MWONGOZO WA MSTAHIKI MEYA

By , in Tamthiliya on .

Mchezo uanzapo, tunakutana na Waridi ambaye ni nesi na Siki ambaye ni daktari. Wote wawili wako kwenye zahanati ya Jiji. Daktari Siki anaonekana mwenye kusumbuliwa na jambo fulani; pengine matatizo ya ukosefu wa dawa zahanatini. Waridi aingiapo, wanaanza kuangazia swala la ukosefu wa dawa kwenye zahanati. Waridi anamwambia Siki kwamba, shehena ya dawa iko bahari kuu na kwamba ingewasili baada ya siku tatu. Hii ni kwa mujibu wa Mstahiki Meya mweneyewe. Zahanati ingepokea dawa hizo baada ya siku tatu zingine baada ya kuwasili nchini. Meya anasema wagonjwa wasubiri dawa, naye daktari anashangaa kana kwamba ugonjwa nao utasubiri. Kutokana na mazungumzo ya Waridi na daktari Siki tunagundua kwamba, zaidi ya kukosekana kwa dawa, wagonjwa hawana pesa za kulipia huduma za matibabu. Hata hivyo, amri ni kwamba, lazima wagonjwa walipie huduma za afya kabla hazijatolewa kwao. Waridi anatetea hali hii kwa kusema kwamba nchi yao ni maskini. Siki anapomuuliza mwenye kusema kwamba nchi ni maskini, Waridi anasema kwamba ameyasikia tu maneno hayo kutoka kwa wanasiasa, vyombo vya habari na wasomi. Siki haelekei kukubaliana naye na anashangaa kwamba ‘ameyasikia tu’. (Hii inadhihirishwa kwamba, vyombo vya habari, wanasias na wasomi wanawapotosha wananchi kwamba nchi yao ni maskini.) Pindi anaingia mama mwenye mtoto mgonjwa. Waridi anamkemea lakini Siki anampokea na kuanza kumhudumia. Tunagundua kwamba, mtoto alikula maharage aliyoletewa na mamake kutoka anakofanya kazi; kwa Mstahiki Meya.Tunaonyeshwa hapa kwamba, jamii hii inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa chakula; haswa pale mama huyu anakiri kwamba huwa wanakula chakula cha mbwa bila ‘dhara yoyote’. Zaidi tunaona kwamba, mtoto huyu ana tatizo la utapiamlo; ushahidi wa kuwa pana ukosefu wa lishe bora. Daktari anapendekeza mtoto alazwe kwenye wadi ya watoto na anajishughulisha kumpa huduma kwa kujitengenezea dawa ya mchanganyiko wa sukari na chumvi kwenye maji moto. Anapendekeza pia kwamba, wagonjwa wote waliolemewa walazwe hata ingawa hakuna dawa huku akisema kwamba wakifa watakufa kwa kukosa dawa lakini si kwa kukosa matumaini. Anasisitiza kwa kusema ‘ganga ganga ya mganga huleta tumaini.’ Tunapata kufahamu pia kwamba,wagonjwa hawa ni wafanyakazi wa Jiji husika.. dakatari anasema “…Asasi na wahudumiwa vyote viko chini ya Meya…” akiwa na maana kwamba, hospitali ni ya Jiji na wagonjwa ni wafanyakazi wa Jiji. Inabidi wagonjwa walazwe huku dawa zikisubiriwa. Wakati uo huo Siki anashangaa ni kwa nini Meya akatoa kauli badala ya Bwana Uchumi na Kazi; inaelekea kuna jambo ambalo linaendelea pale na wanakubaliana kusubiri ili waone yatakayotokea. SASA ENDELEA >>>>>>

MWONGOZO WA : Mstahiki Meya

MWANDISHI: Timothy M. Arege

MCHAMBUZI : James Kemoli Amata

Yaliyomo Utangulizi

SURA YA KWANZA

Mambo Muhumu Katika Maonyesho SEHEMU I [Maonyesho matatu (ku. 1-24)] SEHEMU II [maonyesho manne (ku. 25-51)] SEHEMU III [maonyesho matatu (ku. 52-65)]

SEHEMU YA IV [maonyesho mawili (ku. 66-79)]

SURA YA PILI

Wahusika

SURA YA TATU

Tathmini ya tamthilia ya Mstahiki Meya

SURA YA NNE

Fani (mbinu za kisanaa)

MATUMIZI YA LUGHA NA TAMATHALI ZA USEMI

SURA YA TANO

Maswali ya marudio

Maswali na Majibu Kielelezo Majibu Kielelezo

SURA YA SITA

Mtihani wa KCSE

Mitihani Kielelezo wa KCSE

Marejeleo Mwandishi huyu Utangulizi

Iwapo hujasoma matini ya tamthilia ya Mstahiki Meya, usiusome Mwongozo wa Mstahiki Meya.

Mwongozo wa Mstahiki Meya ni kiangazio tu wala si kitabu kilichoteuliwa. Ili uweze kufaidika kutokana na mwongozo huu ni sharti kwanza kabisa uwe umesoma matini ya tamthilia iliyoteuliwa, Mstahiki Meya, iliyotungwa na Timothy M. Arege, si mara kadhaa tu bali mara nyingi. Baada ya kufanya hivyo, soma mwongozo huu ukiyalinganisha maoni yako na yale ya mwandishi wa mwongozo.

Ni vema uweze kuongeza maoni yako katika maoni ya mwandishi wa mwongozo huu. Ukiweza hata tofautiana na baadhi maoni ya mwandishi wa mwongozo huu, bora tu uthibitishe maoni yako kwa yaliyomo katika matini. Iwapo utafanya hivyo utaweza kuelewa vizuri matini na utaweza kujibu maswali ya mtihani kwa njia ifaayo.

Kusoma matini mara nyingi kutakuwezesha kujibu maswali ya muktadha kwa usahihi zaidi. Pia, kutakuwezesha kuchangia katika majadiliano kwa uzingativu zaidi.

Fanya mazoezi ya kujibu maswali, kila swali moja kwanza, kabla ya kujadiliana na wanafunzi wenzako. Zingatia mafunzo na maelezo ya mwalimu wako.

Kamwe usishawishike kuutegemea mwongozo huu badala ya matini ya Mstahiki Meya.

SURA YA KWANZA

Mambo Muhumu Katika Maonyesho SEHEMU I [Maonyesho matatu (ku. 1-24)] Onyesho I (ku. 1-7)

Wahusika ni Nesi Waridi, Daktari Siki, na mama (mfanyakazi wa Baraza) na mtoto wake (Dadavuo Kaole) na wagonjwa wengi (katika mstari mrefu).

Mahali ni katika zahanati, mjini Cheneo.

Wakati ni jioni, Daktari Siki anapoonekana mwenye wasiwasi, mara amezubaa hadi anapozinduliwa na Nesi Waridi. Ni wakati wa shida ya ukosefu wa dawa katika zahanati na wa pesa za kununulia dawa miongoni mwa wagonjwa na wagonjwa wao.

Maudhui ya onyesho hili yana kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa. Upo mjadala kuhusu ahadi ya Meya kwamba dawa zi njiani katika bahari kuu. Ahadi hii Daktari Siki haiasmini (zake ni kauli za kuanguliwa katika matamshi [uk. 7]) lakini Nesi anaamini ni kweli (Usisahau kuwa Mstahiki Meya mwenyewe amesema [uk. 2]). Kauli ya Daktari Siki wawashughulikie wale ambao dawa za kuwafaa zipo na tatito la wagonjwa kukosa pesa analoliweka wazi Nesi Waridi. Nesi Waridi anazusha lawama kwa Wazungu kwa kuhimiza mfumo wa kugawana gharama. Umaskini wa watu kukosa kila kitu na tofauti baina ya Daktari Siki na Nesi Waridi ni masuala mengine. Upole wa daktari na ukali wa nesi kwa mama mwenye mtoto (mgonjwa wa hali ya utapiamlo) ni jambo jingine linalojitokeza.

Matokeo ya ahadi ya uwongo ni kwamba hali inaendelea kuwa mbaya. Wagonjwa wanalazwa bila dawa. Huku Daktari Siki akitamauka, Nesi Waridi anahimiza subira kwa matumaini.

Dhamira ya mtunzi ni kuonyesha mtanziko katika huduma ya utabibu. Madaktari wanakosa dawa ilihali wagonjwa wanaongezeka. Hali ya wagonjwa inawalazimu madaktari washauri kulazwa kwao lakini amri inakataza mgonjwa kulazwa kama hajalipia huduma. Manesi wanaona afadhali kulazwa wagonjwa kama dawa zipo lakini madaktari wanapendekeza kulazwa kwao angaa wafe wakiwa na matumaini. Kipi muhimu, dawa au matumaini?

Kuonyesha hali mbaya ya umaskini. Wakati uo huo kuonyesha kutowajibika kwa watu walio mamlakani na ahadi zao za uongo.

Onyesho II (ku 8-15)

Wahusika ni Mstahiki Meya Sosi, Gedi – Mpambe wa Meya, Dida – Mhudumu wa nyumbani kwake Meya na Daktari Siki.

Mahali ni nyumbani kwake Meya [kama si sebuleni ni mahali pa kulia chakula].

Wakati fulani asubuhi, wakati wa chakula, siku mbili tangu Daktari Siki ajadiliane na Nesi Waridi kuhusu ahadi ya kuwasili kwa dawa ambazo hazipatikani zahanatini. Ni wakati Daktari Siki anapomtembelea Meya, yeye kama ndugu yake, kumpelekea malalamiko ya watu kuhusu uongozi mbaya wa Baraza la Cheneo na hali mbaya ya maisha ya watu.

Maudhui ya onyesho hili ni ulaji mzuri alio nao Meya huku akionyesha kutotosheka. anayaita mayai ‘viyai’ na kuku walioyataga ‘Bloody hens’. Ulafi wa Meya ambaye anakunywa chai kwa pupa mpaka inamchoma na badala ya ajilaumu anamlaumu mhudumu Dida. Wasiwasi wa Meya kuhusu Daktari Siki kumtembelea. Meya kukataa ukweli wa mambo. Majigambo ya Meya jinsi alivyochaguliwa mara tatu na hata atakavyochaguliwa tena na tena akitaka. Mbinu ya propaganda ya kuwapotosha watu kwa nyimbo za kizalendo. Kitisho cha Meya kuwa Daktari Siki anajitia hatarini. Kutofautiana kwa Meya Sosi na binamu yake Daktari Sosi kiasi cha Meya kumpiga marufuku ‘jengo lake alione paa’ (uk. 15). Hata hivyo, kupo kutishika kwa Meya kiasi cha kuita mkutano wa dharura wa Kamati ya Meya.

Matokeo ya ugeni wake Daktari Siki ni kwamba Meya anaukataa ushauri wa Siki. Anautafsiri vibaya ushauri huo kuwa ati ni uchochezi wa mgomo. Anakasirika mpaka anampiga marufuku asikaribie kwake. Anaitisha mkutano wa dharura kwa sisitizo asikose mtu.

Dhamira ya mtunzi katika onyesho hili ni kuonyesha ubinafsi wa viongozi waliochaguliwa. Wanajali tu masilahi yao. Wanakula vizuri. Pia, ni kuonyesha unafiki na usaliti wa viongozi kudai mambo ni mazuri ilihali hawafanyi chochote cha kuwatumikia na kuwanufaisha watu waliowachagua. Mtunzi ana lengo lakunyesha upofu wa viongozi kutoona shida za watu na ujanja na udhalimu wao wa kujidumisha madarakani. Hawajali undugu uongozi wao unapotishika.

Onyesho III (ku. 16-24)

Wahusika ni Wanakamati ya Meya: Diwani I – Bwana Usalama; Diwani II – Bwana Uhusiano Mwema na Diwani III (Kheri) – Bwana Uchumi na Kazi; Mstahiki Meya (Sosi) na Gedi – Mpambe wa Meya.

Mahali ni ofisi ya Meya (Sosi).

Wakati ni ni alasiri, siku iyo hiyo Daktari Siki aliyokuwa nyumbani kwake Meya. Ni wakati baada ya Daktari Siki kumpasulia wazi Meya ukweli wa hali mbaya ya watu mpaka Meya akatishika. Ni siku hiyo baada ya Meya kumpiga marufuku Daktari Siki asiwahi tena kwenda kwake. Ni wakati ambapo Meya ameita mkutano wa dharura kubuni mikakati ya kuzima malalamiko na kilio cha watu. Ni wakati wa wasiwasi na shauku.

Maudhui ni mkutano wa dharura ulioitwa na Meya kukabiliana na malalamiko ya watu. Kulitetea Baraza la Cheneo dhidi ya shutuma za kutowahudumia watu. Uchoyo na ubinafsi wa Meya. Anamwagiza Gedi ampelekee chupa moja ya maji kutoka katika jokofu ilihali wamo wanne. Uongozi mbaya wa vitisho na kutoweka mbele masilahi watu ni kati ya maudhui mengine. Ubarakala na ukaragosi wa viongozi wengi (Diwani I na Diwani II) ambao wanawazidi nguvu viongozi wa uwazi na ukweli (Diwani III). Ni suala la vita baina ya uongo na ukweli. Kuna utumiaji nguvu kuzima malalamiko na propaganda kuficha ukweli. Ulafi na ubinafsi wa viongozi kujiongezea mishahara na kukataa kulipa kodi.

Uundaji wa kamati nyingi kutetea kiongozi (Meya). Ubadhirifu wa fedha za umma katika mahitaji ovyo ya kibinafsi kama vile kuwavisha madiwani – viongozi – (uk. 21) na uwepo wa maji machafu ya kutoweza kunywika. Udhalimu wa kuwafuta kazi wafanyakazi wanaogoma kwa kufaidika kutokana na ukosefu wa ajira ni kati ya maudhui katika onyesho hili.

Matokeo ya mkutano wa Meya na madiwani unamalizika Meya akijiandaa kwa mkutano mwingine na walinzi wa Baraza. Meya na Diwani I na Diwani II wanaamua wapate nyongeza ya mishahara na wasilipe kodi. Msimamo huu anaupinga sana Diwani III lakini hana la kufanya ila kuitekeleza amri, yeye kama Bwana Uchumi na Kazi wa Baraza.

Dhamira ya mwandishi ni kutilia mkazo uongozi mbaya uliopo. Viongozi wanajinufaisha bila kuwajali watu waliowachagua. Kuna utumiaji vijana vibaya kuutetea uongozi mbaya

– nyimbo na maonyesho ya kizalendo kwa malipo duni (uk. 20). Mtunzi ana nia ya kuonyesha

mipango ya udhalimu wa kuwapiga watu kukomesha migomo.

SEHEMU II [maonyesho manne (ku. 25-51)] Onyesho II (ku. 25-33)

Wahusika ni Meya (Sosi), Bili (rafiki yake Meya), Gedi (Mpambe wa Meya), Sauti (wafanyakazi wanaogoma) na wahusika wasioonekana (wanahabari wanaotaka kumhoji Meya).

Mahali ni katika ofisi ya Meya.

Wakati ni mwezi mmoja tangu mkutano wa dharura wa Kamati ya Meya. Ni wakati wa matukio chungu nzima. Meya anapokuwa katika harakati za kupanga mapokezi ya mameya wa nchi za kigeni. Ni wakati ambapo Meya anajipangia njama ya kumfukuza mwanakandarasi aliyepewa kazi na mtangulizi wake. Pia, ni wakati anapopanga ubadhirifu wa fedha za umma kuwafurahisha mameya watakaozuru. Ni wakati anapotembelewa na rafiki yake Bili, majuma mawili tangu waachane mwisho. Ni wakati ambapo Meya anajigamba jinsi watoto wake wanavyosomea ng’ambo ili wapate elimu ya mafao (ambavyo yeye ni mzazi mwenye maono). Ni wakati ambapo mkewe ameenda ng’ambo mbali na kuwaona watoto wake wanaosomea huko, kujifungua (ambavyo hana imani na madaktari wa nchini – wa kubabaisha tu – uk. 27). Ni wakati ambapo Meya anajigamba ana pesa. Ni wakati ambapo Bili anampa ushauri namna ya kunufaika (kwa ufisadi). Ni wakati wafanyakazi wanagoma wakidai haki yao. Ni wakati ambapo Bili anampa moyo makelele ya wafanyakazi wanaogoma yasimbabaishe. Ni wakati Bili anamhakikishia uungwaji mkono na Mhubiri na hata kumwendea kwa huduma ya maombi. Ni wakati ambapo Nesi Waridi anaacha kazi kwa kukosa dawa za kuwatibia wagonjwa.

Maudhui maudui ya onyesho hili ni ufisadi wa Meya. Amefuta kandarasi kwa njia haramu. Kwa ushauri wa rafiki yake Bili, Meya atadai malipo fulani. Jambo jingine katika maudhui ni elimu duni kwa viongozi kutowajibika na kuwapeleka watoto wao ng’ambo kwa masomo ya mafao. Upo udunishaji wa madaktari wa nchini. Pia, lipo suala la tamaa. ya uraia wa nchi za ng’ambo. Unyakuzi wa ardhi unaoendelezwa na Meya, mpaka anawagawia pia na marafiki zake. Ubadhirifu wa mali ya umma. Utumiaji vibaya mahakama (uk. 29).

Majisifu ya viongozi wenye mali.

Matokeo ya Bili na Meya kukutana yamekuwa sikitiko. Meya anakubali ushauri unaompotosha. Anapuuzilia mbali madai ya wafanyakazi wanaogoma. Anatishia kuwafuta kazi. Anasubiri maombi ya Mhubiri.

Dhamira ya mwandishi ni kuonyesha utumiaji mbaya wa mamlaka. Meya anafulitia mbali kandarasi halali na kuweka mpya ambayo ni haramu. Amemgawia rafiki yake Bili viwanja. Anania ya kuonyesha hali ya viongozi kutokuwa na imani na huduma za nchi – elimu na utabibu. Wao huenda ng’ambo kwa huduma hizi ilihali ni wao wasiowajibika. Anataka kuonyesha ubinafsi wa viongozi. Haja yao ni kutaka kujitajirisha. Kupenda makuu ndiyo hali ya viongozi. Meya anakifurahikia cheo (uk. 28). Mwandishi anataka kuonyesha viongozi hawajali masilahi ya wafanyakazi. Wafanyakazi wana shida ya mishahara duni —-

Onyesho II (ku. 34-40)

Wahusika ni Daktari Siki, Nesi Waridi na Tatu (mwakilishi wa wafanyakazi).

Mahali ni katika zahanati ya Baraza la Mji wa Cheneo, katika ofisi ya Daktari Siki.

Wakati ni uleule Meya na rafiki yake Bili wanapozungumza katika ofisi ya Meya. Ni wakati ambapo wafanyakazi wamegoma na Nesi Waridi amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kazi. Ni wakati ambapo wagonjwa wanaendelea kufa kwa kukosa dawa. Kati ya waliokufa ni binamu yake Nesi Waridi, huku mama mzazi wa mtoto akimtumainia Waridi kumwokolea mwanawe. Ni wakati ule Tatu, mmoja wa wawakilishi wa wafanyakazi anapomwendea Daktari Siki kumwomba awaongelee kwa Meya. Anategemea mbavyo Meya ni binamu yake Meya, (Meya) atamsikiliza. Wao hawampati, hata wakijaribu vipi.

Maudhui ni kutamauka kwa Nesi Waridi na kujiuzulu kazi kwake. Mazingira magumu ya kufanyia kazi wafanyakazi. Kuna ukosefu wa dawa, mishahara duni na wagonjwa kufia mikononi yakiwa mambo ya kutostahimilika. Wafanyakazi kutarajia unasaba baina ya Daktari Siki na Mstahiki Meya kutawafaa wapate usikivu wake Meya. Uamuzi wa kutumia mgomo kama silaha ya kutumia kutetea masilahi yao wafanyakazi ni jambo jingine linalowekwa wazi na mwandishi.

Matokeo ya Meya kukaidi ushauri mwema wa Siki na Diwani III na kutojali hali ya wafanyakazi kunapelekea Waridi kujiuzulu kazi. Tatu anajaribu kumwomba Siki aongee na Meya, yeye akiwa binamu yake Meya. Kwa kuwa hilo halitawezekana, anamshauri watumie fursa ya wageni wanaotarajiwa kushinikiza takwa lao. Ni wakati ambapo Siki ameahidi kumwona na kuongea tena na Bwana Fedha na Kazi wa Baraza la mji (Diwani III).

Dhamira ya mtunzi ni kuonyesha kuwa ukosefu wa dawa katika hospitali husababisha vifo vingi. Pia, anataka kuonyesha hata dawa zikiwepo umaskini unawazuia wagonjwa kumudu bei ya dawa. Hata hivyo, ni afadhali kukosa pesa kuliko kukosa dawa kwani dawa inaweza kupatikana kwa mkopo. Tena anataka kuonyesha mazingira mabaya ya kufanyia kazi huwafanya baadhi ya wahudumu kujiuzulu kazi. Anataka kuonyesha ni jambo la kutovumilika wagonjwa kuendelea kufia mikononi mwa wahudumu na ni jambo la kutaka sana moyo (ustahimilivu) – uk. 36. Mtunzi anaonyesha migomo husababishwa hasa na viongozi kukataa kuwasikiliza wafanyakazi. Bila mawasiliano kazi haiwezi kuendelea.

Jambo jingine ambalo mtunzi anataka kuonyesha ni kwamba wapo wahubiri wanaokubali kutumiwa vibaya na wafisadi.

Onyesho III (ku. 41-44)

Wahusika ni Meya, Mhubiri, Polisi: Askari I na Askari II na Gedi (Mpambe wa Meya).

Mahali ni katika ofisi ya Meya.

Wakati ni adhuhuri ya siku iyo hiyo Bili rafiki yake Meya anapomhakikishia Meya ya kuwa atamfuatia Mhubiri amfae kwa maombi. Ni wakati ambao Meya anakutana na Mhubiri. Ni wakati ambapo Mhubiri ameenda kumwombea Meya. Ni wakati wa maombi ambapo sauti zao Meya na Mhubiri zinatafsiriwa kimakosa kuwa ushambulizi wa watu wanaodai haki zao (vinyangarika wameleta fitina) – uk. 43. Ni wakati ambapo Askari I, Askari II na Gedi wanaenda haraka kwa fujo katika ofisi ya Meya wakidhani Meya amevamiwa.

Maudhui ni maombi ya wahubiri ambao hawana msimamo. Wahubiri wa kujipendekeza kwa wanasiasa na viongozi waovu. Waombezi ambao wanaongozwa na masilahi yao ya kibinafsi. Kuna pia hoja ya wanasiasa kujinyenyekeza mambo yanapowawia magumu.

Hatua zisizofaa kwa ajili ya kutetea masilahi ya uongozi mbaya. Matumizi mabaya ya mamlaka. Meya anaamua kumlipa Mhubiri akitumia hazina ya Baraza la Cheneo (uk. 44).

Matokeo ya maombi ya Mhubiri yanamtia Meya Jazba. Anaazimia sadaka ya kila mwezi ya shilingi laki moja.

Dhamira ya mtunzi ni kuonyesha unafiki wa baadhi ya wahubiri. Pia, anataka kuonyesha makosa katika maamuzi ya vyombo vya usalama. Askari wanaingia kwa fujo ilihali wamedhani tu wala si ati wana uhakika Meya amevamiwa.

Onyesho IV (ku. 45-51)

Wahusika ni Daktari Siki na Diwani III [Kheri] (Bwana Uchumi na Kazi).

Mahali ni nyumbani kwa Diwani III, katika Baraza.

Wakati ni siku ya pili tangu Meya aombewe na Mhubiri kutokana na ushauri wa Bili, rafiki yake Meya. Ni wakati ambapo Daktari Siki amenda kumtembelea Diwani III (Kheri), siku ya pili baada ya Nesi Waridi ajiuzulu kazi katika zahanati ya Baraza la Cheneo. Ni wakati ambapo Diwani III na Daktari Siki wanaburudika kwa sharubati na asusa (pengine karanga tu). Ni wakati ambapo Daktari Siki na Diwani III wanatarajia kila mmoja ana nafasi nzuri ya kumshauri na kumshawishi Meya kusikiliza kilio cha wananchi. Kumbe hapo mwenye nafasi hiyo. Ni wakati ambapo Daktari Siki anatimiza ahadi yake kwa Tatu, mwakilishi wa wafanyakazi, kuwa angeonana na kuongea na Bwana Fedha na Kazi wa Baraza la mji Diwani III (Kheri).

Maudhui ni uongozi mbaya wa Mstahiki Meya Sosi. Pia, kuna maudhui ya tatizo la Meya kushauriwa na vibaraka. Lawama kwa wananchi (waovu) kuwachagua viongozi waovu. Chanzo cha uongozi mbaya ni wananchi wenyewe. Kuzingatia uhusiano (undugu na urafiki) katika kuwachagua viongozi. Kutopatana kwa Daktari Siki na binamu yake Mstahiki Meya Sosi. Wametengana kama mafuta na maji (ku. 45). Meya kumtenga Diwani III kwa sababu ya udadisi wake kuhusu shughuli za Baraza la Cheneo. Imani ya Daktari Siki ya kwamba Diwani III kwa kuwa Bwana Hazina (Fedha, Uchumi) wa Baraza ana ushawishi kwa Meya. Imani ya Diwani III kwamba Daktari siki ana ushawishi kwa Meya kwa kuwa yeye ni binamu yake. Kumbe ukweli ni kinyume na imani hizi. Maudhui mengine ni mamlaka kupindukia aliyo nayo Meya kutokana na Mayor’s Act na Riot Act. Unyonge alio nao Diwani III kutokana na kinachoitwa Collective responsibility. Meya kuleweshwa na mamlaka hata asikumbuke alikotoka. Watu wenye taaluma wanachangia uwepo wa uongozi mbaya kwa kuogopa kujitosa katika siasa. Wageni wanatarajiwa kuuzuru mji ilihali kuna hali mbaya na uvundo katika mji.

Matokeo ya mazungumzo ya Siki na Diwani III ni mtazamo mpya. Wanaweka wazi lawama kwa wananchi ambao huwachagua viongozi wabaya. Wanaamua dawa ni kuung’oa uongozi mbaya.

Dhamira ya mtunzi ni kuonyesha uongozi mbaya unatokana na wananchi wanaowachagua viongozi wabaya. Anataka kuwahimiza watu wenye taaluma waingie katika nyadhifa za kisiasa (uongozi) ili waurekebishe uozo kutoka ndani. Anataka kuonyesha ya kuwa uozo na uvundo wa Cheneo unaakisi ufisadi. Anataka kuhimiza watu wasikate tamaa bali kila mmoja awajibike.

SEHEMU III [maonyesho matatu (ku. 52-65)] Onyesho I (ku. 52-56)

Wahusika ni Meya Sosi na Diwani III.

Mahali ni katika ofisi ya Meya.

Wakati ni asubuhi, siku ya tatu tangu Meya aombewe na Mhubiri. Ni siku inayofuata mazungumzo ya kina baina ya Daktari Siki na Diwani III (Kheri) kuhusu haja ya kumshauri Meya. Ni wakati Diwani III amewasili katika ofisi ya Meya kwa mwaliko wa Meya. Ni wakati ambapo Diwani III anatimiza ahadi yake kwa Daktari Siki ya kuwa angeendelea

kusema na Meya. Ni wakati ambapo wafanyakazi wamegoma. Tena ni wakati ambapo wageni wanakaribia kufika. Ni wakati ambapo Meya amemwagiza Diwani III (Kheri) akiwa Bwana Uchimi wa Baraza awape madiwani nyongeza ya mshahara (licha ya Baraza kutoweza kumudu).

Maudhui ni udikteta wa Meya. Anamwagiza Diwani II, Bwana Uchumi wa Baraza, atekeleze nyongeza ya mshahara mara moja ‘mwezi huu’, ukiwa bado siku mbili tu kwisha. Kutowajali wafanyakazi waliogoma na kutokubali ushauri wa Diwani III. Ukosefu wa maono wa Meya. Anatarajia mikopo kulipia mishahara. Kutojali maisha ya baadaye ya vizazi vijavyo. Kitisho cha Meya kuwa Diwani III anampinga – Insubordination (uk. 55).

Matokeo ni kwamba Diwani III anakubali shingo upende kutekeleza nyongeza ya mishahara ya madiwani. Meya anabaki akiwaza na kuwazua. Analegeza msimamo wake na kuamua awasikilize angaa viongozi wa wafanyakazi.

Dhamira ya mtunzi ni kuonyesha ya kuwa kiongozi ambaye hana maono hutoa maamuzi mabaya. Kiongozi kama huyo hukataa ushauri mazuri. Anataka kuonyesha utumiaji wa mabavu husababisha utekelezwaji wa maamuzi mabaya. Pia, anataka kuonyesha ya kuwa uchaguzi wa viongozi wasiofaa husababishia vizazi vijavyo mzigo usiowafaidia.

Onyesho II (ku. 57-63)

Wahusika ni Sauti (wafanyakazi wanaogoma), Meya, Gedi (Mpambe wa Meya), Diwani I (Bwana Usalama), Diwani II (Bwana Uhusiano Mwema) na Bili (rafiki yake Meya).

Mahali ni nje na katika ofisi ya Meya.

Wakati ni muda fulani baada ya Diwani III kumwacha Meya katika ofisi yake. Ni wakati ambapo Meya anapekuapekua mafaili yaliyo mbele yake huku akipiga mafunda ya chai. Ni wakati ambapo mgomo wa wafanyakazi unaendelea.

Maudhui ni mgomo wa wafanyakazi kudai haki yao. Kuna kuvunjwa kwa mkutano wa wafanyakazi wanaogoma kwa nguvu za polisi kuwafyatulia risasi. Kuna pia furaha ya Meya na washirika wake (Bili, Diwani I na Diwani II) kwa wafanyakazi kutoroka kusalimisha maisha yao polisi wanapofyatua risasi. Maudhui hapa ni utumiaji polisi kukabiliana na mgomo wa wafanyakazi. Njama ya kujilipa marupurupu na hofu ya kutokubalika kwa jambo hilo kwa Bwana Uchumi na Kazi (Diwani III) kwa madai ana wivu na majivuno kuwa ni mkamilifu (mnyoofu, mwadilifu). Njama ya kuiba Fimbo ya Meya ili iuzwe ng’ambo (kwani ni ya dhahabu) halafu wagawane bila Diwani III kujua. Diwani II (Bwana Usalama) anahiari kutumia cheo chake kuipitisha hiyo fimbo kwani yeye hakaguliwi mizigo yake atokapo. Kusingizia wizi wakati wa mgomo wa wafanyakazi na kuanzisha uchunguzi bandia (uk. 62) kunahitimisha njama ya wizi.

Matokeo ni kwamba Meya, Diwani I, Diwani II na Bili wanakubaliana na kutoleana ahadi ya kuweka siri kali hadi kufa.

Dhamira ya mwandishi ni kuonyesha jinsi wafanyakazi wakandamizwavyo kwa kutumia vyombo vya usalama. Pia, mtunzi anataka kuonyesha jinsi mipango ya ndani kwa ndani ifwanywavyo kwa kula njama kuiba vifaa vya umma kwa manufaa ya watu wachache wenye mamlaka.

Onyesho III (ku. 64-65)

Mhusika ni Dida (Mhudumu wa nyumbani kwake Meya) tu.

Mahali ni nyumbani kwake Meya.

Wakati ni siku mbili tangu wafanyakazi wa Baraza la Cheneo waliokuwa wanagoma kutawanywa na polisi kwa amri ya Diwani I (Bwana Usalama). Ni wakati ambapo Dida anafagia.

Maudhui ni dhihaka ya Dida. Anawaigiza polisi katika kwata. Anawachekelea wafanyakazi jinsi walivyokimbia, hasa wazee kwa kuwapiku vijana kwa mbio. Ubinafsi wa Dida. Anajiondoa katika kujishughulisha na mambo ya wafanyakazi, maadamu yeye ana kazi bora, mameya wawepo azinadhifu nyumba zao hata mji ukivunda vipi.

Matokeo ni kwamba Dida anaendelea na kazi yake ya kufagia.

Dhamira ya mtunzi ni kuonyesha watu wamewekwa katika matabaka: kuna binadamu wa kudharaulika (viatu) na wale wa kuheshimika (watu). Watu huchukulia kimzaha masaibu ya watu wengine. Dida anawachekelea watu jinsi walivyotoroka mbio kuyaokoa maisha yao.

SEHEMU YA IV [maonyesho mawili (ku. 66-79)] Onyesho I (ku. 66-72)

Wahusika ni Meya na Wawakilishi wa wafanyakazi – Tatu, Beka na Medi.

Mahali ni katika ofisi ya Meya.

Wakati ni asubuhi. Ni wakati ambapo Meya ana mkutano na wawakilishi wa wafanyakazi. Ni wakati ambapo mgomo wa wafanyakazi unaendelea. Siku moja kabla ya kuwasili kwa wageni wanaotarajiwa.

Maudhui ni matatizo ya wafanyakazi wa Baraza la Cheneo. Wana ajira ndogo. Kuna kucheleweshwa kwa mishahara yao. Upo ukosefu wa dawa. Kuna tatizo la wafanyakazi kushindwa kumudu gharama ya maisha. Watoto wa watu wa chini wanakosa elimu ilihali wa wakubwa wanaendelea kusoma. Madiwani kuongezwa mishahara ni jambo la mara kwa mara na huwa kwa kiwango kikubwa. Shida ya kutakiwa walipie huduma za matibabu bali wakubwa wanalipiwa. Kuna kumalizika kwa subira ya wafanyakazi.

Matokeo ni kuvunjika kwa mazungumzo baina ya Meya na wawakilishi wa wafanyakazi. Mgomo ukawa ni wa kuendelea. Meya anabaki ameshtuka na kuhuzunika.

Dhamira ya mtunzi ni kuonyesha jinsi wafanyakazi wanavyodhalilishwa. Nyongeza za mishara ni haba na ni baada ya muda mrefu. Anakusudia kuonyesha mishahara midogo haitimizi masilahi ya wafanyakazi. Anadhamiria kuonyesha wakubwa wanapendelewa kwa kugharamiwa karibu kila kitu. Pia, ana nia ya kuonyesha mara nying vinara hawatumii busara wanapohitajika kusuluhisha matatizo. Wanajali mambo ya muda mfupi kama vile jina zuri mbele za wageni. Wanajali sifa zao tu. Migomo inaweza kusababisha maradhi (kipindupindu)na bila shaka vifo.

Onyesho II (ku. 73-79)

Wahusika ni Meya, Diwani II (Bwana uhusiano Mwema), Diwani I (Bwana Usalama), Gedi (Mpambe wa Meya) na Polisi: Askari I na Askari II.

Mahali ni ofisi ya Meya.

Wakati ni siku moja tangu mkutano wa Meya na wawakilishi wa wafanyakazi. Ni siku ambayo wageni wanatarajiwa kuwasili. Ni wakati ambapo Meya ana mkutano na Diwani I na Diwani II.

Maudhui ni ukweli wa mambo kuanza kumharibikia Meya. Ana wasiwasi. Jambo jingine ni uozo uliotanda katika mji wa Cheneo. Pia, kuna kuendelea kwa mgomo. Hofu ya kuharibika kwa jina (sifa). Lipo tatizo la ushauri usiofaa wa Diwani I (Bwana Usalama)

kwamba kutangaziwe vijana katika vyombo vya habari ajira. Kuna kuibuka kwa suala la kutoonekana kwa Bili, rafiki yake na mmoja wa washauri wabaya wa Meya, ilihali yeye ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kumpotosha Meya. Ametoweka sasa siku mbili tatu.

Maudhui mengine ni habari za mgomo wa wafanyakazi wa viwanja vya ndege kugoma kwa minajili ya kuwaunga mkono wenzao waliogoma wa Baraza la Cheneo. Kuna ujinga wa Diwani I ambaye haoni cha kuzuia ndege kutua hata kama waelekezi hawapo! Jambo jingine ni hofu ya uwezekano wa mkurupuko wa kipindupindu. Hofu hiyo inapelekea wageni waliotarajiwa kuahirisha ziara. Maudhui mengine yanayojitokeza katika onyesho hili ni ukosefu wa maji safi katika mahoteli. Habari za usafiri kukatizwa kutokana na ukosefu wa mafuta ambao nao umesababishwa na mgomo wa wafanyakazi katika bohari la mafuta.

Kwa ufupi, kuna kuongezeka kwa migomo ya wafanykazi. Majuto ya Meya kwamba angalimsikiliza Bwana Uchumi na Kazi akiona hakuyapenda maneno yake lakini yalikuwa na ukweli Fulani.

Matokeo yanayodhihirika ni kwamba kuna uongozi mbaya. Katika onyesho hili kuna kupendekeza na kukubali utumiaji nguvu. Diwani II anapendekeza Meya atumie mamlaka aliyopewa. Haikosi ni Riot Act. Meya anakubali kuwatumia askari wa Baraza. Mara ile mambo yanabadilika ghafula. Askari I na Askari II wanaingia. Meya na vibaraka wake Diwani I na Diwani II wanafurahi na kuona nafuu. Kinyume na matarajio mambo yanabadilika. Askari I anamjulisha rasmi Meya kuahirishwa kwa ziara ya wageni (mameya wa kigeni). Meya na vibaraka wake wanafurahi kupingukia. Ghafula tena, wanapata habari ya kutakiwa wapelekwe mbele (washikwe) ili waweze kuelezea mbele.

Dhamira mtunzi ni kuonyesha ya kuwa uongozi mbaya una mwisho wake. Wanaotumia vibaya mamlaka wajiandae siku moja kujibu mashtaka – pingu zinawangoja. Wawe tayari kuwajibikia mbatukio yote katika idara zao.

SURA YA PILI

Wahusika

Mhusika katika kazi ya fasihi ni kiumbe cha mtunzi. Katika tamthilia hii anafanana na binadamu. Kwa kuwa tamthilia hii inaegemea katika mitazamo ya kihalisia inamsawiri mhusika kwa namna inayokaribiana sana na watu wa dunia ya kawaida. [Sijui ni mji gani au ni nchi gani unayoiona katika tamthilia hii. Si jui ni taasisi gani unayoiona. Sijui.]

Napendekeza tumchunguze mhusika kwa njia tatu: tuyaangalie matendo ya mhusika huyo; tuyasikilize maneno anayoyasema kwa makini; na maneno wanayoyasema wahusika wengine kumhusu mhusika anayehusika.

Mstahiki Meya (Sosi) wa Baraza la Mji wa Cheneo ni mhusika mkuu. Yeye ndiye anayeitawala sehemu kubwa ya tamthilia ya Mstahiki Meya. Ni mlafi. Anaona mayai ni ‘viyai’. Mezani ana vyakula mbalimbali. Chai anapiga mafunda (uk. 8). Anaishi maisha ya kifahari. Sakafu ya nyumba yake ina zulia lenye mapambo (ruwaza) ya kupendeza.

Anapenda starehe. Ofisini ana jirafu (fridge). Ana ujinga mwingi. Anapopiga funda la chai ambalo linamchoma anamlaumu Dida (mtumishi wake wa nyumbani). Ni mtu asiyekubali ukweli. Ni mkaidi. Anayakataa maneno ya Daktari Siki kuwa watu wana shida. Kwake maneno ya Daktari Siki ni Uongo (uk. 12). Meya ni mwapuza. Anapuuzilia mbali habari ya kitoto kumfia Daktari Siki mkononi kwani huyo ni mmoja tu ilihali ana wengi wanaomwunga mkono. Ni kama hajui bandu bandu huisha gogo.Ni mfisadi. Alifutilia mbali kandarasi halali ya mwanakandarasi wa awali njia haramu na kumpa mwingine (ku. 25-26). Yeye mwenyewe anakiri alimpa kazi mhazili wake kwa upendeleo akijua hakustahili (uk. 77 mtu ambaye hakustahili kupata kazi!). Ni mhalifu. Anaidhinisha pendekezo la rafiki yake njama ya Fimbo ya Meya iibwe, iuzwe ng’ambo wagawane pesa (ku. 61-62). Ni mchoyo kupindukia.

Anaamuru madiwani walipwe nyongeza ya mshahara ilihali wanyakazi wa Baraza la mji wamegoma kwa kudai mshahara na kuna ukosefu wa dawa (uk. 52). Ni mtu wa ubinafsi. Anamwagiza Gedi (Mpambe wa Meya) amletee maji ya kunywa chupa moja. Hawajali madiwani wenzake (uk. 17). Ana shaka na huduma za jijini. Watoto wake wanasomea ng’ambo. Mkewe amempeleka ng’ambo kujifungulia huko (ku 26,27). Ni mtu wa siasa chafu na uongozi mbaya. Amemtenga Diwani III (Bwana Uchumi na Kazi) kwa kuwa yeye humpinga. Amezingirwa na washauri wafisadi (Diwani I (Bwana Usalama), Diwani II (Bwana Uhusiano Mwema) na Bili (rafiki yake ambaye hata si mfanyakazi wa Baraza la Cheneo [ku. 58-63]). Amemkataa binamu yake Daktari Siki (uk. 15. Mwondoe huyu hapa mara moja!—- Jengo langu ulione paa. – uk. 45). Meya amelewa cheo na mamlaka (ku. 28, 47). Hataki binamu yake Daktari Siki amwite kwa jina Sosi bali amwite Meya (uk.10). Ana majigambo. Anajisifia uongozi uliokolea wa Baraza la Cheneo (uk. 54). Ni mtu wa kutotishika. Huwatafuta washauri mambo yanapomlemea tu (uk. 16). Ni mporaji wa viwanja vya jiji. Ametajirika kwa njia haramu. Ameusababishia mji wa Cheneo matatizo makubwa. Umaskini umejaa. Uvundo umejaa. Migomo imejaa. Ni nafiki. Mbele ya mhubiri yeye ni mnyenyekevu lakini mbele ya watu wengine ana kiburi. Hatimaye anaishia pabaya – anazirai wakati wa kukamatwa na polisi unapowadia.

Mstahiki Meya anawakilisha viongozi ambao hawastahili nyadhifa zozote za uongozi. Ni viongozi ambao hawana maadili mema. Watu waliopotoka, wafisadi wanaoiakisi jamii iliyooza na kuozeana.

Nesi Waridi ni mhusika muhimu sana ambaye anatuonyesha jinsi hali ilivyo mbaya katika taasisi za utabibu. Ni mtumishi shupavu. Anajadiliana na Dakitari Siki. Mwanzoni ana imani dawa za kuwatibia wagonjwa zi katika bahari kuu zinakuja (ku. 2, 6, 7). Anajali masilahi ya wagonjwa. Ana subira ambayo msingi wake ni Mstahiki Meya mwenyewe kusema dawa zi njiani. Ni mtiifu. Anazingatia amri za baraza za kuwataka wagonjwa kulipia dawa na kulazwa tu kama wamelipia kitanda. Ni mkali. Anamtaka mgonjwa asubirie nje ya ofisi ya daktari mpaka aitwe. Ametamauka kwa kukosa dawa za kuwapa wagonjwa (uk. 6).

Anaamini katika matibabu kamili. Nesi Waridi anatokea kuwa mhusika kani. Anapoonekana mara ya pili na ya mwisho amekata tamaa kabisa. Amebadilika. Anaacha kazi kwa kushindwa kusubiri. Hana subira tena. Anajiuzulu kazi kwa kutoweza kuvumila kufanya kazi katika mazingira magumu. La mno ni kwamba mshahara duni anaoupata haumfai kitu (uk. 36).

Nesi Waridi anawakilisha wafanya kazi ambao wananyanyaswa kwa kulipwa mishahara duni na wanaofanya kazi katika mazingira magumu. Ni wafanyakazi ambao hatima ya umilivu wao kufikia kikomo ni kujiuzulu kazi. Anaonyesha kazi haina maana bila ya kuwa na vifaa vya kuifanyia kazi hiyo; bila ya mshahara wa maana na tena bila kuona matokeo ya kazi yenyewe. Anatupatia fursa ya kuwakosoa manesi wakali kwa wagonjwa katika hospitali za umma.

Diwani III ambaye jina lake ni Kheri ni Bwana Uchumi na Kazi wa Barazi. Anatambua mamlaka yamo mikononi mwa wananchi. Anafafanua sasa watu wameerevuka wala si kama walivyokuwa zamani. Ni mtumishi wa umma aliye mwadilifu. Ni kiongozi anayewajibika. Anawajali watu waliomchagua. Meya anamtuhumu ati kwa uchochezi (uk. 18). Anajali masilahi na usalama wa watu. Anahofia kuumizwa kwa watu na askari wa usalama (uk. 19). Anakataa ahadi za uongo (ku 19-20). Anapinga hali ya madiwani kutotozwa kodi na wakati uo huo kuongezwa mishahara (ku. 22-23). Anaionea aibu hali ya mji wa cheneo (uk. 45). Anaamini Daktari Siki kwa kuwa binamu yake Meya anaweza kusaidia kumshawishi (Meya) airekebishe hali mbaya ya mji wa Cheneo. Ametengwa na Meya (uk. 48). Amevunjwa nguvu za kuzuia maovu katika Baraza la Cheneo kwa m,amlaka

makuu aliyopewa Meya na Mayor’s Act, Riot Act na Collective responsibility (ku. 48-49). Analazimika kutekeleza amri za Meya shingo upande (ku. 23,56). Ni kiongozi wa kuweka wazi maoni yake. Ni shupavu. Ni kiongozi wa kiasi. Anamburudisha mgeni wake, Daktari Siki, kwa sharubati na asusa [tu].

Diwani III ni kiongozi kielelezo. Uadilifu wake unampelekea kuweka masilahi ya wafanyakazi mbele. Anatumiwa na mtunzi kuonyesha sifa nzuri anazostahili kiongozi na hasa mtu aliyechaguliwa na watu kuwa nazo. Anawajali watu wa chini. Suala la kodi linamkera sana – madiwani wasilipe kodi huku akina mama wauza ndizi wanalipa (uk. 22)!

Diwani I (Bwana Usalama) na Diwani II (Bwana Uhusiano Mwema) ni vibaraka wa Meya. Kazi yao ni kumsifu na kumtukuza Meya. Wanavifurahikia na kuvitetea vyeo vyao (uk. 16). Wanajali masilahi yao tu. Wana ubinafsi. Diwani I ni dhalimu kwelikweli. Anatumia vyombo vya usalama kwa mujibu wa cheo chake kuwanyanyasa watu. Diwani II ni mjanja. Kwa mujibu wa cheo chake anaficha ukweli kuhusu uozo wa Baraza la Cheneo. Anatumia uzalendo kuuhada ulimwengu (uk. 21). Diwani II anawaombea askari nyongeza ya mshahara ili wawe na bidii zaidi ( uk. 22). Naye Diwani I anawatakia mavazi bora madiwani hasa watakapokuwa wanawapokea wenzao (uk. 23) kutoka nchi za nje. Madiwani hawa wanajipendekeza kwa Meya (uk. 59). wanapokutana naye baada ya polisi kuuvunja mkutano wa wafanyakazi waliokuwa wakigoma wanachangamkia tukio hilo, hasa jinsi watu walivyokimbia (uk. 59). Wana ubinafsi tele (uk. 60). Kwao jambo la umuhimu ni kushiba. Wanataka marupurupu na overtime (uk. 61). Wanaunga mkono njama ya kuiba na kuiuza Fimbo ya Meya (uk. 62). Wana fitina na kashifa dhidi ya mwenzao Diwani III (Kheri) – uk.

 1. Ni wafisadi walio tayari kuweka siri. Ni washauri wabaya wa Meya. Wamempotosha kwelikweli. Mambo yanapoharibika Diwani II anageuka. Haungi tena hoja ya kutangaza nafasi za ajira (uk. 74). Anamzindua Meya walimdanganya.

Madiwani hawa wawili ni wahusika wanaowawakilisha viongozi wasiozingatia haki. Ni viongozi wa kutoigwa. Hawafai nyadhifa za uongozi. Wametumiwa kuakisi udhaifu wa watu wanaowachagua watu wasiofaa. Wao ni viongozi waovu na mpaka wawe walichaguliwa na watu waovu. Wanawakilisha uozo kwa jumla na kutowajibika.

Bili ni rafiki yake Meya. Ni mhonyoaji. Anafaidika kwa starehe kwa Meya kuzigharamia. Anakumbuka mkahawa wa kifahari (ku. 26-27). Anaelekea kupenda kumwiga Meya. Anaona hata yeye ampeleke mke wake ng’ambo akajifungulie huko. Sababu? Awaepuke madaktari wa kubahatisha. Watoto wake waweze kupata uraia huko huko. Ni mshauri mfisadi wa Meya (uk. 28). Amemwezesha Meya kutajirika. Anampa ushauri jinsi ya kukabiliana na kesi ya kandarasi aliyoivunja kinyume cha sheria (ku. 28-30). Anampotosha Meya apuuzilie mbali mgomo wa wafanyakazi na maandamano yao (uk. 31) – kelele za chura ni kelele tu. — kawaida ya debe tupu kupiga kelele (uk. 32) — mbio za sakafuni tu (uk. 33). Anaifurahia hatua iliyochukuliwa na askari kuuvunja mkutano wa wafanyakazi waliokuwa wakigoma (uk. 61). Anajiona yeye pamoja na Meya, Diwani I na Diwani III kuwa wao ni werevu zaidi ya Diwani III. Anamwona Diwani III kuwa mjinga (kwa kuyapinga matumizi yasiyofaa ya  fedha za Baraza la Cheneo) – uk. 61. Anapendekeza na kuikuza njama ya kuibwa Fimbo ya Meya, iliyo dhahabu tupu, iuzwe ng’ambo ili waweze kujilipa (ku 61-62). Anamwona Diwani III kuwa mropokaji tu (uk 63). Mhusika huyu ni mnafiki. Mambo yanapoharibika anatoweka (uk. 75).

Bili ni mhusika ambaye mtunzi amemtumia kuwaonya viongozi dhidi ya kuchukua jamaa na marafiki kwa ushauri hasa wanapoongozwa na tamaa na ubinafsi wao.

Mama ni mfanyakazi wa Baraza la mji wa Cheneo. Yeye hufanya kazi kwa Mstahiki Meya. Ni mama yake mtoto mgonjwa Dadavuo Kaole. Anaishi maisha ya shida nyingi. Yeye ni maskini. Anamhofia mwanawe kwa hali yake kuzorota katika siku mbili (uk. 4).

Mama ni mhusika ambaye anawakilisha kundi la maskini. Mtunzi anamtumia kuonyesha maskini wanakosa bidhaa muhimu kama vile kuni na mafuta taa. Kupika ni shida.

Wanategemea makombo ya chakula cha matajiri. Wanatumia hata chakula kilichokusudiwa mbwa wa bwana.

Dadavuo Kaole ni mtoto mdogo wa mama mfanyakazi wa Baraza la mji wa Cheneo. Mama yake anafanya kazi kwa Meya. Ana umri wa miaka mitatu. Yeye ni mgonjwa kutokana na utapiamlo.

Mtunzi anamtumia Dadavuo Kaole kuonyesha umaskini unasababisha msururu wa shida. Mfano ni ukosefu wa chakula, sembuse lishebora. Kutokana na ukosefu wa lishebora kuna maradhi. Kutokana na maradhi kuna shida ya watu kupoteza wakati katika milolongo mirefu katika hospitali.

Siki ni daktari katika zahanati ya Baraza la mji wa Cheneo. Ni binamu ya Meya. Anafadhaishwa na ukosefu wa dawa. Anakerwa na ahadi ya uongo kuhusu kuwasili kwa dawa (uk. 2) – wakisubiri nao ugonjwa utasubiri? Ana Bhuruma. Ana moyo wa kuwahudumia wagonjwa hata kama hawana pesa za matibabu. Siki ni jasiri. Anatenda kinyume na amri ya Baraza la Cheneo anapomwelekeza Nesi Waridi amwite mgonjwa wa kwanza (ku. 2-3) na hata ampeleke katika wadi ya watoto (uk. 5). Anajali masilahi ya wagonjwa angaa kwa kuwapa tu matumaini. Hana imani na Meya. Yeye akitambua undugu kati yake na Meya, Meya anatilia mkazo umeya wake. Anajaribu kumshawishi Meya aone hali mbaya ya maisha ya watu katika mji wa Cheneo lakini Meya anashikilia ya kuwa mambo ni mazuri kuliko kwingineko (uk. 11). Meya anamwona kama msaliti. Tena anamwona kama mtundu. Anamkabili Meya kwa ukakamavu (uk. 14). Ana msimamo thabiti dhidi ya uongozi duni ambao kwao Meya anampiga marufuku kwake. Ni mvumilivu. Watu wengi wanakufa akiona lakini anaendelea kuwa na wagonjwa (uk. 36). Viongozi wa wafanyakazi wana imani naye. Wana tumaini akiongea na Meya, huyo Meya atasikiliza shida zao. Tatu anaenda kumwona (uk. 38). Siki ni mwaminifu. Anamwahidi Tatu ataenda kumwona Diwani III, Bwana Fedha na Kazi wa Baraza (uk. 39) na kwa kweli siku ya pili anaenda hadi kwake (uk. 45). Anamwona Meya kuwa msaliti kwa waliomchagua (uk. 49). Ana tabia ya wanataaluma kukwepa siasa. Anachukia siasa kwa uchafu impakao mtu (uk. 49). Anahofia uongozi wa kiimla (uk. 49).

Daktari Siki anawakilisha watu wenye maono na nia nzuri ya kutaka mabadiliko bila ya kuwa wanasiasa. Mtunzi amemtumia mhusika huyu kuonyesha wanataaluma wamekwepa wajibu muhimu katika uongozi kwa kuwaachia wanasiasa nafasi ya kuendeleza uozo wao. Wajitose katika siasa ndipo waweze kuusafisha uozo wakiwa ndani.

Mhubiri kwa mujibu wa cheo chake ni mtumishi wa Mungu. Anaelekea kuwa mjanja. Anamwinua Meya kiasi cha kumsema kuwa ni sawa na Mungu (uk. 41). Anamsifia upendo wa Bwana ilihali ni mtu ambaye anawadharau watu wengine. Anauombea uongozi wa Meya usiweze kutetemeshwa na udumu milele (uk. 42)! Ni mwoga. Askari wanapowamuru, yeye na Meya walale chini anatii (uk. 42).

Mtunzi anamtumia mhusika huyu kuonyesha wapo wahubiri ambao wamelifanya Neno la Mungu ujasiriamali. Mhubiri anaakisi waombezi wauzao maombi. Waombezi wa balaa. Mhubiri anaelekea kunufaika kifedha na kibinafsi kwa kujikomba kwa Meya.

Tatu, Beka na Medi ni wawakilishi wa wafanyakazi. Wanataka dawa katika zahanati ya mji.

Tatu anaenda kumwona Daktari Siki. Ana tumaini undugu wake yeye Siki na Meya

utamwezesha kusikiwa na Meya kwa manufaa ya wafanyakazi (uk. 38). Haamini Meya amempiga marufuku Siki binamu yake kwake na ofisini. Anaona mgomo utawafaa licha ya Siki kumtahadharisha kuhusu athari za mgomo. Anaupokea ushauri wa Siki watumie suala la mameya wanaotarajiwa kushinikiza takwa lao (ku. 38-39).

Wawakilishi hawa wanapokutana na Meya wanaonyesha ushupavu wao. Tatu anamfahamisha Meya wanayashughulikia masilahi ya wafanyakazi. Wanataka ajira ya kuweza kujivunia, ajira ya maana. Wanasema wazi wamefanywa ‘wakopaji’. Wana matatizo mengi. Anamfahamisha watu wamechoshwa. Anamkataza Meya waziwazi ya kwamba maisha yao, Meya na madiwani (wakubwa) hayawezi kulinganishwa na ya watu wa chini (wafanyakazi) – uk. 69. Watoto wao wanafukuzwa shule kwa kukosa karo ilihali wa wakubwa wanalipiwa karo. Anataka waruhusiwe kushiriki kikao cha madiwani. Meya anapokataa anamsisitizia mgomo utaendelea.

Beka anapinga mishahara ya kuchelewa au kulipwa nusu. Anamwekea wazi Meya ya kuwa kazi hawaoni matunda yake – ni maskini na hawana akiba (uk. 67). Anamjulisha Meya walipoongezwa mshahara zamani, nyongeza ilikuwa vipeni tu (uk. 68). Anapinga ukosefu wa dawa na zitokeapo kuwepo, kuagizwa walipie ilihali Meya na wenzake wana bima katika hospitali kubwa. Anaangazia hali ya wakubwa kujipa mgao mkubwa lakini wafanyakazi wakipewa kidogo (uk. 70). Anataka zitokako pesa nyingi za kuwalipa Meya na madiwani na zitoke kuko huko kuwapa wafanyakazi. Anapinga dai la Meya ati hakuna pesa (uk. 71).

Medi anataka ajira ya kuyajali masilahi na heshima ya watu. Anatofautiana na Meya kuhusu yeye kuwathamini zaidi wageni wanaotarajiwa huku akiwapuuzilia mbali wafanyakazi.

Anamtaka Meya awaone nao pia ni wanadamu (uk. 69).

Mtunzi anawatumia wawakilishi wa wafanyakazi kuonyesha kuwa mwajiriwa ni mtu anayeishi maisha duni. Anakabiliwa na matatizo mengi. Mshahara aupatao unamwumbua kiasi cha kupewa jina ‘mkopaji’. Ni mtu ambaye hana uwezo wa kuweka akiba. Ni mtu ambaye anapostaafu hana chake.

Askari I na Askari II ni polisi. Wamelewa kiu ya kumlinda na kumtetea Meya. Kimakosa wanaingia kwa fujo na nguvu katika ofisi ya Meya. Kelele za maombi zinawafanya wadhani vinyangarika wameingia kuleta fujo (uk. 43). Wanaomba msamaha. Hatimaye askari wao hao waliomlinda Meya kwa jazba ndio wao hao wanaotumwa kwenda kuwakamata yeye Meya na madiwani.

Askari ni wahusika ambao mtunzi amewatumia kuonyesha kazi ya askari ni kuzingatia nidhamu ya kutii amri. Wametumiwa kuonyesha uongozi hautegemei nguvu ukafaulu. Uongozi haudumu kwa nguvu. Uongozi msingi wake ni maadili na unahitaji kuungwa mkono na taasisi na walio wengi.

Sauti ni za wafanyakazi waliogoma. Zimesheheni kilio cha wafanyakazi wakimlilia Meya awasikize. Ni sauti za kudai haki za wafanyakazi kama vile huduma za afya na kuangaliwa masilahi yao (ku. 30-31). Kisha ni sauti ya kiongozi wa wafanyakazi akiwahutubia wafanyakazi wenzake wadumishe umoja hadi mwisho wa kudhalilishwa kwao (uk. 57).

Sauti ni wahusika ambao wanatekeleza wajibu muhimu wa kuonyesha masilahi ya wafanyakazi ni sharti yatiwe maanani. Pia, sauti zinaonyesha migomo ni matokeo ya mateso ya muda mrefu na kuonewa kwa watu wa chini.

Gedi ni Mpambe wa Meya. Ni mhudumu maalumu ambaye anatunza maslahi ya Meya, ukiwemo ulinzi, kila pahali, nyumbani na ofisini. Ni mnyenyekevu na mtiifu kupindukia. Anamwita Meya ‘Mzee’ kumpa heshima ya hali ya juu (uk. 10). Anakaribia kuwa kinyago. Anapoitwa anakimbia nusura aanguke (uk. 8). Ni mtu wa mbio kila wakati na haachi kupiga

saluti (ku. 8, 10, 13, 15, 18, —-). Yawezekana amesoma au amejifunza maneno machache ya Kiingereza hasa sir, Yes sir! na Thank you sir! (ku. 8, 10, 33 —-).

Gedi ni mhusika ambaye anawakilisha watu ambao kazi yao ni kuzingatia kanuni wala si fikira na wawazo yao.

Dida ni mhudumu wa nyumbani kwake Meya. Anawajibikia tatizo la Meya mezani. Kosa la Meya kumwaga chai analipokea kuwa lake (uk. 9). Ana heshima kuu kwa Meya. Anamwita ‘baba’ (ku. 9, 10). Anachukulia kimzaha matukio ya siku mbili zilizotangulia wakati polisi walipouvunja mkutano wa wafanyakazi waliokuwa wakigoma kwa kufyatua risasi (ku. 64- 65). Anaiheshimu kazi ya askari huku akiidharau yake ya ufagizi. Anawasilisha ujumbe wa kuwepo kwa matabaka ya watu – watu wa maana (watu, watu wanaoishi maisha ambayo watu wanastahili kuishi) na watu wasio maana mbele za watu wa maana (viatu, watu wanaoishi maisha duni ambayo hayastahili watu kuishi). Anatambua Meya anaithamini jamaa yake (akaipeleka ng’ambo) huku watu ambao hawana maana wakibaki katika uvundo na hatari (uk. 65). Baada ya kuwazia anaona hahitaji kujishughulisha na yasiyomhusu.

Anajali masilahi yake tu. Ana ubinafsi kwani anatosheka na kuwa na kazi. Bora ana kazi.

Dida ni mhusika ambaye mtunzi anamtumia kuonyesha wapo wafanyakazi ambo roho zao ziko kwingine lakini kwa kukosa kazi nyingine wanaendelea kuzifanya kazi walizoajiriwa kuzifanya.

Wahusika wengine

Wahusika wasaidizi, wanarejelewa tu. Hao hawaonekani. Wapo wagonjwa katika mstari mrefu katika zahanati. Hawa wanarejelewa kuonyesha na hata kusisitiza tatizo la maskini kukosa huduma za afya katika hospitali za umma. Wanakumbana na ukali wa manesi ambao wanakabiliwa na changamoto na mitanziko (uk. 3). Hawa wahusika wanakosa dawa.

Wengine wanakosa pesa za kugharamia dawa hizo zikiwepo.

Mama mdogo wa Nesi Waridi ni mzazi ambaye amempoteza mtoto kwa ukosefu wa dawa. Binamu yake Nesi Waridi ni mtoto mdogo wa mama mdogo wa Nesi Waridi. Alikufa kwa ukosefu wa dawa (uk. 35). Mtunzi anawatumia wahusika hawa wawili kudhihirisha hatari ya kukosa dawa. Wanaonyesha jinsi hali ilivyo ya kusikitisha. Kifo cha mtoto kimemsukuma Nesi Waridi katika kuchukua hatua ya kujiuzulu kazi.

Kerekecha ni mfanyakazi wa Baraza la Cheneo. Alipoteza mtoto wake (uk. 69). Mtoto wa Kerekecha alikufa kwa kukosa dawa. Mtunzi anawatumia wawili hawa kusisitizia suala la ukosefu wa dawa na suala la Meya na madiwani kutojali.

Mhazili hatajwi kwa jina. Ni karani wa Mstahiki Meya. Mambo yanapokuwa yameharibika zaidi hapatikani ofisini Meya anapomhitaji. Yeye ni mmoja wa watu waliofaidika kutokana na ufisadi wa Meya. Kukosekana kwake ofisini kunamtia Meya uchungu mkali.

Mahali ni mji wa Cheneo. Mtunzi ameutumia mji huu kuwakilisha si mji tu bali nchi kwa jumla. Uwe ni mji au iwe ni nchi, wahusika waliomo ni wafanyakazi wanaolipwa vibaya. Wafanyakazi wanapodai haki yao hawana kiongozi wa kuwasikiliza. Uwe ni mji au ni nchi, hali inayodhihirika ni ya shida nyingi. Wafanyakazi wana matatizo chungu nzima. Watu hawana kuni. Sheria za kulinda misitu zimewafinya. Hawana dawa katika hospitali. Ahadi za uwongo kwamba dawa zinakuja ndiyo hali. Wafanyakzi hawana vifaa vya kufanyia kazi. Wa kuzoa takataka hawana glavu za kuzizolea. Ukosefu wa chakula umekithiri. Wafanyakazi wa chini wanalipwa mishahara duni. Wakubwa wanajipa mishaharta mikubwa na nyongeza kubwakubwa za mishahara na marupurupu. Watoto wao wanalipiwa karo. Upo unyonyaji wa hali ya juu. Wakubwa wanalipwa mishahara mikubwa na wanakataa kulipa kodi.

Wafanyakazi wanaogoma wanakabiliwa na vitisho vya kufutwa kazi na vijana waliohitimu ambao hawana kazi kuajiriwa mahali pao.

Shuara ni mji jirani ya Cheneo. Wafanyakazi wa uwanja wa kutua ndege wa Cheneo wanapogoma ndege zinaelekezwa huko. Meya haamiji hilo kuwa jambo linalowezekana kwa kuwa ni mji mdogo.

SURA YA TATU

Tathmini ya tamthilia ya Mstahiki Meya

Mstahiki Meya ni tamthilia iliyotungwa na Timothy M. Arege. Yeye ni mhakiki na mhadhiri wa fasihi. Anafundisha katika Catholic University of Eastern Africa, Nairobi.

Hii ni kazi ya fasihi ya mchezo wa kuigiza. Ni tamthilia-tatizo. Inajadili na kuweka wazi masuala na matatizo makubwa si katika mji wa Cheneo tu bali katika nchi nzima na hata bara zima la Afrika. Kwa jumla ni tamthilia ambayo inaakisi uozo uozo uozo.

Uongozi mbaya ni suala kuu ambalo limetawala tamthilia hii. Suala hili limeifungua tamthilia hii. Limemtia Daktari Siki wasiwasi kiasi cha kujisahau na kuzubaa. Anahuzunikia ukosefu wa dawa na ahadi zisizotimizwa kwa uongo ati dawa zi njiani zinakuja. Nesi Waridi anapomtia moyo awe na subira anashindwa kukubali kwani ugonjwa hautasubiri (uk. 2).

Watu wanakufa kutokana na ukosefu wa dawa. Milolongo mirefu ya wagonjwa wanaotaka huduma inaonekana katika hospitali.

Uchumi unaodorora kwa sababu ya uongozi mbaya ni tatizo jingine linaloangaziwa na tamthilia-tatizo hii. Hata hivyo, viongozi wanaojulikana kama wakubwa, wenye nchi, wanaendelea kuishi maisha mazuri. Wanataka waendelee kuishi maisha mazuri zaidi.

Wanachokitaka wanakipata. Kwa mfano, katika hali ya kudorora kwa uchumi, zamani mayai yalikuwa makubwa. Siku hizi ni madogo. Hata hivyo, Meya anataka mayai makubwa (ku. 5). Umaskini umezidi na nakisi ya Baraza ni kubwa (milioni mia moja) lakini Meya kwa kulewa uongozi mbaya anasisitiza askari waongewe mshahara; madiwani waongezwe mshahara; na ajabu zaidi, anakubali ombi la madiwani kutotozwa kodi. Hii ni amri ya kutekelezwa mara moja (ku. 22, 23)!

Ukosefu wa huduma bora ni tatizo ambalo linatokana na uongozi mbaya usio na maono. Ni hali ya kuonyesha kutowajibika kwa viongozi. Ni hali ambayo inadhihirisha utovu wa maadili. Katika hali hii wakubwa wanawapeleka watoto wao kusomea ng’ambo.

Wanawapeleka jamaa zao kutibiwa ng’ambo. Na si hata wao wenyewe huenda huko ng’ambo kutibiwa? Kwa mujibu wa tamthilia hii, Meya anafanya haya kwa kukosa imani na huduma za mji (ku. 26-28).

Umaskini umekithiri. Watu wa kawaida hawana pesa. Wanashindwa kulipia huduma za matibabu. Wanakosa karo kwa ajili ya elimu ya watoto wao. Wanakosa chakula. Wakiwa na chakula hawana kuni. Tusitaje mafutaa taa! Usafiri ni mgumu. Hata hivyo, wakubwa wana chakula mpaka na cha kusaza. Mama yake Dadavuo Kaole alipata masazo akampelekea mwanawe (uk. 4). Meya ana pesa ambazo analipwa kwa ajili ya starehe (uk. 27). Watu wakubwa kwa jumla wana ubadhirifu. Wanaishi maisha ya anasa. Madiwani wanataka pesa za kununulia nguo nzuri (uk. 23). Nyumba ya Meya ina zulia (uk. 1). Anawapangia wageni makaribisho ya kifahari – vyakula, mvinyo na divai kutoka ng’ambo (uk. 25).

Suala la alaumiwe nani linajitokeza. Wazungu wanalaumiwa kwa kuhimiza mfumo wa kugawana gharama. Wapo wanaokubaliana na lawama hii na wapo wanaoipinga. Katika tamthilia hii ya Mstahiki Meya Nesi Waridi anawalaumu Wazungu. Kisha kuna lawama ya nchi kuwa changa. Lakini nchi itakuwa tu changa tangu izaliwe miaka hamsini iyopita? Ati nchi ni maskini ni hoja ambayo Daktari Siki anaipinga kwa dhati (uk. 3).

Watu wa kulaumiwa kwa matatizo ya Baraza la Cheneo ni wanataaluma na wananchi. Wananchi ndio wanaowachagua watu wasiofaa na kuwaacha wale ambao wangefaa (uk. 49). Wanataaluma hawakwepi lawama kwani wanakwepa siasa ati kwa kuhofia kupakwa tope (ku. 49-50). Kwa hivyo, suluhisho la tatizo la uongozi mbaya ni wanataaluma kujitosa katika siasa nao wananchi wawachague watu bora. Ikumbukwe mtu huvuna apandacho (uk. 49).

Katika hali ya uongozi mbaya wafanyakazi wamedunishwa kiasi cha kulazimika kugoma. Nao wapigakura wanaonekana sawa na watumwa (ku. 23, 53). Hawasikizwi. Meya amelewa madaraka (uk. 47). Kuna tatizo kubwa la ukosefu wa kazi za ajira. Hali hii ina tumiwa na wakubwa kuwakandamiza wafanyakazi. Badala ya kulitatua tatizo wanalitumia kama kifaa cha kuwatesea wafanyakazi. Meya analitumia tatizo la ukosefu wa kazi kuwatishia wanaogoma kuwafuta kazi (ku. 21, 32, 54, 60, 76 na 78).

Ufisadi na upendeleo vimezidi. Kandarasi kuvunjwa hivihivi tu na mwanakandarasi mwingine kupewa ni tatizo katika Baraza la Cheneo (ku. 25, 28, 29). Meya na marafiki zake wana viwanja (uk. 27) walivyovipata kwa njia za ufisadi. Meya anampa Mhubiri ahadi ya sadaka ya shilingi laki moja kila mwezi kulipia petrol kwa kuliombea Baraza (uk. 44). Watu wasiostahili wanaajiriwa kazi kwa upendeleo. Meya alimsaidia mhazili wake kupata kazi ingawa hakustahili (uk. 77).

Wizi wa waziwazi upo. Kuna njama ya kuiba fimbo ya Meya chini ya ulinzi wa Bwana Usalama wa Baraza (ku. 61-62). Pendekezo la kutaka Bili alipwe alihali yeye si mfanyakazi wa Baraza ni wizi mbali na kuwa ufisadi (uk. 61).

Washauri wabaya katika uongozi mbaya hasa ni watu wa ubinafsi. Ni watu ambao haja yao ni kutimiza maslahi yao. Mmoja ni Bili na wengine ni Diwani I na Diwani II. Katika uongozi mbaya, kiongozi anayewategemea washauri wabaya huwatenga washauri wazuri. Meya amewatenga Diwani III (Kheri) na kumpiga marufuku binamu yake Daktari Siki. Wawili hawa anawaona ni wasaliti na wachochezi.

Kuna udikteta na matumizi mabaya ya mamlaka (uk. 48). Meya anatoa amri za kutatiza. Pesa hazipo lakini anaamuru nyongeza za mishahara na kutotozwa kodi kwa madiwani.

Tatizo la utegemezi limekita mizizi katika Baraza la Cheneo. Kuna udhaifu wa kutegemea misaada ya kulipia mishahara (uk. 55) badala ya kufikiria miundomsingi ya kuzalisha pesa na utajiri. Hata hivyo, mishahara yenyewe ni inayolipwa hulipwa wakubwa. Maono kwa manufaa ya vizazi vijavyo hayapo.

Tanzia ni kati ya maudhui katika tamthilia ya Mstahiki Meya. Yanahusu vifo vya watoto na watu wengine kutokana na ukosefu wa dawa katika zahanati ya umma. Ni msiba kwa kuwa watu wana shida nyingi na kuna kilio kikuu cha wafanyakazi. Je, wale watu ambao hawana kazi, ingawa hawajatajwa, wanaishi katika hali gani?

Ubinafsi ndio unaoitawala mioyo ya viongozi.

Kwa ufupi, mabadiliko yameanza kutokea, hata kama mji wa Cheneo umeoza na unavunda. Taasisi zimeoza na zinavunda. Nchi imeoza na inavunda. Bara la Afrika limeoza na linavunda. Hata hivyo, mambo yamebadilika wala si kama zamani. Watu wameanza kuona na wanataka vitendo wala si ahadi tupu. Fauka ya hayo, wakubwa wameanza kuchukuliwa ili wawajibikie vitendo vyao.

Tamthilia hii ni ya uhalisia. Inaakisi ukweli wa mambo na ni ukweli unaouma jinsi ukweli uumavyo daima. Wananchi wanaishi katika dunia yao ya matatizo chungu nzima nao viongozi wanaishi katika dunia yao ya raha na anasa tele.

SURA YA NNE

Fani (mbinu za kisanaa)

Kwa mujibu wa muundo, kazi hii ya fasihi Mstahiki Meya ni tamthilia, mchezo wa kuigizwa. Katika tamthilia wapo wahusika ambao wanamwakilisha mtunzi kwa uzungumzi na vitendo. Tamthilia imeandikwa ili iweze kuigizwa katika jukwaa kwa madhumuni hadhira iutazame mchezo na kusikiliza maneno yanayosemwa.

Mtunzi wa tamthilia ni msanii. Wahusika wanaihuisha kazi ya msanii. Huku mwandishi akiwaza, wahusika huzungumza na kutenda na kutendeana. Usimulizi wa nafsi ya kwanza ndio unaotawala katika uzungumzi.

Maelezo ya jukwaa yametolewa katika mabano katika herufi za mlazo (italiki). Tamthilia hii ina maelezo kuhusu vitendo, hali, mavazi na mandhari ya jukwaa.

Mstahiki Meya ni tamthilia yenye wahusika wanaoonekana wapatao kumi na saba na wasioonekana kadha ambao wanajumuisha wagonjwa, wakiwemo watoto na wafanyakazi.

Tamthilia hii imegawanywa katika SEHEMU NNE na jumla ya maonyesho kumi na mawili. SEHEMU YA KWANZA ina maonyesho matatu; SEHEMU YA PILI ina maonyesho manne; SEHEMU YA TATU ina maonyesho matatu na SEHEMU YA NNE ina maonyesho mawili.

Mahali pa mchezo ni mji wa Cheneo.

Msuko (ploti), yaani, jinsi matukio ya hadithi yanavyotukia na kufuatana kiwakati. Mstahiki Meya ni tamthilia yenye msuko sahili. Matukio yanafuatana kiwakati tangu mwanzo hadi mwisho. Tamthilia inaanza kwa kuonyesha wasiwasi wa Dakitari Siki na tatizo la ukosefu wa dawa katika zahanati ambao umefichwa katika ahadi za uongo kwamba zi njiani zaja.

Kutokana na tatizo la ukosefu wa dawa, tatizo la umaskini linafichuliwa. Hali ikiwa mbaya vile, mtunzi anaibua hali ya maisha ya anasa ya viongozi (Onyesho II, uk. 8) huku uchumi ukidorora. Masuala ya uongozi duni yanaanza kuibuka: gharama ya maisha inazidi kupanda (uk. 11); ukosefu wa mahusiano mema na uhusiano mwema (ku. 12, 13, 14, 15).

Maudhui ya uongozi duni yanaendelezwa kwa undani zaidi (Onyesho III): udikteta wa Meya; tofauti katika Baraza la Meya; ubinafsi wa Meya (uk. 17); vibaraka wa Meya; kutowanufaisha watu wa kawaida (uk. 20); matumizi mabaya ya vyombo vya usalama (uk.

21); ubinafsi na ufisadi wa madiwani (uk. 23) —-

Mtunzi anaendeleza maudhui ya uozo wa ufisadi (Sehemu II, Onyesho I): ubadhirifu (uk.  25); ukosefu wa elimu na matibabu bora (ku. 25-27); unyakuzi wa viwanja (uk. 27); utoaji wa kandarasi kwa njia haramu (uk. 28); mgomo wa wafanyakazi (uk. 30-33) na upurukushani wa Meya; ufuataji wa ushauri wa kupotosha (kutoka kwa Bili [ku. 28-33]).

Kuzorota zaidi kwa huduma za afya yanafafanuliwa katika Sehemu ya Pili, Onyesho la Pili. Watu wanakufa, Nesi Waridi anajiuzulu kazi (uk 35); kuhangaika kwa wafanyakazi mpaka Tatu anamwendea Daktari Siki angaa atumie undugu wake na Meya ajaribu kumshawishi Meya awasikilize wafanyakazi (uk. 38). Kauli ya mwisho inakuwa ni mgomo.

Bili anampa moyo Meya Mhubiri yu pamoja naye (uk. 33). Neno la Bili linatimia katika sehemu ya pili, onyesho la tatu, Mhubiri anapowasili kwa maombi (ku. 41-42). Maudhui ya ufisadi yanaendelezwa. Mhubiri atalipwa sadaka ya shilingi laki moja kwa mwezi (uk. 44).

Katika Sehemu ya Pili, Onyesho la Nne, mtunzi anaendeleza na kusisitiza masuala mbalimbali: mahusiano mabaya kati ya Meya na binamu yake, Daktari Siki (uk. 45); tofauti baina ya Meya na Diwani III (Kheri). Meya akiwa mezani anaonyesha ulafi huku Diwani III akionyesha kiasi – anamstarehesha mgeni wake kwa sharubati na asusa (tu) – uk. 45. Watoto wanakufa, kuna ukosefu wa dawa na ahadi za uongo. Kuna umaskini (uk. 46); Meya kukataa

kusikiliza kilio cha hali mbaya ya watu; Meya kulewa madaraka; na ulafi na tamaa ya viongozi (uk. 47); chanzo cha uongozi mbaya – mamkala Mengi kisheria ya Meya (ku. 48-

49) —wananchi ambao huwachagua watu wabaya, wanataaluma ambao wamejitenga na siasa (ku. 49-50). Lipo suala la suluhisho la tatizo la uongozi mbaya – watu wote washirikiane na wafanye bidii kuibadili hali kwa kuung’oa uozo uliopo (uk. 51).

Sehemu ya Tatu, Onyesho la Kwanza, ni muhimu kwa kuendeleza maudhui ya athari mbaya za uongozi mbaya. Meya amemtenga kabisa Diwani III na maamuzi muhimu ya Baraza (uk. 52). Meya anamwamuru Diwani III, Bwana Uchumi na Kazi wa Baraza kuwapa madiwani nyongeza ya mshahara. Anauupuuza ushauri mzuri wa Diwani III. Anapuuza tahadhari yake dhidi ya kuwabagua na kuwapuuza wafanyakazi waliogoma. Maringo ya Meya pamoja na kulewa madaraka kunadhihirika. Anajipa PhD (uk. 54). Dharau ya Meya kwa wafanyakazi inatiliwa mkazo na udikteta wake unawekwa wazi zaidi. Anatumia kitisho cha insubordination dhidi ya Diwani III. Ni mtu ambaye kinyume na Diwani III hajali masilahi ya watu wa chini na vizazi vijavyo (uk. 55).

Katika Sehemu ya Tatu, Onyesho la Pili, mgomo wa wafanyakazi umepamba moto. Diwani I, Diwani II na Bili wanaendelea kumpa Meya ushauri wa kumpotosha. Wanamtenga Diwani III na kupanga wizi wa Fimbo ya Meya ili waiuze kwani imeundwa kwa dhahabu tupu (ku.

57-63). Polisi wanatumiwa kuvunja mkutano wa wafanyakazi.

Katika Sehemu ya Tatu, Onyesho la Tatu (ku 64-65) mtunzi anaonyesha mtu wa chini akilichukulia suala zito kimzaha na jinsi alivyokata tamaa hadi asijihusishe na mambo anayoyaona kuwa yasiyomhusu. Anajali masilahi yake tu – bora ana kazi kwa Meya. Hata hivyo, ni wazi watu wamewekwa katika matabaka mawili – watu wa kuheshimiwa wanaoishi maisha ya hali ya juu na watu wa kudharauliwa wanaoishimaisha duni. Haya ni makundi ya watu wenye vitu na wasio na kitu.

Sehemu ya Nne, Onyesho la Kwanza, inaonyesha mgomo wa wafanyakazi unaendelea na hali imeharibika zaidi mpaka Meya anakubali kukutana na viongozi wa wafanyakazi. Hii ni hali inayoonyeha viongozi wa kutojali mpaka mambo yaharibike kabisa kabla wachukue hatua.

Hata hivyo, mkutano mrefu kati ya Meya na wawakilishi wa wafanyakazi (Tatu, Beka na Medi) hauzai tunda lolote. Katika huo mkutano kunaangaziwa zaidi mishahara duni, umaskini, ukosefu wa tumaini kati ya wafanyakazi na watu kufa kwa kukosa dawa huku Meya na madiwani wakipewa kila kitu (ku. 66-72).

Sehemu ya Nne, Onyesho la Pili, ni mwisho wa hadithi katika tamthilia hii ya Mstahiki  Meya. Mambo yameharibika kabisa na zaidi. Migomo imeongezeka. Wafanyakazi wa viwanja vya ndege wamegoma (uk. 76). Mafuta hayapo kutokana na mgomo wa wahudumu wa bohari la mafuta! Wageni waliotarajiwa wanaahirisha ziara yao kwa kuhofia tishio la kuweza kuzuka kipindupindu (uk. 77). Hatua hiyo inakuwa afueni kwa Meya. Mji hauna maji safi lakini Meya anayo.

Hadithi inaisha ghafula inapofikia upeo wa mambo kuwa mabaya sana. Uongozi wa Meya unaweza kukisiwa umekwisha. Anatakiwa aende kuelezea katika makao makuu.

Anawalaumu wanahabari (uk. 79). Meya anazirai nao Diwani I na Diwani II wanatiwa nguvuni (uk. 79).

Hatima ya Meya ni nini?

Mtindo

Mtunzi ametumia njia gani kuwasilisha ujumbe wake katika tamthilia ya Mstahiki Meya? Mitindo inayo dhihirika waziwazi ni kama: Maongezi na vitendo ni kawaida ambavyo hii ni tamthilia. Wahusika wanazungumza kuwasilisha mawazo ya msanii. Wakati uo huo

wanatenda kwa ajili ya kuwasilisha hisia na pakubwa kwa ajili ya watazamaji kwani vitendo ni sharti katika mchezo wowote wa kuigiza.

Maelezo ya mtunzi yametumiwa kwa njia ya usimulizi wa nafsi ya mtu wa tatu katika mabano katika herufi za italiki. Mifano ni kama: Kuwasilisha ujumbe wa maumivu aliyo nayo mtoto, mtunzi anaeleza – (Mtoto analia huku akigaagaa —) – uk. 3; kwamba Meya amefunga tai anaeleza – (—-Anaishika tai yake na kuiweka sawa) – uk. 10; kuonyesha hisia za Meya kukasirika anaeleza – (—- Akigonga meza) – uk. 12; kuonyesha matumizi ya mabavu, askari wanavunja mkutano wa wafanyakazi anaeleza – (Mara inasikika milio ya risasi na vilio vya watu wakikimbilia usalama. —-) – uk. 57.

Sauti katika Mstahiki Meya ni maneno ya wazi yanayosemwa na wafanyakazi (ku. 30, 57) na ya kiongozi wa wafanyakazi (uk. 57). Sauti hizi zinasikika wakati wa mgomo wa wafanyakazi wa Baraza la Cheneo. Ni katika Sehemu ya Pili, Onyesho la Kwanza na Sehemu ya Tatu, Onyesho la Pili. Zinawakilisha malalamiko ya wafanyakazi kwa Meya ambaye amekataa kuwasikiliza.

Mkengeuko ni mbinu ya mtunzi kuwapa wahusika kazi ya kuongea na hadhira. Umuhimu  wa ukengeushi ni kuifanya hadhira ikumbuke inatazama mchezo wa kuigiza. Pia, hufanya kazi ya kujitenga na ukweli halisi, kama unavyonekana katika Sehemu ya Tatu katika Onyesho la Tatu lote. Dida anaongea na hadhira. Onesho hili ni kama muhtasari wa tamthilia yote tangu mwanzo hadi mwisho. Linaonyesha yaliyotokea na kwa kiasi fulani yatakayotokea (wakubwa kukana [uk. 65]). Katika mkengeuko huu ipo falsafa ya kinaya. Kwa mfano, Dida ni kama anaipenda na kuitamani kazi ya uaskari lakini si yake huku akiidunisha kazi ya ufagizi ambayo ndiyo yake. Askari ana nguvu kwa bunduki yake sawa na mfalme ilihali hata bwana anajua na ndiye mkubwa lakini uwezo u kwingineko. Watu wakifa wakubwa hukana. Anajitia kando na tatizo la wafanyakazi ilihali yeye naye ni mfanyakazi kama wao.

Kicheko kinatumika kufurahikia au kukejeli (kudhihaki). Kinategemea hali. Diwani I na Diwani II wanacheka kumkejeli Diwani III. Yeye ana mtazamo tofauti na wao (uk. 16). Meya anacheka taratibu kufurahikia wazo ati anajua namna ya kuwafurahisha wageni (mameya) wanaotarajiwa (uk 25). Meya yuyo huyo mmoja anacheka kuufurahikia ushauri wa Bili jinsi atakavyofaidika yeye Meya kutokana na kupelekwa mahakamani na mwanakandarasi (uk. 30). Pia, anafurahikia polisi kuwatawanya wafanyakazi wanaogoma.

Hicho ni kicheko cha ukatili (uk 57). Dida hacheki tu bali yeye anachekacheka. Kuchekacheka kwake kunaonyesha hali ya kufanyia mzaha jambo la umuhimu mkubwa kama kwamba mtu haelewi uzito wake (ku. 64-65). Onyesho lote la tatu limejaa vicheko – kicheko baada ya kicheko na kila kicheko ni kicheko kirefu. Wakidhani wamefaulu Meya (uk. 78) na Diwani I (uk. 79) wanacheka.

Kimya ni mbinu anayoitumia mtunzi kuchochea fikira. Tamthilia ya Mstahiki Meya inajadili masuala chungu nzima yanayohitaji kuwazwa kwa undani la sivyo hayataona utatuzi wowote. Hata kabla ya kujibu, mmoja ananyamaza kwanza, afikiri ndipo ajibu. Kabla Daktari Siki aulize, ‘Wamefika wangapi leo hii?’ – (uk. 7) ananyamaza kwanza. Hao ni wagonjwa katika zahanati ambayo haina dawa. Kabla atoe maoni yake, Nesi Waridi ananyamaza kwanza.

Kimya kinatangulkia jibu lake, ‘Sidhani. ’ – (uk. 7).

Ushairi umetumika katika sauti, ujumbe wa wafanyakazi kwa Meya (ku. 30-31, 57) na hotuba ya kiongozi wa wafanyakazi kwa wafanyakazi (uk. 57). Meya anafurahika kishairi polisi wanapowatawanya wafanyakazi kwa kufyatua risasi na kuwafanya walie wakikimbilia usalama (ku. 57-58). Daktari Siki vilevile anapojisemea baada ya kuongea kwa simu yake ya mkono na Tatu, mwakilishi wa wafanyakazi, anaongea kishairi (uk. 34). Ushairi huipa kasi hadithi. Una mahadhi ya kipekee mbali na usimulizi maalumu.

Sentensi fupifupi zimetumiwa kwa wingi kwa wingi kwa kuwa hii ni tamthilia na usimulizi utawalao ni maongezi. Sentensi fupifupi humwepusha msomaji na uchovu wa kusoma sentensi ndefundefu. Humwezesha msomaji kuifuata hadithi, hasa matukio haraka. Hizi huupa kasi mchezo. Kwa waigizaji, sentensi fupifupi hurahisisha ukumbukaji kwa ajili ya ukaririaji. Mifano mingi ipo ya sentensi fupifupi za neno mojamoja (uk. 1 [Wengi.]; uk. 4 [Chakula]). Zipo za maneno mawilimawili; matatumatatu; na machachemachache tu. Hamna kitu (uk. 1); Nilichotoa kwa bwana (uk. 4).

Ukataji sentensi ni mtindo unaotumika kwa haja mbalimbali.

Kuonyesha hali ya kukosa subira. Kwa mfano: Daktari Siki anapomkatiza Nesi Waridi (uk. 2). Mama anapomweleza Daktari Siki hali ya mtoto. Na leo … Afadhali jana (uk. 4). Bili na Meya wanapoongea (uk. 28).

Meya anapokuwa na hasira kwa sababu ya mayai kuwa madogo (uk. 8).

Dida anapokuwa na wasiwasi na anapokatizwa na Meya ambaye hana haja ya kumsikiliza (uk. 9). Meya anapomkatiza Daktari Siki kwa kuuchukia usemi wake (ku. 10, 11, 12).

Kuonyesha ubishi. Mfano: Diwani III anapokuwa na ubishi na Diwani I na Diwani II (ku. 16, 17).

Kuonyesha kubadilika ghafula kwa usemi wa mhusika. Meya anapozungumza na madiwani kisha anamwita Gedi ili amtume maji (uk. 17).

Kuonyesha hofu. Gedi anasitasita asiweze kueleza waziwazi ya kuwa hali ya mambo ni mbaya (ku. 75, 76).

Mchezo ndani ya mchezo unaonekana katika Sehemu ya Tatu, Onyesho la Tatu. Baada ya askari kuvunja mkutano wa mgomo wa wafanyakazi na watu kutoroka siku mbili awali Dida analiigiza tukio hilo nyumbani kwa Meya. Ufagio wake ndio bunduki yake. Igizo hili ni kumbukumbu ya yaliyotokea. Kumbukumbu hii inatilia mkazo uwepo wa watu (watu) na viatu (watu duni).

Mbinu rejeshi ni ufundi wa kumrudisha nyuma msomaji kwa lengo la kuonyesha yaliyotokea awali wakati wa sasa. Onyesho la Tatu la Sehemu ya Tatu linaigiza tukio la awali, siku mbili baada ya tukio hilo (ku. 64-65).

Taharuki ni mtindo wa kutotiririsha habari, ni mtindo wa kudokeza habari kidogokidogo, hatua kwa hatua, tangu mwanzo wa hadithi. Matokeo yake ni kumtia msomaji hamu ya kutaka kujua kitu kitakachotokea. Hata akijua kimbele kitakachotokea, mbinu hii humtia hamu ya kutaka kujua namna kitakavyotokea. Mifano: Mwishoni mwa Sehemu ya Kwanza, Onyesho la Pili, Meya anaamuru wanakamati wote wahudhurie mkutano wa dharura bila yeyote kukosa. Msomaji anapata hamu ya kutaka kujua ni kitu gani kitakachotokea.

Tamthilia inapokamilika Meya amezirai. Ni kitu gani kitakachompata? Ni nini hatima ya madiwani waliotiwa nguvuni?

MATUMIZI YA LUGHA NA TAMATHALI ZA USEMI

Hadithi katika tamthilia ya Mstahiki Meya imesheheni ukwasi wa lugha. Ufundi wa lugha umedhihirika waziwazi.

Kimsingi hii ni tamthilia ya Kiswahili wastani. Katika tamthilia hii kuna:

Kuchanganya ndimi ambao ni mtindo mwandishi kuwaumba wahusika ambao wana tabia ya kutumia Kiswahili na Kiingereza. Meya kwa maringo yake anaingiza maneno ya Kiingereza katika uzungumzi wake. Mifano ni: Bloody hens, Nonsense – (uk. 8); — vitano incase. —, hasa ile prime plot; nina entertainment vote ya Meya — (uk. 27).

Kumfurahisha Meya, na pengine kwa amri ya huyo Meya, daima Gedi hakosi kujibu, ‘Yes sir!’ Meya anapomwambia kitu (ku. 8, 10, 13, —-). Anachanganya Kiswahili na Kiingereza anapomjibu Meya, ‘Daktari Siki, sir, ‘Sina habari sir,’ (uk. 10).

Kuna uwezekano Meya amemwambukiza Bili tabia ya kuchanganya Kiswahili na Kiingereza. La sivyo, Bili anafanya hivyo kujikomba kwa Meya. Mifano: Gentleman’s agreement Mstahiki Meya’; (uk. 29). …ni kama…Talk of the devil (uk. 31).

Tatu, mwakilishi wa wafanyakazi anasema, ‘Tunaambiwa diary yake imejaa —- (uk. 38). Huenda ikawa matumizi ya msamiati wa Kiingereza unatokana na mhusika kutojua msamiati wa Kiswahili ‘shajara’.

Kuna matumizi mengine ya msamiati wa Kiingereza kutokana na uwezekano wa kutokuwepo na msamiati wa moja kwa moja wa Kiswahili au kukosa uzoefu wa msamiati wa Kiswahili katika muktadha unaohusika. Mifano: Mayor’s Act; Riot Act (uk. 48) na Collective responsibility (uk. 49).

Vilevile kuna mazoea tu baina ya watu wa taaluma moja (uk. 5). Daktari Siki na Nesi Waridi wanapoongea mbele ya mama yake Dadavuo Kaole wanatumia Kiingereza, pengine kwa minajili ya kumweka kando mama huyo.

Kubadili lahaja (uk. 50) katika maneno ya Daktari Siki anapoingiza kidogo lahaja ya Kimvita. Anasema, ‘Ya mwananti kuivunda nti,’ badala ya ‘Ya mwananchi kuivunja nchi.’ Matumizi haya yanaelekea kulingana na lahaja ya methali ya Diwani III (Kheri) katika, ‘Ndiyo yale ya ngome in’tuumiza naswi tu mumo ngomeni.’

Utohozi ni mbinu ya kuyapa maneno ya Kiingereza sura ya Kiswahili na kudumisha maana ileile. Mifano katika tamthilia hii ni: Meya kutokana na mayor; daktari kutokana na doctor; wodi kutokana na ward; nesi kutokana na nurse. Kuna uwezekano jina Siki limetoholewa kutokana na kitenzi cha Kiingereza sick.

Tamathali za usemi huhusu utumiaji wa neno au maneno kwa njia ya kuleta maana batini, maana tofauti na maana ya juujuu, maana ya kawaida. Mifano katika tamthilia hii ni kama:

Majazi ni mbinu ya kuwapa wahusika na kupapa mahali majina ambayo yanaashiria wasifu wa tabia na hali zao.

Waridi ni ua mojawapo. Ni ua lenye harufu nzuri, hunukia. Waridi likiwa ua halidumu. Mmea wenyewe una miiba. Katika tamthilia ya Mstahiki Meya Waridi ni mwuguzi katika zahanati. Kama mhusika, mwanzoni anadhihirisha subira. Hiyo ni sifa nzuri. Subira ni nzuri na ni mojawapo ya uzuri alio nao Waridi. Anasubiri dawa. Katika kazi ya unesi Waridi hakudumu jinsi na ua ambalo halidumu. Alijiuzulu kazi ya unesi. Akiwa kazini ana msimamo mkali, sawa na miiba ambayo ina ukali wa kudunga. Anapomkataza mama wa mtoto mgonjwa angeojee hadi aiitwe usitarajie mama huyo hakuchomwa.

Siki ni maji kama vile ya matunda au nazi yaliyochachuliwa, yaliyotiwa ukali, kuongezea ladha katika baadhi ya vyakula au dawa. Maana nyingine ya ‘chachuliwa’ ni ozeshwa. Katika lugha, kuwa kama siki ni kughadhabika, kukasirika. Kama mhusika katika tamthilia hii yeye ni daktari katika zahanati. Akiwa mhusika ana hasira kwa kutoona dawa zilizoahidiwa. Yeye ni mwanataaluma. Anahitajika katika siasa ili aongezee ladha katika uongozi. Kwa hali ile ya siki kuwa na ukali (uchachu), Daktari Siki ana kiasi cha ukali dhidi ya Meya na uongozi wake mbaya. Hamwogopi Meya (Chunga! Unamkanyaga nyoka mkia – uk. 15). Hali ya kufanywa kuoza inatoa sifa ya Daktari Siki kuashiria mwisho wa uongozi wa Meya.

Anamharibia Meya uongozi wake (uk. 12) na kumtia Meya ukali (uk. 14). Iwapo hili jina limetoholewa kutokana na kiingereza ‘sick’ litakuwa na maana ya kujisikia vibaya, kuwa mgonjwa. Na kwa kweli Daktari Siki anahisi vibaya kwa kutokuwa na dawa katika zahanati anamofanya kazi. Anahisi vibaya wagonjwa kufa ovyoovyo.

Dadavuo kaole ni jina ambalo linatokana na dadavua. Maana ya dadavua ni ‘pata ufumbuzi wa jambo linalotatiza, toa katika shida’. Kwa hivyo, Dadavuo katika tamthilia hii ni jina linaloashiria suluhisho. Kaole ni jina lenye dhana mbili: Moja inatokana na ‘ole’ ya Kikale (Kizamani), lahaja ya Kiswahili cha zamani. Kutokana na kitenzi ‘ola’ (ona, tazama), katika ngeli ya kale ‘KA-‘ ambayo haitumiki katika Kiswahili wastani. Kwa mfano, katika ‘katoto’

kwa maana ya ‘mtoto (mzuri wa kupendeza, wa kuvutia) kwa upatanisho katika ‘Kaole’ tunapata maana ya ‘Katazame, Kaone’. Kaole Dadavuo ni jina litakaloleta maana ya ‘Katazame ukaondolee tatizo’. Maana ya pili inatokana na ‘ole’ ya maana ya kiingizi ‘ole!’ chenye maana ya majuto au masikitiko. Mama anamsikitikia mtoto wake na amefika zahanatini daktari amfumbulie tatizo la huyo mwanawe kuumwa na hali yake kuzorota tangu siku iliyotangulia.

Sosi ni jina la Mstahiki Meya. Katika lugha ya mitaani ‘sosi’ni ‘la’. Watu mitaani husema ‘tunasosi’ kwa maana ya ‘tunakula’. Meya ni mhusika wa kula. Anapenda kula. Ni mlafi. Analipora Baraza la Cheneo.

Kheri ni jina la Diwani III. Katika ushairi ‘kheri’ ni ‘heri’ katika nathari. Maana yake ni hali ya amani. Maana zingine ni neema, baraka, ustawi, ufanisi. Jina hili likitumika kama kielezi lina maana ya afadhali, bora. Diwani Kheri ni mhusika ambaye anatetea uongozi bora. Ana ushauri bora kwa Meya. Anaona ni afadhali wafanyakazi wote wapewe nyongeza ya mishahara badala ya kuwapa madiwani peke yao. Katika Baraza la Cheneo yeye ni Bwana Uchumi na Kazi. Uchumi unahusiana na ustawi.

Shuara ni jina la mji jirani ya Cheneo. Upo uwezekano jina hili ni la kughushi kutokana na neon shwari ambavyo katika mji huo kuna utulivu na ndiyo maana ya ndege kuelekezwa huko mambo yanapozidi kuwa mabaya katika Cheneo.

Bili ni orodha ya vitu vilivyouzwa pamoja na kiasi cha pesa zinazodaiwa. Ikiwa ni kiingizi kilichokatwa na kuwa ‘bili’ badala ya ‘bilikuli’ maana yake itakuwa ‘hata kidogo’, ‘asilani’, ‘kamwe’. Kama ni jina ambalo limekatwa kutokana na ‘biliwili’ litakuwa na maana ya samaki. Kama ni samaki ‘bili’ litakuwa na maana ya utelezi. Si rahisi kumkamata samaki akiwa majini. Pia, kuna biliwili ni mbigili, ambao ni mmea unaotambaa, wenye mbegu zenye miiba. Basi, katika tamthilia ya Mstahiki Meya Bili ni mhusika wa aina gani?

Kama ni kutokana na kiingizi bilikulu, Bili ni mhusika ambaye hastahili bilikuli (hata kidogo, kamwe) kuwa mshauri wa kiongozi yeyote. Yeye ni mkora, mwizi na mpendaanasa. Ni mbinafsi. Kama ni kutokana na biliwili, aina ya samaki, yeye ni njanja ambaye hawezi kushikika. Mambo yanapoharibika haonekani (uk. 75).

Kama ni kutokana na biliwili (bingili) mmea wenye mbegu za miiba, Bili ni mhusika ambaye matunda ya ushauri wake yanachoma, yanadunga kama miiba. Amesababisha mambo machungu.

Cheneo ni jina lenye maana ya kitu kilichoenea mahali pengi; kilichatapakaa. Katika tamthilia hii Cheneo ni mji mkubwa. Unasimamiwa na Meya. Mji wenyewe umejaa takataka. Migomo imeenea. Shida ni nyingi. Katika uongozi wa Baraza la mji wa Cheneo ufisadi umekithiri. Cheneo ni jina ambalo linawakilisha wingi wa ubaya, uozo, uvundo na tishio la kipindupindu (ugonjwa ueneao haraka).

Usambamba ni mbinu ya urudiaji ambao huchukua miundo mbalimbali. Mifano:

—tunawashauri wasubiri (uk. 2).

Kuona nimeona ulivyoona wewe (uk. 46).

Wakisubiri ugonjwa nao utasubiri? Hujui ngoja ngoja huumiza matumbo? – (uk. 2).

Njiani ni njiani na hospitali ni hospitali (uk. 7).

Kuna raha gani watoto wetu wanapofukuzwa shule kwa sababu —Kuna raha gani

kutazama watoto wetu kufa taratibu mikononi — (uk. 70).

Tashbihi (tashibihi, tashibiha) ni tamathali za usemi wa kufananisha kwa kukitaja kitu kuwa namnakingine kilivyo kwa matumizi ya viungio: kama, kama vile, mfano wa, mithili ya, sawa na, ja. Mifano:

Wewe huoni si kama zamani (uk. 9).

— amekufa kama nzi (uk. 69).

Kupinga haya ni sawa na kumkama simba mwenye watoto (uk. 14).

Sitiari ni tamathali za usemi wa kufananisha kitu na kingine kwa kukitaja moja kwa moja kitu hicho kuwa ni kile kingine. Ufananishaji huu hautumii viungo kama vile ilivyo hali katika tashbihi. Badala ya kusema katika tashbihi ‘mimi ni kama ndugu yako’ isitiari itakuwa na ‘mimi ni ndugu yako’ au ‘mimi ndugu yako’. Mifano:

Unamkanyaga nyoka mkia (uk. 15).

Viongozi wote ni chaguo la wananchi (uk. 49).

Kelele za chura (uk. 31) [ni malalamiko ya wafanyakazi wanaogoma].

Ukweli-kinzani ni tamathali ya usemi ambao kijuujuu huonekana kama kwamba unapingana lakini unapofikiriwa kwa makini unakuwa na ukweli fulani. Kwa mujibu wa Waridi: Haraka haraka haina baraka; lakini kwake Siki, —ngoja ngoja huumiza matumbo. Kauli hizi zina upinzani na ukweli kwa pamoja katika zahanati ambapo wagonjwa wanakufa kwa kukosa dawa huku ahadi za kuwataka wasubiri zikiendelea ( uk. 2).

—nchi yenyewe maskini —

Aliyesema hii nchi maskini nani? – (uk. 3). Kutowatii ni kutomtii Mungu (uk. 41) Askari na bunduki yake mfalme

Hata bwana anajua. – (uk. 64)

— watu na viatu (uk. 64) ni watu wa maana na watu wa kudharauliwa.

Tasfida (usafidi) ni ufundi wa kutumia lugha nyepesi kuficha uzito halisi ambao una athari za hisia kali. Hii ni lugha ya kudumisha adabu. Mifano:

Naona anaendesha tu (uk. 4) badala ya ‘anahara’.

itauwezesha mshumaa kuwaka (uk. 6) badala ya itamzuia kufa.

Hata anavyojibu mtu utatambua vitendo vyake tu! (uk. 18) badala ya, ‘Hata wewe ni mmoja wa wanaochochea,’ au ‘Wewe huyu hapa u mmoja wao. ’

— alishapata mgeni — (uk. 26) badala ya ‘amekopoa’ au ‘amezaa’.

Tabaini ni tamathali ya usemi wa kusisitizia jambo kwa kutumia kikanushi ‘si’. Mifano:

Si basi tu! (uk. 3) kwa maana ya haskuna jingine kabisakabisa.

Mji si mji tena (uk. 47) kwa maana ya mji umeharibika kabisakabisa.

Jazanda ni kisa ambacho kina maana tofauti na ya kawaida. Kuku kutaga mayai madogomadogo ni ishara ya kudorora kwa uchumi (uk. 9).

Ishara ni mbinu ya kutumia kitu au maelezo kuwakilisha kitu kingine au hali fulani. Maelezo ya kusema, ‘Anaranda kutoka sehemu moja ya chumba —’ ni ishara ya ukosefu wa utulivu (uk. 1). Daktari Siki na Nesi Waridi wanapoongea Kiingereza ni ishara ya kuonyesha wana elimu (uk. 5). Maneno ya Waridi, ‘Kitoto chenyewe kiriba chaongoza,’ yana maana ya tumbo kuwa kubwa (uk. 5). Ni ishara ya utapiamlo. Meya kugonga meza akiwa na Daktari Siki ni ishara ya kukasirika (uk. 12). Maelezo jinsi Meya anavyopanga kuwapokea mameya kutoka nchi za nje ni ishara ya ubadhirifu. Anaongea kuhusu hoteli ya kifahari na mvinyo na divai kutoka nchi za kigeni —- (uk. 25). Fimbo ya Meya (uk. 61) ni ishara ya umeya na mamlaka yanayoambatana nao. Bila hiyo mji hauna umeya wala mamlaka ya meya. Mfululizo wa migomo ya wafanykazi ni ishara ya uongozi mbaya.

Taswira (picha) ni mbinu ya kimaelezo anayoitoa mtunzi. Huonyesha mandhari ya kunakotokea matukio. Mfano wa taswira ni nyumba nzuri anamoishi Meya. Ina zulia lenye ruwaza (mapambo) za kupendeza. Hiyo inatoa taswira ya nyumba ya kifahari. Meza yake yenye vyakula mbalimbali vinatoa picha ya mtu ambaye ana maisha ya raha. Mlolongo mrefu wa wagonjwa unatoa taswira ya watu wenye shida. Hawana jambo jingine la kufanya ila kungoja. Mara nyingi taswira na ishara zinaingiliana na hata huenda zikawa kitu kimoja, hali ikitegemea mtazamo wa msomaji.

Tashihisi (tashhisi, uhuishaji, uhaishaji) ni mbinu ya kuvipa vitu uhai, vitendo na tabia za binadamu. Mifano:

— kiriba chaongoza (uk. 5). Kutangulia katika mwendo ni uwezo wa binadamu wala si kiungo cha kiwiliwili chake.

kutembeza virungu — (uk. 19) kwaweza kuonekana kama kwenye maana ya virungu kuwa na miguu kuweza kufanywa vitembee. Maana ya maneno haya ni ‘kuwapiga kwa virungu’.

Wanatawala nzi na harufu (uk. 73). Kazi ya kutawala ni ya binadamu. Hivi viwili havina uwezo wa kutawala, kutoa uongozi. Kutawala kwavyo kuna maana tofauti ya kusema, ‘kujaa, kuwepo kwa wingi’.

Lami haina meno lakini inavila viatu (uk. 69).

Takriri ni mbinu ya urudiaji kwa nia ya kutilia mkazo. Mifano:

Wakati wa kuombewa Meya anarudia, ‘Aaameni! Aaamen!’ na pia ‘Aaamen! Aamen!’ (uk. 41). Amesisimka kiasi cha kupandwa na jazba akitaka maombi ya Mhubiri yatimie (pengine mara iyo hiyo).

Katika sauti kuna urudiaji huu ni wa kishairi (uk. 57).

Haki yetu! Jasho letu! Haki yetu! Jasho letu! Damu yetu!

Yule yule aliyepewa — (uk. 28).

Let rat! Let rat! Let rat! Let rat! (uk. 64) ni takriri za Dida akiigiza kwata ya askari ambao husema, ‘Left-right! Left-right! —-’

Tanakali za sauti ni milio, hasa ya kuiga sauti ya kitu kiangukapo au kipigwapo. Mmnm!

(uk. 3) ni mguno wa kutokubaliana na kauli fulani. Siki haamini hii nchi ni maskini.

Methali zimetumika kama si moja kwa moja, kwa kurejelewa. Mifano:

Siki ametumia ngoja ngoja huumiza matumbo kupinga kukawia kuwasilishwa kwa dawa zilizoahidiwa. Waridi anamhimizia Siki umuhimu wa kusubiri kwa kusema, ‘Haraka haraka haina baraka (uk. 2).’ Siki anasema, ‘Sikio la kufa halisikii dawa —’ na anarejelea methali anaposema, ‘Ngoja ngoja hii haisaidii matumbo (uk. 46). ’

Misemo na nahau ni kama:

— kunitoa roho (uk. 77) nahau yenye maana ya ‘kuniua’.

— kuwaua ndege watatu kwa jiwe moja (uk. 30) ni msemo ambao una maana ya kusema ‘kupata faida nyingi, hasa kutatua matatizo mengi, kutokana na kufanya jambo moja’.

Uzungumzinafsi (uzungumzinafsia) ni ufundi wa kumpa mhusika maneno ya kujisemea. Meya anaponung’unika kuhusu mayai kuwa madogo anajisemea (uk. 8). Anapofanya matayarisho ya makaribisho ya mameya wa kutoka nchi za nje anajizungumzia (uk. 25). Siki anajizungumzia baada ya kuagana na Diwani III akiyatilia maanani maneno ya mwisho ya ushauri wa diwani huyo (uk. 56). Onyesho la Tatu, Sehemu ya Tatu ni uzungumzinafsi wa Dida (ku. 64-65).

Udondoshi (ufupishaji) wa maneno ni mbinu ya kuacha herufi au maneno au hata sehemu katika maandishi kwa nia maalumu. Kama ni herufi, mara nyingi huwa kwa lengo la kuigiza lafudhi (matamshi) ya mtu au watu fulani. Mifano:

— nyinyi ndi’o mnajua — badala ya –— nyinyi ndio mnajua — (uk. 5).

— umwambie ’ende kortini (uk. 29) badala ya — umwambie aende kortini.

Tena leo(uk. 10) ni maneno ya Meya. Hakamilishi usemi wake. Haikosi mtunzi ameacha maneno mengine, sehemu fulani, kwa lengo la kumpa msomaji fursa ya kujiuliza au kuwazia suala la bahati mbaya aliyoileta Siki. Habari za ziara ya awali hazipo. Kuonyesha maneno ya mhusika fulani hayatakikani udondoshi hutumika. Usemi wa kukatizwa. Mfano ni Diwani III anapoongea anaeleza na akiendelea, ‘Tusi…’ (uk. 16 Diwani I anamkatiza. Hataki msimamo wa Diwani III.

Udumishaji (urefushaji) ni mbinu ya kuongeza herufi au maneno au hata sehemu katika maadnishi ya kifasihi kwa nia maalumu. Katka hali ya kawaida neno la kukamilishia maombi ni ‘Amen!’. Kuonyesha ni kama Meya amepandwa na jazba maneno anayompa mtunzi ni: ‘Aaamen! Aaamen!’ Naye Mhubiri anapewa: ‘Ameen!’ (ku. 41, 44).

Maswali ya balagha ni mbinu ya kuwapa wahusika maswali ambayo hayahitaji majibu na mengine ambayo majibu yake ni wazi. Kazi ya maswali kama hayo ni kumfanya msomaji afikirie zaidi. Katika tamthilia yanaweza kutumika kwa ajili ya kuihusisha hadhira. Mifano: Wakati wa kutiwa nguvuni Diwani I na Diwani II wanauliza kila mmoja, ‘Kweli?’ – (uk. 79). Waridi anapouliza, ‘Sisi tutafanya nini na nchi yenyewe maskini; ombaomba?’ – (uk. 3) hatarajii Daktari Siki ampe jibu.

Mbinu changamano ni ufundi unaojumuisha tamathali mbili au zaidi katika matumizi fulani. Mfano mzuri ni maneno ya Meya, mwishoni mwa Onyesho la Kwanza, Sehemu ya Tatu: ‘Hawa wanaotaka uwasikilize ni mzizi wa vizazi vya kesho! Yote yanategemea uwezo wetu.’ – (uk. 56). Maneno haya ni ya mbinu ya uzungumzinafsia kwani Meya anajizungumzia. Maneno yaya haya ni ya kumnukuu Diwani III (uk. 55) anapomsisitizia Meya avijali vizazi vijavyo. Mtunzi ametumia mbinu ya udondoaji. Kwa hivyo, ufundi huu ni mbinu changamano. Una uzungumzinafsia na udondoaji. Pia, mbinu hii ina sitiari kwani inawataja watu kuwa ni mzizi. Mbinu hii inatumiwa kuangazia mawazo ya Meya baada ya Diwani III kuondoka. Mfano mwingine ni usemi wa Diwani III, ‘Sikio la kufa halisikii dawa

—- (uk. 46).’ Ni methali ambayo imetumika kiufundi kufanya kazi ya sitiari wakati uo huo.

Hotuba ni maelezo marefu katika tamthilia. Hotuba zinaeleza mambo maalumu. Katika tamthilia ya Mstahiki Meya zipo fupifupi na pia ndefu kiasi. Maneno ya Waridi (uk. 3) ni hotuba fupi. Maneno yake yanazuzngumzia suala la amri ya kuwataka wagonjwa (maskini) walipie huduma wanazozitaka. Siki anapomjibu Waridi anahutubu (uk. 7) kuhusu ahadi za uongo wa Meya. Kiongozi wa wafanyakazi anawahutubia wafanyakazi wanaogoma (uk. 57) kuhusu madhila yanayowazonga.

Tashtiti ni mbinu ya kutumia vichekesho, kinaya na dhihaka. Kawaida ni mbinu ya mzaha wa kisiasa. Tashtiti hufanya kazi ya kuwakejeli wanasiasa. Meya kutaka mayai makubwa katika hali ya uchumi uliodorora kiasi cha kuku kutaga mayai madogomadogo na katika hali ya ukosefu wa chakula ni dhihaka. Mbinu hii imetumika kufichua uovu na ujinga katika jamii. Meya kutaka mpaka binamu yake amwite ‘Meya’ ni dhihaka. Msomaji anafichuliwa uovu wa mtu kulewa cheo kiasi cha kutaka jina lake halisi lisitumike, hata nyumbani; anataka ajulikane kama Meya hata nyumbani, mahali ambapo si rasmi (uk.12).

Aaameni!’ Za Meya zinatoa kinaya kwa mtu mwovu ambaye hajaonyesha toba akijisingizia unyenyekevu na imani mbele za Mungu (uk. 41-44). Kinaya hii inafichua unafiki wa Meya na upofu wa Mhubiri.

Meya anaposisitiza yeye kwenda choo ni mhimu kwa mwajiriwa kupata kazi (uk. 54) na kwamba madiwani kuongezwa mishahara na kutozwa kodi na demokrasia ni kinaya (uk. 22). Ni tashtiti inayoweka wazi ujinga wa baadhi ya viongozi wanaojiona wapo kuhudumiwa badala ya kuhudumu.

Wanajiongeza mishahara huku wakitoa kauli rasmi baraza halina pesa (uk. 71).

Sifa anazozipa Baraza la Cheneo Meya zinaonyesha ujinga wake. Watu wanalilia umaskini na mji umejaa takataka.

Mstahiki Meya ni cheo ambacho kinaashiria ukuu. Kwa mujibu wa wadhifa wa Meya, hata kama hatajwi kuwa mstahiki, ni kiongozi mwenye haki ya kupata kitu na heshima fulani.

Hata hivyo, katika tamthilia hii Sosi ambaye ni Meya hastahili wadhifa huu. Yeye kama Meya hastahili cheo cha ‘mstahiki’. Kwanza yeye mwenyewe si mstahifu. Hana tabia ya kuwaheshimu watu wengine. Hata hawawaheshimu madakatari, waalimu na Diwani III. Yeye kuwa Mstahifu Meya anajitakia makuu na ni kejeli kwa viongozi wengine.

Utata: Siki akiongea kuhusu mameya kutoka miji mingine huku kwingineko kukizungumziwa mameya kutoka nchi za kigeni, ni wazo gani linalokujia?

SURA YA TANO

Maswali ya marudio

Baada ya kusoma na kudurusu ni wajibu wa mtahiniwa kufanya mazoezi. Ukifanya hivi itakuwa kazi rahisi kupita mtihani wako vizuri. Ili uweze kufanya hivyo soma tamthlia hii kwa makini mara nyingi, ielewe vizuri na uyaweke matini akilini.

Ni muhimu ujue barabara aina mbalimbali za maswali na mambo yanayohitajika kulijibu kila swali.

Aina za maswali:

 1. Maswali ya
 2. Maswali ya

Katika aina hizi kuu mbili unaweza kuulizwa:

 • Jadili
 • Eleza
 • Fafanua
 • Tofautisha
 • Fananisha
 • Thibitisha (onyesha ukweli)
 • Toa mifano

(i) Linganisha.

Kwa kuwa maswali yote yatakayoulizwa yatatokana na tamthilia hii (na kwa mujibu wa vitabu vingine vilivyoteuliwa) kujibu swali la muktadha hakikisha unajua barabara:

 • Mahali (mandhari) [Wapi?]
 • Mhusika (au wahusika) [Nani au akina nani?]
 • Wakati (kimuda na kimatukio) [Lini?]
 • Sababu [Kwa nini?]
 • Athari [Matokeo?]

Mifano:

 1. Wakisubiri ugonjwa nao utasubiri? Hujui ngoja huumiza matumbo?
 • Ni nani anayeyasema maneno haya?
 • Anamwambia nani maneno haya?
 • Ni lini anapoyasema maneno haya?
 • Wahusika wako wapi?
 • Kwa nini anamwambia maneno haya?
 • Matokeo ya maneno haya ni nini?
 1. Si nzuri? Ni baraza gani lenye uthabiti kama letu ambalo linaongozwa na Mstahiki Meya sosi? Lipi katika ujirani wetu?

Liweke dondoo hili katika muktadha wake.

 1. Mimi na Meya ni mfano wa mafuta na maji. —-

Likamilishe dondoo hili kisha ufafanue tofauti kati ya wahusika.

 1. Fimbo ya Meya inatekeleza umuhimu gani katika tamthilia ya Mstahiki Meya?
 2. Kuna uhasama gani kati ya Meya na Siki na
 3. Fafanua uhusiano uliopo kati ya Sosi, Siki na
 4. Eleza kwa mifano jinsi tamathali zifuatazo zilivyotumika katika tamthilia ya Mstahiki Meya:
 • Tabaini
 • Usambamba
 • Majazi
 1. Jadili jinsi masuala ya ufisadi yanavyojitokeza katika tamthilia ya Mstahiki Meya.
 2. ‘Manung’uniko ni chumvi ya maisha ya mfanyakazi.’
 3. Uongozi ni kioo cha wananchi. Fafanua.
 4. Jadili chanzo na athari za migomo ya wafanyakazi, ukizingatia tamthilia ya Mstahiki Meya.
 5. Mstahiki Meya ni kiongozi wa aina gani?
 6. Diwani III na Tatu wanashabihiana vipi kuhusu hali ya wafanyakazi?
 7. Tambua na ueleze kwa mifano maudhui makuu katika tamthilia ya stahiki
 8. Jadili dhamira ya mtunzi katika tamthilia ya Mstahiki Meya.
 9. Ni akina nani walio wahusika wakuu katika tamthilia ya Mstahiki Meya?
 10. Toa mifano mitano ya mbinu ya majazi katika tamthilia ya Mstahiki Meya.

Maswali na Majibu Kielelezo

 1. ‘Mwondolee nuksi ya maadui na kinyongo cha ’
 • Haya maneno yalisemwa na nani?
 • Maneno haya yalisemwa lini?
 • Alikuwa anamwambia nani?
 • Wahusika walikuwa wapi?
 • Kwa nini msemaji anayesema maneno haya?
 • Eleza matokeo ya maneno na tukio
 1. (a) Wananchi wanachangiaje katika kuwepo kwa uongozi mbaya?

(b) Ni kwa njia gani uongozi mbaya unaweza kurekebishwa?

 1. Eleza jinsi mbinu zifuatazo zilivyotumika katika tamthilia ya Mstahiki Meya:
 • ishara
 • takriri
 • tasifida
 • hotuba
 • ushairi

 1. ‘Hakikisha mtu huyo halikaribii lango kuu kuanzia sasa. Jengo langu alione

Alright?’

Liweke dondoo hili katika muktadha wake.

Majibu Kielelezo

 1. (a) Ni muhubiri.
 • Maneno haya yalisemwa adhuhuri, siku ileile Bili alipomwahidi Meya angemfuatia Meya amfanyie
 • Hasa anamwomba Mungu Muumba wa nchi na
 • Msemaji yu duniani naye anayeambiwa kwa imani yu Anayeombewa yu duniani katika ofisi ya Meya.
 • Alikuwa anamwombea Mstahiki Meya. Meya alikuwa anakabiliwa na malalamiko ya wafanyakazi wakitaka nyongeza ya Wakati uo huo kumekuwepo na kilio cha ukosefu wa dawa katika zahanati. Pia, alikuwa anawahutumu Daktari Siki na Diwani III (kheri) kwa wachochezi.
 • Meya alijibu, ‘Aaameni,’ Mhubiri akaomba wasiweze kutetemesha uongozi

Meya akajibu,’Aaameni!’ naye Mhubiri akaomba (uongozi wake Meya) udumu milele na milele. Meya alijibu, ‘Aaameni’ na mara ile wakaingia askari wawili na Gedi.

Walipiga mlango teke na kuwaamrisha walale chini mara moja na waweke mikono juu.

Meya na Mhubiri walitii kisha Gedi alimwomba Mstahiki Meya pole. Akalieleza walidhani vinyangarika walikuwa wameingia kuleta fitina. Meya aliwaambia waende naye akabaki na Mhubiri wakiona lilikuwa tukio la Mungu kuwatolea muujiza. Meya alimwahidi Mhubiri sadaka ya shilingi laki moja kila mwezi.

 1. (a) Wananchi ndio wanaowachagua viongozi. Hata kiongozi akiwa mbaya wao ndio wamchaguao tena. Sosi ambaye ni Meya amechaguliwa mara tatu. Watu hushawishiwa kwa ujanja wa wanasiasa. Meya anajidai ana akili. Akili yenyewe anairejelea kuwa ni mali. Kwa akili,ambayo ni ujanja, na mali mwananchi hushawishiwa.

Wananchi hujinyenyekeza kupindukia mbele za viongozi wao. Kwao viongozi ni wakubwa. Mfano ni Gedi, Mpambe wa Meya. Daima humwita, ‘Sir’. Humpigia saluti. Meya huufurahikia unyenyekevu huo. Kujikomba kwa wananchi ni mchango wao kwa uongozi mbaya.

Hata mambo yanapokuwa mabaya wananchi hunyamaza tu. Wanapewa nyimbo na hotuba za kizalendo. Kutokana na kunyamaza, amani ya nje huonekana machoni pa viongozi. Kutotetea haki zao na kutokataa uovu kwa sauti ya juu, wananchi huchangia katika uendelezaji za uongozi mbaya. Wanataaluma wanajitenga na siasa. Wanaogopa uchafu ambao unahusishwa na siasa. Kwa kutojitosa katika siasa wanachangia katika uongozi mbaya wa uongo wa wanasiasa.

Wananchi waweke mbele ubinafsi wao. Kwa kutaka kunufaika wanajipendekeza kwa viongozi. Katika hali hiyo wao huutetea uongozi mbaya kwa ajili ya manufa yao.

Mfano ni Bili. Anafaidika kutokana na kuwa karibu na Meya. Hakosi kumsifu na kumtetea. Naye Mhubiri anamwombea dua njema. Hivyo, Meya anaweza kuyaona makosa yake?

( b) Wananchi wachukue jukumu la kuwachagua viongozi wazuri. Kiongozi asiyejali maslahi yao wasimchague tena.

Wakati wa uchaguzi wananchi wasikubali kudanganywa kwa ujanja na pesa za wanasiasa wasiofaa.

Wananchi wawe katika mstari wa mbele kukataa uovu wao, wao huwachagua viongozi waovu kama wao.

Katika kutambua na kutetea haki zao wananchi wasikate tamaa. Hata viongozi wakikataa kuwasikia waendelelee kudai kwa suti moja ya umoja mpaka wapate haki yao.

Pia, wanataaluma wasiwaachie wanasiasa nafasi zote za uongozi. Wajitose katika siasa ili waweze kurekebisha maovu katika uongozi wakiwa ndani ya uongozi.

 1. (a) Ishara inaweza kuwa kitu chochote cha kuelekeza. Maelezo katika tamthilia ni ishara za mambo mbalimbali. Mtu akiranda katika chumba ni ishara ya kutokuwa mtulivu. Katika miji mikubwa ambayo inaongozwa na Meya, Fimbo ya Meya ni ishara ya mamlaka makuu. Bila hiyo baraza haliwi na uhalali wa kuendesha shughuli zake. Migomo miongoni wafanyakazi kwa viongozi kukataa kuwasikiza ni ishara ya uongozi mbaya, udikiteta na upurukushani. Katika watoto tumbo kubwa ni ishara ya ukosefu wa lishebora. Utapiamlo miongoni mwa watoto ni ishara ya Kimya baina ya mazungumzo ni ishara ya mawazo.

(b) Takriri ni urudiaji wa maneno katika mazungumzo. Urudiaji huo hufanya kazi ya kusisitiza jambo au mambo. Kuonyesha Meya ameshikwa na jaza Meya anarudia “Aaameni! Aaamen!”

Katika nyimbo na mashairi urudiaji unafanya kazi ya kutoa muundo fulani wa shairi. Pengine kikwamba, kwa nia ya kuwatia moyo wanaokaririau wanaoimba wimbo.

Watu wanaogoma hujishajiisha kwa kukariri maneno. Wakati mwengine urudiaji hutoa hakikisho.

(e) Tafsida ni mbinu ya kutumia maneno ya kupunguza ukali waa hisia. Mfano mmoja ni wa kutumia lugha ya adabu. Badala ya kusema ‘hatakufa’ unaweza kusema ‘mshumaa utaendelea mwaka’. Mbele ya watu mtu husema ‘anaendesha’ huku akijua’ anaharisha’. Bili anataka kujua iwapo mkewe Meya ‘alishapata mgeni’ kwa maana ya ‘alizaa’.

 • Hotuba ni maelezo marefu katika tamthilia. Sehemu nyingi ni za maneno machache machache. Mambo muhimu yanafafanuliwa kwa hotuba. Katika tamthilia ya ‘Mstahiki Meya’ kuna hotuba mbalimbali mifano ni hotuba za Siki kwa Sosi, Diwani III kwa Meya (sosi) na kiongozi wa wafanyakazi kwa wenzake
 • Ushairi umetumiwa kuwasilisha ujumbe kwa kutumia lugha ya Unajitokea kama wimbo wafanyakazi wanapokuwa katika mgomo. Manemo ya siki mara tu baada ya kuongea na Tatu ni shairi. Maneno ya ushairi ni rahisi kukumbukwa kwa ajili ya uingizaji.
 1. Siku ya pili baada ya Nesi Waridi kusisitiza dawa zilikuwa njiani Daktari Siki ameenda kwake nyumbani kumwona Meya Sosi. Meya ni binamu yake. Meya anamkasirikia siki kwa kumwita Sosi badala ya Meya anamhutumu kuchochea mgomo mwingine. Siki anamwambia yeye ameenda kumwambia habari za maisha ya watu. Kwamba hali ya maisha ni ngumu.

Meya anasisitiza halipo baraza lenye uthabiti kama lao linaongozwa na Mstahiki Meya Sosi. Siki anapinga msimamo huu wa Meya. Anamwambia yapo yaliyoendelea na kufika upeo na hayakukomea hapo. Meya anamkasirikia kwa kutoona anayoyafanya (yeye Meya). Siki anasisitiza watu wana shida.

Kwa tofauti kali inayozuka Meya anamwona kuwa msaliti. Siki anasisitiza kwa ukakamavu kuwa kinachohitajika ni kuleta afueni katika Cheneo. Meya anakasirika mpaka anamwamuru Gedi amwondoe. Siki anapokuwa ameenda ndipo anapewa hiyo amri ya kuhakisha Siki harusiwi kurudi tena.

Baada ya hapo Meya anakuwa na mkutano wa dharura alasiri. Katika huo mkutano analalamika baadhi ya madiwani wanawachochea watu. Anamshuku Diwani III bila kumtaja. Anamwona sawa na Siki. Katika mkutano huo kunapangwa mikakati ya kukabiliana na mgomo wa wafanyakazi.

SURA YA SITA

Mtihani wa KCSE

Sehemu hii inahusu mtihani wa Kiswahili.

Somo la Kiswahili lina karatasi tatu za mitihani. Karatasi ya Kwanza ni ya INSHA,

Karatasi ya Pili ni ya LUGHA na Karatasi ya Tatu ni ya FASIHI.

Karatasi ya FASIHI ni sehemu tano: Fasihi Simulizi, Hadithi Fupi, Ushahiri, Riwaya na Tamthilia.

Swali la kwanza katika mtihani wa fasihi ni la lazima. Kwa hivyo, ni lazima kila mtihiniwa ahakikishe amejiandaa barabara katika sehemu zote tano za fasihi. Hujui swali la lazima litatoka wapi.

Mitihani Kielelezo wa KCSE

KISWAHILI 102/3

Karatasi ya Tatu FASIHI

Saa2½

Jibu maswali manne peke yake. Swali la kwanza ni la lazima. Chagua maswali mengine matatu kutoka sehemu zilizobaki, yaani, Riwaya, Tamthilia, Hadithi Fupi na Fasihi Simulizi. Usijibu maswali mawili kutoka katika sehemu moja.

Maswali yote yana alama 20 kila moja.

SEHEMU YA A: USHAHIRI

 1. Swali la lazima

Lisome shairi lifuatalo kisha ujibu maswali:

Rossy amezaliwa akiwa safi Ole wake yule wa kumchafua Sawa na theluji safi anang’aa Sina shaka popote anavutia Yowe hapigi kitu akingojea.

Mwangi ni baba yake mtoto Rossy Waziwazi habari yeye husema Aidha kwa nguvuze amesimama Naamini unamfuata wema

Gegole taliona anaposema

Insafu awe nayo na huruma.

Raheli bintiamu yake Rossy Aghalabu hupenda kucheza naye Huba kubwa kuonyesha ni haliye Elimu kuipata ni tamaaye Laazizi ni wangu nimpendaye Ilahi Mwema Ampendelee.

Savane ndilo jina lake la pili Angalau ni jina kubwa la raha Vilevile ni la kubeba furaha Anaposema jambo si kwa kuhaha Nenda kanene naye upate raha Ela usiende kuzusha karaha.

Yvette ndiye dada yake Raheli Vilevile ni mtoto wa kucheka Ebu niendelee kumkumbuka Tangu Likuyani alipoondoka Taita anakaa kuelimika

Elimu inamfunza kuandika.

Rose ni kwambie ni jina la pili Ombi alilonipa nitatimiza Sisemi sasa ila nitajikaza Elimu nitazidi kuisambaza.

Ng’onyere huyo alinifurahisha Ghafula akaenda Voi kwa mama

’Namwombea mambo chekwachekwa mema

Ozi linasubiri kumtazama Najua hazitampata zahama Yeye Mola atampa na karama Elimu yake nzuri haitakoma

Roho yangu yote imemgandama Ewe Mola mjali kwa rehema.

Amani tudumishe kote nchini Maendeleo yaweze kutufaa Angalau wana sikate tamaa Na sisi tuweze rohoni kung’aa Imani sote tukiifurahikia.

 • Eleza kwa fasili aina ya utunzi huu. (alama 4)
 • Ni bahari gani zinazoupamba utunzi huu? (alama 6)
 • Eleza umbo la utunzi huu. (alama 4)
 • Utunzi huu una wito gani muhimu? (alama 2)
 • Nini maana ya:
 • gegole taliona anaposema
 • huba
 • ozi
 • tudumishe? (alama 4)

SEHEMU YA B: RIWAYA

Kidagaa Kimemwozea, Ken Walibora

Jibu swali la 2 au 3

 1. Jadili madhumuni na dhamira ya mtunzi wa riwaya ya Kidagaa kimemwozea. (alama 20)
 2. Liwekee dondoo lifuatalo muktadha wake. (alama 20)

“Hapana. Sijawahi kuiba hata senti moja ya mtu.”

SEHEMU YA C: TAMTHILIA

Mstahiki Meya, Timothy M. Arege

Jibu swali la 4 au la 5

 1. Fafanua ujasiri wa Daktari Siki na jinsi unavyoshabihiana na msimamo wa Kheri. (alama 20)
 2. ‘Iwapo mama muuza ndizi analipa kodi ili kuchangia kulijenga taifa iweje kwamba madiwani wasilipe kodi?’

Liweke dondoo hili katika muktadha wake. (alama20)

SEHEMU YA D: HADITHI FUPI

Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine, Ken Walibora na Said A Mohammed (wahariri)

Jibu swali la 6 au la 7

 1. Kwa mujibu wa hadithi ya Kikaza na Robert Oduori fafanua fumbo la ‘ kikaza’. (alama 20)
 2. ‘Nilimwambia kila kitu; kutoka mwanzo hadi mwisho. Kwa sasa sioni sababu ya kuficha lolote. Hata tusipomwambia atakuja kujua ukweli. —-’ kutoka Mwana wa Darubini, Kristina Mwende
 • Ni nani aliyeseme maneno haya? (alama 2)
 • Kwa mujibu wa dondoo hili, ni kitu gani kilichofanyika? (alama 3)
 • Msemaji anamwambia nani? (alama 2)
 • Wahusika wako wapi? (alama 2)
 • Ni wakati gani maneno haya yanasemwa? (alama 2)
 • Ni kwa nini mnenaji anayesema maneno haya? (alama 2)
 • “Mungu si ”

Fafanua ukweli wa fumbo hili kwa mujibu wa hadithi ya Mwana wa Darubini. (alama 7)

SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI

Jibu swali la 8 au la 9

 1. Eleza kwa kundani tofauti kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi. (alama 20)
 2. Eleza maana na utoe mifano ya:
 • visakale
 • ngomezi
 • nyiso
 • hurafa
 • (alama 20)

Marejeleo

Mstahiki Meya, Tomothy M. Arege, Vide-Muwa Publishers Ltd, 2009

Kamusi ya Fasihi Istilahi na Nadharia, K. W. Wamitila, Focus Publications Ltd, 2003

Mwandishi huyu

James Kemoli Amata ni mwandishi wa jumla na mwalimu mstaafu wa Kiswahili. Aliwahi kufunza katika St. John The Baptist Shule ya Sekondari ya Likuyani, Soy (Februari 2000- 2007); Shule Kuu a Wasichana ya Moi, Eldoret (Septemba 1976-1986 na Julai 1990-Februari 2000) na Shule ya Sekondari ya Wangulu, Wodanga (1987-Julai 1990).

Kati ya vitabu vyake vingine ni Kisa cha Zahara Mage, Taaluma ya Ushairi (na Kitula King’ei), Highly Regretted: An autobiography of a bad Teacher, —-

Facebook Comments
Recommended articles