CHAMA CHA UKUZAJI WA KISWAHILI DUNIANI (CHAUKIDU)

By , in Kidato I-IV Kidato V-VI on . Tagged width:

Katiba ya Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU)

 1. JINA LA CHAMA: Chama hiki kitaitwa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani, na kwa hiyo kifupi chake ni CHAUKIDU.
 2. MAKAO MAKUU YA CHAMA: Makao makuu ya Chama Cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) yatakuwa katika mji na jimbo ambamo rais wa chama hicho atakuwa anaishi na kufanyia kazi. Makao makuu yanaweza kuhamishiwa katika sehemu nyingineyo kufuatia maamuzi ya uongozi wa bodi ya CHAUKIDU.
 3. MADHUMUNI YA CHAMA: Madhumuni makuu ya CHAUKIDU ni: Kuwajumuisha pamoja wadau wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo mahususi yafuatayo:

3.1.  Kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika au inaweza kutumika na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote, uandishi/utangazaji wa habari, uandishi wa vitabu, uchapishaji vitabu na majarida, utayarishaji wa safari za mafunzo katika Afrika ya Mashariki na Kati, n.k.

3.2. Kusambaza habari, mijadala na matokeo ya utafiti kwa kutumia machapisho mbalimbali na teknolojia ya mtandao wa kompyuta juu ya vipengele na masuala mbalimbali yanayohusiana na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili.3.3. Kuwajumuisha wanachama kwa ajili ya kubadilishana mawazo na tajiriba zao katika masuala mbalimbali yanayohusu Kiswahili (k.m. uboreshaji wa ufundishaji, utangazaji, utafiti, uandishi, nk.) kwa njia ya mkutano wa kila mwaka, warsha au semina au kongamano maalumu, na hata kwa njia ya mtandao.

3.4. Kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kujivunia, kuendeleza, na kuheshimu Kiswahili.

3.5. Kushauri ama kushinikiza serikali za nchi ambamo Kiswahili kinazungumzwa kutambua thamani iliyobebwa na rasilimali hii ili kuunda sera muafaka za kukiendeleza kadri ya uwezo wake kwa manufaa ya maendeleo ya nchi na watu wake kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kielimu, n.k.

 1. UANACHAMA: Wanachama watarajiwa ni pamoja na walimu, watafiti, wanafunzi, waandishi wa habari, wasanii, waandishi wa vitabu, wachapishaji, maafisa utalii, taasisi, n.k.

4.1. Kujiunga na Chama: Bodi ya Uongozi itachunguza maombi yote ya uanachama na wanaokubaliwa watajiunga na chama kwa mujibu wa katiba hii. Kwa kuwa kujiunga kwa wanachama wapya hutegemea ulipaji wa ada kwa mwaka, basi kiasi ambacho kitakuwa kikilipwa kila mwaka kitaamuliwa na Bodi ya Uongozi wa CHAUKIDU.

4.2. Uanachama wa kulipia utakuwa wa aina mbili:

4.2.1.   Uanachama wa kibinafsi

4.2.2.   Uanachama wa kitaasisi

4.3. Uanachama wa kutunukiwa: Uanachama huu unaweza kutolewa kwa mtu au taasisi yoyote kufuatia maamuzi ya Bodi ya CHAUKIDU kwa kuzingatia mchango wa mwanachama/taasisi hiyo katika kuchangia kuyafikia malengo ya chama.

4.4. Ada za uanachama zitatofautiana kwa kuzingatia makundi yafuatayo:

4.4.1.     Mwanachama anayekaa/taasisi iliyoko:

4.4.1.1.   Barani Afrika

4.4.1.2.    Kwingineko duniani

4.4.1.2.1. Ada ya mwanachama asiye mwanafunzi

4.4.1.2.2.   Ada ya mwanachama mwanafunzi

4.5. Haki na wajibu wa wanachama: Wanachama wa CHAUKIDU watakuwa na haki na pia wajibu kwa chama.

4.5.1.   Haki za wanachama: Wanachama wote waliolipa ada wana haki zifuatazo:

4.5.1.1. Haki ya kuhudhuria mikutano ya chama

4.5.1.2. Haki ya kupiga kura katika uchaguzi wowote wa chama.

4.5.1.3. Haki ya kutoa maoni yao katika mikutano ya chama kwa njia au utaratibu maalum ulioandaliwa na chama (barua pepe, mtandaoni n.k)

4.5.1.4. Haki ya kupitia na kusoma machapisho yanayochapishwa na chama

4.5.1.5. Haki ya kugombea nafasi ya uongozi katika bodi ya chama au/na kamati za chama

4.5.2.    Wajibu wa wanachama.  Kila mwanachama ana wajibu ufuatao:

4.5.2.1. Wajibu wa kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazoendeleza malengo ya chama

4.5.2.2. Wajibu wa kuhudhuria mikutano ya chama

4.5.2.3. Wajibu wa kulipa ada ya uanachama pamoja na ada ya kila mwaka kama itakavyoamuliwa na Bodi ya Uongozi bila kuchelewa.

4.5.2.4.   Wajibu wa kujiunga na kamati mbalimbali za chama.

4.5.2.5.   Wajibu wa kujibu ujumbe wowote atakaopokea kutoka kwa uongozi wa chama ama wanachama kwa haraka inawezekanavyo.

4.5.2.6.   Wajibu wa kusasisha anuani yake katika kumbukumbu ya chama ili kiweze kuwasiliana naye.

4.5.2.7.   Wajibu wa kulinda na kutetea malengo, maslahi, heshima na hadhi ya CHAUKIDU.

4.6. Kujiondoa kwenye Chama kwa hiari: Mwanachama yeyote anaweza kujiondoa kwa hiari kwa kuiandikia Bodi ya Uongozi tarehe ambayo angelipenda kujiondoa kwenye chama. Tarehe hiyo ikifika, mwanachama huyu atakuwa na haki ya kujiondoa kuwa mwanachama. Kuanzia tarehe ambayo atajibiwa, haki na wajibu wa mwanachama huyo katika chama vinasimamishwa.  Mwanachama anayejiondoa kutoka kwenye chama kwa hiari au kwa kuondolewa kulingana na ibara ya 4.7 au kwa kutotimiza wajibu wake chini ya masharti ya vifungu vilivyoko kwenye ibara ya 4.5.2, hatarudishiwa sehemu yoyote ya ada alizolipa akiwa mwanachama.

4.7. Kusimamishwa na kuondolewa katika Chama: Mwanachama anaweza kuondolewa katika chama kwa muda au moja kwa moja kulingana na jinsi Bodi ya Uongozi itakavyoamua.  Hali hii inaweza kutokea iwapo mwanachama huyo halipi ada ya mwaka, anafanya vitendo au anaonesha tabia ambazo uongozi wa Bodi unaona zinahatarisha maslahi na hadhi ya chama. Baada ya uongozi wa Bodi kutumia mamlaka iliyopewa na wanachama wote kupitisha azimio la kumsimamisha mwanachama, haki na majukumu ya mwanachama huyo vitasimamishwa mara moja.  Kama mwanachama amesimamishwa kwa muda, atarudishiwa haki na wajibu wake mara moja baada ya kumaliza kipindi alichokuwa amesimamishwa. Kipindi hicho lazima kiwe kimewekwa bayana katika azimio la Bodi ya Uongozi lililopitishwa ili kumsimamisha mwanachama huyo kwa muda.

 1. MIKUTANO YA WANACHAMA

5.1. Mkutano wa kila mwaka: Bodi itawajibika kuitisha na kutangaza tarehe na mahali pa mkutano wa wanachama kila mwaka.

5.2. Mikutano ya dharura: Bodi itakuwa na uwezo wa kutangaza mkutano wa dharura wakati wowote.  Ni lazima bodi imjulishe kila mwanachama kwa ujumbe ulioandikwa siku thelathini au zaidi kabla ya siku ya mkutano huo.

5.3. Akidi ya Mkutano Mkuu: Mkutano mkuu wa kawaida wa wanachama unaweza kufanyika kihalali ili kujadili shughuli za chama kwa idadi yeyote ya wanachama halali ambao watahudhuria. Wanachama wengine ambao hawataweza kuhudhuria mkutano huo watajulishwa majadiliano au maazimio ya mkutano huo kwa njia ya barua pepe.

5.4. Utaratibu: Katika mkutano wowote wa chama, Rais wa Chama atakuwa mwenyekiti wa mkutano.  Ikiwa Rais hayupo au hawezi kufanya kazi ya uenyekiti kutokana na udhuru, Makamu Rais wa Chama atachukua nafasi hiyo.  Ikiwa Makamu wa Rais hayupo kutokana na udhuru, wanachama waliohudhuria watachagua mwenyekiti wa muda.  Mkurugenzi wa chama atakuwa katibu mwendeshaji wa mkutano.  Endapo Mkurugenzi hayupo kutoka na udhuru, Naibu Mkurugenzi atafanya kazi hiyo. Na ikiwa Naibu Mkurugenzi pia hayupo kutokana na udhuru, mwenyekiti wa mkutano atachagua katibu wa muda.

5.5. Uchaguzi:  Kila mwanachama halali aliyelipa ada zake ana haki ya kupiga kura moja kuhusu kila suala linalojadiliwa au kuchagua viongozi wa nafasi mbali mbali za chama. Mwanachama asipoweza kuhudhuria mkutano, ataweza kupiga kura bila kuwepo kwa njia ya kieletroniki katika muda uliopangwa. Mshindi atakuwa mgombea ambaye atapata kura zaidi ya wagombea wengine. Endapo kura za wagombea wawili wa juu zinalingana, wanaweza kupigiwa kura ya marudio ili kupata mshindi.

 1. BODI YA UONGOZI

6.1. Majukumu kwa ujumla: Mali ya chama itasimamiwa na Bodi ya Uongozi na wanachama wote watakaokitumikia chama hawatalipwa posho au ujira. Bodi ya Uongozi itaboresha mahusiano na vyama vingine ambavyo vitakuwa na malengo yenye mwelekeo kama wa CHAUKIDU.

6.2. Idadi ya wajumbe wa Bodi:  Idadi ya wawakilishi wa wanachama watakaochaguliwa moja kwa moja na wanachama wenzao kwa ajili ya kujiunga kwenye Bodi ya Uongozi itakuwa ni kumi na mbili (12). Baada ya kuchaguliwa, Bodi itakuwa na uwezo wa kuteua wajumbe wengine wasiozidi wanane (8) ili kuwakilisha maeneo ya kijiografia, jinsia, makundi au taasisi maalum ambazo Bodi inaamini ushiriki wao ni muhimu katika utekelezaji na ufanisi wa shughuli za chama kwa ujumla. Pia kutakuwa na wajumbe maalum wa Bodi wafuatao: rais aliyemtangulia rais wa sasa wa chama, Mwenyekiti wa Tume ya Katiba na Uchaguzi, na Mhariri Mkuu wa machapisho. Wajumbe hawa watakuwa na haki kamili ya kupiga kura kama wajumbe wa Bodi ya Uongozi.

6.3. Taratibu za uchaguzi: Mkutano mkuu wa chama utawachagua Rais, Makamu wa Rais, Mkurugenzi, Naibu Mkurugenzi, Mweka Hazina na Katibu Mwenezi wa Chama na pia wajumbe wengine sita ambao kwa pamoja wataunda Bodi ya Uongozi. Wanabodi hawa kumi na mbili pamoja na wale wanane ambao watateuliwa na Bodi watakuwa uongozini kwa kipindi cha miaka miwili. Viongozi wakuu wa chama yaani Rais, Makamu wa Rais, Mkurugenzi na Naibu Mkurugenzi wanaweza kugombea na kuchaguliwa tena kukaa madarakani kwa vipindi viwili mfululizo (jumla ya miaka minne). Watakuwa na haki ya kugombea tena nafasi hizo baada ya kipindi cha miaka miwili au muhula mmoja wa uongozi mwingine. Masharti haya hayatawahusu wajumbe wengine wowote wa Bodi. Kama kutakuwepo na nafasi ya wazi ya uongozi ambayo inatokana na sababu zozote zile inaweza kujazwa kwa utaratibu utakaotolewa na Tume ya Katiba na Uchaguzi.

6.4. Tume ya Katiba na Uchaguzi (TKU): Kutakuwepo na Tume ya Katiba na Uchaguzi yenye wajumbe watano watakaochaguliwa na wanachama wa mkutano mkuu. Mwenyekiti wa Tume atachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe watano. Muhula wa Tume utakuwa kipindi cha miaka mitatu na uchaguzi wa wajumbe wa tume utafanyika katika mwaka ambao uchaguzi wa Bodi haufanyiki.

6.4.1. Mchakato wa Uchaguzi: Wakati wa uchaguzi wa Bodi, Tume itatangaza nafasi za uongozi zilizo wazi na kuwataka wanachama wanaotaka kugombea watume maombi yao katika muda utakaopangwa na Tume. Baadaye, Tume itapitia maombi hayo na kutangaza majina ya wanachama watakaogombea nafasi mbali mbali za Bodi ya Uongozi. Uchaguzi unaweza kuendeshwa na kukamilishwa katika muda utakaopangwa na Tume ya Uchaguzi kupitia upigaji kura wa njia za kieletroniki. Uchaguzi huo utaendeshwa kwa utaratibu wa kupiga kura kwa njia ya siri na kwa kuzingatia taratibu zilizoko kwenye ibara ya 6.2 na 6.3. hapo juu.

6.4.2. Tume hii pia itakuwa na jukumu la kupokea maoni na mapendekezo ya kufanyika marekebisho ya Katiba ya Chama kulingana na taratibu zilizoainishwa kwenye vifungu vya 11 na 12 vya Katiba hii.

6.5. Mkutano wa mwaka: Bodi itaitisha mkutano wake kwa ajili ya kushughulikia maswala ya chama wakati na mahali itakapoamua mkutano huo ufanyikie. Uamuzi huo unaweza kufikiwa wakati wa mkutano au kwa kuwasiliana kupitia barua pepe.

6.6. Mikutano ya dharura: Mkutano wa dharura utaitishwa na bodi yenyewe kufuatia ombi la Rais wa chama au wajumbe watatu wa bodi hiyo.

6.7. Taarifa ya mkutano wa dharura: Taarifa ya mkutano maalum ya Bodi lazima itolewe kwa kila mwanabodi kwa kumtumia taarifa hiyo katika anuani yake ya barua pepe aliyokuwa akiitumia kwa mara ya mwisho kabla ya taarifa hii. Taarifa hii itatumwa si chini ya siku kumi kabla ya siku ya mkutano.

6.8. Akidi ya vikao vya Bodi: Ili kuweza kuendelea na mkutano wa Bodi lazima wajumbe watakaokuwa wamehudhuria wafikie angalau asilimia hamsini (50%). Ikitokea kuwa wajumbe hawafikii idadi inayotakikana, wajumbe walio wengi wa mkutano huo wataweza kupiga kura za kuuahirisha mkutano huo mpaka hapo baadaye wakati ambapo akidi inayohitajika itatosheleza. Mikutano ya Bodi itafanyika katika muda na wakati ambao utawezesha wajumbe walio wengi waliko maeneo mbali mbali ya dunia waweze kuhudhuria kwa kujiunga kupitia njia ya mtandao.

6.9. Kujiuzulu: Mjumbe yeyote wa Bodi anayetaka kujiuzulu atatoa taarifa ya maandishi kwa Bodi siku thelathini kabla ya kujiuzulu.

6.10. Kuondolewa katika uongozi: Kiongozi yeyote wa Bodi aliyechaguliwa au kuteuliwa anaweza kusimamishwa uongozi muda wowote na Bodi ya Uongozi ikiwa atashindwa kutekeleza wajibu kama kiongozi au kukiuka wajibu na masharti ya uanachama.

6.11. Kuteua kiongozi wa muda: Ikitokea kiongozi mmojawapo hayupo kwa sababu ambazo ni za msingi, Bodi inaweza kumteua mtu mwingine kushika nafasi hiyo kwa kipindi watakachoona kinafaa.

6.12. Kamati mbalimbali: Rais atateua kamati na vitengo mbalimbali kwa kadri zitakavyohitajika baada ya kushauriana na Bodi ya Uongozi. Kila kamati itakuwa na wajibu wa kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa katiba hii. Wajumbe wa kamati hizo hawapaswi kuwa wanabodi ikiwa kazi za kamati hiyo sio kazi nyeti ambazo lazima Bodi izishughulikie. Wajumbe wa kamati na vitengo hivyo wanaweza kuhusishwa kwenye mikutano ya Bodi endapo masuala na ajenda zinazozungumziwa zinahitaji uwepo wao.

 1. MAAFISA WA CHAMA: Bodi ya Uongozi inaweza kuteua Katibu wa Bodi (kama ni lazima) ili kuwa mjumbe wa Bodi asiyekuwa na haki ya kupiga kura kwa muda wa miaka miwili. Bodi ina mamlaka wakati wowote kuunda nafasi nyingine za uongozi na kuchagua viongozi wengine wa kamati au vitengo mbali mbali kwa manufaa ya chama. Bodi inaruhusiwa kuteua maafisa kama ambavyo itaonekana inafaa na kutoa taarifa kwenye mkutano mkuu wa wanachama. Katibu wa Bodi na maofisa wengine walioteuliwa watashika madaraka katika kipindi sawia cha uongozi au sehemu iliyobaki ya kipindi cha uongozi wa Bodi.

7.1. Rais wa Chama na Makamu wa Rais: Rais wa chama ndiye atakuwa msemaji mkuu wa chama na ataongoza mikutano yote ya chama na ya Bodi ya Uongozi. Anaweza pia kuitisha mikutano mbali ya mkutano mkuu wa wanachama wote. Endapo Rais hataweza kuhudhuria kutokana na udhuru, Makamu wa Rais ataendesha mikutano ya chama kwa niaba yake. Rais atakuwa na uwezo wa kusimamia na kukagua masuala ya chama kwa kushirikiana na Bodi ya Uongozi. Atakuwa na madaraka mengine na wajibu mwingine ambao haukuelezwa katika katiba hii kama ambavyo atakuwa amepewa wajibu au jukumu hilo na Bodi ya Uongozi.

7.2. Mkurugenzi wa Chama na Naibu Mkurugenzi wa Chama: Mkurugenzi wa chama atakuwa ndiye Afisa Mtendaji Mkuu (AMM) wa shughuli za chama akisadiwa na Naibu Mkurugenzi wa Chama. Endapo Mkurugenzi hayupo kutokana na udhuru, Naibu Mkurugenzi ataendesha shughuli za chama kwa niaba yake.  Ofisi ya Mkurugenzi itakuwa na majukumu yafuatayo:

7.2.1. Kutunza takwimu na nyaraka zote za chama, ikiwa ni pamoja na kusimamia mawasiliano yote ya chama na wadau, ofisi au vyombo vingine nje ya chama;

7.2.2. Kuwajulisha wanachama wapya kuwa uanachama wao umeidhinishwa;

7.2.3. Kutunza nyaraka zikiwa na majina na anuani za wanachama;

7.2.4. Kuwa Katibu wa Bodi na kutunza mihtasari ya mikutano ya Bodi ya Uongozi (endapo hakuna Katibu wa Bodi aliyeteuliwa);

7.2.5. Kwa kushirikiana na Mweka Hazina, kutunza pesa na nyaraka muhimu za chama;

7.2.6. Kwa kushirikiana na Mweka Hazina, kutoa risiti za ada na malipo mengine zinazolipwa katika chama;

7.2.7.  Kwa kushirikiana na Mweka Hazina, kuweka pesa benki au kuziweka katika kampuni za uwekezaji pesa zilizopokelewa;

7.2.8. Kwa kushirikiana na Mweka Hazina, kuripoti matumizi na mapato katika Bodi ya Uongozi;

7.2.9. Kwa kushirikiana na Mweka Hazina, kuwaonyesha wajumbe wa Bodi ya Uongozi vitabu vya mahesabu;

7.2.10. Kwa kushirikiana na Mweka Hazina, kushughulikia kuchangisha pesa kwa ajili ya chama;

7.2.11. Kwa kushirikiana na Katibu Mwenezi, kuhamasisha wanachama wapya;

7.2.12. Kwa kushirikiana na Katibu Mwenezi, kusimamia mawasiliano na uboreshaji wa mahusiano baina ya chama na wadau, ofisi, serikali au vyombo vingine vya nje vyenye malengo au maslahi yanarandana na madhumuni ya chama.

7.2.13. Kwa kushirikiana na Jopo la Uhariri, kuchapisha vipeperushi, makala au kuteua mtu au watu wa kushughulikia tovuti, mitandao (kama facebook) na vijarida vya chama;

7.2.14. Kufanya shughuli nyingine ambazo Bodi ya Uongozi itaziidhinisha 

 1. JOPO LA UHARIRI

8.1. Kutakuwa na Jopo la Uhariri ambalo litaundwa na wajumbe saba wakiongozwa na Mhariri Mkuu. Wajumbe wa Jopo watachaguliwa na Mkutano Mkuu, na muhula wao utakuwa wa muda wa miaka mitatu.

8.2. Jopo la Uhariri litahakikisha kwamba chama kinatekeleza kikamilifu moja ya madhumuni yake makuu yaliyoanishwa kwenye kifungu cha 3.2 cha Katiba, ambayo ni kusambaza habari, mijadala na matokeo ya utafiti unaohusiana na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili duniani kote.

8.3. Jopo la Uhariri litasimamia ukusanyaji, uchambuzi, uchapishaji na usambazaji wa maoni na maandiko ya kitaaluma, ikisiri, makala na majarida mbali mbali yatakayoandaliwa na wanachama na kutolewa na chama.

 1. MICHANGO, KUWEKA PESA BENKI, HUNDI (CHEKI), MIKOPO NA MIKATABA:

9.0. kitengo cha Uhamasishaji, Michango na Ufadhili: Kutakuwa na Kitengo chenye jukumu la uhamasishaji, michango na ufadhili. Mbali na kuhamasisha wanachama na wadau kutoa michango ya aina mbali mbali kama vile kuandaa “Harambee”, kitengo hiki pia kitakuwa na jukumu la kushughulikia maombi ya ufadhili wa Chama kutoka au kwenda kwa wanachama, watu binafsi, wadau, taasisi au vyombo vingine rafiki. Kitengo hiki kitakuwa na wajumbe wawili pamoja na mwenyekiti watakaochaguliwa wakati mmoja na wajumbe wa Bodi. Muhula wa wajumbe wa kitengo hiki utakuwa muda wa miaka miwili.

9.1. Kuweka pesa benki: Pesa za chama lazima ziwekwe benki na/au katika kampuni za uwekezaji kama itakavyoamuliwa na Bodi ya Uongozi. Bodi itaamua ni benki ipi inafaa kutumika kwa minajili hiyo.

9.2. Hundi (Cheki), n.k. Hundi zote na nyaraka za uthibitisho wa madeni ya chama lazima zisainiwe na ofisa au maofisa au wadhamini wa chama kama ambavyo Bodi ya Uongozi itaona inafaa. Ahadi ya pesa zilizoahidiwa na ambazo zinatakiwa kuwekwa katika akaunti ya chama zifanyike kulingana na Bodi itakavyoona inafaa.

9.3. Mikopo: Hakuna mkopo au malipo ya awali yatakayofanywa kwa niaba ya chama na hakuna vithibitisho vya madeni vitakavyotolewa katika jina la chama, isipokuwa viwe vimeidhinishwa na Bodi ya Uongozi. Uthibitishaji wowote wa namna hiyo unaweza kuwa wa aina mbalimbali au matukio mahsusi kama vile ahadi, usalama wa mikopo au malipo ya awali yaliyopitishwa, na vitu vingine vikiwemo vitu binafsi vinavyoshikiliwa na chama.

9.4. Mikataba: Hakuna mikataba itakayoidhinishwa kwa niaba ya chama isipokuwa ile tu iliyoainishwa na Bodi ya Uongozi kwa niaba ya chama.

9.5. Kuhamisha fedha au mali ya Chama: Watu watatu, yaani Rais, Mkurugenzi, na mjumbe mmoja wa Bodi aliyeidhinishwa na Bodi ya Uongozi watakuwa na mamlaka ya kuidhinisha uhamishaji kama wa amana, pesa na mali nyingine kwa niaba ya chama.

 1. MWAKA WA FEDHA: Mwaka wa fedha wa chama utaanza tarehe Mosi Oktoba na kumalizika tarehe 30 Septemba.
 2. MAREKEBISHO YA KATIBA: Katiba hii itafanyiwa marekebisho kupitia mchakato ambao utasimamiwa na Tume ya Katiba na Uchaguzi. Mapendekezo ya marekebisho ya Katiba yanaweza kutolewa na Bodi ya uongozi au azimio la Mkutano Mkuu. Mwanachama yeyote ana haki ya kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Katiba kwenye Bodi ya Uongozi.
 3. KUIDHINISHA KATIBA:  Katiba hii pamoja na marekebisho yake vitaidhinishwa na kutumiwa kuchukua nafasi ya katiba zozote zilizotangulia. Lazima katiba hii au marekebisho yake vikubaliwe na theluthi mbili za wanachama halali ambao watapelekewa mapendekezo ya marekebisho ya katiba kwa njia ya kieletroniki na kupiga kura zao. Tume ya Katiba kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Chama watatuma nakala ya Katiba inayopendekezwa kwa wanachama wote kwa njia ya kieletroniki, ili ipigiwe kura katika kipindi cha muda wa maalum utakaopangwa na Tume. Mkurugenzi atatangaza matokeo ya upigaji kura kwa wanachama wote na kuwajulisha wakati marekebisho ya Katiba yatakapokuwa yameidhinishwa rasmi.
 4. KUTOA MAPATO: Mapato ya chama hayaruhusiwi kutolewa kwa ajili ya wanachama, maofisa au watu wengine binafsi, isipokuwa kuwalipa watu waliotoa huduma.