ATHARI ZA FASIHI SIMULIZI KATIKA FASIHI ANDISHI

By , in Kidato V-VI on . Tagged width:

FASIHI Andishi imeathiriwa pakubwa na Fasihi Simulizi kimaudhui na kifani kadri inavyobainika katika vipengele vifuatavyo:

Dhamira

Kuna mfanano mkubwa kati ya maudhui katika fasihi andishi na fasihi simulizi.

Maudhui katika fasihi simulizi na fasihi andishi yanafanana. Masuala mengi yanayoshughulikiwa na fasihi andishi yamekwisha jadiliwa na fasihi simulizi. Kile ambacho  fasihi andishi hufanya ni kuongezea masuala mapya kutokana na jamii ya kisasa.

Kwa mfano, asasi ya ndoa na nafasi ya  mwanamke katika jamii  ni maudhui katika fasihi simulizi . Maudhui haya pia  yameangaziwa katika kazi mbalimbali za fasihi andishi.

Kwa mfano, riwaya ya utengano yake Said Mohammed imeangazia suala la nafasi ya mwanamke katika jamii ambapo mwanamke amesawiriwa kama chombo cha starehe, asiye na sauti mbele ya mwamamme na amekandamizwa.

Aidha, dhana ya majaaliwa hujitokeza sana katika kazi za kinathari za fasihi simulizi. Katika baadhi ya ngano, kuna watu ambao, kupitia kwa majaaliwa wanatajirika kimiujiza baada ya kuwa maskini.

Majaaliwa ni uwezo wa mungu. Wazo  la majaaliwa katika tamthilia kama vile mfalme Edipode, ambapo Edipode anajaribu sana kukimbia utabiri kwamba angemuua babake na kimuoa mamake mzazi.

Mwishoni mwa tamthilia, utabiri huu unatokea na hivyo majaaliwa yanatimia 

Jukumu kubwa la kijamii la fasihi simulizi ni kuadilisha. Ngano, semi , nyimbo na mawaidha ni baadhi ya tungo za fasihi simulizi zilizotumiwa kuadilisha.

Kwa mfano, ngano inayohusu kisa cha fisi kumkosa ndama kwa kuila kamba iliyokuwa imemfunga ndama, ni mfano wa ngano inayotahadharisha kujiepusha na tamaa na ujinga.

Dhamira hii ya kuadilisha inajitokeza katika tungo za fasihi andishi kama vile  katika riwaya ya Adili na nduguze ya Shabaan Robert ambapo ndugu zake Adili wanageuzwa kuwa nyani kama adhabu kwa kumdhulumu Adili.

Nyenzo na malighafi

Fasihi simulizi na fasihi andishi hutumia lugha kuwasilisha mawazo ya binadamu.Fasihi simulizi ndiyo ya kwanza kutumia lugha  kiufundi kama malighafi yake.

Lugha ilitumiwa kwa njia ya methali,  na fani nyingine kama vile nyimbo na maghani.Vivyo hivyo, fasihi andishi kama vile tamthilia na riwaya iliibuka kimaandishi kutumia lugha kwa ufundi kama malighafi.

Tanzu za kimaandishi kama vile tamthilia ,riwaya, hadithi fupi na hata mashairi hutumia tamathali za usemi kama vile methali, nahau, tashbihi na jazanda.

Usimulizi

Msingi wa fasihi simulizi ni usimulizi.

Tanzu nyingi za fasihi simulizi huwasilishwa kwa  masimulizi kama vile tendi, majigambo na rara. Riwaya   kama vile lila na Fila na kipendacho roho  zimeandikwa kwa mtindo wa ngano za kimapokeo; hali  inayoonyesha athari za tanzu za fasihi simulizi.

Katika tungo za fasihi simulizi, fanani husimulia hadithi katika nafsi ya tatu.Kazi ya fasihi andishi pia hutumia nafsi ya tatu.

Utendaji

Fasihi simulizi ni tendi.  Vivyo hivyo, upo uwezekano wa kutenda fasihi andishi.Kwa mfano, tamthilia huigizwa jukwaani, ngonjera huambatanishwa na vitendo.Tamthilia kama vile kifo kisimani na Mstahiki Meya zimeigizwa jukwaani kama ilivyo katika fasihi andishi.

Fani

Fani ni mbinu ambazo msanii hutumia kuwasilisha maudhui. Baadhi ya vipengele vya fani katika fasihi simulizi hupatikana katika fasihi andishi kama vile;

Ploti

Tanzu za kinathari za fasihi simulizi( ngano, visasili na mighani) huwa na ploti sahili. Sifa hii pia inajitokeza katika baadhi ya riwaya za Kiswahili kama vile siku njema yake Ken Walibora ambazo ni nyepesi kueleweka.

Wahusika na Uhusika

Fasihi simulizi imeathiri fasihi andishi katika upande wa wahusika.Fasihi simulizi hutumia wahusika wanyama, mizuka na binadamu. Fasihi andishi nayo hutumia wahusika wa aina mbalimbali kuwasilisha ujumbe.

Nyimbo

Mtambaji bora wa ngano za fasihi simulizi hutumia nyimbo katika usimulizi. Vivyo hivyo, baadhi ya kazi za fasihi simulizi kama vile tamthilia hutumia nyimbo.

Fantasia

Fantasia ni sifa ambayo hupatikana katika ngano na visasili. Sifa hii pia hupatikana katika baadhi ya tungo za fasihi andishi.

Baadhi ya riwaya za Kiswahili zina matukio ambayo yamekiuka uhalisia .

Kuwepo kwa wahusika wasio wa kawaida kama vile mazimwi katika fasihi simulizi na fasihi andishi ni mfano wa fantasia.

Kwa mfano katika riwaya ya Rosa Mistika yake E. Kezilahabi imesawiri wahusika Rosa na  zakaria wakiwa mbinguni mbele ya hukumu ya mungu. Haya ni mandari yasiyo ya kawaida na hii ni fantasia.