutafsiri au ktumia mbinu ya ufafanuzi
kuwafanya hadhira lengwa kujua nini kinachomaanishwa.
Kwa mfano:
   Khanga,  Kiko,
Kitenge

Dini:
kwa wafasiri masuala ya dini pia ni changamoto kubwa sana, kwani baadhi ya
maneno mfano yatumiwayo katika utamaduni wa Waingereza yanayotaja nyama kama
vile nyama ya nguruwe  Pork-nyama
ya nguruwe.
Harm-paja la nguruwe lililokolea chumvi na kukaushwa katika moshi.
Bacon-nyama ya nguruwe iliyotiwa chumvi au kutengenezwa isioze.
Ni vigumu sana kupata visawe vyake katika lugha ya Kiswahili kutokana na kwamba
utamaduni wa Waswahili kuathiriwa kwa kiasi fulani utamaduni wa
lugha  ya kiarabu ambayo waamini wake wengi ni waislamu. Wafasiri
wanachokifanya ni kutumia mbinu ya kuyahawilisha maneno haya kama yalivyo na
kuyapeleka katika matini lengwa.
Kwa mfano: Kadhi, Hijabu, Nikabu., Sheikh.

Semi
ni tungo au kauli fupifipu za kisanaa zenye lugha ya mafumbo ambazo hukusudia
kuleta mafunzo kwa jamii husika. Semi ni moja ya kipengele kigumu katika
kufanya kazi ya kutafsiri. Hii ni kutokana na tofauti kati ya utamaduni wa jamii
moja na nyingine. Semi hizi zinaweza zikatumika katika jamii moja na jamii
nyingine zisitumike semi hizo. Kwa hiyo hujidhihirisha katika vipengele vyake.
Kwa mfano:
Methali –  Ndondondo si chururu, chururu si ndondondo.

Nahau 
     –Mkono
mrefu 
(mchoyo),  –Zunguka mbuyu (toa
rushwa), -Amevaa miwani(amelewa)
Misimu –   Amejaa upepo (amekasirika),
Amenitoa upepo ( nimempa fedha)
Vitendawili- Kuku wangu anataga mibani (nanasi),  –Popo
mbili zavuka mto
 (macho)
Misemo –   Mtu ni afya (kuzingatia
usafi),  –Maji ni uhai (kulinda vyanzo vya maji).
Metheli za kiingereza kama vile

Advance
is least heeded when most needed
.
Maana yake when the
problem is serious people often don’t follow the advice given.
-All cats are grey in the dark.
Maana yake people are
undistinguished until they have made a name.
-A bad tree does not yield good apples. Maana yake a bad parent
does not raise good children.
Hivyo basi wafasiri wengi wanachokifanya ni kutafuta semi ambazo huwa
zinakaribiana na zile za lugha lengwa kwa lengo la kufikisha ujumbe
uliokusudiwa  kwa hadhira lengwa hali ambayo inaweza kupotosha maana
halisi ya semi husika ya matini chanzi ambayo inafungamana na utamaduni husika.
Kwa ujumla suala la kufasiri semi ni changamoto kubwa kwani semi nyingi
hufungamanishwa na utamaduni wa jamii husika. Hivyo ni vizuri kufanya utafiti
wa kina kwa wafasiri wote kabla ya kufanya tafsiri kwa hadhira chanzi kwa lengo
la kuepukana changamoto hizi kwa kiasi fulani.
Changamoto hizi namna zitakavyoepukwa na wafasiri katika shughuli nzima
ya kutafsiri kama ifuatavyo
:
Suala la msingi kwa mfasiri ni lazima afahamu fika utamaduni wa lugha lengwa:
hii itamsaidia mfasiri au wafasiri kufanya kazi za kutafsiri kwa ufanisi.
Sululisho hili ni kwa mujibu wa maoni ya Mwansoko na wenzake (2006:36).
Kwa maelezo ya
wataalamu hawa mfasiri itamlazimu kutafiti kiundani sana utamaduni wa lugha
ambayo anashughulikia.
Mfasiri anapaswa awe na umulisi wa lugha chanzi na lugha lengwa: ili anapokosa
visawe mwafaka aweze kutumia mbinu ya ufafanuzi ili kuweka wazi wazo lililopo
katika matini chanzi anapolitafsiri katika matini lengwa kwa lengo la kumfanya
mteja au hadhira lengwa waelewe nini kinachomaanishwa.
Wataalamu wamejaribu kupendekeza mbinu kadha za kuepukana na changamoto za
kiutamaduni wakati wa kutafsiri kwa mfasiri kama vile:

Matumizi ya tafsiri huru
: mfasiri awe na
ubunifu wa kuunda visawe vipya vinavyokubalika na lugha lengwa, hii itamsaidia
mfasiri kupata visawe vinavyoendana na lugha chanzi wakati wa kufanya kazi yake
ya kutafsiri kwa matini ambayo anaishughulikia.
Kukopa maneno: ni mbinu nzuri zaidi kwa mfasiri wakati wa
kukabiliana na vipengele vya kiutamaduni vya matini chanzi kwa kutumia visawe
vinavyokaribiana au kufanana na vile vya matini lengwa ambavyo vinafahamika na
wasomaji wa matini lengwa. Kwa kuzingatia sheria na kanuni za lugha lengwa kwa
dhana zisizofahamika. Ukopaji huu upo wa aina mbili yaani wa moja kwa moja
(uhawilishaji) yaani ambao unafanyika pasipo kubadili umbo lolote la neno la
lugha chanzi.
Kwa mfano:
 kiingereza   (data)       Kiswahili   (data)

Kiswahili      (ugali )      Kiingereza   (ugali)

Ukopaji
wa kubadilisha umbo la matamshi na umbo la neno (utohoaji): ukopaji ambao kuna
mabadiliko kidogo ya kisarufi kwenye maneno ambayo yamekopwa kutoka lugha
chanzi au lugha nyingine ambako neno hilo limekopwa kama vile  ya
kimatamshi na kimaumbo.
Kwa mfano:
Kiingereza        (Account,
Photo)
Kiswahili          (akaunti,  Foto)
Matumizi ya tanbihi: mfasiri anatakiwa kutoa maelezo ya ufafanuzi wa kina zaidi
kuhusu zile dhana ngumu ambazo zinakuwa vigumu kueleweka na hadhira lengwa au
mteja, wakati aisomapo matini husika kila mwishoni mwa kila ukurasa. Pamoja na
faharasa mwishoni mwa kazi yake ya tafsiri.
Hitimisho: mfasiri hana budi kuzingatia kwa makini kipengele cha utamaduni
pindi afanyapo kazi ya kufasiri ili asiweze kuhuisha maana iliyomaanishwa
katika matini chanzi. Wakati anafanyapo kazi ya kuifasiri matini ambazo
zinafungamanishwa na utamaduni wa jamii fulani.
MAREJEO
Mwansoko, H. J. M. na wenzake, (2006) Kitangulizi cha Tafsiri:
Nadharia na Mbinu
.
Dar es Salaam: TUKI.
Newmark, P. (1988) A Textbook of Translaton. London: Prentice Hall.
Nida, A. E. na C. R Taber, (1969) The Theory and Practice of
Translation
. London: Prentice Hall.
Ruhumbika, G. (1978) “Tafsiri za Kigeni katika Ukuzaji wa Fasihi
ya Kiswahili
” Makala kwenye Semina za Kimataifa ya Waandishi wa
Kiswahili Dar es Salaam : TUKI.
Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!